Tanzania bado inaendelea kushika kasi na kushikilia nafasi nzuri kwenye utalii na sehemu nyingi zenye mvuto na hadhi za kimataifa kutembelea. Maeneo yaliyo tulivu na yaliyo katika uasili wake ndio yameifanya Tanzania kutajwa mara kwa mara na mashirika makubwa duniani kuwa ndio sehemu bora kwa utalii. Nashawishika kusema Tanzania itaendelea kuwa bora wakati wote kwa sababu bado kuna mengi yanafanyiwa utafiti na hayajawekwa wazi kimataifa, siku yakija kuwekwa wazi dunia itashangaa.

Licha ya kuwa na idadi kubwa ya watu wanaoongezeka kuzaliwa na kufanya shughuli mbali mbali, bado Tanzania imeendelea kuwa na dhamira nzuri na ya dhati kwenye utunzaji na uhifadhi wa maeneo ya asili na maeneo yenye vivutio kwa kila kona ya nchi. Licha ya kutokuwa na utangazaji mkubwa na kutofahamika kama baadhi ya maeneo duniani, bado kwa njia hiyo ndogo tumeweza kutajwa na gazeti maarufu duniani linalojulikana kama National Geographic kuwa moja ya hifadhi kubwa kuliko zote Tanzania, hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni sehemu bora zaidi duniani kutembelea kwa mwaka 2018. Hili ni jambo zuri sana kwani kwa njia hii wameitangaza vizuri sana hifadhi ya Ruaha na nchi nzima ya Tanzania.

Nafasi hii ya kutajwa kuwa sehemu bora zaidi duniani kutembelea itasaidia pia kufungua milango mingi kwa hifadhi nyingine za kusini ambazo hazijajulikana na kuwa maarufu kama ilivyo kwa hifadhi za kaskazini mwa Tanzania. Hivyo kazi kubwa inabakia kwetu kama taifa na kama wahifadhi kushughulika na kuweka mazingira kuwa bora zaidi ili kuvutia watu wengi kwenye utalii wa nchi yetu.

Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kutajwa kuwa sehemu bora duniani kwa utalii ni jambo ambalo watu waliofika au waliowahi kutembelea hifadhi hii walilitarajia kwa sababu ni zaidi ya hapo, kama waliangalia wanyama, wapo zaidi ya hao walio waona, kama waliangalia ndege wapo zaidi ya hao walio waona, kama waliangalia miti na uoto wa asili upo zaidi ya huo walioona, kama waliangalia reptilia wapo zaidi kama ni mandhari nzuri na jografia ya hifadhi basi waliona sehemu chache. Hifadhi ya taifa ya Ruaha ni hifadhi kubwa sana, ni hifadhi ya kwanza kwa ukubwa ikiwa na ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 20,226. Hifadhi hii ni kubwa kuliko visiwa  vya Zanzibar, ni kubwa kuliko nchi ya Ruanda. Hivyo kama hujawahi kutembelea hifadhi hii basi mengi ambayo unayakosa kwenye hifadhi nyingi za Taifa utayapata hapa kwenye hifadhi hii nzuri.

Kwa upande mwingine watafiti wa mambo haya ya wanyamapori waliotumia muda mrefu kwenye utafiti na kuichunguza hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa miaka mingi wamewahi kusema kuwa hifadhi hii ya Ruaha kama utailinganisha na hifadhi nyingine kwa uzuri na idadi kubwa ya wanyama na mazingira asilia wanasema ubora wa hifadhi hii ni sawa na kuchukua hifadhi ya Taifa ya Serengeti ujumlishe na hifadhi ya Taifa ya Tarangire ndio angalau itafikia ubora na hadhi ya hifadhi hii kubwa. Kuna mengi yanayoelezeka na yasiyoelezeka unapotembelea hifadhi hii, hutatamani kuondoka maana utashibishwa na kila hali ya asili inayovutia.

Kwa hifadhi hii kuona wanyama adimu kama simba, chui, fisi, duma, nyati na wakati mwingine mbwa mwitu sio lazima uwe na bahati ili uwaone, utawaona tuu, uwe una bahati au uwe huna bahati, wanyama hawa wapo wengi sana kwenye hifadhi hii kubwa. Maana kwenye hifadhi nyingine watakwambia kama una bahati utaona simba, nakwambia sio hivyo kwa hifadhi hii ya Ruaha, simba wapo wengi sana tena makundi makuba yenye watoto, madume na majike. Kwa kweli kwenye ardhi ya hifadhi hii kuna historia nyingi sana za kuvutia ambazo nikaandika kwenye makala hii nitachukua siku na miezi mingi kumaliza. Nakushauri tu panga kutembelea hifadhi hii utaniambia na kusimulia kila utakapokuwa hakika utaondoka na kumbu kumbu nzuri isiyoisha.

Unaweza kujiuliza hifadhi hii ipo wapi hapa Tanzania, maana wengi hawaijui hifadhi hii, mwingine ukitaja ruaha anawaza na ruaha mbuyuni wanakolima nyanya na vitunguu, hahaha, hapana hii ni Hifadhi ya taifa ya Ruaha ambayo ipo mkoa wa Iringa. Hifadhi hii inafikika kwa usafiri wa anga au kwa kutumia barabara ya vumbi kutoka Iringa mjini hadi getini. Uchaguzi ni wako uje na ndege au uje na gari yote yanawezekana na utafika katika hifadhi hii kubwa. Kwa wengi wasio fahamu kama unatumia barabara kutoka Iringa mjini hadi kufikia geti la hifadhi hii ni kilomita 100. Ni umbali mrefu kidogo, hivyo kama unapanga kutembelea ujipange kwa hilo, lakini yote utafurahia safari yako na wala hutajuta, maana mtapita kwenye barabara yenye vivutio na uoto mwingi wa asili, hivyo utaanza kutalii kuanzia unapokuja kutoka Iringa mjini hadi getini. Karibuni sana Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Nimalizie makala hiikwa kukupa hamasa hii, panga kutembelea hifadhi hii kabla yam waka huu kuisha, njoo uone kwanini wanaiseme hifadhi hii kuwa ni sehemu bora zaidi duniani. Njoo uone zaidi ya hayo, karibu kwenye hifadhi kubwa kuliko zote Afrika Mashariki. Njoo uone fahari ya Tanzania, njoo uone miji na tamaduni za wenyeji ambako hifadhi hii ipo, njoo ufurahi, njoo ujifunze, njoo ruaha National Park. Karibu sana kwa maswali, maoni, ushauri, mapendekezo, karibu sana.

UKIJA KUTEMBELEA HIFADHI YA RUAHA USISAHAU KUJA NA KAMERA YAKO.

Ahsante sana

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania