Katika zunguka zunguka yangu kwenye mitandao nilijikuta nimeangukia kwenye misitu na mapori ya hifadhi ya jamii ya Ipole iliyoko huko Sikonge mkoani Tabora, nikajifunza na kukushirkisha moja ya makala niliyoiandika kuhusu eneo hilo la hifadhi ya jamii, ni moja ya kazi niliyoifanya jana. Lakini nilibahatika kutoka katika misitu hiyo inayosifika kuwa na ufugaji wa nyuki na asali na kuamua kutua katika mkoa mwingine na hapa nilijikuta natumia muda mwingi kwenye miji na vijiji vya mkoa huu. Huu ni mkoa wa Njombe, ndio ni mkoa wa Njombe maana kuna watu wengine hawajui kuwa huu ni mkoa, wanajua ni Wilaya tu ya mkoa wa Iringa, sasa kama ulikuwa hujui fahamu huu ni mkoa mkubwa na unaokua kwa kasi sana .
Watu wengi sana wanaufahamu mkoa wa Njombe kwa umaarufu wake wa kilimo, hasa cha mahindi na viazi. Baada ya kukaa chini na kuanza kujifunza taarifa za mkoa huu nilivutiwa na taarifa hizi, hizi ni taarifa zinazovutia na kushangaza kama sio za kuogopesha, baada ya kusoma katika mtandao mbali mbali na pia nilibahatika kusoma kwenye tovuti ya Bodi ya Ualii Tanzania na kupata hakika ya mambo niliyokuwa nayasikia na kuambiwa kuhusu mkoa wa Njombe. Hakika nilifanikiwa kuona kuwa mambo haya kweli yapo katika mkoa huu wenye watu wakarimu na wenye historia ndefu sana inayogusa mambo ya kitaifa na kimataifa.
Mkoa wa Njombe una hazina kubwa sana ya maliasili na vivutio vya kustaabisha na vingine vya kuogopesha. Nimeamini tunahitaji kujifunza nchi yetu kwa kina kwa sababu unaweza kuamini tu kwamba utalii Tanzania unategemea wanyamapori, lakini kwenye jambo hili ni zaidi ya wanyamapori, utalii wetu ni wa kila aina, kwa mkoa wa Njombe maisha na tamaduni za watu wa mkoa huu tu ni kivutio tosha kabisa, mabaki ya kihistoria na uwepo wa maajabu mengine ni baadhi tu ya vivutio vingi vilivyoko katika mkoa huu ambavyo havijulikani na watu wengi, hasa watanzania wenyewe.
Sasa ngoja tuone vivutio nane usivyovijua kuhusu mkoa wa Njombe. Mambo haya nane ni baadhi tu ya mambo mengine mengi yaliyopo kwenye makoa huu, hivyo tutajifunza hapa moja baada ya jingine.
1.Msitu wa Nyumba Nitu
Watu wa Njombe wanaufahamu vizuri sana msitu huu, lakini asilimia kubwa ya watanzania wengine hawaufahamu msitu huu, wanaweza wakawa wameusikia lakini hawajui ulipo. Kwa mkoa wa Njombe msitu huu ndio unaosifika kwa kuwa na mambo mengi ya kushangaza na kuogopesha. Huu ni msitu unaohusianisha historia ndefu sana ya mila na tamaduni za Wabena na Wahehe na watu wa mkoa wa Iringa. Ingawa kwa sasa mkoa huu unakaliwa na watu wa kabila la Wabena. Ni msitu ambao ulitumika kama sehemu za maficho kipindi cha vita vya Wabana na Wahehe na pia ni sehemu muhimu iliyotumiwa na wahenga kujificha kunapotokea vita vya mara kwa mara hasa kipindi cha ukoloni.
Nyumba Nitu, ikiwa na maana ya nyumba nyeusi ndani ya msitu huu kuna pango kubwa ambalo ndio hutumika kama eneo na sehemu ya maficho kipindi cha hatari. Msitu huu ni msitu wa asili kabisa na mapango yaliyopo humu ni ya asili hayajatengenezwa na mtu yeyote, ndani ya pango lililopo katika msitu huu kuna giza totoro. Msitu huu upo katika kijiji cha Mlevela kata ya Mdandu, kilomita 15 kutoka mji wa Njombe.
- Maporomoko ya maji ya Luhaji
Kwa wale wanaopenda maporomoko ya maji, basi hata Njombe yapo, maporomoko haya yaliyopo kwenye mji wa Njombe yanatokana na uwepo wa mto Luhaji uliopo Njombe. Sehemu hii imekuwa kivutio kikuu sana kwa wageni kutalii na kutembelea eneo hili, kupiga picha na pia mwonekano mzuri wa eneo hili umeifanya kuwa sehemu pekee inayovutia sana.
- Mawe ya Ajabu
Ndio ni mawe ya ajabu, mawe haya yamekua kivutio kukubwa sana kwenye mkoa huu wa Njombe. Mawe haya yanayongaa na kuzungukwa na uoto wa nyasi fupi yanapendezesha sana mkoa huu na kuwa kivutio kwa wengi. Inakadiriwa zaidi ya hakari 7 za eneo hili zimejaa mawe haya ya ajabu. Inapendeza sana hii ndio Njomne ya Tanzania bana.
- Makburi ya Mashujaa wa Kibena
Hii ni sehemu ambayo itavuta hisia na kufanya yale uliyokuwa unajifunza darasani kipindi upo shule kuwa halisi na kuona kweli kuna watu walijitoa kupigana na kutetea nchii hii hadi kifo, hili ni kaburi ambalo miili ya mamia ya mashujaa wa kabila la kibena walizikwa kwa pamoja baada ya kuuwawa kwenye vita vya maji maji miaka ya 1906. Na Kama unavyojua vita hivi vilipiganwa sehemu za Kusini mwa Tanzania, hivyo kati ya watu waliokuwa msitari wa mbele kwenye vita hivi walikuwa mashujaa hawa waliolala kwenye kaburi hili. Hii ni sehemu yenye mvuto sana kutokana na historia yake.
- Mjengo ya Zamani
Kutokana na sehemu hii ya Njombe kuwa na malighafi na rasilimali nyingi muhimu, Wajerumani waliamua kuweka makazi na majengo yao maeneo haya. Majengo ambayo yana miaka mingi sana ni majengo ya makanisa makubwa, kuna kanisa la Katoliki na Kanisa la Lutherani, kutokana kukaa kwa muda mrefu maeneo haya yamekuwa kivutio kwa watu wengi sana kutoka nje na dani ya nchi. Pia uwepo wa mahakama za kusuluisha masuala mbali mbali ya kiuongozi kipindi cha utawala wa wajerumani bado yapo hadi leo. Majengo haya yote ya kihistoria yapo katika mji wa Njombe.
6.Mashamba Makubwa ya Chai
Licha ya mambo mengi sana ya kihistoria yanayoifanya Njombe kuwa sehemu kuvutia kwa utalii, bado kuna sehemu kubwa sana za mashamba makubwa ya chai yenye historia ndefu sana tokea kipindi cha ukoloni. Mashamba haya yapo katika mkoa huu wa Njombe ndio mashamba makubwa sana kwa Nyanda za Juu Kusini.
- Pia uwepo wa Pori la Akiba ya Mpanga Kipengele na Hifadhi ya Taifa ya Kitulo.
Hii ndio Njombe bana, uwepo wa hifadhi za wanyama katika mkoa huu unafanya mkoa huu kuwa muhimu sana hasa kwenye ukuzaji wa pato la taifa kupitia utalii na matumizi mengine ya maliasili.
- Uwepo wa Ziwa Nyasa
Uwepo wa ziwa Nyasa katika sehemu ya mkoa wa Njombe ina maana kubwa sana kwenye maendeleo ya utalii katika mkoa huu. Ziwa hili ambalo lina hazina ya fukwe kubwa kwa ajili ya matumizi mbali mbali itasaidia sana kuinua uchumi kwa siku zijazo.
Hivyo basi, tumeona utajiri na rasilimali zilizopo katiaka mkoa huu wa Njombe, nyingi ya rasilimali hizi tulikuwa hatuzifahamu, lakini sasa tunazifahamu, kazi inabakia kwetu kuendelea kuzitunza na pia zinufaishe jamii na mkoa wote wa Njombe.
Ukiangalia kwa haraka utaona bado sana sehemu hizi hazijulikani kwa wageni na hata sisi wenyewe watanzania hatuzijui sehemu hizi. Ili kunufaika na rasilimali hizi zilizopo kwenye makoa huu zinahitajika juhudi za makusudi za kuutangaza mkoa wa Njombe kitaifa na kimataifa sambamba na kuhimiza uhifadhi wa rasilimali hizi adimu, pia endapo uhifadhi na utunzaji wa rasilimali hizi utafanyika kwa weledi Njombe inaweza kuingia kwenye orodha ya sehemu za urithi wa dunia, kazi ambayo inafanywa na Shirika la kimataifa linaloshughulikia Elimu, utamaduni na sayanisi (UNESCO).
Kazi ni kwetu sasa!
Kwa wale wanaovutiwa na mambo ya kihistoria na ya kitamaduni Njombe ndio sehemu nzuri sana ya kuanzia kwenda, kuna historia na visa vingi sana vipo kwenye mkoa huu, kwa hili tuanahitaji kuanza kulifanyia kazi sisi wenyewe. Naamini kabisa kutoka ndani ya moyo wangu, endapo umesoma makala hii hadi kufikia hapa utakuwa umehemasika na kutamani kwenda kujionea mwenyewe sehemu hii ya maajabu. Na endapo utafika mkoa wa Njombe basi utakuwa na ushuhuda mzuri ambao utawafanya wale ambao hawajawahi kwenda waende, hii ndio njia nzuri sana ya kukuza na kuinua utalii wa ndani.
Kwenye jambo kama hili tusiwategemee wazungu tu ndio waje waone vitu ambavyo sisi wenyewe hatujaviona. Tuanze sisi wafuate wao. Wala hili sio jambo gumu hata kidogo, linawezekana kabisa. Aisee! Natamani niendelee kuandika mambo haya lakini nitamaliza uhondo wote,
Ombi langu, uambie ushuhuda wako kama ulishatembelea Mkoa wa Njombe katika moja ya sehemu hizo nilizotaja na kuzielezea, andika hapa chini ya makala hii. Pia endapo una maswali, maoni, ushauri na hata mapendekezo wasiliana nami kwa mawasiliano hapo chini.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255742092569/ +255 683 862 481