Kwa utangulizi niliotoa kwenye makala za jana na juzi nadhani utakuwa umepata picha ya kitu kikubwa kinachofanywa na CITES, kuna mambo mengi sana ambayo nchi wanachama wananufaika na kuwa washiriki kwenye mapambano haya ya kuhakisha biashara za kimataifa za wanyamapori na mimea zinadhibitiwa ili kuendeleaza mazingira halisi ya wanyama na viumbe hai wengine. Kama nilivyo kwisha kueleza kwamba CITES ina jumla ya nchi wanachama 183, ambao ndio wanaofanya mikutano na mikataba mbali mbali kuhusiana na biashara, hali ya wanyamapori na mimea.
Kuna mambo mengi makubwa yamefanyika na CITES, najaribu kufikiria kungekuwa hakuna makubaliano ya kimataifa kuhusu biashara hii ya viumbe hai, nadhani hali ingekuwa mbaya sana. Kwa sababu licha ya faida nyingine nyingi zinazotokana na CITES, bado kuna watu au nchi zina endesha biashara haramu za viumbe hai wa mwituni. Nimependa sana juhudi hizi za kuhakikisha maliasili tulizojaliwa na zinaendelea kuiwepo kwa vizazi vingi, ili na mazingira salama ya kuishi watu na viumbe hai wengine yawepo. Kuna faida nyingi sana zinazotokana na nchi kuwa mwanachama wa CITES, nitaelezea hapa.
- Kuzuia kutoweka kwa spishi za wanyamapori na mimea
Kazi inayofanywa na nchi wanachama na kamati mbali mbali za CITES, ni kubwa sana taarifa tunazopata kuhusu hali za wanyama na mazingira yake zinasaidia sana nchi husika kujipanga na kutumia kila njia kukabiliana na hali inayopelekea kupotea kwa viumbe hai hao, mfano kama ni biashara ya wanyama au sehemu za wanyama au miti basi, watafanya kazi kubwa sana kuzuia biashara inayohusisha wanyamapori hao au mimea hiyo. Kama tunavyozuia biashara za meno ya tembo na faru.
- Ushirikiano na msaada mkubwa kwa nchi
Nchi zimetofautiana viwango vya idadi ya wanyama na mimea pia, kuna sehemu nyingine kuna idadi kubwa sana ya wanyama na mimea, na pia kuna mazingira mazuri ambayo yanatunza idadi kubwa ya viumbe hai, hivyo bila kuwepo kwa juhudi za dhati kwa nchi hiyo kufanya utafiti na njia nzuri zaidi za kuendelea kuyatunza mazingira hayo yanaweza kuharibika na kusababisha vifo kwa maelfu ya viumbe hai waliokuwa wanategemea kuishi kwenye maeneo hayo. Ushirikiano wa wataalamu, vifaa na hata fedha kwa ajili ya kutunza na kuendeleza viumbe hai kwenye nchi wanachama ni jambo ambalo limekuwa liukifanyika na CITES.
- Kuwa na sera na sheria imara za uhifadhi wa viumbe hai
Kumbuka hapa ninapozungumzia viumbe hai namaanisha wanyamapori na mimea. CITES huwa wanafanya mikutano mbali mbali yenye lengo la kupitia makubaliano yao, utekelezaji, na jinsi nchi wanachama zilivyo simamia masuala ya usafirishaji wa kimataifa wa wanyamapori na mimea iliyo hatarini kutoweka. Hivyo kila mwaka nchi wanachama huwasilisha ripoti iliyoeleza utekelezaji, usimamizi, vibali vilivyotolewa kwa kuuzwa kwa wanyamapori na mimea. Baada ya kupitia kila ripoti kutoka kwa nchi wanachama ndipo yanapofanyika maazimio mbali mbali ili kuboresha utekelezaji wa makubaliano yao. Ambayo hupelekea nchi husika kuwa na sheria na kanuni nzuri za kuhifadhi viumbe hai na mazingira yake.
- Usalama wa wanyamapori na mimea dhidi ya magonjwa
Kwa kuwa lengo la CITES ni kudhibiti, kusimamia biashara za wanyamapori na mimea ambayo ipo hatarini kutoweka. Imetengeneza utaratibu mzuri wa kuendesha biashara hizi za kimataifa. Hii ni biashara inayofanyika kwa umakini wa haili ya juu sana, baina ya nchi ambazo zinataka kuuziana wanyama au mimea, kunakuwa na wataalamu wa afya za wanyama na watalaamu wa afya za mimea kwa ajili ya kupima hali ya afya ya spishi unayaotaka kuuza. Hii ni njia nzuri ya kuzuia magonjwa ya kuambukiza kwa wanyama na mimea mingine. Hivyo endapo mnyama anayetaka kusafirishwa atakugundulika kuwa na kasoro na matatizao kama magonjwa hataruhusiwa kuvuka mpaka wa nchi nyingine.
- Elimu na mafunzo mbali mbali
CITES inaendeshwa na watalaamu walio bobea kwenye masuala ya wanyamapori, mimea na mazingira pia wana uwezo mkuwa sana wa kuwasaidia wengine ili waweze kupata maarifa ya namna ya kuendesha uhifadhi na mafunzo kwa watu wanaohusika na wanyamapori na mazingira kwa ujumla. Unaewaza kutembelea website yao ukaona jinsi wanavyofanya kazi, www.cites.org
- Hamasa ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira ya Viumbe hai
Pia utaratibu waliouweka wa kupanga wanyamapori na mimea kwenye makundi matatu waliyoyaita Appendix I, II na III, imefanya watu, nchi na wadau wengine wa sekta hii kuwa na hamasa ya kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kunusuru wanyamapori na mimea wasiingie kwenye orodha ya wanyama walio hatarini kutoweka. Kwasabau CITES wamewapanga wanyamapori na mimea yote iliyo hatarini kutoweka kwa kuiweka kwenye makundi matatu ya Appendix, ambayo kila kundi linaonyesha kiasi ambacho wanyamapori na mimea ilivyo katika hatari kubwa. Kama utasoma utaona jinsi walivyopanga ni zaidi ya wanyamapori na mimea 36,000, ambayo ipo hatarini kutoweka na imewekwa kwenye makundi ya appendix ili kudhibiti biashara ya wanyamapori na mimea hiyo.
Asante kwa kusoma makala hii,
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255683 248 681/+255742 092 569
www.mtalaam.net/wildlifetanzania