Habari Rafiki, karibu tena kwenye uwanja wetu wa kupeana maarifa na taarifa mbali mbali za uhifadhi wa wanyamapori, utunzaji wa mazingira na utalii. Kwa miaka mingi tumekuwa hatuna utaratibu wa kutembelea vivutio kwenye maeneo mbali mbali kama vile hifadhi, sehemu za kihistoria, makumbusho, na sehemu nyingine zinazovutia. Mara nyingi watu wengi wanaposikia masuala ya utalii, huwa wanajitoa kabisa na kuona kuwa hawastahili kuwa kwenye kundi la watalii, wanaamini watalii ni wazungu tu. Wengine wanafanya hivyo kwa kuwa hawajaona faida za kuwa watalii, hawaoni faida za kutembelea maeneo yenye vivutio mbali mbali. Sasa leo nitakueleza faida za kutalii.
- Unaiburudisha Akili yako
Unaposafiri kwa lengo la kwenda kuona wanyamapori au vivutio vingine ambavyo hajawahi kuviona huwa akili yako inafurahi sana na kuwa kama mpya, unaipa akili yako chakula, kama tunavyojua kazi ya akili zetu ni kufikiri, na huwezi kufikiri kitu ambacho hujakiona au kukisikia au hata kukisoma, kwa hiyo unapo kuwa mtalii, maana yake unailisha akili yako mambo mapya, ambayo itayatafakari. Naweza kusema kama vile unavyosoma kitabu na kufurahia mambo ambayo ni mageni kwako, je si zaidi kuyaona mambo mageni kwa kutembelea hifadhi mbali mbali, au sehemu mbali mbali zenye vivutio? Ilishe akili yako mambo mapya.
- Utakutana na Fursa nyingi
Fursa zipo kila mahali, ila unahitaji macho tu kuziona, lakini kuna njia nyepesi sana inayotumiwa na watu wengi waliofanikiwa kujua fursa ipo wapi, njia hiyo ni kwa kutembelea sehemu hizo, watu wengi wanao fanyabiashara wameona fursa kwa kuwa maeneo ambayo ni tofauti na maeneo waliyozoea. Kwa kutembelea hifadhi na vivutio mbali mbali hapa Tanzania utajionea fursa nyingi sana za uwekezaji, biashara, kilimo, ufugaji na nk. Fursa ambazo huwezi kuziona kwa kukaa tu sehemu moja maisha yako yote. Amka hapo ulipo nenda nje ya eneo ulilopo. Usiogope gharama kwasababu ni muhimu sana kwako kusafiri, jipe nafasi ya kuona mambo mapya kabisa ambayo akili yako haijawahi kuyaona. Pia hizi ni sehemu nzuri kwa kuangalia masoko ya bidhaa zako ulizonazo.
- Utapata marafiki wapya
Naamini ukikutana na watu wapya kwenye maisha yako, hata mambo mapya yanaanza kuingia kwenye maisha yako, kama una marafiki wa muda mrefu na hujawahi hata kuwa na marafiki wengine tofauti na hao wa miaka mingi, hii ni fursa yako ya kukutana na watu wapya. Watu ndio wanamchango mkubwa kwenye mafanikio na ndoto zako, jipatie watu sahihi kila uwezapo kwenye maisha yako, watu ni fursa watu wana vitu vizuri. Hivyo unaweza kukuza mtandao wako na watu wengine kwa upya kabisa. Wanasemaga tembea uone.
- Ushirikiano kwenye masuala ya uhifadhi wa wanyamapori na rasilimali
Naamini watu wanapotembelea maeneo ya mbuga za wanyama, au vivutio vingine watapata na muda wa kupewa maarifa na watu wanaofanya kazi kwenye maeneo hayo, wata elezea mafanikio, jinsi wanavyofanya kazi, wataelezea na changamoto wanazokutana nazo wakiwa kazini. Kwa mfano ikiwa watu watatembelea hifadhi za wanyama wataelezwa changamoto kubwa ya kukosa wageni, ujangili na kukosa wataalamu wa fani fulani. Hivyo kwa watu kupata taarifa za namna hii wanaweza kusaidia kwa kutoa ushirikiano na msaada mbali mbali yenye lengo la kuhifadhi maliasili zetu, misaada hivyo inaweza kuwa ya mawazo, au ya kifedha hivyo ni muhimu tukawa na utaratibu wa kutembelea vivutio vyetu.
- Ni sehemu nzuri sana ya kujifunza na kupata elimu
Unapotembelea hifadhi au maeneo yaliyohifadhiwa, unapata nafasi ya kuelimika na kupata maarifa kwa njia mbali mbali kama kwa kuona mwenyewe na pia kwa njia ya kufundishwa na kuelekezwa na wataalamu walioko maeneo hayo. Kwa kupitia maelezo na taarifa utakazopata itakusaidia kujifunza vitu mbali mbali vitakavyo saidia kuboresha maisha yako na uhifadhi wa maliasili zetu. Pia kama ni wanafunzi au ni watoto wataelewa misingi na wataweza kuchagua kuingia kwenye fani ya kusomea mambo ya wanyamapori na utalii, wengine itawasaidia na kuwapa maeneo ya kufanya tafiti mbali mbali za kisayansi na za kijamii.
- Njia bora ya kutangaza utalii wetu
Watu wanapokuwa na utamaduni mzuri wa kutembelea maeneo yenye vivutio mbali mbali ndani ya nchi yetu, ndio huwa watangazaji wazuri wa utalii wetu. Kama tunataka maliasili zetu zijulikane kila mahali basi tunatakiwa kuwa na utamaduni wa kutembelea maliasili zetu. Vitu watu watakavyoviona ndivyo watakavyosimulia na kuwaambia wengine. Mtu hawezi kutangaza jambo au kitu ambacho hajakiona au hakielewi. Njia nzuri ya kila Mtanzania kuwa balozi mzuri kwenye kuutangaza utalii wetu ni kwa njia ya kutembelea hifadhi na maeneo ya vivutio. Mimi naamini sana katika hili na ni njia ya gharama nafuu sana kuutangaza utalii na vivutio vyetu.
- Kuinua uchumi na kuharakisha maendeleo
Watu wanapokuwa na utamaduni wa kutembelea hifadhi na maliasili nyingine wanakuwa ndio wachangiaji wakuu wa ukuaji wa uchumi wetu kwa kuongeza mapato ya ndani. Kupitia utalii na maliasili. Kwa kiingilio ambacho watatoa kwenda hifadhini au maeneo ya vivutio itasaidia sana kuinua uchumi wa nchi yetu. Ni njia nzuri sana ya kuanzia ili tuitoe nchi yetu kwenye utegemezi mkubwa wa misaada ya kifedha kutoka kwa mataifa mengine. Tukiwa na utamaduni wa namna hii wa kutembelea hifadhi na vivutio mara kwa mara, tutaipeleka nchi yetu mbali sana kiuchumi.
Naamini umepata mwanga na sababu za msingi kabisa za kutembelea maeneo ya vivutio, kuna sababu nyingi lakini hizo saba zitufikirishe. Usisahau kumshirikisha mwingine makala hii. Jijengee utaratibu huu, ni mzuri sana utaimarisha afya ya akili na afya ya mwili nay a roho yako pia.
Asante sana Rafiki, karibu sana hifadhini.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
0742092569/0683248681