Habari rafiki na msomaji wa mtandao huu wa wildlife Tanzania, naamini unaendelea vizuri na shughuli zako za kila siku. Karibu tena kwenye uwanja wetu wa masula ya wanyamapori na maliasili kwa ujumla. Kama nilivyotangulia kuandika kwenye blog hii tangu mwanzo kuwa lengo la blog hii ni kutoa maarifa ya uhifadhi wa wanyamapori kwa jamii kubwa ya watanzania. Baada ya kujifunza mambo haya nimegundua na kujua kuwa Tanzania ni nchi ya kipekee sana na ina rasilimali nyingi sana ambazo zinahitaji kutambuliwa na jamii ya watanzania lakini kikubwa zaidi rasilimali hizi zinahitaji kutunzwa na kuwanufaisha watanzania wote.

Ndio maana nimeamua kutumia lugha ya Kiswahili kuelezea mambo mengi sana ambayo yapo hapa Tanzania lakini pia maandishi mengi yanayoelezea maliasili zetu na matumizi, usimamizi wake yameandikwa kwa lugha ya kingereza hivyo naamini kwa kuanzisha mtandao huu kila mtanzania atakuwa huru kujifunza wakati wowote kupitia mtandao huu.

Makala ya leo nimekusudia kutoa uelewa kidogo jamii kuhusu haki ya kumiliki wanyamapori, kwenye maandiko mengi hasa kwenye sheria zinazosimamia maliasili kama vile misitu, ardhi, madini na wanyamapori watu wengi hawajui nani huwa ni mmiliki wa mali yote ya Tanzania. Sisi kwa upande wetu, upande wa maliasili tunataka upate ufahamu huu na kujua kwa mujibu wa sheria za nchi zilizopo maliasili ya wanyamapori ipo chini ya nani. Hili ni jambo zuri sana endapo tutalifahamu mapema maana litatupa namna mpya ya kufikiri na kuchukua hatua stahiki.

Sheria ya uhifadhi wa wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009. Mwanzo kabisa katika kifungu cha 4 kinaelezea kuwa wanyamapori wote waliopo Tanzania wataendelea kuwa ni mali ya umma na zitakuwa chini ya uangalizi wa Rais kwa niaba ya watanzania wote. Hivi ndivyo kifungu hiki cha sheria ya wanyamapori kinavyotamka na kuweka wazi kuhusu rasilimali za wanyamapori waliopo hapa Tanzania. Hivyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndio mwenye mamlaka ya mwisho kwenye matumizi ya rasilimali hizi. Kwa kuwa yeye ndiye aliyepewa dhamana ya kusimamia kwa niaba ya watanzania wote maliasili hizi ambazo kisheria ni mali ya umma, au mali ya watanzania wote.

Kwa mantiki hio jamii inatakiwa kufahamu kuwa wao ndio wahusika wakuu wa rasilimali hizi, na pia wanatakiwa kuzielewa rasilimali zao vizuri, hapa kwenye uelewa wa rasilimali zao inatakiwa jamii iwe na macho ya kutazama na kuangalia usalama wa rasilimali hizi ikiwa ni pamoja na usimamizi wake na uongozi kwenye rasilimali za nchi. Uzalendo wa kweli ni kufahamu na kusimamia rasilimali ambazo zinakuhusu wewe na jamii yako bila uoga, na kukosoa vitendo vyote vya ubadhirifu na unyonyaji kwenye mali ya umma, uzalendo ni kuwa sauti ya wale wasio na sauti kwa ajili ya kulinda haki zao za msingi. Huwezi kuwa mzalendo wa kweli kama hujui nini kinaendelea kwenye nchi yako, kwenye jamii yako, kwenye usimamizi wa mali na rasilimali za nchi yako, unatakiwa kufahamu na kuchukua hatua za makusudi kwa mujibu wa shria za nchi.

Naamini umepata maarifa ya kukusaidia, juifunze kuhusu rasilimali za nchi yako, zitambue na anza kuzitunza na kuwafundisha wengine kuzihifadhi na kuzitunza. Asante nakutakia kazi njema.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania