Habari msomaji wa wildlife Tanzania, naamini unaendelea kupambana ili kuboresha maisha yako. Karibu tena kwenye mfululizo wa makala za uchambuzi wa sheria ya uhifadhi wa wanyamapori Tanzania. Kama nilivyokwisha kuandika kwenye baadhi ya makala za nyuma, sheria hii ina mambo mengi ambayo kila moja wetu anapaswa kuyafahamau, kuna watu wanafanya kazi kwenye sekta ya wanyamapori, kuna wanaofanya kazi kwenye sekta ya utalii, na wengine ni wawekezaji kwenye sekta hii ya wanyamapori na utalii. Kwa namna moja ama nyingine katika eneo ambalo upo na unajihusisha au unaishi karibu na maeneo ya hifadhi ya wanyama au mbuga za wanyamapori, uanapashwa kuifahamu sheria hii vizuri.

Hivyo  naamini katika maarifa haya yatasaidia sana kuimarisha uelewa kwenye eneo la kazi au kwenye kutatua changamoto mbali mbali wanazokutana nazo wafugaji na wakulima waliopo kando ya maeneo ya hifadhi ya wanyamapori. Kwa mfano katika makala ya jana kuna kifungu cha sheria kinaeleza masharti ya mtu kutaka kuishi au kufanya ujenzi wa aina yoyote karibu na eneo la hifadhi ya wanyamapori. Kifungu cha 74, kinasema ujenzi wowote au makazi au shughuli zozote za kibinadmu hazitakiwi kufanyika ndani ya mita mia tano (500m) kutoka kwenye mpaka wa eneo la hifadhi ya wanyamapori. Hivyo basi sheria imesaidia kutoa maelekezo kwa watu wanaotaka kuendesha biashara au kilimo, makazi, au shughuli nyingine yoyote kwenye maeneo haya, na endapo watu tungezingatia mambo haya migogoro ingepungua kwa kiasi fulani.

Katika makala ya leo ambayo tutaichambua Sehemu ya Tisa (Part IX) ya sheria hii tutajifunza na kuelewa Usajili wa Nyara (Registration of Certain Trophy). Nyara ni vitu ambavyo havieleweki haraka kwa watanzania wengi, isipo kuwa wale wanaofanya kazi kwenye sekta ya wanyamapori na maliasili watakuwa wanaelewa tunapozungumzia “nyara”. Hivyo basi sehemu yote ya tisa kwenye sheria hii ambayo inaanzia kwenye kifungu cha 77, inaelezea nyara na usajili wake. Ikumbukwe kwamba nyara zote huwa ni mali ya serikali kwa mujibu wa sheria hii.

Nyara (trophy) ni nini? Kwa mihjibu wa sheria hii, nyara ni sehemu yoyote ya mwili wa mnyama akiwa hai au akiwa amekufa, nyara inajumuisha pia mnyama mwenyewe hata kama hajatolewa sehemu yoyote kwenye mwili wake, yani mnyama akiwa mzima ni nyara akiwa hai ni nyara. Kwa hiyo nyara zinaweza kuwa Ngozi, kucha, meno, nywele, mifupa, manyoya, pembe, kwato, au sehemu yoyote ya mnyama ni nyara. Kwa ufahamu zaidi watu wengi hufikiri nyara ni meno ya tembo na faru pekee, hapana hata meno ya boko, au meno ya kiboko na meno ya wanyama wengine hata pembe sio pembe za faru pekee, hapana hata pembe za swala ni nyara.

Aidha suala la nyara linaenda mbali kabisa, yani hata kama nyara hizo za wanyama zimeshatengenezwa bado ni nyara halali (manufactured trophy), vitu vyoyote vilivyotengenezwa na sehemu za wanyama kama vile meno, pembe, Ngozi kucha, kwato, manyoya, nywele hizo ni nyara kwa mujibu wa sheria hii, au nyara zilizotengenezwa. Masuala ya nyara yanasimamiwa vizuri sana na serikali na sheria za kimataifa, hivyo sio jambo jepesi kama wengi tunavyodhania.

Kuna sheria nyingi na makubaliano ambayo nchi mbali mbali husaini na kukubaliana kuhusu nyara za wanyama na wanyama wenyewe. Watu wengi sana wametiwa hatiani kwa kujaribu kuficha au kuiba nyara za serikali, kuna watu wanataka kutumia njia ya mkato kujimilikisha nyara za wanyama. Kuna kesi nyingi sana za ndani na nje ya nchi kuhusu masuala ya nyara. Na kwa kuwa mambo haya hufanywa  kwa ushirikiano na nchi nyingine hivyo imekuwa ni rahisi kuwagundua watu wanaosfirisha nyara isivyo halali.

Kuna wanyama ambao wapo hatarini kutoweka nao wamekuwa wakitumiwa na watu kwa sababu mbali mbali. Na hivyo nchi wanachama wa CITES wameamua kuunda sheria za usafirishaji na ukaguzi wa wanyama au nyara za wanyamapori. Naamini kwa makala zijazo nitaeleza vizuri zaidi kuhusu CITES na majukumu yao kuhusu wanyama walio hatarini kutoweka na kushamiri kwa biashara ya nyara au ya wanyamapori. Hivyo nikwambie rafiki yangu endelea kufuatilia makala hizi ambazo zinakwenda hewani kila siku. Leo tumeanza tu na utangulizi kuhusu masuala ya nyara, makala ijayo tutaingia ndani ya sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009 tuone maelekezo na mapendekezo ya sheria kuhusu sehemu hii, karibu sana.

Ukiwa na maswali maoni, ushauri usisie kuwasiliana nasi kwa mawasiliano hapo chini, pia unaweza kucomment hapo.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania