Kiashiria ni alama ambayo inatoa taarifa au tahadhari juu jambo fulani zuri au baya na kukufanya uweze kuchukua  hatua mapema. Katika uhifadhi au sayansi ya wanyamapori kiashiria ni biolojia ya viumbe ambayo hutumia kuwepo au kutokuwepo kwao katika ikolojia au mazingira Fulani kama kipimo cha afya, ubora au mabadiliko. Wanyama jamii ya amphibia na reptilia wanaweza kutumika kupima mabadiliko ya hali ya hewa kama , ukame, uchafuzi wa mazingira na kuharibika au kusitawi kwa ikolojia, nk.

Katika uhifadhi, ndege wamekuwa ndio alama bora zaidi ya kupima afya ya mifumo mingi ya kiikolojia. Mfano ndege wanaishi katika mazingira mengi nchi kavu (ardhini) na kando au ndani ya maji. Ndege ni kiashiria cha kibaolojia kwani huishi mazingira ambayo mahitaji muhimu kama chakula, makazi ya kuzalia, na uwezo wa  kupambana na maadui (usalama) unakuwepo.

Ndege ni  wataalamu wa kupima afya ya ikolojia kwa kuhusianisha mahitaji yao na mazingira ya kikolojia au vitu vinavyounda ikolojia hiyo. Mfano heroe (flamingo) ni ndege wanaoishi maeneo yenye maji  mfano hifadhi ya ziwa Manyara. Hivyo uwepo wa heroe hutokana na misimu wa wao kuja nchini Tanzania kwa ajii ya kuzaliana na wakitokea Ulaya. Kwa maana hiyo mfumo wa kiikolojia wa ziwa manyara ni bira kwa maisha endelevu ya ndege hawa.

Kiashiria kingine kwa ndege ni uwezo wao wa kuweza kutambua   kwa haraka  uchafuzi wa mazingira, mabadiliko ya hali ya hewa na kuweza kuhama, milipukopuko wa magonjwa, kutambua msimu wa  mavuno mfano kwelea domojekundu. Kutokana na hayo ndege huishi kwenye mfumo fulani wa kiikilojia kulingana na mahitaji yao muhimu

SABABU ZA NDEGE KUTUMIKA KAMA KIASHRIA KATIKA SHUGHULI MBALIMBALI ZA UHIFADHI

Ndugu msomaji wa makala , hapa tunajifunza  sababu au sifa za ndege kuwa kiashiria bora katika ikolojia au uhifadhi wa wanyamapori. Ndege wanaotumika kama kiashiria cha kibaolojia ni wale wanaopatikana kwa muda mrefu katika hayo mazingira, mfano ni ndge ‘chozi’ ndani ya bustani ya miti ndani ya Chuo Kikuu cha Kilimo SUA.  Uwepo wao umekuwa wa kudumu kwa sababu ya kuwepo kwa miti mingi ya maua.

  1. Ndege wanauwezo wa kuhisi mabadiliko kwa haraka, hivo kusaidia kutoa  taarifa za mapema juu ya hali ya hewa au vijenzi vya mazingira kwa haraka kwa kutumia mfumo wa hisia, kuona na harufu.
  2. Ndege wanauwezo wa kukabiliana na mabadiliko ambayo hayana mpangilio maalumu.
  3. Pia sifa zingine ni pamoja na uwezo wa kuonekana kwa urahisi kuliko viumbe wengine kutokana na rangi zao nzuri, sauti au nyimbo
  4. Ndege wanaishi mazingira tofauti tofauti na uwezo wa kupaa angani (kuhama) . Hivyo kama kuna mabadiliko yoyote basi idadi ya ndege inaweza kupungua katika ikolojia hiyo, kwa kuhama, kufa au kubadili tabia za kujitafutia chakula.

NUKUU: Ndege huhisi mabadiliko ambayo yanaweza kuwa mazuri hivo kuvutia kuishi katika ikolojia hiyo au mabadiliko mabaya hivyo huhama au kufa na kusababisha kupungua idadi yao.  Mfano ongezeko la uchafu, ,mabadiliko ya hali ya hewa mfano tufani, au kimbunga, majira ya mwaka kubadilika na ndege hubadili tabia na mazingira ya kuishi. Pia shughuli za binadamu mfano ujangili, kuchoma mioto hovyo, ukataji miti hovyo  na kusababisha ndege kubadili mwenendo wao

Vile vile kuna maeneo ambayo ndege wanaweza kutumika kama kiashiria katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake mfano;

Kupima uchafuzi wa mazingira.

Hapa tunawatumia ndege kama vile kunguru na tumbusi ambao wanatumia mizoga kama chakula.  Mfano , hifadhini maeneo ambapo utawaona ndege tumbusi wengi ni kiashiria kuwa mahali hapo kuna mzoga wa mnyama ambao umetokana na sababu mbalimbali kma vile kuuwawa na wanyama wanaokula nyama, majangiri au kifo cha asili. Kadhalika kunguru ambao wamesambaa katika mazingira mengi duniani wanaitwa wasafisha miji kwani wao hutumia chakula chochote. 

Licha ya umuhimu wa ndege kwenye mazingira yetu bado wanakabiliwa na changamoto kubwa mfano ndege tumbusi kumekuwa na taarifa za kuwekewa sumu kwenye mizoga ambayo huliwa na ndege hawa hivyo kupelekea kupungua kwa kiasi kikibwa kwa kufa kutokana na sumu hizo. Tumbusi ni muhimu katika ikolojia za hifadhi zetu maana husaidia katika usafi wa hifadhi kwa kuwa na uwezo wa kula mizoga yenye magonjwa kwa sababu ya uwepo wa asidi kali tumboni (PH 0) ambayo inaweza kuuwa vidudu vya magojwa kama vile kimeta na kichaa cha mbwa. Kutokana na umuhimu wake kuna wakati wanaitwa SABUNI YA SAVANA.

Pichani :ndege tumbusi wakila mzoga uliokufa mwituni.

Kupima ubora wa makazi na upatikanaji wa mahitaji.

Ndege wengi wanaweza kutumika kama kipimo au alama ya ubora wa mazingira au ikolojia wanayoishi. Hii hutokana na uharibifu unaofanywa na shughuli za kila siku za binadamu.  Hapa tutawatizama ndege wa majini yaani ndege wanaopatikana maeneo ya maji. Mfano  kichi (kingfisher), kitwitwi (sandpiper), sile-maua (African jacana), jamii za bata na heroe mnandi ( cormorant bird). Hawa hupima ubora wa ikolojia za kwenye maji kwani wanahisi mabadiliko mapema kama uchafuzi wa maji na kupungua au kuongezeka kwa viumbe wa majini(chakula) kama vile samaki, minyoo, na wadudu. Hivo uwepo wao katika eneo Fulani ni ishara kwamba eneo ni bora na salama.

Pichani : ndege wa majini  sile maua ( african jacana bird)

Mabadiliko ya majira ya mwaka na uzalianaji wa ndege.

Ndege mahususi ambae hutumika sana katika nyanja hii ni “kwelea domojekundu” ,ambao huonekana  kama  kikwazo kwa wakulima hasa msimu wa mavuno. Wanaishi kwa kuhama hama kutafuta maeneo ambayo kuna mazao kama mpunga, mahindi nk. Hivyo uwepo wao ni kiashiiria tosha kuwa ni msimu wa mavuno. Kwelea domo jekundu ni jamii ya kwera (weaver) ambao wanaishi kwa makundi na  uwepo wao hunatoa taarifa au alama ya kuchukua tahadhari mapema ili kuzua uhalibifu.

Pichani ni kwelea domo.jekundu

MAHITAJI MUHIMU ILI KUWATUMIA NDEGE KAMA KIASHIARIA.

  • Tunahitaji kukusanya taarifa za ndege husika kulingana na kiashiria
  • Majira ya mwaka ambayo ndege wanaishi( kama wapo wanaishi kwa kuhama hama
  • Makadirio ya idadi yao kwa muda fulani kwani kundi la ndege linaweza ongezeka au kupungua

CHANGAMOTO ZA NDEGE KAMA KIASHIRIA CHA KIBAOLOJIA.

  • Uharibifu wa makazi ya ndege au upotevu wa makazi na kupelekea ndege kuhama
  • Majanga ya asili mfano tufani, mabadiliko ya hali ya hewa  kupelekea vifo
  • Vitisho kutokana na shughuli za binadamu mfano uchafuzi wa maji, ukataji wa miti, na matumizi ya kemikali kuwa uwa ndege kama kwelea domojekundu, tumbusi nk.

Asante kwa kusoma makala hii, imehaririwa na Alphonce Msigwa, Mwikolojia Hifadhi za Taifa Tanzania, TANAPA.

Mwandishi wa makala hii ni,

Shadrack Andrea Kamanga

Simu: 067857786

        Email: bigstarshadrack@gmail.

Sokoine University of Agriculture ( SUA,Morogoro.