Ndege ni moja wa viumbe hai ambao hutofautiana na  wanyama wengine kwa sifa zifuatazo; umiliki ama uwepo wa  mabawa yanayomwezesha kuruka angani vile vile kuwa na sifa ya hutaga mayai. Viumbe hawa wako wa aina nyingi, wakubwa na wadogo, kama vile Tai, Mbuni, Korongo domokijiko, Bundi, Mwewe na wengine wengi. Mbayuwayu, kiwizi shingo nyeusi, sholwe, Chiriku, Kwelea kwelea hii ni mifano michachae ya ndege wadogo. Kuna wanaokula nyama,wanao kula wadudu wa aina tofauti, wanaokula mbegu, nyasi na matunda mbalimbali. Wapo wenye rangi mbalimbali na zenye mvuto katika macho ya binadamu. Kama walivyo wanyama wengine ndege wengine hupendelea kufanya shughuli zao usiku na wengine mchana, hata wengine alfajiri.

Ni vizuri tukafahamu kuwa tunaposema Wanyama wa porini ama wanyamapori tunamaanisha kwamba wanyama wote ambao hawapo chini ya uangalizi wa binadamu. Yaani kwa muda wote wa maisha yao huishi msituni au katika maeneo yaliotengwa kisheria kwa ajili ya kuhifadhi wanyamapori.

Mamalia ni kundi mojawapo la wanyama wa porini hawafugwi na ambao wanaishi katika maeneo maalumu yaliyotengwa kama hifadhi za taifa nakadhalika. Mammalian na Reptilia ni baadhi ya makundi ya wanyama wanaoishi porini. Mamalia wana sifa zifuatazo ambazo hutofautisha kundi hili na makundi mengine sifa hizo ni kama zifuatazo;-sifa yao kubwa ni kwamba wanazaa, pia wana sifa yakunyonyesha, kuwatunza watoto wao.

Wanyama hawa wamegawanyika katika makundi mbalimbali, kutokana na maumbile yao ambayo husababisha kuibuka kwa tabia mbalimbali.Kuna wanyama wanaokula nyasi kama vile mbogo, pundamilia, twiga, kifaru, tembo  na wengine wengi.Simba, duma, chui, na fisi ni mifano ya wanyama walao nyama. Mbali na hao lakini wanyama kama nyani wao hula karibu vyakula vya aina zote.

Mamba na nyoka ni mfano wa reptilia.Wengi wao hutaga mayai vile vile kuna wanaoishi nchi kavu na majini. Kama ilivyo kwa ndege pia mamalia na reptilia hawa kuna wenye maumbile madogo na wenye maumbile makubwa,Pia kuna wanyama ambao wanapendelea kufanya shughuli zao wakati wa usiku na wengine mchana.

Maisha ya wanyama wa porini jamii hii ya mamalia na reptilia hutegemea sana mazingira asilia.  Ambayo huwafanya kuishi kwa amani, furaha na raha mustarehe. Mazingira yakiharibiwa husababisha kuhamia mahali pengine au kutokomea na hata kupotea  kabisa kwa viumbe hawa. Hupendelea kuishi mahali penye utulivu na panapovutia kufanya shughuli zao za kila siku.

Uwepo wa idadi kubwa na aina toafauti za wanyama wa porini ni moja ya ishara zinazoonyesha kuwepo kwa mazingira bora na yenye tija kwao hivyo huwafanya waweze kufurahia uwepo wao hapa duniani. Wanyama hawa hupendelea zaidi kukaa katika mazingira ambayo yanawasaidia kupata chakula kiurahisi, kuweza kujilinda dhidi ya maadui wao.

Mbali na mamalia pamoja na reptilia, ndege nao huishi kwenye mazingira tofauti kulingana na aina au jamii husika. Lakini wengi huishi katika misitu iliyofunga na wenginge kwenye maeneo ya wazi. Wengine hujenga viota  misimu ya kuzaliana na wengine vya mda mrefu. Viota hivi hujengwa kwa kutumia majani,Udongo na vijiti.

Vilevile wapo ndege waishio mapangoni. Viota vya ndege hujengwa kwa ustadi mkubwa ili kuwakinga na baradi, mvua, maadui na upepo mkali wakati wa kuzaliana. Ndege wengi hutumia viota kwa kuzaliana  na sio kuishi. Ndege hupendelea kujenga viota  vyao juu ya miti, ndani ya mapango, kwenye paa au kona za nyumba ili mradi tu sehemu hizo ziwe za usalama. Aidha mahali hapo ni lazima pawe pana maji, chakula, upepo, na pia mandhari mazuri. Ndege wengine hupendelea kuishi majini, kwa mfano batamaji. Wengine hupenda kuishi kwenye ardhiowevu.

Mahusiano kama yalivyo na umuhimu kwa binadamu, vile vile hata kwa wanyama wa porini yana umuhimu sana. Kuna aina nyingi za uhusiano, ambayo mengine husababisha kumuumiza kiumbe mwingine na mengine viumbe wote hupata faida yaani wahusika wote wawili hufaidika.  Kiumbe mmoja kumtumia kiumbe mwingine kwa ajili ya kupata chakula na kumsababishia madhara kiumbe mwingine kama vile kupe kutegemea miili ya wanyama, hapa kiumbe mmoja anapata faida na mwingine hasara. Hvyo uhusiano huu sio mzuri.

Vile vile kuna uhusiano ambao hushirikisha viumbe wawili kati ya hao kiumbe mmoja hupata faida kwa kutumia rasilimali za  kiumbe mwingine bila kusababisha madhara. Nao uhusiano huu ni mzuri kiasi.

Katika hii mada tunazungumzia Muingiliano ama uhusiano chanya, kwa lugha ya kiikolojia unaojulikana kama “symbiotic mutualism relationship” ina maana kwamba viumbe wawili wa aina tofauti wanaweza kuishi sehemu moja na kutegemeana bila kusababisha madhara kwa kila mmoja yaani kila mmoja kufaidika na  uwepo wa kiumbe kingine.

Hapa tunazungumzia muingiliano huu chanya kati ya viumbe wawili yaani ndege na wanyama wengine wa porini hasa mamalia na reptilia, ni uhusiano wenye tija na kufanya kila mmoja katika sehemu hiyo kufaidika kutokana na uwepo wa kiumbe kingine  hivyo kuwafanya kuishi kwa raha mustarehe.

Viumbe hawa wawili mara nyingi utawakuta wamekaa pamoja,wakifurahia shughuli zao za kila siku hasa za kujitafutia chakula na kuhakikisha ulinzi kwa maadui zao. Mfano mzuri ni pale unapomuona ndege Shashi na wanyama wengine wakubwa wanao kula majani. Unapoona ndege yupo juu ya mgongo wa mnyama sio tu anapata lifti yani usafiri kama watu wengi wanavyofikiri lakini ndege hawa wamsaada sana.

Ndege Shashi wakiwa juu ya mgongo wa Nyati

Shashi hupendelea sana kukaa  na wanyama wanaokula nyasi wakiwasaidia kutoa kupe na wadudu wengine kwa maana hiyo wao hupata chakula na hao wanyama wengine  kuweza kupunguza wadudu  wanaonyonya damu katika miili yao hivyo huepushwa na magonjwa mbalimbali.

Pia ndege hawa kwa kua wanakaa juu ya migongo ya wanyama hawa huwa rahisi kuwaona maadui na hivyo hupiga kelele mfano ndege wengine hutoa sauti yenye kumaanisha ondoka ambayo huwafanya hawa Wanyama wa porini waweze kuondoka eneo hilo hatarishi kwa haraka. Muda mwingine kitendo cha ndege aliyekuwa mgongoni mwa mmnyama kuondoka haraka ni ishara tosha kuwa eneo limeingiliwa na adui na ndio maana huweza ona mnyama husitisha kula chakula. Huu ni uhusiano mzuri wenye tija kwa pande zote mbili.

Ndege mwingine anajulikana kama  Ndoero na mamba;- ni kitu cha kushangaza na kustaajabisha unapoona mdomo wa mamba upo wazi na ukaona ndege hawa wakiwa ndani ya mdomo wa huyu mnyama mkali lakini ndio uhusiano chanya wenyewe kati ya hawa ndege na mamba. Hapa kinachotokea ni kwamba mamba anaacha mdomo wazi na kuruhusu hawa ndege waingie ili kuweza kula mabaki ya chakula kwenye meno ya mamba wakati huo hawa mamba wanakua wamesafishwa midimo yao kwa chakula kipya kwa lugha ya kawaida ninaweza kusema wanakuwa wamepiga mswaki kuondoa uchafu au mabaki ili kuweza kula tena, Mswaki wa mamba ni hawa ndege. Ndege hawa huwa na amani wakiwa katika midomo wazi ya mamba kuliko kiumbe chochote kile.

Ndoero akiwa kwenye mdomo wa mamba

Tunamuona pia ndege huyu anaejulikana kama asali mwongozo na mnyama ajulikanae kama nyegere. Ndege anahitaji kupata asali ndani ya mzinga wa nyuki lakini hawezi kupata kiurahisi moja kwa moja, kutokana na hali hiyo amejifunza kuwaongoza  viumbe vingine  kama nyegere na binadamu kwenda kwenye mzinga wa nyuki ili waweze kuingia na kutoa chakula na yeye kawaida anasubiri mabaki na kuyatumia kama chakula. Hivyo hawa viumbe wawili hufanya kazi kwa ushilikiano ili waweze kupata chakula kirahisi kila mmoja akimtegemea mwenzie. ndivyo huleta mahusiano chanya kati ya viumbe hawa. Sio kitu cha ajabu kwa nyegere kupata mizinga zaidi ya mitatu kwa siku kukiwa na uwepo wa ndege huyu mahiri kwa kujua mizinga ya nyuki ilipo.

Muingiliano mwingine chanya ni kati ya ndege huyu anayejulikana kama kunguru  na  mnyama ambaye ni jamii ya mbwa anayeitwa “wolve”. Hawa  viumbe hushirikiana sana katika shughuli zao  za kila siku za kujitafutia chakula mara nyingi huwa pamoja na kucheza pamoja sababu ambayo kunguru hukaa na mbwa mwitu ni kwamba kunguru ana uwezo wa kutafuta mizoga kwa urahisi na wepesi zaidi kuliko mbwa mwitu lakini hana uwezo wa kuweza kufungua mzoga huo anachofanya huwa anapiga sana kelele, mbwa mwitu baada ya kusikia kelele hizo anaenda katika eneo hilo na kutumia meno yenye ncha kali na taya  lake lenye nguvu kuufungua mzoga huo na kufanya uwe rahisi  kuliwa. Muda mwingine unaweza kuwaona kunguru wanazunguka windo au nyara  na kupiga kelele kuwaita mbwa mwitu waweze kuwaua kirahishi ili aweze jipatia chakula.

Faida ya mahusiano chanya kwa viumbe hawa yanajionyesha dhahiri katika shughuli  wanazo fanya kila  siku faida hizo ni kama zifuatazo;-

  1. Kwanza unawasaidia viumbe hawa kujipatia chakula kiurahisi katika mazingira yao kama inavyojulikana chakula ndio kila kitu katika maisha, chakula kinawapatia nguvu kuweza kufanya shughuli za kila siku kama kuzaliana katika kitendo hicho nguvu inaitajika.  Ukiachilia mbali kitendo cha kuzaliana, watoto wanaozaliwa wanahitaji  mahitaji muhimu  kutoka kwa wazazi kama chakula  na malazi na kuwalinda dhidi ya maadui. Bila  ya mahusiamo chanya upatikanaji wa chakula utakuwa mgumu. Kutokana na uwepo wa mahusiano haya chanya hupelekea watoto wa viumbe hawa kukua wakiwa na afya njema kabisa na idadi yao kuongezeka katika mazingira yao.
  2. Pili mahusiano haya huwasaidia viumbe hawa kuwakimbia maadui zao mfano mzuri ndege anayeitwa shashi yeye huwa anapiga sana kelele mara aonapo adui hivyo humsaidia mnyama kuondoka eneo hilo ambalo linaweza kumsababishia matatizo, kwa lugha rahisi ni kuweza kujihami dhidi ya maadui Pia huweza kuongezea ujasiri katika kufanya shughuli zao kwa sababu wanategemeana sana
  3. Tatu mahusiano haya huwasaidia viumbe hawa kuweza kuepukana na magonjwa yanayo sababishwa na vimelea vinavyoletwa na kupe na wadudu wengine mbali na kusambaza magonjwa kwa wanyama pia kwa jamii ambayo ipo jirani na hawa wanyama pori wanaweza ambukizwa magonjwa. Jambo lingine ni kwanba hawa wadudu kama kupe wananyonya sana damu hivyo kuwasababishia maumivu hawa wanyama hivyo ndege wanasaidia sana kupunguza idadi ya hawa wadudu katika mazingira na kuwafanya wanyama wawe hawapo katika hatari ya kupoteza damu, na maambukizi ya magonjwa kiujumla.
  4. Nne wanyama hawa wanasaidia kuweka usawa wa kimazingira kwa lugha ya kiingereza ni “ecosystem balance” inatokea pale wanapojitafutia chakula hivyo husaidia jamii fulani ya wadudu kupungua na hivyo kupunguza kugombania chakula na hata makazi baina ya hawa wadudu.

Wito kwa watanzania unahitajika katika kutunza mazingira  ya viumbe hawa kwani viumbe hupendelea kukaa katika mazingira  asilia, pia katika utunzaji wa mazingira hufanya mahusiano haya chanya kuendelea . Kuweza pia kujua uhusiano chanya wa hawa viumbe katika maisha yao ya kila siku unafaida kwao pia, mfano uwepo wa ndege katika mazingira hayo huweza kupunguza kuenea kwa magonjwa mbalimbali yasababishwayo na wadudu ambao ni chakula cha hawa ndege.

Watanzania wanaitwa katika kujifunza mambo mengi kuhusu muingiliano huu kwa kufanya utalii wa ndani na kujionea wenyewe jinsi wanyama wa aina tofauti  jinsi wavyoweza kuishi katika sehemu moja na bila kudhuliana kwa namna yoyote zaidi huwa wanasaidiana.Hii itaongeza uelewa na usambazaji wa taarifa kuhusu viumbe hawa na kuamasisha utalii wa ndani uzidi kuongezeka hivyo kuongeza pato la Taifa.

Serikali ikisaidiana na idara ya wanyama pori  na wadau mbalimbali wanahitajika kuandaa matamasha mbalimbali ili kuweza kueneza uelewa kuhusu umuhimu wa viumbe hawa hii itasaidia watanzania katika kushiriki katika shughuli za uhifadhi wa mazingira ya wanyama hawa mfano utunzaji wa miti ambayo ndio makazi kwa ndege na kujenga viota vyao kwa ajili ya kuzaliana kikubwa tunahimizwa kupanda miti na sio kukata miti.

Kwa maswali, maoni na ushauri unaweza kuwasiliana na mwandishi wa Makala hii kwa namba zilizopo hapo chini, mwisho wa Makala hii.

Ahasante sana.

Mawasiliano

Naomi Mnyali

+255 788 706 476

Barua pepe : naomimnyali@gmail.com