Tembo wanapatikana katika maeneo ya Kusini mwa Jangwa la Sahara hasa maeneo yenye misitu ya maji, savanna, na maeneo ya jangwa. Mara kwa mara tembo huwa wanahama kwa vipndi maalumu vya mwaka na ni ngumu kutabiri mwelekeo wao katika kipindi hiki. Hivyo basi maeneo ambayo tembo wanahamia na kuyatembelea ndio maeneo yao asili yanayohitaji kutunzwa na kuhifadhiwa.
Rafiki msomaji wa makala hii ya uchambuzi kutoka katika ripoti hii maarufu inayoitwa ELEPHANT IN THE DUST, THE AFRICAN ELEPHANT CRISIS. Ni ripoti inayoelezea kwa kina mambo mengi yanahusiana na historia, makazi, maisha, biashara na ujangili wa tembo na biashara ya meno ya tembo. Hivyo kwa sehemu tu nimejaribu kukuchambulia yale muhimu ambayo nakwenda kukushirikisha kwenye makala hii fupi. Kama utahitaji ripoti hii ili uisome kwa kina tuwasiliane. Karibu sana tuendelee na uchambuzi wetu.
Tembo wa Kaskazini mwa Afrika walishatoweka tangu enzi ya zama za Kati za utawala wa nchi za Ulaya (European Middle Ages) na sasa wanapatikana katika nchi 35-38 zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara. Hata hivyo uwepo wa tembo kwenye nchi hizi tatu za Senegali, Somalia na Sudani upo mashakani sana. Kama makadirio yanavyoonyesha kuwa asilimia 39 ya tembo wote wa Afrika ipo Kusini mwa Afrika, wakati asilimia 29 ipo Afrika ya Kati na asilimia 26 tu ndio ikionyesha idadi ya tembo waliopo Mashariki mwa Afrika na wakati huo takwimu zikionyesha kuwa ni asilimia 5 tu ya tembo wote wa Afrika ndio wapo Afrika Magharibi.
Hata hivyo kujua kwa ufasaha kuhusu maeneo yote yenye tembo ni zoezi gumu sana maana ukusanyaji wa taarifa hizi mara nyingi huwa ni wa mtu mmoja na wakati mwingine anakuwa hana uwelewa wa kutosha kuhusu wanyama hawa na miendendo yao. Hii ni kwa mijibu wa takwimu na jinsi mambo yanavyochukuliwa kuhusu tembo.
Inaaminika na ndivyo ilivyo kuwa maisha ya tembo ni ya kuhama hama kwa vipingi maalumu vya mwaka, hata hivyo katika kutotambua tabia hizi za asili za wanyama hawa kumechangia kutokuwa na taarifa za kutosha na nzuri katika sensa ya wanyama hawa. Wakati mwingine unaweza ukafikri tembo wapo tu ndani ya hifadhi, na bila kujua kuwa wanaweza kuvuka mipaka na kuingia nje kabisa ya maeno yao ya kawaida.
Wakati ujangili wa tembo ukiwa ni njia ya moja moja katika kuhatarisha uwepo wa tembo , maeneo ya tembo na kutoweka kwa makazi asilia ya tembo imetajwa kuwa ndio hatari moja kubwa zaidi inayotishia maisha ya wanyama hawa hapa duniani.
Kuna sababu nyingi nzuri za kuelezea kuwa kuna kutoweka kwa maeneo ya wanyama hawa kwa zaidi ya miongo miwili iliyopita. Mwaka 1995 eneo lote la tembo wa Afrika lilikadiriwa kuwa ni asilimia 29, hata hivyo ripoti ya hivi karibuni inayoelezea hali ya tembo wa Afrika inasema kuwa eneo la asilimia 15 tu ya bara la Afrika ndio limebaki kama eneo la makazi, mapito na maingilio ya tembo.
Pamoja na taarifa hizo, tunatakiwa kujua kuwa kupungua kwa maeneo ya tembo barani Afrika ni kutokana na sababu za uharibifu wa mazingira, upanuzi wa makazi ya watu kutokana na ongezeko la watu, kukua kwa miji, upanuzi wa mashamba na ujenzi wa miundombinu mbali mbali ya maendeleo.
Hata hivyo taarifa zinasema kuwa ingawa Afrika Magharibi imepoteza kwa kiasi kikubwa maeneo ya asili ya tembo kwa sababu za maendeleo ya watu na miji, hali ni tofauti kabisa kwa nchi ya Botswana ambayo ipo Kusini wa bara la Afrika, inaonyesha kuwa makazi na maeneo ya tembo kwenye nchi hii yameongezeka na kutunzwa vizuri sana, jambo ambalo linafanya nchi hii kuwa na idadi nzuri ya wanyama hawa.
Hata hivyo kwa taarifa za satellite zilizopigwa katika bara hili zinaonyesha hali ya mabadiliko ya tabia nchi, kubadlika kwa uoto na jinsi ambavyo shughuli za kibinadamu kama vile uchimbaji madini, uchafuzi wa mazingira, ukataji wa miti hovyo na mambo mengine mengi yanayochangia kuharibika kwa misitu na maeneo asilia ya wanyamapori muhimu kama tembo. Katika mwenendo wa aina hii kwenye makazi ya wanyamapori inasemwa kuwa hali ikiachwa itasababisha asilimia 63 ya uharibifu zaidi kwa miaka 40 ijayo, utabiri huu unaelekezwa zaidi kwa upande wa Mashariki mwa bara hili la Afrika.
Aidha, hali hii ikiendelea bila kutafutiwa ufumbuzi watalaamu wa mambo haya wanasema itasababisha janga kubwa sana kwa tembo wa Afrika Mashariki, na hapo ukiongezea na ujangili mambo ndio yatazidi kuwa mabaya zaidi. Ujangili pamoja na uharibifu wa mazingira na makazi ya wanyamapori itasababisha kutoweka kwa haraka kwa wanyama hawa na makazi yao. Hata hivyo utabiri huu unaenda mbali sana kwa upande wa nchi zilizo Magharibi mwa Afrika ikiwa hawatachukua hatua na maamuzi magumu kuokoa maliasili zao, basi wanyamapori hawa wanaweza kutoweka kabisa kwenye nchi hizo.
Rafiki msomaji wa makala hizi, katika uchambuzi wa sehemu hii ya pili ambapo tulikuwa tunachambua matukio na makazi ya tembo. Kuna mambo mengi yametajwa sana kwenye makala hii ambayo yamepelekea na yanapelekea kupungua kwa idadi ya tembo na maeneo yao.
Hivyo basi nchi zetu zinatakiwa kutunza sana maeneo ambayo wanyama hawa wanayatumia kama sehemu yao asilia ya kuishi na kuzaliana. Tembo ni wanyamapori wanaohitaji maeneo makubwa kwa ajili ya usalama wao. Hata hivyo maeneo hayo makubwa yana faida si kwa uwepo wa tembo tu bali hata kwa wanyama na vumbe hai wengine wanaoishi katika maeneo hayo.
Ahsante sana kwa kusoma makala hii hadi mwisho!
Uchambuzi huu umeandaliwa na;
Hillary Mrosso
+255 683 862 481/255 742 092 569
www.mtalaamu.net/wildlifetanzania