Habari msomaji wa makala za blog yako ya Wildlife Tanzania, naamini unaendelea vizuri kabisa na sghughuli zako za kila siku ili kujenga maisha yako vizuri. Leo nimekuandalia makala ya kutufanya tufiri kwa upana sana kwenye hii sekta ya wanyamapori na mazingira yao. Ninachokiandika hapa ni uzoefu wangu kwenye maeneo haya na jinsi ninavyofanya kazi na jamii nyingi za watu waishio kando ya hifadhi na maeneo mengine muhimu yaliyohifadhiwa. Pia ni matokeo ya tafiti nyingi zilizofanywa na watalamu mbali mbali kwenye eneo hili la wanyamapori, kwenye ripoti nyingi za jamii na wanyapori, au mahusiano ya jamii na wanyamapori, bado ni swali ambalo halijajibika vizuri na kupata majibu ya kuridhisha sehemu mbali mbali zilipofanyika tafiti za namna hii. Inaonekana bado kuna uzito, bado kuna kutopatikana kwa muafaka wa kudumu kati ya watu na wanyamapori.

Tanzania imebarikiwa kuwa na watu wengi wenye sifa tofauti tofauti na tamaduni tofauti tofauti, ambazo zimewafanya kuamua aina ya maisha ya kuishi na pia sehemu za kuishi, kuna wakulima, kuna wafugaji, kuna wafanyabiashara na wafanyakazi wa serikali au mashirika mbali mbali, mtawanyiko wa watu katika nchi yetu umezaa tamaduni nyingi zisizofanana. Tanzania ina wafugaji wengi sana na pia wakulima wengi sana. Mgawanyiko na mtawanyiko wa watu umefanya wengine kuwa sehemu ambazo kwa kiasi kikubwa wamemulikwa na elimu, na kuelimika na wengine kukosa fursa hiyo. Kutokana na kila mtu kufanya anachokijua ambacho amekuta wazazi wake au babu na bibi zake wanafanya, hivyo yeye kama mtoto anachojua ni kuendeleza kile ambacho baba au mama yake ameakiacha au amemkabidhi.

Tukubaliane kwamba kile wazazi wako wancho kifanya mara nyingi na kukitegemea kama ndio msingi wa maisha yao ndio kinakuwa cha thamani sana kuliko vitu vyote. Kwa mfano wazazi wako ni wafugaji tangu miaka mingi iliyopita na wametumia hii kama ndio njia ya msingi ya kuendesha maisha na hivyo wanachojua kwenye maisha ni kwamba kinachotakiwa ili maisha yaende ni kuwa mfugaji, au kuwa na ng’ombe au mbuzi au mifugo mingi. Kwanini nimeeleza yote haya, ninachotaka tuone hapa ni kwamba, hii ndivyo ilivyo kwa wafugaji wengi wa nchi hii ambao kwa asilimia kubwa wanaishi au kufanya shughuli zao za maisha karibu na maeneo yaliyohifadhiwa. Hali hii ipo kwa wote kwa wafugaji na wakulima. Mtu au jamii itaendelea kuamini kwamba msingi wa maisha ni kuwa na mifugo mingi na hakuna kitu kingine cha muhimu zaidi kuliko hicho mpaka wapate elimu ya kutosha ya kujitambua. Tukishindwa kuwapa jamii hii elimu ya ukombozi na ya mageuzi kifikra matatizo yataendelea kuwepo miaka na miaka bila kuisha.

Sasa fikiria jamii iliyojijenga kwenye misingi ya namna hii ya kwamba hakuna kitu kingine kinaweza kuwa cha muhimu zaidi kuliko mifugo yao na mazao yao yaliyopo mashambani. Na mtu wa namna hii unakuta yupo karibu na hifadhi za wanyama, au maeneo mengine yaliyohifadhiwa. Endapo mnyama kama simba atakuja kuvamia na kula mifugo yake, au kwa mkulima Tembo au nyani amekuja na kula mazao yake shambani. Hapa ndipo yatainuka magomvi na migooro mikubwa isiyoisha, hapa ndio kutakuwa na hasira, hapo ndipo kutakuwa na chuki, hapo ndipo kutakuwa na visasi. Moja kwa moja mfugaji atatumia hasira na kwenda kumuwinda huyo simba na kumuua, na mkulima atatoka na wenzake ataenda kumuua huyo tembo au nyani aliyesababisha uharibifu kwenye mazo yake.

Hivyo basi mfugaji atasukumwa na hasira na mkulima atasukumwa na hasira, na popote atakapomwona mnyamapori wa aina hizo atawaua, hata kama siye mnyama aliyesababisha uharibifu kwake. Hasira itasababisha mauaji yasiyoisha na pia hata wakimwona simba amelala sehemu kitu kitakachokuwa kwenye akili yao ni adui yao ni lazima auwawe. Hali kama hii ikiendelea kuachiwa itatengeneza uhasama na chuki dhidi ya wanyamapori. Watu watakuwa hawawapendi wanyama wa namna hiyo. Inawezekana kabisa hii ndio sababu kubwa ya kupungua kwa wanyama kama simba na tembo kwenye hifadhi zetu. Unajua ni vigumu kumpenda adui yako, hapa ndipo panahitaji ukombozi wa watu ili watoke kwenye chuki na visasi walivyonavyo dhidi ya wanyama hawa. Na hii chuki haitaondoka kwa kuwapa tu elimu na ufahamu, badala yake wafundishe kwa vitendo kabisa jinsi ilivyo muhimu kuwaunza na kuwalinda wanyamapori wetu, hii ni pamoja na kuwapa faida za moja kwa moja ambazo zitawafanya waone kweli huyu simba ingawa anasababisha uharibifu lakini anafaida kubwa kwetu. Bila kufanya hivyo suala la uhifadhi litakuwa mzigo mzito sana na tutashindwa kwenda mbele na kutimiza malengo yetu kama taifa kwenye sekta hii muhimu.

Kila mtu anafahamu jinsi sekta hii inavyoingiza fedha nyingi kwenye nchi, hivyo mpango wa muda mrefu unatakiwa kutengenezwa kutokana na hali ya mambo inavyokwenda kwenye hifadhi zetu, hasa kwenye kujenga mahusiano na jamii hizi zilizo kando kando ya hifadhi za wanymapori. Najua jambo hili litachukua muda mrefu mpaka lieleweke kwa watu hawa, lakini cha msingi tusiruhusu mila natamaduni za namna hii haziendelei kwa watoto wa jamii hizi maana hazina tija.

Cha msingi tunatakiwa kufikiria jinsi ya kujenga mfumo mzuri mapema sana dhidi ya jamii hizi, kama tumeshajua kuwa kinachosababisha mauaji ya wanymapori ni kitu fulani, ni rahisi kutengeneza kila nafasi ambayo itakuwa ni kulenga kudhibiti kuendelea kwa hali hii. Tunatakiwa kutengeneza mazingira imara na salama kwa pande zote, kwa watu na wanayamapori wetu. Hili ni jambo ambalo tunatakiwa kulifikiria kwa undani na upana wake, kwa maslahi ya sasa na miaka mingi ijayo. Hebu fikiria kidogo kwa hali ilivyo sasa kwenye maeneo mengi ya hifadhi na sehemu nyingine zilizohifadhiwa, watu wanalalamika na wanaona wanaonewa kwenye mali zao kutokana na wanyama ambao wao hawaoni faida inayotoka kwenye wanyama hawa, hali hii itaisha lini au ni njia gani za kumaliza mambo hayo.

Asante kwa kusoma makala hii

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

0742092569/0683248681

hillarymrosso@rocketmail.com