Nchi yetu imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ikiwa ni pamoja na wanyamapori, jiografiia nzuri ya uwanda wa mabonde, miinuko na milima, mapango na michoro ya zamani, miji mikongwe na tamaduni mbalimbali za makabila zaidi y amia moja yanayopatikana nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa sheria, hivi vyote vipo chini ya wizara ya maliasili na utalii. Ikumbukwe sekta ya utalii imekuwa ikiongoza kwa miaka mingi katika kuchangia pato la taifa kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni.
Ukiachana na janga kubwa la homa ya virusi vya Corona lililoikumba dunia nzima na changamoto nyingine za ndani ya nchi. Vivutio vya utalii kama vile uchache wa miundo mbinu mfano hoteli na viwanja vya ndege hasa hasa katika kipindi cha wageni wengi, bado sekta ya utalii imeendelea kukua kwa kasi zaidi.

Pichani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Samia Suluhu Hassan katika kampeni ya kutangaza utalii wa Tanzania
Mfano mwaka 2020 na 2021, nchi ilipokea wageni wasiozidi milioni moja, mwaka 2022 wakaongezeka kufikia 1,454,920, mwaka 2023 – 1,808,205, mwaka 2024 – 2,026,378 na mwaka huu 2025 inakadiriwa kufikia milioni tano hii ni hesabu ya watalii wote wa ndani na wa nje ya nchi.
Namba hizi za watalii zimekuwa zikiongezeka kutokana na jitihada mbalimbali za serikali, kampuni za utalii na watu binafsi kuwekeza katika kutangaza vivutio vya utalii na kubuni na kutengeneza vivutio vingine.
Jitihada hizi zote bado haziwezi tosha peke yake pasipo msaada wa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Vifaa vya kisasa kama vile simu janja, kamera, televisheni na kompyuta vina mchango mkubwa katika kutangaza utalii.
Pamoja na kukuza utalii kwa kutumia teknolojia mbalimbalia, pia kuna vichochezi vingine ambavyo ni
1.Mitandao ya kijamii
Vitu vingi vimeanza kuonekana na kuvifuatilia kwa urahisi kupitia mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram, Thread, X, TikTok, Linklden na blogs mbali mbali kama vile blog ya Wildlife Tanzania.
Mitandao hii imefanyika fursa kubwa kwa serikali na watu binafsi kurusha na kusambaza makala, picha na hata video mbalimbali zihusuzo utalii na shughuli zinazoendana na utalii.
Hii imesaidia sana utangazaji wa vivuvtio vya utalii na imeweza kuwafikia watu wengi zaidi kwa muda mfupi. Si hivyo tu pia kuwavutia watalii kutembelea vivutio hivyo
2.Michezo mbalimbali katika hifadhi za taifa na miji mikubwa
Taasisi mbalimbali chini ya wizara ya maliasili na utalii kama Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii, zimekuwa na mchango mkubwa katika kutangaza na kuvutia watalii wengi zaidi kupitia michezo mbalimbali ndani ya hifadhi.
Michezo hii ni kama uendeshaji wa baiskeli na marathoni kuanzia ndani hadi nje ya mipaka ya hifadhi. Mfano Serengeti Safari Marathon hufanyika mwezi Novemba kila mwaka na The Great Ruaha Marathon ambayo hufanyika mwezi Julai kila mwaka.
Mchezo huu wa mbio umekuwa kichocheo kikubwa kwa watanzania wengi sio tu kutembelea hifadhi za taifa bali hata kwenye utalii wa miji mikubwa nchini mfano kupitia NBC Dodoma marathon hufanyika Julai na CRDB marathon ndani ya jiji la Dar es salaam hufanyika mwezi wa nane.

Pichani; Watalii wa ndani walioshiriki The Great Ruaha Marathon, Julai 2023 kwa ajili ya kukuza na kuchochea utalii wa ndani
3.Tuzo mbalimbali za utalii kitaifa
Kuanzia kwenye utangazaji wa upigaji kura hadi ugawaji wa tuzo hizo, kumesaidia kutangaza vivutio vya utalii na kuongeza idadi kubwa ya watalii. Wengi wetu tumekuwa mashahidi na naamini tulipata bahati ya kupigia kura vivutio vyetu kwenye vinyanganyiro mbalimbali vya tuzo za utalii duniani.
Baadhi ya maeneo ya vivutio vya utalii Tanzania yamekuwa kwenye vipengele mbalimbali na kushinda kama vile hifadhi ya taifa ya Serengeti ikishinda tuzo ya hifadhi bora barani Afrika kwa miaka minne mfululizo (2021 – 2024).
Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro kama kivutio bora zaidi cha watalii barani Afrika kwa miaka sita (2013, 2015, 2016, 2017, 2018 na 2024). Lakini pia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imekuwa ikipokea tuzo ya bodi bora zaidi ya utalii barani Afrika kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2022 – 2024.
Si hivyo tu bali pia uwanja wa ndege wa Msembe uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ulishika nafasi ya kwanza barani Afrika na nafasi ya pili duniani kama uwanja wenye mvuto zaidi duniani mwaka 2020. Utangazaji na ugawaji wa tuzo hizi umefanyika kichocheo kikubwa duniani kwa kuvuta watalii kutembelea nchi yetu na kujionea vivutio mbalimbali.
4.Maonesho ya mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ya kutangaza vivutio vya utalii
Maonesho makubwa ya kitaifa yenye kuvuta watu wengi zaidi ni pamoja na maonyesho ya sikuku ya wakulima ya nane naneambayo hufanyika kikanda na maonesho ya biashara ya saba saba ambayo hufanyika jijijin Dar-es-salaam.
Kupitia maonesho haya taasisi za kiserikali zinazojihusisha na uhifadhi na utalii kama vile TANAPA, Mamlaka ya usimamizi wa eneo la Ngorongoro (NCAA) pia TAWA asasi, kampuni na watu binafsi wamekuwa wakiyatumia maonyesho hayo kuuza bidhaa na mazao mbali mbali ya utalii.
Hii imekuwa ni chachu kubwa ya kutangaza utalii kwa urahisi na kuwafikia watu wengi zaidi. Pia kupitia maonesho hayo, kumewapa fursa wageni wengi kuuliza maswali na wakati mwingine hata kuwaandalia safari za kitalii kwa gharama nafuu.
Na kwa uchache baadhi ya maonesho makubwa ya utalii yenye kulenga soko la nje zaidi ni pamoja na Swahili International Expo (S!TE) lililoanzishwa 2018 na bodi ya utalii pia Karibu – KILIFair onyesho hili huandaliwa na umoja wa makampuni ya utalii nchini (TATO).

Pichani; Mwandishi wa Makala hii Leena Lulandala alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika maonesho ya Sabasaba jijini Dar es salaam mwaka 2024.
5.Tanzania safari channel
Ukiachana na vipindi vya utalii, malikale, na maliasili vinavyorushwa na vituo mbalimbali vya habari, Tanzania Safari Channel imechangia kwa asilimia kubwa katika kukuza utalii wa ndani.
Chaneli hii ya televisheni imekuwa ikielimisha, kufundisha na kutangaza vivutio vya utalii hususani kwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili na hata mara chache hutumia lugha ya kifaransa na kiispaniora.
Chaneli hii imefanyika msaada sio tu kwa jamii ya watanzania pia kwa wanafunzi wengi na imeongeza ufahamu wa vivutio vya utalii, wanyamapori wapatikanao maeneo mbalimbali ya nchi yetu na shughuli nzima za uhifadhi kwa ujumla.
6.Miradi, Sera na hashtag mbalimbali zinazoendana na utalii
Mradi mkubwa wa “The Royal Tour” uliofanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Samia Suluhu Hasani Aprili mwaka 2022.
Mradi huu ulilenga soko la nje, uliweza kuzalisha “hashtag” (#) nyingi katika mitandao ya kijamii kama Instagram #theroyaltourtz. Kumekuwa na sera na hashtag nyingi ziilizotengenezwa na baadhi ya mawaziri waliokuwa wanasimamia wizara ya maliasili na utalii.
Baadhi yao ni Hamisi Kingwangala aliyewahi kuwa waziri wa Maliasili na Utalii alianzisha mradi wa kutembea na wasanii wakubwa nchini kwenye vivutio vya utalii ili kutangaza vivutio hivyo.
Lengo la kampeni hiyo ilikuwa ni wasanii kutangaza utalii kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii. Mradi mwingine ulikuwa ni “Pori kwa pori”. Waziri Dr. Pindi Chana, akiwa Iringa kuhamasisha jitihada za kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana Kusini mwa nchi alianzisha sera na “hashtag” ya Kusini kumenoga.
Jitihada hizi zote zimechangia kutangaza na kukuza utalii, mfano wa “hashtag” kubwa nyingine ni pamoja na #tzunforgettable, #twendezetukileleni, #theroyaltour, #porikwapori na #vibekitalii hii ikiwa chini ya the great Ruaha Marathon.

Pichani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan, katika kampeni maarufu ya The Royal Tour, kutangaza vivutio na utalii wa Tanzania duniani
7.Ongezeko kubwa la wanaharakati, wakereketwa na vyombo vya Habari
Masomo mengi nchini yenye mitaala ya utalii na pia safari za kitalii shuleni kwa pamoja zimechangia kuongezeka kwa uelewa wa vivutio vya utalii.
Mtu mmoja mmoja au vikundi vimeongezeka kwa kasi vikilenga kutangaza na kukuza utalii nchini kwa njia mbalimbali. Mfano kuandaa safari za kutembelea vivutio hivyo pia kuvitangaza kwa njia za makala za maandishi, video na picha kwa mfano mzuri ni blogu yetu ya Wildlife Tanzania.
Pia vyombo vya habari vimeongezeka vikiandaaa vipindi maalumu vya kutangaza vivutio vya utalii na kuielimisha jamii kama vile; kipindi cha Chetu ni Chetu – ITV, kipindi cha makala za makabila na bahari yetu – UTV na vingine vingi.
8.Ongezeko kubwa la wawekezaji wa utalii wa ndani
Hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la wawekezaji wazawa katika sekta ya utalii hususani upande wa hoteli , maduka ya zawadi na migahawa ya kitalii.
Hivi vyote vimesaidia kwa kiasi kikubwa ongezeko la safari za kitalii kwa wazawa kwa sababu wawekezaji wazawa viwango/ gharama zao zimekuwa nafuu zenye kuendana na uchumi wa wananchi wengi. Tofauti na wawekezaji wa nje ambao hulenga zaidi soko la watalii wa nje ya nchi hivyo gharama zao kuwa kubwa.
9.Safari za sherehe mbalimbali
Siku za karibuni kumekuwa na mwitikio mkubwa wa watu kutaka kufanya sherehe, harusi au matukio mengine ya furaha katika hifadhi au vivutio vya utalii. Mfano wengine wataenda fungate katika hifadhi za wanyama, au watenda Zanzibar au sehemu zenye mandhari nzuri ya kuvutia.
Pamoja na hayo, Tanzania imekuwa ikipokea watalii wanaokuja kufunga ndoa katika fukwe mbalimbali hususani Zanzibar na hifadhi za taifa, safari zote hizi zimekuwa zikichangia kukuza na kutangaza vivutio na mazao yetu ya utalii.

Pichani, sherehe za harusi na ndoa katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori.
Naamini kupitia makala hii umetambua jitihada ambazo zinasaidia kutangaza na kukuza sekta ya utalii nchini. Hizi ni baadhi tu, zipo nyingine kama ukarimu wa watanzania, amani nchini, miundo mbinu bora hususani mijini pia vivutio vingi vinavyopatikana sehemu moja kama vile kanda ya utalii Kaskazini.
Mwandishi wa Makala; Leena Lulandala
Mhariri: Alphonce Msigwa.
Kwa maswali, maoni na nyongeza wasiliana na mwandishi,
Leena Lulandala+ 255 755 369 9684 & leenalulandala0@gmail.com
Tunaandika makala hizi ili tuongeze uelewa wetu kuhusu wanyamapori, tunaamini tukipata uelewa tutachukua hatua kushiriki katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake asilia.Kazi hii tunafanya kwa kujitolea na hakuna malipo yoyote, endapo umefurahia kazi zetu unaweza kutuunga mkono kwa kiasi chochote ili tupate mtandao, vifaa vyua kufanyia kazi kama kamera na komputa. Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana kwa mawasiliano haya; hmconserve@gmail.com |+255-683-862-481