Habari msomaji wa makala hizi, karibu tujifunze moja ya kivutio kilichopo katika hifadhi ya taifa ya Arusha. Kama nilivyoeleza kuwa hifadhi ya Arusha ina vivutio vya kipekee sana, na moja ya kivutio hicho ni mlima Meru. Hivyo kwa watu ambao watapenda shughuli za upandaji wa mlima Meru, kuna mambo ya kufahamu ili ujipange ili ufurahie.
Utaratibu huu wa upandaji wa mlima Meru ni kwa mujibu wa uongozi wa hifadhi ya taifa ya Arusha, na mamlaka ya hifadhi za taifa Tanzania TANAPA. Kwa maelezo zaidi unaweza kupata utaratibu huu kwenye tovuti www.tanzaniaparks.go.tz .Hapa ni maelezo na utaratibu huo, karibu sana Arusha, karibu tutalii mlima Meru.
Watalii wapandao mlima Meru hupita katika mazingira mbali mbali ya asili, yenye mimea mizuri na ya aina tofauti yenye mvuto wa aina yake. Safari ya kufika kileleni na kurudi inahitaji siku nne.
Siku ya kwanza
Lango la Momella (mita 1,500) hadi kituo/ mabanda ya Miriakamba (mita 2,500). Siku hii watalii hutembea hadi Miriakamba na kulala. Kuna njia mbili kutoka lango la Momella, njia ya Kusini na Kaskazini.
Njia ya Kusini; hutumia wastani wa masaa 5 hadi 6 kutembea hadi kituo/ mabanda ya Miriakamaba. Watalii hupita msitu wa montane wenye vivutio mbali mbali kama vile tao la mti, maporomoko ya maji ya Maio na aina tofauti za mimeana na wanyama kama nyati twiga, tembo, pongo n.k pia ndege aina mbali mbali.
Njia ya Kaskazini; hutumia wasatani wa masaa 3 kutoka lango la Momella hadi kituo/mabanda ya Miriakamba. Hii ni njia fupi na yenye mpando mkali. Upitapo njia hii mlima Kilimanjaroo na maziwa ya Momella huonekana vizuri sana.
Siku ya pili;
Kituo cha Miriakamba hadi Saddle (mita 2,500 hadi 3,500) wageni hutembea kwa saa 3 hadi 4. Watalii wawapo njiani hufurahia mandhari nzuri ya mlima Kilimanjaro, maziwa ya Momella, Kasoko ya Meru, Ash-cone na jabali la Meru kubwa na ndogo. Wanyamapori huonekana kwa uchache sambamba na mabadiliko ya uoto wa asili kwa kadri mwinuko unavyoongezeka. Uwapo katika kituo cha Saddle unaweza kupanda Meru ndogo siku hiyo hiyo ambapo huchukua muda was aa moja.
Siku ya tatu:
Kutoka katika kituo cha Saddle hadi kileleni (mita 3,500 – 4,566 kutoka usawa wa bahari) hutumia saa 4 hadi 5. Hili ni eneo ambalo watalii hufurahia zaidi mandhari ya mlima Kilimanjaro, Meru ndogo (mita 3,820) kasoko ya Meru, Ash- cone na maziwa ya Momella. Vivutio vingine ni jabali la mlima Meru, nyanda za juu Ngorongoro, mji wa Arusha, machweo na mawio ya jua, mau ‘Evalastin flower’ na ndege aina ya tumbusi huonekana. Wageni hurudi kutoka kileleni hadi kituo cha Miriakimba kupitia kituo cha Sddle.
Siku ya nne:
Siku hii ni ya mwisho, watalii huanza safari kutoka Miriakimba hadi lango la Momella kwa kutumia njia moja wapo kati ya ile ya Kaskazini au ya Kusini. Njia ya Kaskazini hutumia saa 2 kuteremka na saa 3 hadi 4 kwa njia ya Kusini.
Uangaliaji wa wanyamapori
Safari za matembezi; matembezi ya miguu hutoa fursa ya kuona aina mbali mbali za wanyama kama vile mbogo, nyani, mbega mweupe, tembo, twiga, funo, fisi, kuro ngiri, chui, aina tofauti za ndege na uoto wa asili. Hifadhi hutoa askari mwenye silaha ili kulinda na kuwaongoza watalii watembeao kwa miguu. Matembezi huchukua muda usiozidi masaa 4.
Malazi:
Hifadhi ina kambi za jumuiya za watalii zipatazo tatu na kambi maalumu za watalii mbili. Hifadhi pia ina nyumba ya kupumzikia wageni na mabanda ya kulala wageni mlimani. Kuna hoteli mbili ndani ya hifadhi Momella na Hatari. Kuna hoteli nyingine nyingi nje ya hifadhi, mji mdogo wa Usa- river na katika miji ya Arusha na Moshi.
Huo ndio utaratibu wa kupanda mlima Meru na kushuka, mamlaka ya hifadhi yamewaka na muda mzuri wa kupanda na kushuka mlima Meru. Kuna mengi ya kufahamu utakapofika katika hifadhi hii ya Arusha.
Asante sana!
Hillary Mrosso
+255 683 862 481
www.mtalaamu.net/wildlifetanzania