Habari za mapumziko ya mwisho wa wiki ndugu msomaji wa makala hizi za wanyamapori. Ni matumaini yangu hujambo kabisa na umekuwa na mapumziko mazuri ya mwisho wa wiki na kuburudika kwa amani sana, Basi kama ilivo kawaida yangu nami nazidi kukuongezea furaha ya mwisho wa mapumziko ya wiki kwa kukuletea makala hii kuhusu wanyamapori na ujifunze machache kuhusu wanyama hawa. Leo tutamuweka mezani mnyama mwingine tena kama ilivo kawaida mwisho wa makala ilopita hutufungulia fursa ya kuwajua wanyama qwengine kwa ufasaha zaidi. Endelea kuwa name ili ujifunze mengi kuhusu wanyama hawa. Na leo moja kwa moja tutamzungumzia mnyama aitwae “PAA au SWALA PAA”

Kabla ya kuendelea napenda ndugu msomaji ujue kuwa kuna Paa wa aina mbili ambao ni

1.Swala paa wa kawaida na

2.Swala paa mwenye uso mweusi.

Sasa leo tutamzungumzia Swala Paa  mwenye uso mweusi

 

UTANGULIZI

Paa ni wanyama ambao wapo kwenye kundi la wanyama jamii ya swala. Kama utakuwa mfuatiliaji wa makala hizi nadhani utakuwa unajua baadhi ya wanyama ambao wapo kwenye kundi hili la wanyama wajulikanao kama swala kwani nimewahi wataja kwenye makala mbalimbali katika mfululizo wa makala hizi. Sasa leo tutamzungumzia mnyama Swala Paa au kwa klifupi Paa.

SIFA NA TABIA ZA PAA(PAA MWENYE USO MWEUSI)

1.Wana manyoa yenye rangi ya kahawia mchanganyiko na wekundu huku maeneo ya tumboni kwa chini wakiwa na rangi ya kupauka.

2.Ukiwachunguza vizuri utagundua wanyama hawa wana alama nyeusi katika maeneo ya kiunoni na mkiani.

3.Wana alama nyeupe kwa juu ya macho na sehemu ya upande wa chini wa mkia pia utaona alama hii nyeupe.

4.Wana matezi ya harufu katika miguu ya nyuma na sehemu ya mbele kichwani.

5.Ni wanyama wenye uwezo wa kutoa sauti hasa dume hali kadhalika na watoto pia pale wanapohisi hatari au kumuona adui.

6.Wanapo muona adui huanza kurukaruka na sababu ya kufanya hivi ni kumuonesha adui kuwa wako vizuri na adui asijaribu hata kuwafuatilia.

7.Ni wanyama wenye uwezo wa kutunza sana muda majira ya mchana na kipindi jua linakaribia kuzama na muda huu huutumia kwa kula na kutafuta maji.

8.Huishi kwa makundi na kundi huwa na Paa 100 hadi 200 hususani kipindi cha ukame. Kipindi hiki makundi madogo madogo hujikusanya pamoja na kuanza kutafuta chakula wakiwa pamoja. Inapofika kipindi cha chakula cha kutosha basi makundi haya hutawanyika na kila kundi huwa na mtawala mmoja ambae ni dume.

9.Dume huwa na pembe wakati majika huwa hawana pembe kabisa.

10.Ni wanyama wenye uwezo wa kukimbia kwa kasi kubwa sana na wana uwezo wa kukimbia hadi kilomita  60km kwa saa. Wanapo kuwa wanakimbia huweza kuruka juu hadi futi 7 na kuendelea.

11.Dume anapokuwa mtawala wa kundi la majike huwalinda na kuweka alama katika himaya yake kwa kutumia mkojo na kinyesi.

12.Wana rangi nyeusi katika paji la uso na hii hasa ndio huwa tofautishwa aina hizi mbili za Swala paa.

UREFU, KIMO NA UZITO

Urefu=Paa huwa na urefu wa hadi futi 3.5 – 5. Na mkia huwa na inchi 10 – 16

Kimo=Hufikia kimo cha  futi 2.5 – 3.1

Uzito=Paa hufikia uzito wa kilogramu 40kg – 65kg.

MAZINGIRA

Paa ni wanyama ambao wanapendelea maeneo yenye savanna, miti miti na majani ambayo pia yapo karibu na maji pia. Wanyama hawa hupatikana barani Afrika tu na wameenea katika nchi mbalimbali kama Tanzania, Kenya, Uganda, Angola,  Botswana, Afrika Kusini, Namibia na kwengineko.

CHAKULA

Paa ni miongoni mwa wanyama walao majani na kutokana na mazingira wanayoishi ni wanyama wenye uwezo wa kula majani ya juu na chini pia. Hula pia mizizi, na baadhi ya matunda.

Wanapokuwa wanakula huwa wanajitahidi kutafuta maji pia kwani hawa ni wanyama ambao hupenda kunywa maji karibu kila siku.

KUZALIANA

Kabla ya kuwa mtawala wa kundi la majike huwa kuna pambano kubwa sana kati ya madume na dume anaeshida katika kupigana ndiyo huwa mtawala wa kundi la majike hao. Mara tuu baada ya kutawala majike hao dume huweka mipaka katika himaya yake kwa kutumia mkojo na kinyesi ili madume wengine wasiingie katika himaya yake.

Hutumia muda mwingi kuwalinda majike wasiondoke na kuwakusanya kila wakati. Wakati huu dume hupunguza hata muda wa kula kwani huwa na kazi ya kulinda majike tu wasimtoroke.

Mara nyingi Paa hupanda majike kipindi cha mwezi wa tatu hadi wa tano na hapo majike karibuni wote hubeba mimba kwani dume huwa na uwezo wa kupanda majike wengi sana kwa kipindi kifupi. Paa jike hubeba mimba kwa muda wa siku takribani 194 – 200 (sawa na miezi sita na zaidi).

Mara baada ya kipindi hiki cha mimba paa anapo karibia kuzaa hujitenga kwenye kundi la wenzie na kutafuta sehemu salama kwa ajili ya kuzaa. Huzaa mtoto mwenye uzito wa takribani kilogramu 5kg na hukaanae karibu ili kumlinda kutokana na maadui. Mtoto anapoanza kuchangamka baada ya siku chache hujiunga na kundi la watoto wenzie ili kuanza kujifunza mambo mengine hususani kuishi kwenye kundi.

Watoto wa kiume wanapo fikia umri wa kuweza kupanda majike hasa wafikishapo mwaka mmoja hufukuzwa kwenye kundi na hivyo kulazimika kuunda kundi lao. Katika kipindi chote hiki madume hawa huwa hawawezi kupanda majike japo wamefikia umri wakufanya hivyo na hii ni kwasababu huwa hawana uwezo wa kupigana na madume wakubwa ili kutawala kundi la majike. Paaa majike huweza kuzaa mara wafikishapo umri wa mwaka mmoja na nusu. Swala ni miongoni mwa wanyama wenye kuzaliana kwa kasi kubwa sana.

Paa wanapouwa katika mazingira yao asili hususani katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori huweza kuishi myaka 10 hadi 15. Apo anapokuwa anafugwa huwezakuzidi umri huo.

UHIFADHI

Kutokana na maelezo ya Shirika la umoja wa mataifa linalo shughulika na uhifadhi wa maumbile Asili (International Union for Conservation of Nature – IUCN) wanyama hawa bado hawajawa hatarini kutoweka duniani.

Takwimu zao zinaonesha kuwa kuna zaidi ya Paa milioni 2 na katika idadi hiyo asilimia 50% wapokatika maeneo ya ardhi binafsi, 25% wapo katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori na 25% wametawanyika maeneo mbalimbali. Hii inafanya shirika hili kuona wanyama hawa idadi yao ipo vizuri na wanaongezeka kwa uelekeo mzuri.

MAADUI NA TISHIO KWA PAA

Maadui wakuu wa Paa ni binaadamu, simba, chui, duma,mbwa mwitu pamoja na baadhi ya jamii nyingine za wanyama wala nyama.

Moja kati ya matishio makubwa sana kwa Paa ni ujangili ulio kithiri katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori hasa kutokana na matumizi ya nyama pamoja na biashara haramu za wanyamapori na malighafi zao. Watu wamekuwa wakiwawinda sana wanyama hawa na kusababisha waishi kwa wasiwasi sna katika maeneo yao.

Uharibifu wa mazingira umepelekea sana kuharibika kwa mahitaji ya kiikolojia ya wanyama hawa nakusababisha wahame au kutembea umbali mrefu sana kwa ajili ya kutafuta mahitaji muhimu sana hivyo kupata shida sana.

Uzuiaji wa varanda au mapitio ya wanyamapori kutokana na uvamizi wa watu kutafuta makazi katika mapitio ya wanyamapori. Hii imesababisha wanyama hawa kushindwa kutawanyika katika baadhi ya maeneo ambayo kwa hakika walikuwa wakitembelea sana hapo zamanai kabla ya uvamizi wa maeneo hayo.

Jamii ya wafugaji pia imekuwa ni tatizo kubwa sana kwa kuingiza mifugo ndani ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori kwani wanyama hawa wamekuwa wakilazimika kugombania majani na Paa hivyo kufanya chakula kupungua kwa upande wa Paa.

NINI KIFANYIKE KUTATUA MATISHIO HAYA KWA PAA

Kuhakikisha na upambanaji wa matukio ya ujangili kwa kuishirikisha jamii ili kuwafichua majangili mahali walipo kwani wengi wao tunaishi nao katika jamii zetu.

Wizara husika hasa wizara ya maliasili na utalii na wizara ya mazingura ili kuhakikisha kuna utekelezaji wa sheria za mazingira ili kunusuru uharibifu wa mazingira kwa wanyama hawa na wengine waishio katika mazingira asili.

Serikali ihakikishe inawataftia watu makazi hasa wale walovamia maeneo ya mapitio ya wanyamapori kwani limekuwa ni tatizo kubwa sana na kufikia hatua wanyama kuwa na maeneo madogo ya kutawanyika.

Kuna maeneo mengi sana hapa nchini yana chakula cha kutosha kwa mifugo hivyo basi jamii za wafugaji zitafutiwe maeneo kama haya ili waweze kuondoka karibu na maeneo ya hifadhi za wanyamapori na kupunguza adha ya magonjwa lakini pia vifo kwa mifugo kwani wanyamapori wana stahimili magonjwa kuliko mifugo.

HITIMISHO

Wanyama hawa wanahitaji kutunzwa sana kwani ni rasilimali kubwa sana hasa hapa kwetu Tanzania kwani wamekuwa na mchango mkubwa sana katika pato la taifa letu. Jambo la kushukuru ni kwamba wanyama hawa bado hawajawa hatarini kutoweka na tuna deni kubwa sana kuhakikisha wanaendelea kuwepo na kwa mazingira bora ili wendelee kuzaana vizuri.

Tutambue kwa dhati mchango wa mashirika yanayo saidia katika uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini hususani TANAPA, TAWA, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro-NCCA kwa kazi kubwa sana wanayoifanya katika

kuhakikisha wanyama hawa wanaendelea kuwepo katika hifadhi zetu za wanyamapori.

Nasi kama jamii ambayo tunafaidika kupitia uhifadhi wa wanyama hawa hatunabudi kuwaunga mkono wale wote wanao jitolea kwa hali na mali kulinda rasilimali zetu zisitoweke kwani uwepo wa rasilimali hizo unalipataifa sifa kubwa sana dhidi ya mataifa mengine.

Kumbuka kauli hii “HUWEZI ONA THAMANI YA KITU MPAKA PALE KITAKAPO TOWEKA”

AHSATENI

Endelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi ndugu msomaji ili uweze kujifunza mengi kuhusu wanyamapori na maendeleo ya uhifadhi wa wanyama hawa.

Kwa maoni, ushauri na mengine mengi kuhusu makala hizi wasiliana na mwandishi kupitia

Sadick Omary

Simu= 0714 116963/0765 057969/0785 813286

Email=swideeq.so@gmail.com

Au tembelea= www.mtaalamu.net/wildlifetanzania

”I’M THE METALLIC LEGEND”