Mpendwa msomaji wa makala hizi za wanyamapori, leo nimewaletea makala hii inayohusu farasi wa baharini (seahorse) au kama anavyojulikana kwa jina lake la kisayansi Hippocampus species. Farasi wa baharini ni aina ya samaki wanaopatikana katika bahari ambao maumbo yao yanafanana sana na farasi, ndiyo maana wakaitwa farasi wa baharini.
Wengi wetu tunatambua samaki kama sangara, sato, kibua, kaa, pweza, kamba na taa nk. Leo tunaenda kujifunza aina ya samaki ambao hujawahi kuwasikia mara kwa mara, lakini ni samaki wenye sifa na tabia za kipekee sana tofauti na samaki wengine unaowajua. Karibu sana tusome makala hii ili tujifuze kwa kina upekee wa samaki hawa na umuhimu wao katika mifumo ya ikolojia ya majini.
Kuna takribani spishi 47 za Farasi wa baharini duniani, lakini idadi hii inaweza kubadilika endapo tafiti mbalimbali zitafanyika kuhusiana na spishi hizi.
Farasi wa baharini hupatikana baharini tu. Kutokana na umbo lao na kukosa mapezi ,watu wengi hudhani kwamba viumbe hawa sio samaki, lakini hawa ni samaki kama samaki wengine , wana kibofu cha kuogelea au kibofu hewa (swim bladder) ambacho huwasaidia kuogelea kwenye maji. Pia kama Samaki wengine Samaki hawa wana matamvua (gills) kwa ajili ya kupumulia.
Picha hii ya farasi wa baharini imetolowa kwenye tovuti ya illegalwildlifetrade.net
Sifa za farasi wa baharini
Farasi wa baharini ndiye samaki mwenye kasi ndogo kuliko samaki wote kwa sababu hawana mapezi ya pembeni ambayo yanasaidia katika kuogelea kwenye maji. Badala yake wanatumia pezi moja dogo lililopo mgongoni ambalo halimuwezeshi kuogelea vizuri na haraka.
Picha hii ya farasi wa baharini imetolowa kwenye tovuti ya AZ animals.
Mkia wao una uwezo wa kushika vitu mbalimbali.
Mwili wao umezungukwa na mifupa midogo midogo.
Picha hii ya farasi wa baharini imetolowa kwenye tovuti ya https//worldanimalfoundation.org
Wana uwezo wa kubadilika badilika rangi ili kuendana na mazingira.
Picha hii ya farasi wa baharini imetolowa kwenye tovuti ya AZ animals
Hawafumbi macho yao wakati wa kulala kwa sababu hawana kope kwa ajili ya kufunga macho yao
Picha hii ya farasi wa baharini imetolowa kwenye tovuti ya www.charatoon.com
Urefu
Urefu wa farasi wa baharini hutegemea na aina ya spishi. Kwa ujumla farasi wa baharini wanakadiriwa kuwa na urefu kuanzia sentimita 1.5 mpaka sentimita 35, lakini kwa wastani urefu wao ni kati ya sentimita 18 hadi sentimita 28.
Uzito
Uzito wa farasi wa baharini huwa ni gram 0.007 kwa mtoto aliyetoka kuzaliwa na kwa mkubwa uzito huongezeka mpaka gramu 35, uzito huu hutegemea sana na aina ya spishi, umri, na hatua ya uzazi.
Chakula
Chakula kikuu cha Farasi wa baharini ni mwani,uduvi,kaa na minyoo.Kwa ujumla hawa ni carnivora yaani wala nyama.na kutokana na umbo lao kuwa dogo hata viumbe wanaowala huwa ni wadogo sana.
Kutokana na umbo lao kuwa dogo na mwenye kasi ndogo ya kuogelea uwindaji wao wa chakula huwa kwa kutumia uwezo wao mkubwa wa kuona ambao huwawezesha kutambua aina ya chakula wanachotaka.
Pia farasi wa baharini wana uwezo wa kujifananisha na mazingira hivyo wanapokuwa kwenye mawindo hujishikiza kwenye mimea ya majini na kujifananisha rangi mpaka pale atakapoona mawindo yake na kuvamia.
Baada ya kuvamia mawindo, hutumia pua yake nyembamba kuvuta na kulamba mawindo yake.
Farasi wa baharini hawana tumbo hivyo mmeng’enyo wa chakula hufanyika katika utumbo. Kongosho yao hufanya kazi ya kuzalisha na kusambaza vimen’genya vya chakula kama kimeng’enya cha protein, kimeng’enya cha sukari na kimeng’enya cha fati Kwenda kwenye utumbo ambapo ndipo chakula humeng’enywa na kutoa virutubisho kwenye mwili.
Hivyo basi farasi wa baharini hupaswa kula mara kwa mara ili kuweza kudumisha kiwango cha nguvu katika miili yao. Inakadiriwa kwa wastani farasi wa baharini mkubwa hula mara 30 mpaka 50 kwa siku.
Kuzaliana
Farasi wa baharini dume ndiye anayebeba mimba na kujifungua Watoto. Farasi wa baharini dume hana mayai au mji wa mimba lakini ana kifuko cha kizazi kama sehemu ya mwili wao ambacho kinapokea mayai ambayo hayajarutubishwa kutoka kwa jike. Kifuko hiki kinapatikana mbele ya tumbo lao.
Picha hii ya farasi wa baharini imetolowa kwenye tovuti ya AZ animals
Farasi wa baharini huwa na mwenza mmoja tu kwa kipindi chao chote cha maisha. Kila asubuhi jike na dume hukutana katika maeneo ya dume ambapo hucheza pamoja kwa kuzungukana, kuzunguka kitu, kubadilishabadilisha rangi na pia kushikana mikia, wanafanya hivi ili kuweza kuimarisha uhusiano wao.
Picha hii ya farasi wa baharini imetolowa kwenye tovuti ya www.oceanconservancy.org
Farasi wa baharini jike ana oviposta, ambao ni mfereji unaotumika kutoa mayai nje ya mwili wake. Hivyo jike anapokuwa tayari kuhamisha mayai huweka oviposta yake kwenye kifuko cha kizazi cha dume na kuhamisha mayai ambayo bado hayajarutubiswa. Inakadiriwa jike huweka mayai mpaka 2000 kwa dume kwa ajili ya kurutubishwa na kuatamiwa.
Picha hii ya farasi wa baharini imetolowa kwenye ukarasa wa instagram wa Lopxans .
Dume hurutubisha mayai haya na kuatamia mayai kwa muda wa wiki mbili mpaka nne .Muda wa kuzaa ukifika dume hupata mikazo mikali ya misuli ya tumbo, ambapo misuli hupanuka na kusinyaa. Hivyo kadri anavyapata mikazo ya misuli ndivyo ambayo vitoto vilivyokamilika hutoka kwenye tumbo lake. Vitoto hivi vya farasi wa baharini vinaitwa “fry”
Baada tu ya kuzaliwa fry huachwa na wazazi wao wajitafutie chakula na makazi wenyewe, hivyo ni wachache tu kati ya maelfu wanaozaliwa hufikia ukubwani.
Wanasayansi wanafikiri kwamba sababu ya farasi wa baharini dume kuzaa na sio jike ni kutokana na kuwa fry mara nyingi huliwa na samaki wengine hivyo, dume kubeba mimba inamruhusu jike kupata nafasi ya kutengeneza mayai mengine badala ya kusubiri mpaka azae ndiyo atengeneze tena mayai yeye mwenyewe.
Endapo mwenza mmoja kati yao atakufa, mwenzake naye hukaa siku chache naye atakufa pia, kwani hataweza kuishi bila mwenza wake.
Uhifadhi
Katika mkutano wa mwaka 2002 wa “CITES” shirika la kimataifa linalohusiana na kusimamia na kufuta biashara za kimataifa za spishi ambazo ziko kwenye hatari ya kutoweka, Farasi wa baharini waliorodheshwa katika Appendix II ambayo inahusiana na spishi wote ambao wanaweza wasiwe katika hatari ya kutoweka sasa lakini wanaweza kutoweka endapo hakutakuwa na sheria na kanuni kali za kuweza kuzuia biashara ya spishi hawa.
Mamilioni ya farasi wa baharini huvuliwa na kuuzwa kila mwaka hivyo kutokana na tafiti za Umoja wa Kimataifa wa Kulinda Uasili (IUCN) farasi wa baharini wametajwa wako karibu kutishiwa kutoweka (near threatened, NT).
Nchini Tanzania Farasi wa Baharini Wanapatikana mara chache Dar-es Salaaam, mara kadhaa Lindi na Unguja na Wanapatikana mara nyingi kaskazini mwa Tanzania maeneo ya Tanga, Kigombe, Pangani, Mtwara, Kusini Pemba, Bagamoyo na Rufiji.
Inasadikika kati ya kilo 630 mpaka kilo 930 husafirishwa kila mwaka kutoka Tanzania Kwenda Asia na usafirishaji huu huhusisha farasi wa baharini walio kaushwa (Dried seahorse) (J.M McPherson & A.C J Vicent, 2004). Soma makala nyingine kuhusu viumbe wa baharini hapa Fahamu Maajabu Ya Kiumbe Wa Baharini Aitwae Kasa
Maadui wa Farasi wa Baharini
Kutokana na kuwa ni Samaki wasio na kasi kuliko wote baharini, huwa ni chakula rahisi sana kupatikana kwa maadui zao, kwani njia pekee ya wao kujilinda ni kujifananisha na mazingira hivyo akiwa nje na mazingira ambayo hujifananisha nayo ni rahisi sana kuonekana na kukamatwa.
Maadui wakubwa wa farasi wa baharini ni kaa, Papa, Jodari, Samaki ray na penguins.
Pia farasi wa baharini si chakula pendeleo kwa viumbe wengi baharini kutokana na kuwa na mwili wenye mifupa na kutokuwa na nyama
Tishio la farasi wa baharini.
1.Uchafuzi wa mazingira
Uchafuzi wa mazingira ni moja ya tishio kubwa kwa farasi wa baharini,shughuli kama uchimbaji wa madini,matumizi ya mbolea,maji machafu kutoka viwandani ambayo huelekezwa baharini husababisha
kuchafua maji baharini hivyo kuathiri Samaki hawa .
2.Uvuvi wa kupita kiasi.
Farasi hawa wanapata changamoto kutokana na uvuvi wa kupita kiasi ambapo wavuvi huwavua kwa bahati mbaya kutokana na maumbo yao kuwa madogo au wakati mwingine huvuliwa kwa makusudi kwani watu hutumia samaki hawa kama dawa,mapambo au wengine kwa ajili ya kujipatia kipato kwani samaki hawa huuzwa kwa bei kubwa sana.
Mapendekezo
Mapendekezo yangu ni kwamba sisi Kama wahifadhi na wananchi wa Tanzania tusimame kidete kuhakikisha sheria za uvuvi zinafuatwa zinazo kuzuia uvuaji haramu na holela wa farasi wa baharini.
Tuyatunze mazingira ya baharini kwani ndiyo makazi ya farasi wa baharini, hivyo tukiyatunza mazingira yao tutakuwa tumewatunza nao.
Mashirika mbalimbali na watu mbalimbali waanzishe kampeni za kuwalinda farasi wa baharini, kwani hii itaongeza uelewa wa umuhimu wao katika ikolojia na itasababisha sheria za udhibiti wa biashara ya farasi wa baharini iwekewe mkazo hivyo kuzuia au kupunguza biashara hii.
Tusisahau kuwa Samaki nao ni wanyamapori hivyo tuwaongelee, tuwalinde, tuwatuze kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Hitimisho
Kwa kuhitimisha napenda kuwakumbusha wapenzi wasomaji kwamba farasi wa baharini ni nadra sana hivyo uvuvi na biashara ya viumbe hawa inahatarisha sana uwepo wao katika dunia hii. Hivyo basi tuwalinde ili waendelee kucheza na wenza wao kila asubuhi na madume waendelee kubeba mimba na kuzaa.
Asante sana kwa kusoma makala hii, shukrani za kipekee ziende kwa Sadick Omari Kashushu ambaye amehariri makala hii na kunishauri kuiboresha. Usiache kuwashirikisha wengine maarifa haya; kama una maoni, ushauri na maswali, usiache kuwasiliana na Mwandishi wa makala hii.
MONICA C. MAHILANE
+255 652 267 935