Mnyamapori aina ya tembo ameonekana kuwa na ukaribu sana na mazingira yenye uoto wa asili wenye miti aina ya mibuyu. Hii ni miongoni mwa sababu zinazofanya baadhi ya hifadhi zenye uoto huo kama Ruaha na Tarangire kuwa na makundi makubwa ya tembo.
Uhusiano wa tembo na miti aina ya mibuyu umepelekea kuwapo na uvamizi wa tembo katika mashamba ya wanakijiji wanaoishi karibu na hifadhi zenye tembo. Uvamizi huu hutokea hasa kipindi cha ukame ambapo tembo huingia mashambani wakitafuta miti hiyo aina ya mibuyu. Hivyo mashamba ambayo yana miti aina ya mibuyu imekuwa na changamoto kubwa ya kuharibiwa na wanyama hawa.
Kwa asilimia kubwa imesadikika kuwa ushirikiano kati ya mibuyu na tembo imekuwa miongoni mwa vichochezi vya ongezeko kubwa la tembo kutokana na faida wanazozipata tembo kutoka kwenye miti aina ya mibuyu .Faida hizi zimepelekea kuongezeka kwa mazalia ya tembo bila kujali msimu wa kiangazi na masika.
Mmbuyu ni mti gani?
Mbuyu ni mti wakitropiki, mkubwa na wenye matawi mengi mapana na magome yenye nyuzinyuzi nyingi. Mbuyu unasifa ya kufyonza na kuhifadhi maji wakati wa mvua hupelekea mti huu kuwa na upaa mkubwa na maji mengi. Katika msimu wa ukame, mti wa mbuyu hupoteza maji yake na kupelekea upana wa mti huu kupungua sambamba na kutoa matunda yake ambayo hukomaa wakati wa kiangazi. Baadhi ya sifa za mti wa mbuyu ni Pamoja na;
Mbuyu ni miongoni mwa miti mikubwa duniani kutokana nakuwa na upana mkubwa.
Asili yake ni Africa na hupatikana kwa wingi katika visiwa vya madagascar na kwa uchache katika nchi zaTanzania, Kenya n.k.
Mti huu una matunda yanayoliwa na wanyamapori mbalimbali pamoja na binadamu.bMatunda ya mbuyu huifadhiwa ndani ya kokwa au ganda gumu.
Maua ya mti wa mbuyu huwa na rangi nyeupe na huchipukia kutoka kwenye matawi na kuning’inia kuelekea chini
-Mbuyu unasifa ya kuishi miaka mingi mfano Katika hifadhi ya taifa ya Mikumi, kuna mti wa mbuyu ambao umekadiriwa kuishi zaidi ya miaka mia tatu iliyopita.
Tembo ni mnyama wa aina gani??
Tembo ni miongoni mwa mnyamapori mkubwa anaepatikana katika jamii ya mamalia(wanyama wanaozaa nakunyonyesha).
-Tembo anamwili mkubwa, mkonge mrefu unaofanya kazi vyema pamoja na masikio makubwa.
-Tembo wanarangi ya kijivu, vinyweleo vichache katika miili yao na mkia mrefu wenye rangi nyeusi mwishoni.
_Tembo wa jinsia zote mbili wana ndovu, ila kwa jinsia ya kiume ndovu huonekana kuwa kubwa zaidi.
-Tembo ni miongoni mwa wanyama wanaoishi mazingira tofauti tofauti, kama savana, maeneo ya kitropiki n.k.Na mtawanyiko wao husababishwa zaidi na kiwango cha maji kilichopo.
-Tembo wanakula aina nyingi za majani.
-Mara nyingi huonekana wakiishi katika makundi ya 2 hadi 50 , haswa katika kipindi cha mvua na hugawanyika kipindi cha kiangazi.
Sababu za tembo kupenda miti aina ya mibuyu.
1-Kupata maji wakati wa ukame.
Miti aina ya mibuyu inasifa ya kuhifadhi maji mengi hivyo kipindi cha ukame tembo wengi hupenda kufyonza maji kutoka kwenye miti hiyo baada ya kubandua na kuharibu magome ya miti hiyo.
Uwepo wa virutubisho vingi pamoja na vitamini(vitamini C) ambavyo vina umuhimu katika ukuaji wa mnyama tembo. Virutubisho hivi hupatikana wakati wa ukame. Kipindi cha kiangazi sio rahisi sana kupatikana katika vyakula vingine ambavyo tembo anakula. Na hivyo ubuyuhuitwa kama chakula chenye nguvu.
3- unga uliopo ndani ya tunda la mbuyu una virutubisho vingi. Hivyo, kipindi cha ukame matunda ya mbuyu hudondoka na tembo hukanyaga na kuvunja matunda hayo ili kupata vilivyomo ndani ya tunda hilo.
4-Mbuyu una majani na matunda laini msimu wa mvua yanayofaa kuliwa na wanyama hasa tembo. Ulaini wa majani ya mbuyu hupunguza nguvu yakumeng’enya na kupata virutubisho .
5-Magome ya mti wa mbuyu yana ladha inayofanana na tikiti maji hivyo tembo hupendelea kula kama chakula wakati wa ukame. Pia mbegu za mbuyu zina mafuta na carbohydrate (wanga), ambavyo ni muhimu kwa afya ya tembo.
7-Husaidia kivuli kwa tembo hasa wakati wa kiangazi.
8 nyuzinyuzi zinazopatikana katika mbuyu husaidia katika mmeng’enyo na uboreshaji wa mfumo wa chakula kwa mnyama tembo.
Jinsi mbuyu unavyonufaika na Tembo
Tembo husaidia usambaaji wa mbegu za mbuyu kwa haraka na kupelekea miti hii kuota na kusambaa katika maeneo tofauti tofauti na kupunguza athari za kupotea kwa uoto huu. Ndio sababu maeneo yenye tembo wengi huwa uoto wa mibuyu ni wa kiwango cha juu.
_Kutokana na ugumu wa mbegu za mbuyu tembo husaidia kulainisha mbegu hizo wakati wa umeng’enyaji wa chakula hivyo hupelekea mbegu kuota kwa haraka wakati wa masika.
-Tembo huwa na kinyesi chenye majani na baadhi ya vyakula ambavyo havijameng’enywa vizuri. Hivi husaidia katika upatikanaji wa mbolea inayosaidia na kuharakisha ukuaji wa mimea kama mibuyu.
Madhara ya uhusiano wa tembo na miti aina ya mibuyu.
-Tembo wakati wa kiangazi huwa wanapata maji kwa kufyonza maji katika mibuyu na kutokana na ukubwa wa mnyama tembo huhitaji pia maji yakutosha. Hii hupelekea mti kuishiwa maji, kukauka na kuanguka.
-Mbali na hili, mti wa mbuyu kutokana na uzito wake, wakati mwingine huweza kumwangukia tembo na kumjeruhi maeneo ya kichwani na sehemu nyingine za mwili na kupelekea vifo vya tembo.
Wito wangu kwa serikali na wadau wa mazingira.
-Kuhimiza na kufuatilia uhifadhi na utunzaji wa miti aina ya mibuyu kwani ni ya muhimu kwa maisha ya tembo pamoja na ikolojia kwa ujumla.
-Kuundwa sheria na kanuni za usimamizi na ufuatiliaji wa uoto wa mibuyu katika hifadhi zetu na kuweka mikakati ya kuongezeka kwa miti aina ya mibuyu.
-Kuhimiza utunzaji na ulinzi wa tembo pamoja na kukomesha ujangili , kwani tembo na mbuyu kwa pamoja ni fahari na huiwakilisha Afrika.
Makala hii imeandikwa na Shoo Marylove Gasper wa Chuo Kikuu cha Sokoine Morogoro na kuhaririwa na Alphonce Msigwa, Mwikolojia wa Hifadhi za Taifa Tanzania
Ahsante sana kwa kusoma makala hii, kwa maswali maoni ushauri na mapendekezo kuhusu makala hii usisite kuwasiliana na mwandishi kwa mawasiliano hapo chini.
Simu:255(0) 783 682 765
email: marylovegasper478@gmail.com