Habari msomaji wa makala za blou hii, naamini u buheri wa afya, karibu katika makala ya leo. Lengo la blogu hii imekuwa ni kukupa maarifa na pia kufahamu mambo mbali ambayo yanaendelea katika meaneo haya yenye vivutio vingi. Hivyo nimedhamiria kukupa uelewa na maarifa mazuri. Leo nimekuandalia utaratibu wa kutebelea hifadhi ya taifa ya Arusha.

Nakiri kuwa taarifa za makala hii, utaratibu na mambo yote yaliyoandikwa kwenye makala ni kama ilivyoandikwa na mamlaka ya hifadhi ya taifa ya Arusha, hivyo nimeyawaka hapa ili kukupa msaada pale unapotaka kufahamu utaratibu wa kutalii Arusha na kwenye hifadhi nyingine iwe rahisi kwako kuchukua hatua, karibu sana tujifunze pamoja.

 

Hifadhi Ya Taifa Ya Arusha

Hifadhi ya Taifa ya Arusha ilianzishwa mwaka 1960. Ukubwa wa eneo la hifadhi hivi saa ni kilomita za mraba 322 ikijumlisha mlima Meru wenye urefu wa mita 4566, juu ya usawa wa bahari. Mandhari nzuri ya mlima Kilimanjaro huonekana na kuvutia vizuri ukiwa juu ya mlima Meru.

Historia fupi

Historia ya hifadhi ilianza mnamo mwaka 1876, ambapo Mhangari aitwaye Count Teleki alipotembelea maziwa ya Momella na kuhadidhia juu ya wingi wa viboko na faru aliowaona (hivi sasa faru hawapatikani tena katika hifadhi yataifa ya Arusha). Mwaka 1907 familia ya mzungu aitwaye Trappe ilihamia Momella kwa shughuli za ufugaji na uhifadhi wa wanyamapori. Wakati hifadhi hii inaanzishwa mwaka 1960 enelo la shamba hili lilijumlishwa ndani ya hifadhi.

Jinsi ya kufika hifadhini

Hifadhi inafikika vizuri kwa njia ya barabara pekee. Hakuna kiwanja cha ndege ndani ya hifadhi. Umbali kutoka mjini Arusha ni takribani kilomita 32. Kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ni kilomita 40.

Wakati unaofaa kutembelea hifadhi

Unaweza kutembelea hifadhi hii kwa mwaka mzima. Hata hivyo hali ya hewa ni nzuri zaidi kati ya Juni na Februari. Mvua za muda mfupi (vuli) hunyesha mwezi Novemba. Mvua za masika hunyesha kuanzia mwezi Machi hadi Mei.

Vivutio

Hifadhi ina vivutio vingi vya utalii, kama vile wanyama, Kasoko ya Ngurdoto, Maziwa, Misitu, Mlima Meru.

Serengeti ndogo

Jina Serengeti ndogo lina maana ya mbuga ndogo inayofanana na hifadhi ya taifa ya Serengeti. Wanyama wa aina mbali mbali wa mbuga za wazi huonekana kwa urahisi na kwa makundi katika eneo hili. Baadhi ya wanyama hao ni ngiri, pundamilia, kuro, twiga na mbogo.

Jumba la makumbusho Ngurdoto

Hili ni eneo ambalo wanyama, ndege na waudu waliokaushwa hupatikana. Pia jumba limezungukwa na msitu wa Ngurdoto ambao ni makazi ya mbega.

Kasoko ya Ngurdoto (Crater)

Ina ukubwa wa kilomita za mraba takribani 8 na ina mzunguko wa kilomita 10.67 na kina cha mita 333. Eneo lenye mwinuko wa juu zaidi kwenye ukingo wa Kasoko linaitwa Leitong. Sehemu hii ina urefu wa takribani mita 1824 juu ya usawa wa bahari. Ukiwa juu ya eneo hili barafu ya mlima Kilimanjaro, maziwa ya Momella na shughuli za kilimo vijijini huonekana vizuri sana. Kutokana na unyevu na ukungu mwingi katika eneo hili mimea kama vile kuvumwani, feni, okidi na kavu (kuvumwani yenye vivyweleo) hustawi vizuri. Ndani ya Kasoko makundi ya wanyama kama vile nyati huonekana kwa urahisi.

Msitu wa asili wa Ngurdoto

Eneo hili lina aina nyingi za miti, kwa utambuliwa wa majina ya miti hiyo, vibao vyenye majina vimewekwa kwenye baadhi ya miti, mfano ole asps. Pia mbega weupe wanapatikana kwa wingi.

Ziwa Longilihili

Ndio ziwa pekee hifadhini lisilo na maji ya chumvi chumvi na samaki aina ya tilapia (perege) hupatikana. Wanyama kama vile viboko, mbogo na kuro huonekana katika eneo hili. Ziwa hili lina mimea aina ya mafunjo (pypyrus) na matete (mace) ambayo huonekana kama visiwa na huhama kulingana na uelekeo wa upepo. Ndege kama vile African jacana, red knobbed coot, Africana na fish eagle pia hupatikana.

Maziwa ya Momella

Maziwa haya hupokea maji ya mito iliyopo chini ya ardhi na hayana kina kirefu. Maji yake yana chumvi chumvi na wanyama hunywa maji katika baadhi ya maziwa haya. Ndege aina ya heroe wakubwa kwa wadogo hupatikana zaidi katika ziwa la Momella kubwa, ambalo ndilo lenye alkalini nyingi kuliko maziwa mengine ya Momella. Viboko huonekana mara chache katika ziwa la Momella ndogo ambapo kiwango cha alkalini ni ni kidoo. Maziwa haya pia ni makazi ya ndege wakazi na ndege wasio wakazi, baadhi ya ndege hawa ni makoa majini kutoka kizio cha kaskazini.

Kilima cha Tululusia

Barabara inayoelekea mlima Meru hupitia kando kando ya kilima cha Tululusia chenye mandhari nzuri ya kuvutia. Ukiwa juu ya mwinuko wa kililima hiki utaona vizuri maeneo ya chini ya uwanda wa hifadhi, mlima Meru na mlima Kilimanjaro.

Maporomoko ya maji

Maporomoko ya maji ya Tululusia na Maio ndio marefu zaidi ndani ya hifadhi, yanavutia sana kwa uzuri wake. Maporomoko ya Tululusia yana urefu wa takribani mita 28 na yapo karibu na lango la Momella, wakati yale ya Maio yapo pembezoni mwa barabara iendayo mlimani.

Tao la mti (Fig Tree Arc)

Mara upitapo Tululusia, kituo kinachofuata ni mkuyu mkubwa wenye pango. Mti huu uliota baada ya ndege wala matunda kudondosha punji za mkuyu kwenye miti na baadaye kuota kama tao. Tao hili ni kubwa kiasi kwamba gari lenye ukubwa wa tembo linaweza kupita.

Ndege

Ndege wa aina mbali mbali wakazi na wahamao huonekana hifadhini. Baadhi ya ndege waonekanao hifadhini ni ndege wawindao kama vile mwewe, kozi, shekevele. Ndege wa majini kama vile mabata bukini, mabata kitwitwi na wengineo. Ndege wakubwa kama vile kanga, kwale na chiriku akiwemo kinengea, chozi, zaukulu, na hondo hondo hupatikana.

Mandhari ya kitoto

Uwazi mkubwa uanaotazamana na misitu huwezesha mwonekano mzuri wa mazingira ya Momella, pori la wazi na mlima Kilimanjaro.

Kasoko ya Meru

Mara upitapo kitoto kuna njia nyembamba ionekanyo msituni ambayo huishia kwenye Kasoko ya Meru. Kitu kilichosimama kama ukucha wa ndege wa kuparua ndani ya Kasoko ni majivu ya volcano yeneye umbo kama pia. Katika kasoko hii pia jabali la mlima Meru huonekana vizuri sana. Kasoko ya meru ni mojawapo ya maeneo mazuri na yakuvutia hifadhini. Eneo hili ni tamarare na unaweza kuona vizuri sana mofolojia ya mlima hasa siku zisizo na mawingu. Hii ni pamoja na majivu ya volcano yenye umbo kama pia.

Mandhari ya Njeku na Eneo ya kitamaduni

Njia nyembamba inayoanzia kosoko ya Meru kuelekea kwenye mandhari ya Njeku kupitia mandhari nzuri ya Ash-cone na kasoko. Pana jukwaa kwenye mwinuko wa juu unaotazamana na maporomoko ya maji katika korongo la mto Ngarenanyuki. Wakati w ukame watu wa Meru hutambikia mungu wao chini ya mti uitwao Mtarakwa (African pencil cidar) ambao upo karibu na tamarare ya kasoko. Kadri miaka inavyokwenda matambiko na shughuli za kimila hifadhini zinazidi kupungua. Maeneo haya yanaendelea kuwa vivutio vya kihistoria kwa wageni.

Shughuli za utalii

Shughuli za utalii katika hifadhi hii zimegawanyika katika makundi matano

  1. Kupanda mlima hadi kilele cha Mlima Meru au kufika moja wapo ya mabanda ya watalii
  2. Matembezi ya miguu ambayo huchukua hadi masaa manne
  3. Utalii wa kutembea kwa magari
  4. Utalii wa kuendesha mitumbwi katika ziwa dogo la Momella.
  5. Utalii wa kupanda Farasi

Shughuli hii ya mitumbwi huratibiwa na mawakala wa utalii kampuni ya the “Green Footprints Adventure Limited” iliyopewa leseni, kwa mawasiliano tumia namba za simu (+255 782 297 503 au +255 684 153 882).

Kupanda mlima Meru

Watalii wapandao mlima Meru hupita katika mazingira mbali mbali ya asili, yenye mimea mizuri na ya aina tofauti yenye mvuto wa aina yake. Safari ya kufika kileleni na kurudi inahitaji siku nne.

Siku ya kwanza

Lango la Momella (mita 1,500) hadi kituo/ mabanda ya Miriakamba (mita 2,500). Siku hii watalii hutembea hadi Miriakamba na kulala. Kuna njia mbili kutoka lango la Momella, njia ya Kusini na Kaskazini.

Njia ya Kusini; hutumia wastani wa masaa 5 hadi 6 kutembea hadi kituo/ mabanda ya Miriakamaba. Watalii hupita msitu wa montane wenye vivutio mbali mbali kama vile tao la mti, maporomoko ya maji ya Maio na aina tofauti za mimeana na wanyama kama nyati twiga, tembo, pongo n.k pia ndege aina mbali mbali.

Njia ya Kaskazini; hutumia wasatani wa masaa 3 kutoka lango la Momella hadi kituo/mabanda ya Miriakamba. Hii ni njia fupi na yenye mpando mkali. Upitapo njia hii mlima Kilimanjaroo na maziwa ya Momella huonekana vizuri sana.

Siku ya pili;

Kituo cha Miriakamba hadi Saddle (mita 2,500 hadi 3,500) wageni hutembea kwa saa 3 hadi 4. Watalii wawapo njiani hufurahia mandhari nzuri ya mlima Kilimanjaro, maziwa ya Momella, Kasoko ya Meru, Ash-cone na jabali la Meru kubwa na ndogo. Wanyamapori huonekana kwa uchache sambamba na mabadiliko ya uoto wa asili kwa kadri mwinuko unavyoongezeka. Uwapo katika kituo cha Saddle unaweza kupanda Meru ndogo siku hiyo hiyo ambapo huchukua muda was aa moja.

Siku ya tatu:

Kutoka katika kituo cha Saddle hadi kileleni (mita 3,500 – 4,566 kutoka usawa wa bahari) hutumia saa 4 hadi 5. Hili ni eneo ambalo watalii hufurahia zaidi mandhari ya mlima Kilimanjaro, Meru ndogo (mita 3,820) kasoko ya Meru, Ash- cone na maziwa ya Momella. Vivutio vingine ni jabali la mlima Meru, nyanda za juu Ngorongoro, mji wa Arusha, machweo na mawio ya jua, mau ‘Evalastin flower’ na ndege aina ya tumbusi huonekana. Wageni hurudi kutoka kileleni hadi kituo cha Miriakimba kupitia kituo cha Sddle.

Siku ya nne:

Siku hii ni ya mwisho, watalii huanza safari kutoka Miriakimba hadi lango la Momella kwa kutumia njia moja wapo kati ya ile ya Kaskazini au ya Kusini. Njia ya Kaskazini hutumia saa 2 kuteremka na saa 3 hadi 4 kwa njia ya Kusini.

Uangaliaji wa wanyamapori

Safari za matembezi; matembezi ya miguu hutoa fursa ya kuona aina mbali mbali za wanyama kama vile mbogo, nyani, mbega mweupe, tembo, twiga, funo, fisi, kuro ngiri, chui, aina tofauti za ndege na uoto wa asili. Hifadhi hutoa askari mwenye silaha ili kulinda na kuwaongoza watalii watembeao kwa miguu. Matembezi huchukua muda usiozidi masaa 4.

Malazi:

Hifadhi ina kambi za jumuiya za watalii zipatazo tatu na kambi maalumu za watalii mbili. Hifadhi pia ina nyumba ya kupumzikia wageni na mabanda ya kulala wageni mlimani. Kuna hoteli mbili ndani ya hifadhi Momella na Hatari. Kuna hoteli nyingine nyingi nje ya hifadhi, mji mdogo wa Usa- river na katika miji ya Arusha na Moshi.

Sheria na taratibu za hifadhi;

Wapanda mlima lazima waongozwe na askari mwenye silaha.

Watalii wanatakiwa kila mara kufuata ushauri wa askari au kiongozi wa wageni. Kila wakati tembeeni kwa kundi, epuka kuteremka au kupanda mlima peke yako.

Kuapanda hadi kwenye Ash- cone inawezekana baada ya kupata kibali cha Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA.

Wapanda kilele cha mlima Meru wanashauriwa kupanda na kuteremka kwa siku sizizopungua 4.

Muda chini ya siku 4 inaweza kusababisha kuchoka sana na homa ya miinuko ya juu ya milimani.

Wapanda mlimani wanatakiwa kuwa na vifaa vyote vya kupandia mlima, chakula na maji kwa siku zote watakazokuwa mlimani.

Watoto chini ya miaka 10 hawaruhusiwi kupanda zaidi ya mita 3700 juu ya usawa wa bahari.

Wapanda mlima lazima waandae safari ya kupanda mlima kupitia mawakala wa utalii waliosajiliwa.

Mawakala wa utalii wanatakiwa kukodisha wapangazi kutoka chama cha wapangazi kilichosajiliwa na uhakiki wa wapangazi lazima ufanyike kwenye malango ya hifadhi.

Mpangazi anaruhusiwa kubeba mzigo wenye uzito usiozidi kilo 20 wakati wa upandaji wa mlimani.

Usienda zaidi ya mita 3000 usawa wa bahari kama una mafua, matatizo ya mapafu, au moyo. Endapo unatumia dawa muone daktari kabla ya kupanda mlima.

Epuka ulevi wakati wa kupanda mlima.

Watalii wataingia hifadhini au kupanda mlima kwa ridhaa yao wenyewe.

Acha hifadhi katika uasilia wake kwa kutoongeza au kuchukua chochote.

Tumia njia au barabara zilizowekwa na hifadhi na zingatia ushauri wa kiongozi wa utalii.

Uchafu huaribu sura ya uasili. Hakikisha wewe na kila mmoja kwenye kundi anatoka na takataka zote nje ya hifadhi.

Usiwashe moto au kusababisha moto hifadhini.

Uendeshapo gari usizidishe mwendo wa kilomita 50 kwa saa. Mwendo uliopendekezwa ni kilomita 25 kwa saa ili kukwepa ajali na kukuwezesha kuona wanyama vizuri.

Usiwasumbue wanyama kwa njia yoyote ile. Kumbuka wanyama wana haki zote wawapo porini.

Tafadhali usipige kelele, honi au kuwasha redio wakati wa uangaliaji wa wanyama, wakati wa kutembea na upandaji mlimani.

Ili kuonyesha unajali na mwenye busara kwa watalii wenzako, usiwasumbue wao wala wanyama wanao waangalia.

Usiingie hifadhini na mnyama wa kufugwa nyumbani au silaha.

Usishuke kwenye gari isipokuwa maeneo yaliyotengwa kuangalia wanyama na mandhari au kambi za wageni maeneo maalumu yanayoruhusiwa.

Using’oe, usikate au kuharibu mmea wowote au kumiliki/ kubeba sehemu au kipande chochote cha mmea hifadhini.

Ni marufuku kuwa ndani ya hifadhi kuanzia saa 12:30 jioni hadi sasa 12:30 asubuhi isipokuwa kwenye kambi za wageni, hotelini, nyumba za kupumzikia au maeneo maalumu yaliyotengwa na hifadhi.

Kibali cha kuingia hifadhini huwa ni halali kwa muda was aa 24 tu.

Kibali cha mpanda mlima ni halali kwa wakati wa mchana tu. (day light)

Ada za hifadhi mara zinapolipwa hazirudishwi.

TANAPA hufanya kazi na mawakala wa utalii wenye leseni halali za TALA.

Kuweka au kushikilia kambi maalum ya watalii malipo ya jumla ya mteja mmoja kwa idadi ya siku atakazolala hufanyika makao makuu TANAPA – ARUSHA. Malipo ya mabanda hufanyika hifadhini.

Mawakala wa utalii wanahitajika kulipa malipo yote kwa jumla ya wateja kwa angalau siku (30) thelathini kabala ya kuingia hifadhini.

Angalizo: watumishi wa hifadhi wapo tayari muda wakati wote kwa moyo mkunjufu kutoa huduma, ushauri au msaada.

Tozo mbali mbali

  • Tozo ya uhifadhi:
  • Zaidi ya miaka 16 waafrika mashariki 10,000 na watoto mika 5 -15 ni 2,000 na watoto chini ya miaka 5 ni bure. Hii ni kwa wageni wote wanaotoka Afrika Mashariki.
  • Wasio wa Afrika mashariki, zaidi ya miaka 16 Dola 45 na watoto kuanzia miaka 5 – 15 ni dola 15 na chini ya miaka 5 ni bure. Hii ni kwa wageni ambao sio wa Afrika Mashariki.

 

  • Kupanga mahema – Maeneo ya Jumuiya
  • Zaidi ya miaka 16 shilingi 5,000, watoto kuanzia miaka 5 – 15 ni shilingi 2500 na watoto chini ya miaka 5 ni bure. Tozo hizi ni kwa ajili ya wageni wanaotoka Afrika Mashariki.
  • Kwa wageni ambao sio wa Afrika Mashariki kuanzia miaka zaidi ya 16 watalipa dola 30, na watoto kuanzia miaka 5 – 15 watalipa dola 5. Watoto chini ya miaka mitano ni bure.

© Kupiga mahema – maeneo maalumu

  • Zaidi ya miaka 16 watalipa shilingi 10,000 na watoto kuanzia miaka 5 – 15 watalipa shilingi 5,000. Wtoto chini ya miaka 5 ni bure. Tozo hizi ni kwa wageni waliotoka Afrika Mashariki.
  • Kwa wageni ambao hawajatoka Afrika Mashariki, zaidi ya miaka 16 watalipa dola 50, na walio na miaka kuanzaia 5 – 15 watalipa dola 10, na watoto chini ya miaka mitano ni bure. Tozo hizi ni kwa wageni wote ambao hawajatoka Afrika Mashariki.

(d)Kupiga mahema- kambi za kuhama

Flying camp 5,000 kwa walio wa Afrika Mashariki na dola 50 kwa wageni wasio wa Afrika Mashariki.

( e) Tozo za malazi

  • Vituo vya Miriakamba na Saddle shilingi 2,000 kwa walio wa Afrika Mashariki na dola 30 kwa wageni wasio wa Afrika Mashariki
  • Vyumba vya kulala wageni walio wa Afrika Mashariki ni shilingi 15,000 na wasio wa Afrika Mashariki ni dola 30.

(f) Tozo za Hosteli, kwa walio wa Afrika Mashariki ni shilingi 5,000 kwa wageni ambao sio wa Afrika Mashariki ni dola 10.

(g) Tozo za kupiga makasia ziwani

(i) Kwa mtu mzima ni shilingi 5,000, kwa watoto ni shilingi 2,000. Tozo hizi ni kwa wageni wote ambao wanatoka Afrika Mashariki.

(ii) Kwa wageni ambao sio wa Afrika Mashariki, mkubwa anatoa dola 20 na watoto watatoa dola 10.

(h) Tozo wa utalii wa kupanda Farasi, kwa wageni wanaotoka Afrika Mashariki watalipa shilingi 50,000 na wageni wasiotoka Afrika Mashariki watalipa dola 50.

(i) Tozo za kupiga picha za kibiashara kwa mtu kwa siku ni Dola 250 (Hii inajumuisha tozo ya uhifadhi, kambi na upigaji picha).

(j) Faini za ajali ndani ya hifadhi (magari ya aina zote) ni shilingi 200,000.

(k) Tozo za kutembea kwa miguu

(i) Matembezi mafupi (saa 1 hadi 4), zaidi ya miaka 16 ni shilingi 5,000 na watoto miaka 12 -15 shilingi 2,500. Tozo hizi ni kwa wageni waliotoka Afrika Mashriki.

(ii) Matembezi mafupi kwa wageni ambao sio wa Afrika Mashariki watalipa dola 20 na watoto miaka 12- 15 watalipa Dola 10.

  • Matembezi marefu (zaidi ya saa 4) kwa wageni kutoka Afrika Mashariki kuanzia miaka 16 watalipa shilingi 10,000 na watoto miaka 12 -15 watalipa shilingi 5,000.
  • Wageni wasiotoka Afrika Mashariki kuanzia miaka 16 watalipa Dola 25, na watoto kuanzia miaka 12 – 15 watalipa Dola 15.

(l) Tozo za mwongoza wageni/huduma ya askari mwenye silaha (kwa kundi)

(i) Mwongoza wageni (mtumishi wa hifadhi) atalipwa shilingi 5,000 na wazawa, na wageni watatoa Dola 20.

(ii) huduma ya askari wakati wa kupanda mlima Meru shilingi 10,000 kwa wazawa na Dola 15 kwa wageni ambao sio kutoka Afrika mashariki.

(m) Tozo ya uokoaji, kwa wazawa ni shilingi 2,000 na kwa wageni ambao sio wa Afrika mashariki ni Dola 20.

(n) Tozo ya utalii wa kula chakula (hot meals), kwa wazawa ni shilingi 5,000 na kwa wageni ambao sio wa Afrika Mashariki ni Dola 5.

(O_) Tozo ya watoa huduma watanzania (crew) kwa siku ni shilingi 3,500 (Hii ni kwa ajili ya waongoza wageni, wapangazi, na wapishi. Hii inajumisha gharam za uhifadhi shilingi 1,500 na gharama ya kambi/banda shilingi 2,000.

(p)Faini ya mwendokasi uliovuka kiwango hifadhini hii ni kwa magari yote ni shiingi 50,000.

(q) Viingilio vya magari zenye usajili wa Tanzania

(i) Pungufu au sawa na kg 2,000 ni shilingi 20,000, na Dola 40 kwa magari yasiyo na usajili wa Tanzania.

(ii) kati ya kg 2001 – 3000 ni shilingi 35,000, na Dola 150 kwa magari yasiyo na usajili wa Tanzania.

(iii)Kati ya kg 3001 – 7,000 ni shilingi 60,000, na Dola 200 kwa magari yasiyo na usajili wa Tanzania.

  • Kati ya kg 7001 – 10000 ni shilingi 150,000 na Dola 300 kwa magari yasiyo na usajili wa Tanzania.
  • Magari ya wazi yatatozwa asilimia 50 zaidi.

(r) Tozo kwa wanafunzi watanzania kutoka vyuo/ shule za Tanzania baada ya kuomba kibali na kupata kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu/ Mkuu wa Hifadhi ni shilingi 1,000. Na wanafunzi ambao sio watanzania watatozwa Dola 10. Kibali kitahusu tozo za hifadhi tu, tozo nyingine zitalipwa kama zilivyo.

(s) Kibali maalumu kwa Wakurugenzi wa makampuni ya utalii (Director’s pass) ni Dola 100.

(t) Tozo kwa watanzania wanaosafiri/ kupitia hifadhini kwa magari ya kubeba abiria ni shilingi 2,000.

(u) Tozo kwa watanzania wanaosafiri kupitia hifadhini na magari binafsi ni shilingi 5,000.

NB: TOZO HIZI NI BILA VAT 18%.

TOZO HIZI ZINAWEZA KUBADILIKA MUDA WOWOTE

MALIPO YANAFANYIKA KWA KADI ZA TANAPA ZINAZOTOLEWA NA BENK YA CRDB PIA KAD ZA VISA NA MASTER ZINATUMIKA.

WAKURUGENZI WA MAKAMPUNI WENYE VIBALI HAWARUHUSIWI KUONGOZANA NA WAGENI.

WAGENI WAKAZI (EXPATRIATE WANAWEZA KULIPA KWA FEDHA ZA KITANZANIA (TSH).

KITAMBULISHO NI MUHIMU KABLA HUJAINGIA HIFADHINI

TOZO ILIYOLIPWA HAIWEZI KURUDISHWA,

Naamini kufikia hapa utakuwa umeelewa na kupata ufahamu utakaokusaidia kufanya maamuzi ya kutembelea hifadhi hii. Kwa msaada zaidi kuhusu hifadhi ya Taifa ya Arusha unweza kutumia mawasiliano haya www.tanzaniaparks.go.tz, barua pepe arusha@tanzaniaparks.go.tz au mawasiliano ya simu 255 767 536 136.

Nakushukuru sana Rafiki yangu kwa kusoma makala hii ndefu, lakini iliyosheheni mambo ya msingi ya kutusaidia tunapotaka kutembelea hifadhi au mbuga za wanyamapori, tukutane kwenye makala ijayo ambayo nitaelezea utaratibu wa hifadhi nyingine ya taifa.

Asante sana!

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com