Kuna vitu vipo kwenye mazingira ya kawaida lakini watu wengi hatujui madhara yake mpaka ukitumie au kuona mwingine anakitumia. Uelewa wa kitu au vitu vilivyopo kwenye mazingira yetu unatupa uhuru wa kuvitumia vizuri. Kama usipoelewa uwepo wa kitu fulani hata matumizi yake yatakuwa ya kubahatisha na hapa ndipo kuna changamoto kubwa inayotukumba sisi wanadamu. Mfumo wetu wa maisha umetengenezwa kwa namna ya kujifunza mara zote kwenye kila mazingira na kitu tunachokutana nacho. Uzuri ni kwamba wale waliotangulia wanapojifunza na kuvitumia vitu vilivyopo kwenye mazingira yetu wameviandika na vipo kwenye maandishi. Hivyo ni kazi kwetu kujifunza na kuelewa kuwa ni kitu gani ambacho ni hatari na ambacho sio hatari.
Kwa maisha na mazingira ya porini mambo ni yale yale, kama unavyojua maisha ya porini yanaongozwa sana na kanuni za asili kabisa alizoziweka Mungu mwenyewe. Swala anajua kipi ni hatari kwake, nyani anajua kipi ni hatari kwake, duma anajua kipi ni hatari kwake, na pia wanajua kipi ni rafiki kwao, au kipi sio hatari kwao wanajua nini wale na nini wasile, kila kitu kwenye mazingira yao wanakielewa. Niseme tu kila kitu kinaeleweka kwa wanyama wa porini, mfumo wao wa maisha na mzingira yao ya kila siku. Ninachotaka kusema hapa ni kwamba kwa watalamu waliojifunza mambo ya wanyama na tabia za wanyamapori kwa muda mrefu wamekuja na vitu vingi sana ambavyo vinatusaidia kuboresha mahusiano yetu na wanyamapori, hii ni pamoja na kujifunza wanyama hawa na kuwaelewa vizuri, na kujua yupi ni hatari kwa binadamu na yupi sio hatari kwa binadamu.
Katika sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 imeeleza na kuwataja wanyamapori ambao ni hatari zaidi kwa binadamu, na pia hata kwa baadhi ya wanyama wengine. Wanyamapori hao wametajwa kwenye Jedwali la Nne, la sheria hii. Hivyo ni vizuri tukawataja hapa ili kila mtu anayekwenda au kutembelea porini ajue mazingira yapoje anapokutana na wanyama hawa.
Najua ni wanyamapori ambao wanafahamika na watu wengi sana, lakini sio watu wengi wanafahamu kuwa ni wanyama hatari kwa binadamu. Kwa hiyo sio wanyama wapya, ni wale wale tuliowazoea kuwasilikia lakini, ni wanyama wanaosababisha madhara kwa binadamu kuliko wanyama wengine. Pia ikumbukwe kuwa wanyama hawa ni wanyama pori, ni ngumu sana kuwazoea na hawazoeleki kirahisi hasa wakiwa kwenye mazingira yao ya asili. Hivyo ni jukumu letu kuchukua tahadhari mapema kuhusu wanyama hawa hatari.
Taarifa mbali mbali na kusikia na kuona mwenyewe watu wengi wamepoteza maisha yao kutokana na wanyama hawa, watu wengine ni wazoefu kwenye mapori lakini wanapokutana na wanyama hawa wanashindwa kufanya kitu, wangine wanaliwa na wanyama hawa kwa kutojali sheria au kupotezea ushauri wa wataalamu, wengine wameuwawa na wanyama hawa kwa kutokujua, wengine ni ajali kazini, wengine ni kutaka kupambana na wanyama hawa au anataka kuwafukuza pale wanyama hawa wanapokuja kula mazao, au mifugo yao, wengine wameliwa kutokana na ubishi, au kutembea ndani ya hifadhi kwa miguu bila usafiri, hizo ni baadhi tu ya sababu na mazingira yaliyopelekea watu kuliwa na wanyamapori.
Katika makala hii nitawataja wanyama hawa, kama walivyotajwa kwenye Jedwali la nne, nitawataja kwa majina yao yote ili tujifunze na tuyaelewe yote, kuna jina la Kiswahili, jina la kingereza na jina la kisayansi. Karibu tuwajue wanyama hatari zaidi waliotajwa kwenye sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009.
Jina la Kiswahili | Jina la Kingereza | Jina la Kisayansi |
Faru | Black Rhinoceros | Diceros bicorns |
Fisi | Spotted Hyeana | Crocuta crocuta |
Kiboko | Hippopotamus | Hippopotamus amphibious |
Mamba | Nile Crocodile | Crocodylus niloticus |
Nyati (Mbogo) | Buffalo | Syncerus caffer |
Simba | Lion | Panthera leo |
Tembo (Ndovu) | African Elephant | Loxodonta Africana |
Hawa ndio wanyamapori wenye madhara na hatari sana kwa maisha ya binadamu. Kuna wengine ni hatari ila hawa ndio wanaongoza kwa kuuwa watu. Ukifuatilia historia ya mauaji ya watu kutokana na wanyamapori utawaona wanyama hawa kwa kiasi kikubwa wanahusika. Hivyo unapokuwa porini au unapotembelea hifadhi au mbuga za wanyama ukiwaona wanyama hawa utaelewa somo zima tulilojifunza hapa.
Mwisho, nikushukuru kwa kuwa msomaji wa makala hizi muhimu ambazo tunajifuza kuhusu wanyamapori na mambo mengine mengi sana. Naamini baada ya kujifunza utapata uelewa ambao utakuwa msaada sio kwako tu bali hata kwa watu wengine, usiache kuwashirikisha wengine makala hii muhumu ili kwa pamoja tuzielewe na kuzitunza maliasili zetu.
Asante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 248 681/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania