Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania, nikupongeze kwa kuingia mwezi mwingine, mwezi Julai. Katika makala ya leo nimekuandalia historia fupi ya biashara ya uwindaji wa kitalii Tanzania. Makala hii ninayokuandalia ni baada ya kusoma majarida mbali mbali na kuiona makala hii iliyoandikwa kwenye jarida maarufu la KAKAKUONA toleo namba 13 la Julai – Septemba 2010, makala hii nzuri iliyoandikwa na Hochi Rajabu, inapatikana katika ukurasa wa 20 wa jarida hili maarufu la Kakakuona. Baada ya kuisoma makala hii nimevutiwa sana , nikaamua niiandike kama ilivyo kwenye blog hii ili kukushirikisha haya ambayo nimejifunza kuhusu biashara ya uwindaji wa kitalii Tanzania, hivyo nikukaribishe ufuatane nami ili upate mwanga na maarifa haya muhimu.
Uwindaji ni moja ya shughuli za kijadi katika jamii nyingi za Kiafrika. Uwindaji wa jadi ulikuwa kwa madhumuni ya jamii kupata kitoweo, ingawa mapambo kama ngozi vilionyesha ushujaa wa aina fulani miongoni mwa sababu kuu za uwindaji wa kijadi.
Mfano ni kwa kabila la Kimasai ambapo kijana haonekani na jamii kama ni shujaa iwapo hatakuwa amepambana na simba au chui na kumuua. Iwapo kijana au morani wa kimasai atafanikiwa kuua mmoja kati ya wanyama hao atakuwa amejipatia kibali cha kuoa au kuwa na boma lake.
Mila hizo kwa sasa hazitumiki tena kama kigezo cha kijana kuonekana kuwa amepevuka na kustahili kuoa au kuonekana shujaa katika jamii inayomzunguka. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wanyama hao kwa sasa ni adimu kuwapata na kuonekeana kwa mila hizo kwenda kinyume na uhifadhi wa wanyamapori.
Tofauti na uwindaji wa sasa, uwindaji wa jadi haukuwa na kibali chochote. Wanajamii walikuwa wanapanga ni lini na wapi wakawinde. Aidha, hakukuwa na vigezo ni mnyama gani wa kuwinda isipokuwa kwa wanyama kama simba au chui labda awea ameshambulia wanadamu au mifugo ndipo wanajamii hupanga kumwinda mnyama husika.
Kwa upande mwingine upo uwindaji wa kitalii. Tofauti na ule wa jadi, uwindaji wa kitalii ni wa kupangwa kuanzia mnyama wa kuwinda kwa aina,idadi na wapi. Aidha huwezi kuwinda bila kuwa na kibali siku hizi. Uwindji wa kitalii ni moja ya vyanzo vya mapato kwa nchi yetu. Kwa mfano kwa miaka miwili ya nyuma (2008 na 2009) uwindaji huu umeiingizia Tanzania kiasi dola za Kimarekani 38,205,693.00. (Miaka miwili ya nyuma kabla ya mwaka 2010, na kabla ya kuchapishwa kwa makala hii katika jarida la Kakakuona).
Nchini Tanzania uwindaji wa kitalii ulianzishwa kabala ya vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, chini ya sharia Kuu ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura 302 ya mwaka 1956 (Fauna conservation Ordinance Cap.302 of 1956). Uwindaji ulisimamiwa na watu binafsi na wawindaji walitoka nchi mbali mbali duniani.
Mwaka 1964 Shirika la “Tanganyika Wildlife Development” liliundwa ili kusimamia shughuli za uwindaji badala ya watu binafsi. Shirika hilo lilikuwa na wakala 25. Wakala hizo zilikuwa za kigeni ambapo waliajiri wawindaji bingwa wa kigeni.
Utengaji wa maeneo ya uwindaji wa kitalii (vitalu) ulianza mwaka 1967 wakati Pori la Akiba la Selous lilipogawanywa katka vitalu 47 na baadaye utengaji huo uliendelea kufanyika katika maeneo mengine. Mwaka 1973 hadi mwaka 1978, serikali iliamua kufunga shughuli zote za uwindaji nchini kutokana na kuongezeka kwa ujangili, hususani Tembo na Faru. Katika muda huo serikali ilichukua hatua zifuatazo. Kwanza ilifuta sharia ya kuhifadhi wanyamapori (Fauna conservation Ordinance Cap. 302 of 1956) na badala yake ikatunga sharia ya Hifadhi ya Wnyamapori (The Wildlife Conservation Act No.12 of 1974) kwa ajili ya kusimamia masuala yote yanayohusu uhifadhi na uendelezaji wa wanyamapori nchini.
Pili. Iliunda shirika la Umma la Wanyama wa porini (Tanzania Wildlife Corparation – TAWICO) mwaka 1976, ambalo lilikabidhiwa jukumu la kusimamia shughuli za matumizi endelevu ya wanyamapori ikiwa ni pamoja na uwindaji wa kitalii.
Mwisho iliunda kikosi dhidi ya ujangili kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la ujangili mwaka 1978. Mwaka huo huo 1978 serikali ilifungua shughuli za uwindaji wa kitalii na kukabidhiwa usimamizi kwa Shirika la Wnayama wa porini Tanzania (Tanzania Wildlife Corparation – TAWICO). Hata hivyo kutokana na ukubwa wa maeneo ya uwindaji wakati huo (Mapori ya Akiba, Mpori Tengefu na Mapori ya Wazi), Shirika la Wanyama wa porini halikuwa na fedha na vifaa vya kutosaha kuweza kuendesha uwindaji wa kitalii ipasavyo, hivyo lilikaribisha makampuni binafsi kuendesha biashara ya uwindaji wa kitalii, chini ya usimamizi wake kwa kutoza asilimia 45 ya ada ya kila siku.
Mwaka 1988 serikali iliamua kuwa Mashirika ya Umma yasijishughulishe na masuala ya usimamizi na badala yake kuweka juhudi kwenye uzalishaji. Kutokana na uamuzi huo, usimamizi wa shughuli za uwindaji ulirejeshwa Wizara ya Maliasili na Utalii, chini ya Idara ya Wanyamapori, ambayo bado inaendelea na jukumu hilo hadi sasa.
Mpaka kufikia hapa naamini umepata mwanga kidogo kuhusiana na historia ya biashara ya uwindaji wa kitalii Tanzania. Haya mambo ni muhimu kuyajua ili tuelewe mifumo, na utendaji kwenye sekta hii nyeti ya wanyamapori Tanzania. Naamini kabisa kwa kadri siku zinzvyokwenda tutaendelea kujifunza mengi naya muhimu sana kwenye wanyamapori na maliasili zetu kwa ujumla. Hivyo endelea kufuatilia na kuwashirkisha wengine maarifa haya muhimu.
Asante kwa kusoma makala hii,
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
0742092569/0683862481