Habari ndugu Watanzania, hongereni ndugu zetu Waislam kwa kufikia kilele cha mfungo wenu wa mwezi mtukufu, naamini mmejipanga na kujitathini vizuri kwenye kipindi chote cha mfungo. Katika kuadhimisha sherehe hizi za Eid, ningependa kutoa salamu zangu za kheri kwenu nyote. Najua kwenye kipindi hiki cha sikikuu watu wengi hupenda kukaa nyumbani na familia zao kufurahia kwa pamoja, na wengine hupenda kwenda sehemu nyingine nzuri na tulivu wakiwa na familia zao, hivyo basi kwa kuliona hilo nimeamua kujumuika na ninyi kwa njia ya makala hii ili kwa wale wanaopenda kwenda kusherekea sehemu nyingine tofauti na nyummbani kwao, waweze kuelewa sehemu nzuri na zinazofikika kwa urahisi bila bugudha yoyote. Kuna wanao penda kwenda kwenye fukwe za bahari, kuna wanaopenda kwenda makumbusho, kuna wanaopenda kwenda kwenye mighahawa mizuri, kuna wanaopenda kwenda kwenye maeneo yenye vivutio vya kihistoria, na pia kuna wanaopenda kwenda kutembelea hifadhi za taifa.

Lengo kuu la kuandika makala hii ni kuwapa mwanga wale ambao wanatamani kutembelea hifadhi za taifa lakini hawajui waanze na hifadhi ipi au watembelee hifadhi gani.  Najua idadi kubwa ya watu ipo kwenye miji ya Dar es salaam na Morogoro, hivyo basi ningependa kuwashauri hifadhi rahisi kutembelea kipindi hiki ni HIFADHI YA TAIFA YA MIKUMI, kuna sababu nyingi nimekwambia utembelee hifadhi hii, kama unataka kufurahia katika kipindi hiki cha sikukuu, hivyo kwa wale wanaotaka kutembelea hifadhi kwenye kipindi hiki cha mapumziko ya sikukuu za Eid, hifadhi ya Taifa ya Mikumi ndio rahisi na isiyo na usumbufu wa gharama na  usafiri. Zifuatazo ni sababu kwa nini utembelee hifadhi ya taifa ya mikumi kipindi hiki cha mapumziko ya sikukuu.

  1. Ni rahisi sana kufikika

Hapa nawalenga watu wanaotoka mikoa ya Dar es salaam, Morogoro, Dodoma, Iringa, n ahata singida, watu wanaotaka kutembelea hifadhi hii kwa urahisi kipindi hiki cha mapumziko ya sikukuu za Eid, wanaotoka kwenye mikoa niliyoitaja hapo juu wanaweza kufanya hivyo kwasababu ya kupunguza na kuepuka gharama za usafiri. Hivyo kama upo Dar es salaam unatumia barabara kuu inayotoka Dar  es salaam kwenda Zambia.  Ni hifadhi ambayo inajulikana na ipo njiani kabisa hivyo ni rahisi kufika kwa wakati na kuanza kufanya shughuli za kitalii ndani ya hifadhi hii ya kipekee. Pia unaweza kuja hifadhini kwa usafiri wa gari au hata ndege maana kuna kiwanja cha ndege.

  1. Upekee na uzuri wa hifadhi Taifa ya Mikumi

Hifadhi ya Mikumi ni hifadhi ya nne kwa ukubwa baada ya Ruaha, Serengeti na Katavi, hifadhi hii ina ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 3,230. Hifadhi hii ipo katikati ya milima iliyoinuka na miinuko yenye misitu ya Mto Mkata. Kwa upande wa Mashariki zipo safu za milima ya Uluguru iliyoinuka kufikia futi 900, wakati upande wa Kusini Magharibi vipo vilele vinavyochomoza vya milima ya Lumango. Kutokana na ukubwa wa hifadhi hii, ina idadi kubwa  sana ya wanyama na ndege.

Hifadhi hii yenye wanyamapori wengi kama vile makundi makubwa ya tembo, makundi makubwa ya nyati,  simba, pundamilia, twiga, nyumbu, swala, ngiri ambao wanaweza kuonekana kirahisi kabisa katika kipindi chote cha mwaka. Kuna aina mbali mbali za Reptilia wanaoishi katika hifadhi hii mfano nyoka, chatu, kenge na mamba.

Vile vile kuna aina nyingi sana za spishi za ndege zipatazo 300 ambazo zimekwisha kubainishwa, na baadhi ya hizo zikiwa zimehamia kutoka Bara la Asia na Ulaya. Hii ni fursa nzuri sana kuona wanyama na ndege wakitoka sehemu mbali mbali duniani wakija kutembela na kufanya makazi yao ktiaka hifadhi hii ya mikumi.

Nisieleze sana nikamaliza uhindo wate, ngoja niachia hapa ili utakapoenda utaona vingi zaidi ya haya yaliyoandikwa humu. Lakini pia unapokuwa unaeenda kutembelea hifadhi hii inawezekana unataka sehemu nzuri za kulala, au kula, basi zipo tele, tena kwa bei mbali mbali, kulingana na uwezo wako utachagua utumie huduma gani. Pia hata magari ya kitalii yapo ya kutosha kukuzungusha ndani ya hifadhi ili uone vivutio vilivyoko huko.

Sambamba na hili, unaweza kutembelea hifadhi lakini pia kuna vivutio vingine ambavyo vipo nje ya hifdhi ya Mikumi, kama vile Snake Park ambayo ipo Mikumi mjini. Hivyo unaweza kuchagua kutembelea vyote ili ufurahie na ujifunze mambo mbali mbali ya wanyamapori. Hii ndio njia nzuri ya kutumia kukuza uchumi wa nchi yetu. Huu ni utamaduni mzuri sana, tuufanyie kazi.

Kwa wale ambao wapo mikoa mingine ya mbali na unataka kutembelea hifadhi kipindi hiki cha mapumziko ya sikukuu, basi angalia makala zilizopita ambazo nimeandika kuhusu vivutio mbali mbali vilivyoko kwenye hifadhi zetu. Uzuri karibu kila mkoa katika nchi hii, una hifadhi za wanyama, hivyo kwa mkoa wowote uliopo angalia ni hifadhi gani ipo karibu ambayo unaweza kwenda kwa urahisi. Pia kama unataka kuja Mikumi, ni jambo zuri pia, karibu sana.

Nakutakia kila la kheri kwenye maandalizi yako ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Hillary Mrosso

0742092569

Wildlife Conservationist

hillarymrosso@rocketmail.com