Ndugu wasomaji wa makala hizi za wanyamapori, kama ilivo kawaida yetu tunapo pata wasaa kama hivi basi hatuna budi kujuzana machache na yenye thamani kubwa sana kuhusu wanyamapori hususani hapa nchini kwetu Tanzania. Basi kama kawaida leo tena tuta jifunza mambo machache na nikusihi kuisoma makala hii kwa undani zaidi kwani ina utofaiti kidogo na makala zilizo pita.

Katika makala takribani mbili mpaka tatu nilianza kuelezea aina mbalimbali za ndege hasa wapatikanao hapa nchini Tanzania na tulijifunza mengi sana kupitia makala hizo. Makala ya leo haitokuwa nje ya ndege ila kama nilivo tangulia kudokeza hapo juu, makala hii itakuwa tofauti kidogo kwani itaelezea matukio ambayo mimi kaka muhifadhi na muandishi nimekutana nayo hivi punde katika shughuli zangu za kila siku.

Katika makala ya leo nitaelezea machache niliyo kutana nayo na changamoto zinazo wasibu ndege aina ya Heroe (Flamingo) wanao patikana mkoani Manyara, wilaya ya Hanang, tarafa ya Balangda katika ziwa Balangda.

Naendelea tena kukusihi kuisoma makala hii kwa umakini sana na utulivu ili uweze kutambua na kuelewa mausdhui ya makala hii kwani kwa kuelewa kwako ndugu msomaji unaweza kuwa ni miongoni mwa mabalozi wazuri ambao watasaidia katika uhifadhi na ulinzi wa ndege hawa ambao wanakumbwa na changamoto nyingi sana kwenye mazingira wanayo ishi.

Picha hii inaonyesha ndege aina ya Heroe au kama wengi wananyowafahamu kama Flamingo. Picha hii imepigwa na Andey Gudkov

 Heroe ni ndege ambao wanapatikana maeneo machache sana hapa nchini Tanzania hasa kutokana na mazingira wanayo pendelea ndege hawa na upatikanaji wa chakula pendwa cha ndege hawa. Maranyingi ndege hawa hapa nchini wanapatikana mikoa ya kaskazini kwani ikolojia ya maeneo haya huwa na mahitaji muhimu kwa ajili ya heroe hasa chakula na maeneo ya kuzaliana. Hali hii ndiyo iliyo pelekea ndege hawa kupatikana maeneo machache sana hapa nchini na kwa uhakika pamoja na kupatikana kwa uchache wao bado ndege hawa wanakumbwa na changamoto nyingi sana katika maeneo wanayo patikana.

Hapa nchini Tanzania heroe wanapatikana sana mikoa miwili, Arusha na Manyara lakini tafiti zinaonesha kuwa eneo pekee ambalo ndege hawa hutumia kwa kuzaliana ni katika ziwa Natron ambalo lina patikana kaskazini mwa Tanzania mkoani Arusha. Hivyo utaona ni kwa namna gani ndege hawa walivyo na chaguzi za mazingira na endapo tu mazingira haya yataharibiwa basi kuna uwezekano mkubwa ndege hawa wakahama hapa nchini.

Katika pita pita zangu nilifanikiwa kufika eneo moja liitwalo Balangda lililopo wilaya ya Hanang mkoani Manyara. Eneo hili ni mji mkubwa tu wenye idadi kubwa ya watu na idadi inazidi kuongezeka kutokana na uzalishaji lakini pia kilimo kinacho endelea katika mji huu. Kutokana na ongezeko la watu katika mji huu basi kuna faida na madhara pia hasa kwa ndege hawa heroe.

Moja kati ya rasilimali muhimu sana uliyo barikiwa mji huu ni uwepo wa ziwa Balangda. Ziwa hili ni rasilimali muhimu sana kwa wakazi wa mji wa Balangda kwani shughuli za uvuvi huendelea katika mji huu lakini pia kwa wale ambao hupendelea kilimo cha umwagiliaji basi ziwa hili ni msaada mkubwa sanakwao. Ziwa hili limepakana na vijiji vingine tofauti na mji wa Balangda na moja kati ya vijiji hivyo ni kijiji cha Lalaji.

Ziwa hili ni la maji chumvi hivyo huwa na chakula cha kutosha kwaajili ya heroe. Moja kati ya vyakula ambavyo hupendelewa sana na heroe ni mwani (algae) hasa mwani wa kijani na mwani mwekundu. Lakini pia uwepo wa wadudu wa majini, viwavi vya wadudu, konokono na viumbe wingine jamii ya kaa ni sababu kubwa zilizo pelekea heroe kuwepo katika ziwa Balangda.

Heroe husafiri umbali mrefu sana kutafuta maeneo mazuri kwaajili ya chakula hasa msimu wa kuzaliana unapoisha. Tumeona hapo juu kuwa eneo ambalo ndege hawa hulitumia kuzaliana hapa nchini ni ziwa Natron hivyo hakuna shaka kuwa ndege hawa husafiri kutoka ziwa Natron na ziwa Manyara ambalo linajumuisha eneo zima la Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara na kuja mpaka katika ziwa Balangda kwaajili ya kutafuta chakula. Unapo fika msimu wa kuzaliana ndege hawa huondoka ziwa Balangda na kwenda ziwa Natron kwaajili ya kuzaliana hivyo ni ndege wachache sana hubaki ziwani hapo.

Hivyo katika safari zao za utafutaji wa chakula, ndege hawa hukutana na changamoto nyingi sana na miongoni mwa changamoto hizi niliweza kuzi shuhudia kwa macho yangu mwenyewe lakini nyingine kusikia kupitia wakazi wa mji wa Balangda. Changamoto hizo ndio zilizo nipa hamasa ya kukuandalia makala hii ndugu msomaji wa makala hizi za wanyamapori.

CHANGAMOTO KWA HEROE ZIWANI BALANGDA

  1. UJANGILI; ndege hawa wana windwa sana na wakazi wa maeneo ya Balangda hali ambayo kama haito dhibitiwa mapema basi ita sababisha madhara makubwa sana hapo baadae hasa kwenye upatikanaji wa ndege hawa katika ziwa Balangda. Vijana wamekuwa wakiwatega lakini wakati mwingine kwa manati pia kuwavamia usiku wanapokuwa wamelala kwa kuwamulika na taa zenye mwanga mkali kisha ndege hawa wanashindwa kuona vizuri.

Katika udadisi wangu nilifanikiwa kukutana na baadhi ya vijana na kuongea tu kama utani kuhusu ndege heroe na hapo ndipo nilipata kujua mengi yanayo endelea kuhusu uwindaji wa hero. Vijana walikuwa wakijisifu sana kuhusu umahiri wao katika uwindaji wa heroe na wamekuwa wakifanya hivyo mara kwa mara. Sikuishia hapo tu bali hata watoto wadogo wana  taarifa nyingi sana kuhusu uwindaji wa heroe kwani wamekuwa wakiwaona kaka zao wakiwinda na wao  pia kufaidika kwa kupata kitoweo.

  • KILIMO NDANI YA ENEO LA ZIWA; moja kati ya changamoto nyingine niliyoiona ni mashamba katika eneo la ziwa. Watu wanalima mashamba mpaka eneo la ziwa hali ambayo inapelekea uharibifu wa mazingira lakini pia upatikanaji wa chakula kwa heroe. Ndege hawa huishi kwenye fukwe za maziwa kwani ndio sehemu ambazo wanapata chakula kwa urahisi zaidi hivyo shughuli za kilimo katika maeneo haya zina sababisha upungufu wa chakula kwani mwani ambao unapatikana maeneo hayo huathirika kutokana na shughuli za kilimo. Pia wadudu ambao ni chakula pendwa cha heroe wamekuwa wakiathirika sana na maendeleo ya shughuli za kilimo katika eneo la ziwa.
  • UINGIZWAJI WA MIFUGO KIHOLELA ZIWANI; si mara moja au mara mbili, kila napo tembelea eneo la ziwani huwa nakutana na kundi la mifugo likiwa ziwani bila hata kujali uchafuzi wa maji lakini pia uchafuzi wa fukwe ambazo ni mazingira pendwa ya heroe. Kundi la mifugo hupelekea sana uharibifu wa mwani kutokana na ukanyagaji wa mifugo kitu ambacho hupelekea upungufu wa chakula kwa heroe. Mbali na hili pia huenda ikawa ni sababu ya kuenea kwa maghonjwa kati ya wanyamapori na wanyama wafugwao. Hii haita waathiri heroe tu bali hata wanyama wafugwao kwani wanyamapori wamejaaliwa kuwa na uvumilivu mkubwa sana wa magonjwa ukilinganisha na wanyama wafugwao.
Picha hii ikionyesha jinsi ziwa Balangda linavyokabiliwa na changamoto ya mifugo mingi kuingia ziwani na kuharibu makazi na ikolojia ya Heroe. Picha hii imepigwa na Sadick Omary
  • UKOSEFU WA ULINZI MAHIRI ENEO LA ZIWA; eneo la ziwa linaonekana kuwa huru sana kwani watu wamekuwa wakiingia na kutoka bila hofu yoyote. Hali hii nadhani inaweza ikawa ni sababu pia iliyo changia kuongezeka kwa ujangili eneo hili lakini pia watu kulima mpaka kwenye eneo la ziwani. Eneo lolote lenye rasilimaliasili kama litakosa ulizi madhubuti kamwe eneo hilo haliwezi kuwa zalishaji na siku baada ya siku litazidi kupoteza sifa yake na hatimae kubaki kuwa historia tu.

NADHANI KUNA MASWALI YA KUJIULIZA HAPA

  1. Je, ulinzi na uhifadhi wa ndege hawa upo chini ya mamlaka zilizopo chini ya wizara ya maliasili na utalii au serikali ya kijiji?
  2. Ziwa Balangda lina tambulika vizuri tu serikalini. Je, shughuli zote zinazo fanyika ziwani zina ratibiwa na nani na serikali ina faidika vipi kupitia shughuli hizo?
  3. Kuna sheria mbalimbali zinazo simamia uhifadhi wa maziwa hapa nchini. Je, ziwa Balangda lina simamiwa ipasavyo kupitia sheria hizo?
  4. Wizara ya maliasili na utalii imeshawahi angalau kwa uchache kutambua changamoto zinazo wakumba heroe katika ziwa Balangda? Na kama inazitambua changamoto hizo ni hatua gani zimechukuliwa mpaka sasa?

Endapo maswali haya yatapatiwa majibu basi utakuwa mwanzo mzuri wa kuwalinda heroe wapatikanao maeneo ya ziwa Balangda.

USIYO YAJUA KUHUSU HEROE

Kwa mtu ambae hana moyo wa uhifadhi hawezi kujua umuhimu wa ndege hawa kwababu fikra zake zitakuwa kwenye uwindaji tu kwaajili ya kitoweo. Sasa kwa ufupi tu nakujuza mambo mawili au matatu muhimu kuhusu ndege hawa.

  1. Heroe ni ndege wa taifa nchini Bahamas
  2. Vizazi vya mwanzo nchini Peru walimchukulia heroe kama ndege wa kuabudia
  3. Jamii za Andean ambao ni Colombia, Chile na Argentina hapo zamani zilikuwa zikivuna mafuta ya heroe kwa kuamini mafuta ya heroe ni tiba nzuri ya kifua kikuu hasa kwa wachimba madini katika zama hizo.
Ndege Heroe au Flamingo wakiwa katika kundi. Picha hii imepigwa na Andey Gudkov

HITIMISHO

Kama tusipoweza kushughulikia tatizo likiwa bado dogo basi tujiandae kuingia gharama kubwa sana hapo baadae na huenda tukaingia gharama kubwa na tusilitatue taizo hilo kabisa. Matatizo madogo haya tunayo yaona katika ziwa Balangda hasa kwa ndege hawa muhimu sana kwenye sekta ya utalii niwazi yapo maeneo mengine mengi tu lakini kwasababu hayaja pata mtu wa kuya zungumzia basi huonekana kama hayapo.

Mamlaka husika hazina budi kutafuta suluhu haraka zaidi dhidi ya changamoto hizo ili kuendeleza uatawi wa wanyamapori hapa nchini lakini pia kuhakikisha jamii mbalimbali zinatambua umuhimu wa wanyama hawa hapa nchini kwani kupitia wanyamapori katika utalii nchi inaingiza fedha nyingi sana za kigeni na kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Elimu ya uhifadhi ni muhimu sana kwa jamii kwani ni suala ambalo kama halipewi kipaumbele hapa nchini. Endapo tutatoa elimu hii basi tutazaliwa mabalozi wazuri sana ambao wata saidia uhifadhi wa wanyamapori lakini pia kufichua wale wote wenye kuhujumu rasilimali zetu kwa manufaa yao wachache kitu ambacho ni hatari katika ustawi wa uchumi wan chi yetu.

Asante sana kwa kusoma makala hii hadi mwisho, makala hii pia imehaririwa na Hillary Mrosso. Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori na uhifadhi wasiliana na mwandishi wa makala hii  kupitia.

Sadick Omari Hamisi

Simu: 0714116963/0765057969

Email: swideeq.so@gmail.com

“I’m The Metallic Legend”

Shares:
2 Comments
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *