Habari rafiki na msomaji wa mtandao wetu wa Wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo. Katika makala ya leo nimeandika mambo kwa ufupi sana kwa sababu ni jambo linaloeleweka sana. Lakini ingawa jambo hili linaeleweka kwa wengi, sio wengi wanalipa kipaumbele kwenye mipango na malengo yao. Nilitaka kukumbusha jambo hili mapema kabisa kabla hatujaenda mbali au kabla mwaka huu haujasogea sana, na ninaamini kabisa kuwa ulishajiwekea malengo yako kwa mwaka huu wa 2018, kwamba unataka kufanyi nini, unataka kukamilisha nini, lakini katika orodha ya malengo na mipango yako inawezekana kabisa umesahau jambo moja la muhimu sana kwako, na hujaliandika kwenye malengo yako, jambo lenyewe ni mwaka huu unataka kutembelea vivutio gani?, au unataka kutembelea hifadhi gani ya wanyama?
Naamini kabisa kwa wengi hawajaweka lengo hili kwenye orodha ya mipango yao ya mwaka 2018. Rafiki yangu ngoja nikushauri kitu, mara zote ni wewe unafanya kazi, ni wewe unahangaika huku na huko kutafuta fedha za kuendshea maisha yako, unaamka asubuhi unarudi jioni umechoka na maisha yanaendelea kuwa na changamoto nyingi sana. Nataka nikwambie kitu kimoja hata kama unapata fedha kidogo namna gani lazima kuwe na sehemu kidogo ya fedha hizo unazozipata kwa shida na taabu unazitumia kwa ajili ya kufurahi, starehe kidogo na mapumziko mazuri ambayo hayana usumbufu kabisa. Hivyo tenga sehemu ndogo ya fedha au mshahara wako unaoupata ili unapoamua kupumzika labda mwishoni mwa mwaka, au kulingana na ratiba yako basi utakuwa na fedha za kwenda sehemu yoyote na kuzitumie fedha zako.
Kwa sasa zama zimebadilika sana kipindi cha nyuma watanzania wengi walikuwa hawana utaratibu wa kutembelea hifadhi za wanyama au vivutio mbali mbali ndani ya nchi yao. Lakini kwa miaka ya hivi karibuni mambo yamebadilika na watanzania wameanza kuchukua hatua, utawaona wapo hifadhini na familia zao, marafiki zao wakipiga picha wanyamapori na vitu vingine vinavyovutia. Jambo hili linatia moyo sana na ni jambo ambalo tunatakiwa kulifanya na kuwafundisha marafiki na majirani zetu kuhusu kutembelea hifadhi za wanyamapori na vivutio vingine.
Ninachoamini kabisa sio kwamba watanzania hatupendi kutembelea mbuga za wanyama au vivutio vingine, bali ni fursa hizi hazikuwa wazi na kueleweka kwa watu wengi hivyo jambo hili kuwa gumu na kutofahamika kwa watu wengi. Lakini kwa sasa tupo kwenye zama za taarifa na vifaa kama simu na mitandao ya kijamii imerahisisha sana kuwafikia watu wengi na kutangaza kitu chochote kupitia mitandao hii. Hata mimi ninahamasika sana kuandika makala hizi kwa sababu najua zinawafikia watu na wanazisoma na kuchukua hatua, hata kama hawatachukua hatua sasa lakini naamini kwa ufahamu na maarifa anayopata atakuja kuyafanyia kazi siku moja. Hivyo basi unapopata maarifa na taarifa kama hizi na kuzisambaza au kuwatumia wengingine utakuwa umefanya jambo kubwa na la kizalendo kwani unasambaza taarifa nzuri na zenye tija na watu watakushukuru kwa jambo hilo.
Sasa basi rafiki yangu, kama ulikuwa hujaweka lengo la kutembelea hifadhi yoyote au sehemu yoyote ya kuvutia, weka lengo lako hilo kwenye orodha ya malengo yako ya mwaka huu. Na sio lazima uweke lengo la kutembelea hifadhi tu, kuna sehemu nyingine nzuri sana za kutembelea, kama vile sehemu za utamaduni wa kale au sehemu za kihistoria, sehemu kama kwenye fukwe za bahari, kupanda milima, kwenye sehemu zenye vivutio vya maporomoko ya maji, jangwani au hata kwenye miji mikubwa, makumbusho mbali mbali, nk. Hivyo anza pale ambapo unaweza kwenda kwa urahisi lakini usiache kuweka lengo lako la kutembelea kivutio chochote mwaka huu. Nimekuambia jambo hili mapema ili uliweke na kujipanga kufanya hivyo.
Nitafurahi sana kujua unataka kutembelea kivutio gani kwa mwaka huu, pia inawezekana unatamani kutembelea vivutio ila hujui uanzie wapi, au uanze na wapi, usisite kuwasiliana nasi tutakujuza na kukusaidia ili ujue kisha uchague pa kwenda kutembelea. Pia hata kama kwenye malengo yako umeandika una mapango wa kutembelea sehemu fulani, nitafurahi kujua hilo pia. Naamini utaandika na kuongeza lengo hili ambalo umelisahau, liandike basi kwenye notbook yako au diary yako, halafu lipitie mara kwa mara na uweke uwezekano na mikakati ya kulifikia na kulitimiza.
Asante sana kwa kusoma makala hii, mshirikishe na mwenzako makala hii aisome ili kama amesahau kundika lengo hili aliandike mapema. Naamini utafanya hivyo, nakushukuru sana rafiki yangu. Tukutane kwenye makala nyingine bora zaidi.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania