Ni siku nyingine tena wasomaji na wadau wa makala hizi za wanyuamapori bila kuwasahau wahifadhi na mamlaka zote za uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini. Tunakutana tena katika darasa letu huru la wanyamapori na kujuzana mengi yenye manufaa kuhusu wanyamapori na faida ya uwepo wa wanyama hawa hapa nchuni hasa kwenye pato la taifa. Bila kusahau changamoto mbali mbali zinazo wakumba wanyama hawa hasa kwenye maweneo yao asilia na hapa nikimaanisha katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba ya uhifadhi wa wanyamapori.

Kama kawaida leo nakuletea makala nyingine tena ambayo kwa hakika utafurahia uchambuzi wa mnyama kwenye makala yetu ya leo kwani kuna sifa kubwa sana na kujivunia sana kwa uwepo wa mnayama huyu hapa nchini. Tuna kila sababu ya kupenda vilivyo vyetu na kuvitunza tena kwa umakini na moyo wa kujitolea kwa ari na nguvu zaidi.

Tanzania ni moja kati ya nchi pekee duniani inayo jivunia uwepo wa idadi kubwa na jamii nyingi za wanyamapori. Nasi kama watanzania hatunabudi kutembea vifua mbele kwa kujivunia kuwa watanzania na kuwa na rasilimali nyingi hapa nchini hasa kwa upande wa wanyamapori. Moja kati ya sababu zinazo ifanya Tanzania kuwa ya kipekee hususani kwenye suala la uwepo wa jamii nyingi za wanyamapori ni mazingira rafiki kwa wanyamapori lakini pia mipango mikakati ya usimamizi na ulinzi wa rasilimali hii.

Katika makala ya leo nimepanga kukujuza mambo machache na yenye kuvutia kuhusu mnyama jamii ya swala ambae mnyama huyu anapatikana nchi 2 tu duniani kote na katika nchi hizo mbili ni baadhi maeneo matatu tu ambayo mnyama huyu anapatikana. Tanzania ni moja kati ya nchi hizo mbili zinazo jivunia uwepo wa swala huyo.

Mnyama huyo jamii ya swala hujulikana kama NUNGA au PAA NUNGA (Aders’ duiker). Jina lake la kisayansi anajulikana kama Cephalophus adersi. Swala huyu hapa nchini anapatikana Zanzibar tu. Japo kuna majina mengi kuhusu mnyama huyu kama Mwalimu, Kungu marara, Harake na Guno (majina matatu ya mwisho ni kwa nchini Kenya), ila jina maarufu hususani kwa hapa nchini Tanzania swala huyu hujulikana kama NUNGA. Hivyo nakusihi kuwa pamoja nami mwanzo mpaka mwisho wa makala hii HASA ENEO LA UHIFADHI kwani utajifunza mambo mengi sana kuhusu mnyama huyu.

UTANGULIZI

Katika mfululizo wa makala hapo nyuma nilikuwa nikigusia kundi la wanyama jamii ya swala kwa kiasi kikubwa sana na niwazi wengi wetu tulijifunza mambo mengi kuhusu kundi hili la wanyama jamii ya swala. Kundi hili la wanyama jamii ya swala lina aina nyingi sana za wanyama kama nilivo kwisha kuelezea hapo mwanzo na watu wengi huwachanganya wanyama hawa kutokana na kufanana.  Lakini pia wapo baadhi ya watu ambao walikuwa wanajua mnyama swala ni mmoja tu, kumbe swala ni neon lililo beba wanyama aina aina nyingi sana.

Mnyama nunga pia ni miongoni mwa wanyama katika kundi la wanyama jamii ya swala ambae kwa haraka haraka kwa watu ambao sio wataalamu wa wanyamapori wanaweza kumchanganya nmnyama huyu na digi digi kwani wanafanana sana na utofautii sana zaidi upo kwenye ukubwa wa miili yao. Kwa wataalamu wa wanyamapori basi ni rahisi sana kuweza kuwatofautisha nunga na digi digi kwani wana utofauti mkubwa sana. Nunga ni miongoni kati ya swala wazuri na wenye kuvutia sana katika kundi la wanyama jamii ya swala. Katika swala watatu wazuri basi huwezi kumuacha nunga.

Hivyo kupitia makala yetu ya leo basi utaweza kujifunza mambo mengi sana kuhusu mnyama huyu na namna ya kuweza kumtofautisha na wanyama wengine jamii ya swala. Kwani nimepanga kumuelezea kwa kina hasa kutokana na hali ya uwepo wa mnyama huyu hapa nchini lakini pia changamotyo zinazo wakumba swala hawa na kuwa hatari kutoweka.

Picha ya Nunga kwa hisani ya https://www.wildplanettrust.org.uk/research-projects/aders-duiker/

SIFA NA TABIA ZA NUNGA

Miili yao imezungukwa na manyoa malaini sana mfano wa Hariri huku ngozi yao ikiwa nyembamba na laini sana.

Sehemu ya mbele usoni wana manyoa mengi yenye rangi ya wekundu inayo ng’aa.

Sehemu ya juu mkiani, kwenye sehemu ya juu miguu ya nyuma na mgongoni wana rangi ya kahawia ambayo inataka kuelekea kwenye wekundu huku kadri unavoelekea maeneo ya shingoni wana rangi ya kijivu.

Sehemu ya chini tumboni wana rangi nyeupe inayong’aa na mstari ambao unaunganisha rangi nyeupe na nyekundu mpaka sehemu ya paja na nyuma. Mstari huu ni alama ya kipekee inayo patikana kwa nunga hawa tu na si jamii nyingine.

Wana miguu yenye rangi ya wekundu ambayo karibu na kwato rangi hubadilika na kuwa nyeusi. Miguu yao ina alama ya vidoti vyeupe hasa miguu ya mbele.

Wana kishungi chenye rangi ya wekundu sehemu ya kichwa. Wote madume na majike wana pembe ndogo zenye urefu wa sentimita 3-6 na masikio yenye urefu wa sentimita 7-8.3.

Sehemu ya pua na mdomo vimechongoka huku ncha ya pua ikiwa ni bapa. Sehemu ya shingoni pia wana alama ya manyoa ambayo yametengenezeka mfano wa duara.

Nunga ni miongoni mwa wanyama jamii ya swala wenye aibu sana na wana uwezo mkubwa sana wa kusikia na kujificha hasa wanapohisi kuna kitu tofauti kwenye mazingira yao.

Wana uwezo wa kuona vizuri zaidi majira ya asubuhi na mchana hivyo shughuli za utafutaji wa chakula hufanyika mara nyingi mchana mpaka majira ya jioni jua linapo karibia kuzama.

Nunga ni wanyama wanaoishi kwa kujitenga yaani kila mmoja huishi pekeyake japo kuna wakati unaweza kuwakuta kwenye kundi ambapo wanakuwa wawili au watatu.

KIMO, UREFU NA UZITO

Kimo=Nunga mkubwa huwa na kimo cha kati ya sentimita 30-40.

Urefu= Kuanzia kichwani mpaka mkiani huwa na urefu wa sentimita 80-84.

Uzito= Uzito hutofautiana kutokana na mazingira au maeneo. Mfano kwa nunga wanaopatikana mashariki mwa Zanzibar huwa na uzito wa wastani wa kilogramu 12 na kwa wale wapatikanao maeneo ya kusini huwa na wastani wa uzito wa kilogramu 7.5. Japo tafiti zinaonesha uzito wa wanyama hawa ni kati ya kilogramu 7-12.

MAENEO WAPATIKANAYO NUNGA

Kama nilivyo dokeza hapo juu kuwa nunga wanapatikana bara la Afrika tu na katika bara zima la Afrika wanapatikana nchi mbili tu ambazo ni Tanzania na Kenya. Nchini Kenya wanyama hawa wanapatikana maeneo mawili tu ambayo ni Boni-Dodori na Arabuko-Sukoke huku hapa nchini Tanzania wanapatika Zanzibar tu tena katika kisiwa cha Unguja.

Nadhani unaweza ukaona ni kwa jinsi gani tunatakiwa kuwalinda wanyama hawa kwa hali na mali kwani idadi ya wanyama hawa ilipungua kwa kiasi kikubwa sana hali ambayo ilipelekea wamewekwa kwenye wanyama walio hatarini kutoweka nchini Tanzania. Kuhusu suala hili tutalichambua zaidi kwenye kipengele cha uhifadhi.

MAZINGIRA

Nunga wanapendelea maeneo yenye miti mingi na misitu ambapo mazingira haya yanawapo uwezo wa kujificha lakini pia makazi salama kwao. Japo wanapendelea maeneo yenye miti ila kwa maeneo yenye miti mirefu sana huwezi kuwaona kwani mazingira kama haya sio rafiki sana kwa wanyama hawa.

Wanapendelea pia mazingira ya misitu ya pwani ambayo inapaka na bahari lakini pia mazingira yenye matumbawe.

CHAKULA

Chakula kikubwa cha wanyama hawa ni mauwa, majani na matunda ambapo hutegemea sana chakula kinacho dondoka toka kwenye matawi ya miti. Wkati mwingine wanyama hawa hupendelea sana kuishi maeneo ambayo kuna idadi kubwa ya makundi ya nyani kwani hunufaika sana na chakula hasa kwa majani na matunda ambayo huangushwa na nyani. Lakini pia hula hata majani ambayo yanakuwa toka aridhini pamoja na baadhi ya matunda mengine.

Wanapendelea sana kula majira ya asubuhi na jioni na mara nyingi mchana pumzika na kucheuwa ili kutafuna majani upya. Japo kuna wakati huonekana pia wakitafuta chakula majira ya mchana.

Nunga ni wanyama wenye uwezo wa kuishi muda mrefu sana bila kunywa maji. Hii ni kwasababu chakula wanacho kula wanyama hawa kina kiwango kikubwa sana cha maji na hivyo kusababisha waweze kukaa muda mrefu bila uhitaji wa maji ya kunywa.

Picha ya Nunga akiwa katika makazi yake ya asili.

KUZALIANA

Taarifa kuhusu kuzaliana kwa wanyama hawa ni chache sana hivyo kuna umuhimu mkubwa sana wa kufanya utafiti kwa wanyama hawa hasa uzalianaji wao.

Japo baadhi ya tafiti chache zinaonesha wanyama hawa mara nyingi hubeba mimba kuanzia kipindi cha mwezi wa 6-11 na mara nyingi huzaa motto mmoja tu.

Kwa mamlaka husika na mamlaka nyingine za uhifadhi nadhani hii ni fursa kubwa sana kufanya utafiti ili kujifunza namna wanyama hawa wanavyo zaliana na malezi hali kadhalika umri wa watoto kuzaliwa mpaka kufikia hatua ya kuzaa.

UHIFADHI

Moja kati ya maeneo ambayo ndugu msomaji wa makala hii napenda usome tena kwa utulivu ni hii sehemu ya uhifadhi kwani imebeba funzo na ujumbe mkubwa sana kuhusu mnyama nunga.

Kutokana na tafiti na uchapishaji unaofanywa na shirika la umoja wa mataifa linalo shughulika na uhifadhi wa maumbile asili duniani (International Union for Conservation of Nature-IUCN), Tanzania tuna wanyama aina mbili ambao wapo katika hali ya hatari zaidi kutoweka hapa nchini. Wanyama hawa ni Faru na Nunga.

Utafiti ulio fanyika Zanzibar mwaka 1999 ulibaini kuwa idadi ya nangu ilikuwa ni 600±45 (hii ikiwa inamaanisha wanyama hawa wapo 600 kwa kutoa au kuongeza 45). Mnamo mwaka 1985 tafiti zinaonesha wanyama hawa walikuwa 5000 na zaidi, tafiti za mwaka 1996 zilionyesha kupungua kwa idadi ya wanyama hawa visiwani humo na kufikia 2000. Hali ya hatari zaidi ni utafiti wa mwaka 1999 ambo ndo ulionesha kupungua kwa kiasi kikubwa cha wanyama hawa na kufikia 600±45.

Hii nisawa na kusema ndani ya miaka 17 wanyama hawa wamepungua kwa asilimia 87.7%, hii ni hali ya hatari sana tena sana na ndiyo sababu iliyo pelekea IUCN kuwaweka wanyama hawa katika kundi la wanyama waliyopo katika hatari zaidi ya kutoweka hapa nchini. Hali hii imepelekea baadhi ya nunga kuchukuliwa na kuhifadhiwa katika maeneo binafsi ya uhifadhi kama visiwa vya Chumbe na Mnemba na wengine kupelekwa katika hifadhi ya Zanzibar visiwani Unguja. Mpango huu unaonekana kuleta faida kwani idadi ya nunga inaonekana kuongezeka japo bado sio kwa kiwango cha kuridhisha ili kuweza kuwatoa kwenye kundi la wanyama waliyo hatarini kutoweka hapa nchini.

Moja kati ya taarifa ya kushtusha ni ile ya IUCN iliyoonesha endapo hali ingeendelea kama hapo mwanzo basi mpaka kufikia 2018 basi wanyama hawa wangekuwa wamesha toweka hapa nchini Tanzania kutokana na idadi kupungua kwa kiasi kukibwa ndani ya muda mfupi. Utafiiti wa mwisho kufanyika kuhusu wanyama hawa huko Zanzibar ulikuwa mwaka 1999. Hivyo mpaka sasa hakuna data kamili juu ya idadi ya wanyama hawa na kupelekea umuhimu mkubwa sana wa kufanya utafiti ili kubaini idadi yao.

Upungufu wa wanyama hawa unatokana na sababu kuu mbili ambazo tutaziona kwenye kipengele kinacho fuata. Jmbo kubwa la kujiuliza ni kuhusu idadi ya wanyama hawa kwasasa kwani tumeona ni miaka takribani 24 sasa tangu utafiti ufanyike kwa mara ya mwisho.

SABABU ZINAZO PELEKEA KUPUNGUA KWA NUNGA

Kama nilivyo dokeza hapo juu kuna changamoto kuu mbili ambazo zinapelekea wanyama hawa kupungua kwa kasi kubwa sana katika mazingira yao asilia, sababu hizo ni Ujangili na Uharibifu wa mazingira.

Ujangili na uvunaji ulio pitiliza; wanyma hawa wamekuwa wakiwindwa kwa kasi kubwa sana na majangili. Hii inatokana na uwepo wa biashara haramu ya nyama ya wanyamapori katika maeneo mbali mbali hapa nchini. Moja kati ya changamoto kubwa sana ni namna ya kutokomeza ujangili kwani tafiti kama zilivyoonesha idadi ya wanyama hawa ilipungua kwa zaidi ya 87% ndani ya miaka 17 tu. Baadhi ya watu ambao hawana uchungu na rasilimali za taifa wamekuwa wakijinufaisha wao bila kujali maslahi ya wengine. Baadhi ya tafiti pia zinaonesha wanyama hawa wamekuwa wakiwindwa kutokana na shughuli za kitamaduni hali ambayo ilipekea uvunaji nuliyo kithiri kwani ni wazi kabisa inaonekana usimamizi wa uvunaji wa wanyama hawa haukuwa wenye kufuatiliwa kwa kina zaidi.

Uharibifu wa mazingira; maeneo ya matumbawe ambayo nunga wanapendelea yanatengeneza ikolojia tata yenye thamani kubwa sana ya bioanuai kwa mimea na wanyama kwa ujumla. Hivyo uharibifu wa mazingira wa maeneo ya ikolojia ya misitu iliyo baki inaonekana kuwa ni changamoto kubwa sana kwa wanyama hawa. Kutokana na mahitaji ya jamii kama kuni, jamii nyingi zinazoishi maeneo ya pembezoni mwa misitu ya pwani zimekuwa zikikata miti kwa kasi kubwa sana na kusababisha uharibifu wa mazingira hali ambayo imepelekea nunga wengi kuyakimbia maeneo yao kwa kukosa makazi na wengine hata kushindwa kuishi kutokana na kuhangaika kutafuta makazi mapya.

Kilimo cha kuhama, ufyekaji na uchomaji moto inaonekana ndio njia kuu ya ulimaji kwa upande wa Zanzibar. Hii imepelekea kupungua kwa maeneo ya misitu lakini pia kupungua kwa ubora wa misitu. Kupungua kwa maeneo ya misitu na ubora wake kumesababisha upungufu mkubwa sana wa chakula kwa nunga pamoja na makazi kwa wanyama hawa na kupelekea nunga kufa na wengine kulazimika kuhama maeneo hayo. Kwa jicho la juu juu huwezi ukaona athari hii lakini tafiti zinaonesha wazi kabisa kuwa moja kati ya changamoto kubwa inayo pelekea kupungua kwa kasi kubwa kwa nunga ni uharibifu wa mazingira ukilinganisha na ujangili.

Changamoto nyingine inayo wakumba nunga ni uwepo wa idadi kubwa ya mbwa wasiofugwa katika maeneo wapatikanayo nunga. Mbwa hawa wanaonekana kuwala wanyama hawa kwa kiasi kikubwa sana hali ambayo inapelekea kupungua kwa nunga katika maeneo yao asilia. Ongezeko la mbwa kila siku ni tishio kubwa sana sio tu kwa nunga bali hata kwa wanyama wengine wapatikanao kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori kwani mbwa hawa hawana ulinzi na hivyo kuzurura pia kusababisha uharibifu mkubwa sana wa maliasili zetu.

NINI KIFANYIKE ILI KUEPUKANA NA CHANGAMOTO HIZI NA KURUDISHA IDADI YA NUNGA INAYO RIDHISHA HAPA NCHINI

Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar haina budi kuongeza nguvu kwa kusaidiana na mamlaka mbali mbali za uhifadhi kama TANAPA na TAWA kwa kujifunza mbinu mbali mbali za kupambana na ujangili pia kuongeza doria katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori ambayo nunga wanapatikana ili kutokomeza wimbi la ujangili. Kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza kasi ya uwindaji wa wanyama hawa na kurudisha idadi yao katika hali inayo ridhisha. Njia kubwa zaidi ya kupunguza ujangili ni kuongeza idadi ya askari wa doria lakini pia kuhakikisha askari wanao ajiriwa katioka maeneo hayo wanakuwa na elimu ya uhifadhi ili kuleta chachu ya utendaji kazi wao.

Kutoa elimu ya uhifadhi kwa vijiji na jamii zinazoishi maeno yanayo pakana na misitu ya pwani. Elimu ya uhifadhi ni muhimu sana kwa jamii hizo kwani itasaidia jamii kutambua thamani ya uwepo wa wanyama hao. Lakini pia serikali hainabudu kuwaeleza wanajamii au jamii hizo juu ya uelekeo au hali halisi ya nunga kwasasa kutokana na tafiti zilizofanywa. Endapo jamii itafahamu hali halisi ya wanyama hawa basi watu watakuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi lakini pia watasaidia kuwafichua majangili na watu wote wenye malengo mabaya na maliasili zetu.

Kupambana na tatizo la uharibifu wa mazingira na uchomaji moto wa misitu unaoendelea kutokana na shughuli za kibinaadamu. Mamlaka husika kwa kusaidiana na serikali lazima ziwe na mipango mikakati ya kuhakikisha tatizo la uharibifu wa mazingira linakwisha kabisa kwani linaonekana ndio sababu kubwa sana iliyo pelekea nunga kupungua kwa kasi sana. Lakini suala la uchomaji moto wa misitu hasa kipindi cha maandalizi ya mashamba nalo lazima liangaliwe kwa umakini zaidi kwani limesababisha nunga wengi kuyahama makazi yao na wengine kuishia kufa kutokana na kukosa maeneo ya kuishi.

Usimamizi wa utekelezaji wa sharia kwa wale wote ambao wanakiuka sharia za uhifadhi wa wanyamapori lakini pia wale wanao kiuka sharia za utunzaji wa mazingira. Kwa kufanya hivyo itasaidia watu kuwa makini na kupunguza uharibifu wa mazingira. Moja kati ya adhabu kubwa ambazo zinatakiwa kutolewa ni ulipaji wa fidia ambao kiwango chake kitakuwa tishio kwa watu, kama ilivyo kwenye majiji sharia ya usafi na inaonekana kufanya kazi vizuri basi hata kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori inawezekana.

Uanzishwaji wa mitaala ya elimu ya uhifadhi kuanzia ngazi ya elimu ya msingi mpaka sekondari pia ni moja kati ya njia nzuri ya kupunguza ujangili lakini pia kukuza chachu ya uhifadhi. Endapo mwanafunzi atakuwa amesoma elimu ya uhifadhi kuanzia shule ya msingi basi ni wazi kwamba atakuwa na uchungu lakini pia hamasa ya uhifadhi wa wanyamapori. Baadae atakuja kuwa balozi mzuri na kuhamasisha wengine kuhusu umuhimu wa uwepo wa wanyamapori hapa nchini na faida zao hasa kwenye pato la taifa kupitia shughuli za kitalii.

Kuwauwa mbwa wote ambao hawana wamiliki mambao wamekuwa wakizurura hovyo misituni na kusababisha hasara kwa kuwala nunga. Mbwa ni wanyama ambao wanazaliana kwa kasi kubwa na kusababisha idadi yao kuongezeka kwa kasi sana. Endapo hawata shughulikiwa mapema basi kadiri idadi yao inavyoongezeka ndivyo tishio la kupungua kwa idadi ya nunga litakuwa linazidi kwa kiasi kikubwa sana.

Ufugaji wa wanyama hawa kwenye maeneo binafsi au maeneo ya serikali kama inavo fanyika huko Zanzibar pia ni njia mojawapo nzuri ya kuhakikisha tunaendelea kuwa na wayama hawa hapa nchini. Serikali ijitahidi kuwashirikisha wadau mbali mbali wa uhifadhi ili waweze kuiwekeza zaidi katikakuwafuga wanyama hawa lakini pia pale idadi inapooongezeka basi wawe wanawaachia katika hifadhi za wanyamapori. Kwa kufanya hivyo itasaidia kurudisha idadi ya wanyama hawa kama hapo zamani tena kwa muda mfupi.

HITIMISHO

Uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori ni jukumu la kila mmoja na sio la serikali pekee. Hali halisi ya uwepo wa nunga hapa nchini niwazi kwamba hairidhishi kabisa na serikali isipo simama kidete basi wanyama hawa watatoweka kabisa hapa nchini. Itashangaza sana kumpoteza mnyama mzuri kiasi hiki ambae hata watafiti wamwamua kumuweka miongoni mwa swala wazuri katika kundi kubwa la wanyama jamii ya swala lenye jamii 15 na zaidi za swala.

Wanyama hawa wanapatikana nchi mbili tu duniani kote ambazo ni Tanzania na Kenya. Hivyo ni moja kati ya sifa kubwa sana kama taifa kuwa na wanyama hawa na kama watatumika vizuri basi wanaweza kuwa ni chanzo cha mapato kwa taifa kwani watu wengi wanaweza kuhamasika katika kuwafahamu wanyama hawa. Lakini pia tumeona hapo juu kuwa taarifa nyingi kuhusu wanyama hawa hazijulikani hivyo hii inatoa fursa kwa serikali kukaribisha wadau wa utafiti ili kuwekeza katika tafiti zitakazo gusa moja kwa moja uelekeo wa nunga hapa nchini.

Kuna tafiti moja nilisoma siku chache hapo nyuma kuhusu chui wa Zanzibar. Lakini inasadikika mpaka sasa chui hao wamesha toweka na hawapo tena na mara ya mwisho inaonekana kuna chui mmoja tu alinaswa na kamera mwanzoni mwa miaka ya 80 na hivyo mpaka sasa hakuna chui aliye salia. Sidhani kama kuna aliye tayari kuona na nunga wanabaki tu kwenye historia kwamba walikuwepo hapa nchini. Itakuwa ni dhambi kubwa sana kwa kizazi chetu kwani tutakuwa tumewanyima wajukuu wetu haki ya kufurahia uwepo wa wanyama hawa ambao hata sisi tumewakuta na tuna kila sababu ya kuhakikisha wanaendelea kuwepo hapa nchini na waje kushuhuduwa vizazi na vizazi.

MWISHO

Asante msomaji wetu kwa kusoma makala hii nzuri iliyosheheni mambo mengi kuhusu sifa na uhifadhi wa swala NUNGA. Usiache kuwashirikisha wengine makala hii nao wajifunze ili elimu na maarifa haya yawafikie wengi. Ili kupata mengi zaidi kuhusu wanyamapori wasiliana nami kupitia

Sadick Omary Hamisi,

Simu=0714116963/0765057969

Email=swideeq.so@gmail.com

Instagram=wildlife_articles_tanzania

Facebook= Envirocare and wildlife conservation au Sadicq Omary Kashushu

Au tembelea tovuti yetu= www.wildlifetanzania.home.blog

”I’M THE METALLIC LEGEND