Habari Rafiki yangu, karibu kwenye makala ya leo ambayo tunaangalia dhana pana kidogo ili tupanue uelewa wetu kwenye masuala ya uhifadhi wa wanyamapori. Siku zote huwa naamini kabisa kuwa endapo watu watapewa elimu ya wanyamapori na uhifadhi watawapenda na wakiwapenda wataendelea kujifunza na wakijifunza watachukua hatua stahiki na kushiriki katika kuwahifadhi wanyamapori. Dhana ya uhifadhi ni pana kidogo na hivyo kwakuwa tupo pamoja kwenye blog hii tutajifunza na kupeana mambo muhimu yanayohusu wanyamapori na sekta hii ya maliasili kwa ujumla. Hili ni eneo ambalo watu wengi hawalijui kwa undani, watu wanao elewa mambo haya ni wasomi wa mambo haya au waliopata uzoefu na kufanya kazi kwenye maeneo haya, hivyo basi kwa mtanzania wa kawaida ni ngumu kuelewa kinachoendelea kwenye maliasili na sekta hii nyeti.
Tunapozungumzia kuwahifadhi wanyamapori kwa haraka haraka akili za watu zinarukia kwenye uhifadhi wa tembo, faru, simba, nyati, chui nk. Ni sawa kabisa ndiyo tunatakiwa kuwahifadhi wanyama hawa. Lakini pia ni vizuri tukafahamu kwa upana wake tunaposema tunawahifadhi wanyama hawa hatuishii tu kuwahifadhi wanyama pekee, kwenye makazi ya wanyamapori hawa kuna viumbe hai na rasilimali nyingine muhimu sana ambayo ndio inafanya wanyama tunaowahifadhi waendelee kuwepo, kuna viumbe ambavyo vipo ili viumbe vingine viwepo, kuna mimiea na miti ambayo uwepo wake unasababisha uwepo wa baadhi ya wanyama na mimea mingine, kuna wadudu ambao uwepo wao unasababisha baadhi ya wanyama na mimea kuendelea kuwepo, hivyo basi sio kitu kimoja kinatufanya kuzungumza na kunadi kwa jamii na dunia nzima kuwa tunahifadhi wanyamapori, bali ni muunganiko wenye kuhusisha vitu vingi kuanzia vitu hai na vitu visivyo hai.
Kwenye ardhi ambayo ina wanyamapori, kumbuka hakuna kinachoweza kuota kwenye ardhi isiyohifadhiwa vzuri, ardhi inabeba mamilioni ya maisha na vitu ambavyo vinasababisha maisha kuendelea, hivyo kwenye uhifadhi wa wanyamapori huwezi kuondoa ardhi au kupuuza ardhi, ardhi inatumika kubeba maji kwa ajili ya wanyama, mimea na wadudu, ardhi inabeba chakula na madini muhimu kwa ajili ya afya za wanyama na mimea, ardhi inahifadhi mamia na mamilioni ya maisha ya wanyama, wadudu, na mimea. Ardhi ina maana sana kwenye mambo ya uhifadhi wa wanyamapori. Aidha misitu minene yenye afya tunayoiona sio kwasababu nyingine ila ni kwasababu ya utunzaji wa ardhi ambayo inatoa virutubisho na madini muhimu kwa misitu hiyo kuwepo, na uwepo wa misitu una manufaa yasiyo kifani kwenye suala zima la uhifadhi, misitu inabeba uhai wa maisha ya wanyamapori, ndege, wadudu na mimea mingine. Hakuna uhifadhi wa wanyamapori bila uwepo wa misitu.
Hivyo Rafiki yangu tunapozungumzia uhifadhi ni dhana inayoenda mbali sana hadi kufikia sehemu za chini kabisa za bahari ambapo kuna maisha yanaendelea na pia unaenda juu sana hadi kufikia kwenye mazingira yanayomfaa tai kuruka na kuzurura akiwa pekee, uhifahi unaenda kwenye maeneo yote ouvu, mabonde na mito, mabwawa na sehemu kame zisizofikiriwa kuishi kiumbe chochote, uhifadhi unaenda mpaka kwenye vilele virefu vya milima Kilimanjaro, unaenda kwenye tamabare na savanna isiyo na mwisho ya Serengeti. Hivyo dhana ya uhifadhi ni muhimu sana kwenye kuweka usawa kwa maisha ya wanyamapori. Lakini kubwa zaidi sio kwamba kwa juhudi kubwa zinazowekwa kwenye uhifadhi ni kwa ajili ya kufanya maisha ya wanyamapori yawe bora peke yake, lakini ni njia bora ya kufanya maisha ya binadamu kuwa bora hapa duniani.
Hivyo basi tunavyoweka juhudi kubwa kuhakikisha mazingira mazuri na ya kudumu kwa viumbe hai wetu, moja kwa moja tunakuta tunajifanyia wenyewe maisha yetu ya sasa na ya baadaye kuwa bora. Hivi ndivyo inavyotakiwa kueleweka na kujulikana kwenye masuala ya uhifadhi wa wanyamapori. Sio kwasababu tunawapenda saana wanyama lakini kwasabau kwa kufanya hivyo maisha yetu hapa duniani tunayaweka salama, na pia tunaifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi sisi na viumbe wengine. Hili ndilo jukumu tunalotakiwa kulifanya kwa nguvu zetu zote hadi siku tunaondoka hapa duniani.
Kuna mambo mengi tutajifunza kwa kadri siku zinavyokwenda, endelea kufuatilia na kujifunza kupitia mtandao huu wa Wildlife Tanzania, mengi mazuri yanakuja. Asante sana kwa kusoma makala hii, karibu kwa makala nyingine.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania