Habari Rafiki, karibu tena kwenye makala ya leo ambayo tutaangazia maeneo yote ya Tanzania ambayo uwindaji unaruhusiwa kisheria. Kama tunavyojua Tanzania ni kubwa sana na imetenga maeneo mbalimbali yenye hadhi tofauti tofauti kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine muhimu kwa ajili ya sasa na vizazi vingi vijavyo. Maeneo hayo yamegawanyika katika sehemu kuu mbili, maeneo ambayo wanaruhusu uvunaji wa wanyamapori na maeneo ambayo hawaruhusu uvunaji wa wanyamapori. Maeneo ambayo uvunaji wa wanyamapori au uwindaji wa kitalii hauruhusiwi ni maeneo yote ya hifadhi za Taifa ambazo zipo 16. Ngoja tuangalia moja baada ya nyingine.

  1. Hifadhi za Taifa

Hifadhi za Taifa ndio sehemu ya uhifadhi wa wanyamapori ambayo uwindaji wa kitalii hautakiwi kabisa kwa mujibu wa sharia na pia sehemu ambayo inasimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania yaani TANAPA. Maeneo hayo ni pamoja na hifadhi za ; Mkomazi, Rubondo, Mikumi, Uduzungwa, Manyara, Gombe, Kitulo, Arusha, Tarangire,  Saanane, Sadani, Ruaha, Katavi, Kilimanjaro, Mahale na Serengeti. Maeneo haya nadhani umeshayasikia na kutembelea mengine. Maeneo haya ndio wanaruhusu ujenzi wa mahoteli kwa ajili ya wageni na pia utalii wa picha unaruhusiwa sana kwenye maeneo haya. Ni meaeneo ambayo usimamizi na ulinzi wa wanyamapori unafanyika kwa kiwango cha juu sana.

  1. Eneo la Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro

Hili ni eneo ambalo lipo kwa mujibu wa sharia za wanyamapori, ni eneo lenye wanyamapori wengi na vivutio vingi sana vya kiasili na vya wanyamapori. Eneo hili ni moja ya maajabu nane ya dunia kutokana na idadi ya vivutio vingi vilivyopo kwenye eneo hili. Ndani ya eneo hili la Ngorongoro shughuli za kibinadamu zinaruhusiwa, shughuli kama ufugaji na kilimo vinafanyika ndani ya hifadhi hii, na watu wazawa wa eneo hilo wengi wao wakiwa ni wafugaji wa Masai wanaishi ndani ya eneo hili na mifugo yao, huku shughuli za uhifadhi wa wanyamapori ukiendelea humo humo. Eneo hili lipo chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, na sio chini ya TANAPA kama wengi wanavyofikiri. Kwenye eneo hili shughuli za uwindaji wa kitalii haziruhusiwi kabisa. Utalii wa picha ndio unaruhusiwa kwenye eneo hili, pia kuna mahoteli na mabanda ya hadhi za kulala watu mbali mbali.

  1. Mapori ya Akiba, Mapori tengefu, Maeneo ya Hifadhi ya Jamii na Mapori ya Wazi

Haya ni maeneo mengine yanayomilikiwa na kusimamiwa na serikali kupitia idara ya wanyamapori Tanzania. Idara hii inaitwa Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori Tanzania – TAWA. Hawa ndio wanaosimamia mapori yote ya akiba na maeneo yote ya hifadhi ya wanyamapori Tanzania. Kwenye maeneo haya shughuli za utalii wa picha hufanyika sambamba na shughuli za utalii wa uwindaji. Haya ndio maeneo ambayo unaeza kuomba kufanya uwindaji na pia unaweza kuomba kuwa mmiliki wa kitalu au vitalu vya uwindaji. Maeneo haya ni mengi sana. Kwenye mapori ya akiba kama Selous, Burigi, Grumeti, Ibanda, Ikorongo, Kigosi, Kigereshi, Kimisi, Rukwa,Swagaswaga, Uwanda, Muhesa, Msanjes, Moyowosi, Maswa nk.

Maeneo mengine ya mapori ya akiba ambayo yanaendesha utalii wa uwindaji ana picha ni maeneo Tengefu, au mapori Tengefu mfano wa maeneo haya ni; Mlele, Msima, Mto wa Mbu, Simanjiro, Ugunda, Nchwa nkima, Makao, Lugazo, Longido, Loliondo, Burunge, Gombe nk. Maeneo haya yapo kila kona ya Tanzania.

Pia mapori ya hifadhi ya jamii kama WMAs, yapo mengi sana Tanzania hivyo unaweza kufanya uwekezaji kwenye maeneo haya kwa kuwasiliana na serkili ya Kijiji au wilaya maeneo mfano wa maeneo haya ni; Enduimeti, Ikona, Makame, Mbarang’ande, Ng’arambe- Tapika, Liwale, Ipole, Pawaga – Idodi ,nk. Hivyo ni maeneo ambayo unaweza kuomba kumiliki kitalu hata kuendesha biashara za uwindaji wa kitalii Tanzania.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania