Habari za mwisho wa wiki ndugu zangu wasomaji wa makala za wanyamapori. Siku zote huwa nasema upatapo wasaa wa kufanya shughuli zako huku ukiwa na afya basi huna budi kumshukuru Mwenyezimungu kwa huruma yake kukupa njema. Na kama kawaida mwisho wa makala iliyopita ndo mwanzo wa makala nyingine huku tukiendelea kujuzana mengi kuhusu wanyamapori, uhifadhi wao hali kadhalika uelekeo wa wanyama hawa duniani kote kwaujumla.
Katika makala ya leo nitaendelea kukujuza machache na yenye faida kuhusu wanyama jamii ya paka. Na kwa kusema hivi basi niwazi kabisa makala ya leo tutamuelezea mnyama ambae yupo kwenye kundi la wanyama jamii ya paka kwani kama nilivo tangulia kusema kwenye makala iliyopita kuwa kundi hili lina wanyama wengi japo halijafikia lile la swala.
Bila kupoteza muda makala ya leo tutamjua mnyama ajulikanae kama “SIMBAMANGU” ambae kwa lugha ya kiingereza hujulikana kama “CARACAL”. Basi nikusihi endelea kuwa nami mwanzo mpaka mwisho wa makala hii ili uweze kujifunza mengi ambayo ulikuwa huyajui kuhusu mnyama huyu adimu sana na mwenye sifa kemkem zenye kuvutia.
UTANGULIZI
Simbamangu ni miongoni mwa wanyama jamii ya paka ambao mazingira yao asilia ni porini. Wanyama hawa wanapatikana maeneo mengi sana hapa barani Afrika na maeneo machache ya bara la Asia. Hawa ni miongoni mwa wanyama wenye aibu sana hivyo kuwaona kwao huwa ni kwa kubahatisha sana.
Jina la wanyama hawa asili yake limetokana na lugha ya kituruki “karakulkak” likiwa na maana sikio leusi. Miaka ya nyuma wanyama hawa walikuwa wanapata mafunzo kwaajili ya ukamataji wa ndege hasa njiwa katika nchi za India na Iran. Walikuwa wanawekwa eneo lenye njiwa wengi kisha wanaanza kufundishwa namna ya kukamata njiwa hao.
Kusema kweli wanyama hawa wanavutia sana hasa wawapo katika mazingira yao asili kutokana shughuli zao za kila siku. Wanyama hawa wamekuwa pia na umuhimu mkubwa sana katika ikolojia kwenye mazingira wanayoishi kutokana na uwindaji wao lakini pia hata vinyesi vyao kwa ukuwaji wa mimea ambayo hutumiwa kama chakula na maeneo ya kujifichia kwa wanyama wengine.
SIFA NA TABIA ZA SIMBAMANGU
Simbamangu ukiwatazama usoni wana alama nyeusi na nyeupe maeneo yanayo zunguka macho na midomo yao huku sehemu ya mashavuni wakiwa na alama nyeupe sehemu ya mashavu kwa chini.
Wana masikio marefu na yaliyo chongoka huku sehemu ya nchani masikio yao yako manyoa manene na marefu yenye rangi nyeusi na yaliyo chongoka. Sehemu ya nyuma ya masikio yao wana rangi nyeusi ambayo imechanganyikana na manyoa meupe madogo madogo.
Miguu yao ya nyuma ni mirefu kidogo kiliko ya mbele. Sifa hii huwafanya wanyama hawa wanapokuwa wamesimama kuonekana kama wameinamia sehemu ya mbele zaidi.
Wana mikia mifupi hasa ukilinganisha na maumbile au urefu wa miili yao na nchani ikiwa butu haija chongoka kama walivyo wanyama wengine wengi jamii yap aka.
Miili yao ina manyoa mafupi, nyororo yenye rangi iliyo kolea. Rangi zao huwa zina shabihiana na njano inayo fanana na kahawia, wekundu uliyo pauka au rangi ya tofali la kuchoma na wakati mwingine huonekana kama rangi ya kijivu au mchanga.
Sehemu ya chini ya miili yao wana rangi nyeupe. Simbamangu ni miongoni mwa wanyama wachache jamii yap aka ambao miili yao haina madoa madoa au mistari.
Simbamangu ni wanyama ambao huishi kwa kujitenga hasa kwenye himaya. Ni mara chache sana kuwakuta wakiwa zaidi ya mmoja na ukiwakuta hivyo basi ujue ni kupindi cha kuzaliana.
Hawa ndio paka wakubwa kwenye kundi la wanyama jamii ya paka wenye maumbo madogo. Wanyama jamii ya paka wamegawanyika katika makundi mawili kutokana na maumbile yao, yaani paka wakubwa na paka wadogo.
Katika wanyama jamii yap aka wadogo, simbamangu ndio paka wenye nguvu kuliko paka wengine wote walio salia kwenye kundi hili la paka.
Simbamangu wanauwezo wa kuona zaidi usiku kuliko mchana, hivyo shughuli zao nyingi huzifanya majira ya usiku. Japo kwenye baadhi ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori wanyama hawa wamekuwa wakionekana kuwinda hata majira ya mchana mara chache.
Wana uwezo mkubwa sana wa kuruka hewani na warukapo, simbamangu wana uwezo wa kukamata au kujeruhi ndege 10-12 kwa wakati mmoja. Hii inaonesha ni kwa jinsi gani wanyama hawa wana uwezo mkubwa sana kwenye uwindaji.
Wana uwezo mkubwa sana wa kusikia na kuona. Mawasiliano kati ya wanyama hawa huwa wana tumia sauti mbalimbali hawa baina ya mama na watoto au dume na jike unapofika msimu wa kuzaliana.
Simbamangu ni miongoni mwa wanyama wenye uwezo mkubwa wa kukimbia. Na wana kadiriwa kuwa na uwezo wa kukimbia hadi kilomita 80 kwa saa moja.
Madume huwa na miili mikubwa kidogo kuliko na majike.
KIMO, UREFU NA UZITO WA SIMBAMANGU
Kimo= Simbamangu huwa na kimo cha wastani wa sentimita 40-50.
Urefu= huwa na urefu wa wastani wa sentimita 73-78.
Uzito= Simbamangu mkubwa hufikia uzoto wa kilogramu 8-18.
MAZINGIRA
Wanyama hawa kama nilivyo tangulia kusema hapo juu wanapatikana maeneo mengi hapa barani Afrika isipokuwa maeneo ya Sahara ya kati na maeneo yenye misitu mingi hasa Afrika ya magharibi lakini pia wanapatikana sehemu ya bara la Asia. Hii ni kutokana na wanyama hawa kuwa na uwezo wa kuishi katika mazingira mbalimbali.
Mazingira wapendeleayo wanyama hawa ni pamoja na mazingira ambayo yana miti mingi, maeneo yenye vichaka na misitu midogo midogo na maeneo yenye miamba. Lakini maeneo ambayo ni pendeleo zaidi kwa wanyama hawa ni maeneo ya savanna kavu na maeneo yaliyo na tambarare na yenye nyasi nyasi ambazo hazija fungamana sana zenye kutoa nafasi kwa wanyama hawa kuona mbali.
CHAKULA
Nilitangulia kudokeza hapo juu kuwa wanyama hawa ni miongoni mwa jamii ya wanyama walao nyama. Hivyo zaidi ya asilimia 90 ya chakula cha wanyama hawa ni nyama. Miongoni mwa viumbe au wanyama wawindwao sana na simbamangu ni pimbi, sungura, swala wadogo kama digi digi, panya, ndedere wadogo na ndege.
Mfumo wa umeng’enyaji wa chakula wa wanyama hawa hauna uwezo wa kumeng’enya manyoa. Hivyo huwalazimu wanyama hawa kuondoa manyoa katika mawindo yao kabla ya kula kwa kutumia makucha yao makali.
Wanyama hawa huwa hawanywi maji mara kwa mara kwani hupata maji kutokana na aina ya vyakula wanavyo kula. Hivyo hii huwafanya wanyama hawa kuwa na uwezo wa kuishi muda mrefu sana bila hata kunywa tone la maji.
KUZALIANA
Wanapotaka kuzaliana au msimu wa kuzaliana ndipo unaweza kuwakuta wanyama hawa jike na dume wakiwa pamoja na wanyama hawa wana uwezo wa kuzaliana majira yoyote ya mwaka lakini mara nyingi wameonekana kupandana kati ya mwezi wa 8 na 12. Simbamangu wana sifa ambayo huweza kuwa tofautisha na wanyama wengine jamii ya paka hasa kwenye suala la kuzaliana. Wanyama hawa sifa yao ni kwamba dume mmoja ana uwezo wa kupanda majike zaidi ya mmoja kama ilivyo kwa jike nae pia ana uwezo wa kupandwa na dume zaidi ya mmoja kwa muda huo huo ambapo anakuwa kwenye kipindi cha kubeba mimba.
Mara baada ya kupandana jike hubeba mimba kwa muda wa siku 78-81 na baada ya hapo huzaa watoto 1-4 japo wastani mkubwa sana huwa wana zaa watoto 2. Mara nyingi jike huzalia kwenye mapango, sehmu ya miti au mashimo yaliyo achwa na wanyama wengine kama mhanga. Watoto huweza kufumbua macho siku hiyo hiyo wanayo zaliwa japo huchukua siku 1-6 ili kuweza kuona vizuri kabisa. Watoto huwa chini ya uangalizi wa mama kwa muda usio pungua wiki 10, na kwa kipindi chote hiki mama hulazimika kuwahamisha watoto mara kwa mara ili kuwakinga dhidi ya maadui. Watoto hawa huwachini ya uangalizi wa mama kwa muda wa mwaka mmoja.
Simbamangu huwa na uwezo wa kuanza kuzaliana wafikishapo umri kati ya miezi 12-16 na kwa wakati huu huwa tayari wanaishi maisha ya kuji tegemea tofauti na kumtegemea mama kwani ndani ya mwaka mmoja tu mama hulazimika kuwafukuza watoto na kujiandaa kuzaa tena.
Maisha ya simbamangu wawapo katika mazingira yao asilia huwa ni myaka 19 japo kama wanafugwa kwenye bustani za wanyama huweza kuzidi umri huo.
UHIFADHI
Tafiti zinaonesha kuwa idadi ya wanyama hawa bado ni ya kuridhisha hivyo bado hawajawa hatarini kutoweka duniani. Maeneo ya kusini mwa Afrika na mashariki mwa Afrika wanyama hawa wamekuwa wakionekana kwa wingi na idadi yao ina ridhisha. Kwa maeneo ya magharibi na kaskazini mwa Afrika wanyama hawa wameanza kuwa adimu hivyo kuna changamoto zinazo wakumba wanyama hawa katikamaeneo hayo. Na hii ni kutokana na tafiti iliyo fanyika mwaka 2013 iliyo chapishwa na shirika la umoja wa mataifa linalo shughulika na uhifadhi wa maumbileasili (International Union for Conservation of Nature-IUCN).
Baadhi ya maeneo ya Asia hasa nchi kama India na Iran wanyama hawa wamekuwa wakipungua sana hali ambayo inatishia sana uwepo wa wanyama hawa katika maeneo hayo. Nchini Uturuki simbamangu ni wanyama ambao wapo kwenye orodha ya wanyama wanao karibia kutoweka nchini humo.
Kuna changamoto nyingi sana zinazo wakumba wanyama hawa japo tumeona hapo juu kuwa idadi yao inaridhisha kwa takwimu za ulimwenguni kote. Hapa Tanzania hatuna budi kujisifu kwakuwa idadi ya wanyama hawa ina ridhisha nah ii ni kutokana na usimamizi mzuri wa sheria na uhifadhi wa wanyamapori.
CHANGAMOTO NA TISHIO KWA SIMBAMANGU
Uharibifu wa mazingira, hili ndio tatizo kubwa sana linalo pelekea wanyama hawa kutoweka baadhi ya maeneo. Uharibifu wa mazingira umepelekea wanyama hawa kupungua baadhi ya maeneokutokana na upungufu wa chakula lakini pia maeneo yao ya kuzaliana yamekuwa yakiharibiwa sana hali ambayo inafanya wanyama hawa kuyakimbiamaeneo hayo na kutafuta maeneo mengine.Hali hii inasababishwa na ufugaji karibu au ndani ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori, uvunaji wa rasilimali misitu na maendeleo ya miji.
Wanyama hawa wamekuwa wakiuwawa sana na jamii za wafugaji kutokana na kuliwa kwa mifugo yao kama mbuzi, kondoo na kuku. Hali hii huwafanya wafugaji kuwauwa simbamangu kwa mishale au sumu hali ambayo inapelekea wanyama hawa kupungua siku hadi siku na tusipokuwa makini wanyama hawa watakuwa hatarini kutoweka baadhi ya maeneo hapa nchini Tanzania.
Simbamangu wamekuwa wakiuliwa kwa ajili ya biashara ya nyama na manyoa au ngozi zao. Baadhi ya wana kijiji au hata kwenye nchi zilizo endelea wanyama hawa wamekuwa wakitumiwa kama kitoweo huku ngozi zao hutumika kama vazi au mapambo ya kifahari. Hili limepelekea biashara haramu ya wanyamapori kukua kwa kiasi kikubwa katika maeneo hayo kitu ambacho kina sababisha wanyama hawa kupungua sana.
NINI KIFANYIKE KUWALINDA SIMBAMANGU HASA HAPA NCHINI TANZANIA
Kupambana na uharibifu wa mazingira kwani tumeona hapo juu hili ndo tatizo kubwa sana ambalo linapelekea wanyama hawa kupungua au kuyahama maeneo yao asilia kutokana na ukosefu wa mahitaji yao unao sababishwa na uharibifu wa mazingira.
Wizara ya maliasili kwa kushirikiana na wizara ya mifugo na uvuvi kufuatilia changamoto za wafugaji ambao wanaingiza mifugo yao maeneo tengefu ya hifadhi za wanyamapori. Sheria kali zitumike na kufuatiliwa kwa ukaribu zaidi ili kutokomeza kabisa tabia hii ya wafugaji kuingiza mmifugo yao katika maeneo hayo.
Kuongeza idadi ya askari wa wanyamapori ili kupambana na majangili ambao wamekuwa waki wawinda wanyama hawa kwaajili ya nyama. Niwazi kwamba idadi ya askari ikiwa ya kutosha basi majangili hawatakuwa na nafasi ya kuingia hifadhini na kuwawinda wanyama hawa. Hili lime jidhirisha kwenye upambanaji wa ujangili dhidi ya tembo na wote tumeona kwasasa umepungua sana na tembo wanazidi kuzaliana kwa wingi hapa nchini.
Kuzuiya biashara ya wanyama hawa mpaka pale wizara itakapo jiridhisha kuwa idadi ya wanyama hawa inaridhisha na wanaweza kuruhusu uwindwaji wao. Kulifanya hili serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii hainabudi kuzuiya leseni na vibali vyote vya uwindaji wa wanyama hawa kwa wale walionavyo mpaka pale takwimu halisi kuhusu wanyama hawa zitakapokuwa zimetolewa.
Utoaji wa elimu juu ya uhifadhi na umuhimu wa wanyamapori hapa nchini. Hili nimekuwa nikilisisitiza sana kwenye makala mbali mbali kwani ili tuweze kuwa na mafanikio makubwa kwenye suala la uhifadhi basi jamii ni ya kwanza kabisa kushirikishwa. Lakini pia serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii na wizara ya elimu, sayansi na mafunzo ya ufundi iandae mitaala ya elimu kuhusu uhifadhi wa wanyamapori kuanzia ngazi ya elimu ya msingi mpaka sekondari ili kupata mabalozi wengi watakao kuwa na moyo wa kusimamia rasilimali zetu za wanyamapori hapa nchini.
HITIMISHO
Siku zote huwezi kuona thamani ya kitu mpaka pale utakapo kipoteza. Kwasasa idadi ya simbamangu hapa nchini ina ridhisha sana hivyo hatuna budi kuendelea kupambana kuhakikisha wanyama hawa wanaendelea kuwepo tena kwa idadi kubwa zaidi kwa faida ya vizazi vijavyo Kuna baadhi ya nchi wanyama hawa wapo hatarini kutoweka kama nilivosema hapo juu lakini nchi kama Burundi wanyama hawa inasemekana huenda wakawa wametoweka mana ni muda mrefu tangu kuonekana kwao nchini humo.
Napenda kuwapongeza TANAPA, TAWA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCCA) kwa kazi kubwa sana na jitihada mnazo zionesha katika suala zima la uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yao hapa nchini. Mbali na changamoto mnazo pitia katika kutimiza majukumu yenu ila hamjakata tamaa ili tu kuhakikisha wanyamapori wanaendelea kuwepo hapa nchini. Kuna baadhi ya askari wana jeruhiwa na majangili lakini hata wanyama pia ila bado mnaendelea na utekelezaji wa majukumu yenu bila hofu.
Pongezi pia kwa waziri wa malliasili na utalii Mh. Hamisi Kigwangala kwa kazi kubwa sana unayoifanya kupitia wizara yako. Mfano mzuri ni kampeni ya kulinda tembo uliyo iongoza hasa kusini mwa Tanzania katika pori la akiba la Selous tumeona matunda ya kampeni ile na tembo wetu kwa sasa wapo kwenye ulinzi na mazingira tulivu kabisa.
Na sisi kama jamii au wadau wa uhifadhi tutazidi kushirikiana na nyie kwa pamoja kulisukuma gurudumu hili la uhifadhi ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi ambayo kila nchi duniani inaizungumzia kutokana na uwepo wa wanyamapori wakutosha na mazingira salama kwaajili ya utalii.
………MWISHO……….
Endelea kufuatilia makala hili ili uweze kujifunza mambo mengi sana kuhusu wanyamapori.
Kwa ushauri, maswali au maoni kuhusu makala hizi au kujua mengi kuhusu wanyamapori basi usisite kuwasiliana nami kupitia mawasiliano yafuatayo:
Sadick Omary Hamisi
Simu= 0714116963/0765057969
Email= swideeq.so@gmail.com
Instagram= wildlife_articles_tanzania
Facebook= Sadicq Omary Kashushu
Au tovuti= www.wildlifetanzania.home.blog
……………….”I’M THE METALLIC LEGEND”………..