Baada ya kusoma uchambuzi wa ripoti hii maarufu inayoitwa “EUROPE DEADLY IVORY TRADE”, sasa ni wakati wa kujifunza mapendekezo ya ripoti hii baada ya kufanya utafiti wa kina. Haya ndio mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Ulaya baada ya kubainika kwa tatizo kubwa walilokuwa nalo. Mapendekezo haya ndio yanayoonyesha hatua za dhati watakazochukua Ulaya ili kukomesha kabisa biashara haramu ya meno ya tembo, pia kufunga masoko yote ya meno na bidhaa za meno ya tembo. Mapendekezo haya ndio yanahitimisha uchambuzi wa ripoti hii. Karibu tujifunze pamoja.

SOMA:Mambo Usiyoyajua Kuhusu Nchi Za Umoja Wa Ulaya Zilivyochangia Kushamiri Kwa Ujangili Wa Tembo Barani Afrika

Kutokana na utafiti uliofnyika kila kitu sasa kipo wazi, na Ulaya haina budi kuachana na msimamo wake kuwa haijihusishi na biashara haramu ya meno ya tembo, kutokana na mwanya uliokuwepo uendeshaji wa biashara za bidhaa ya vitu na mapambo yaliyotengenezwa na meno ya tembo kufanyika bila kibali chochote kulitengeneza nafasi na mianya mikubwa ya biashara haramu kushamiri, hivyo kuchochea ujangili wa tembo katika bara la Afrika. Hivyo basi sasa ni wakati wa kuchukua hatua za kusitisha kabisa biashara za aina hiyo kwa nchi za Ulaya.

Tume ya Ulaya imetangaza kuweka mazuio mengine kwa biashara ya meno ya tembo miezi michache ijayo. Watafiti wa mambo wanasema mazuio hayo yatakuwa na tija endapo yatazibiti biashara ya bidhaa au mapambo ambayo yametengenezwa na meno ya tembo ambayo ndio hutoa mwanya kwa biashara nyingine haramu kuendelea bila kujulikana Ulaya nzima.

SOMA: Teknolojia Ya Kutumia RADIOCARBON Ilivyosaidia Katika Vita Dhidhi Ya Ujangili Na Biashara Haramu Katika Nchi Za Umoja wa Ulaya

Kusitisha kwa biashara ya meno ya tembo inaoendelea sasa katika umoja wa Ulaya itasaidia sana katika kuweka mfano au kielelezo kizuri kwa nchi nyingine za Ulaya kuchukua hatua katika kusitisha na kupambana na ujangili.

Pamoja na kwamba ulaya imedhamiria kusitisha biashara ya meno ya tembo kwenye masoko yake ya ndani, imetoa msamaha kwenye vitu hivi ambavyo vingi villitengenezwa na meno ya tembo;

Vitu au bidhaa zilizotengenezwa na meno ya tembo chini ya asilimia 10 (kwa ujazo) na ambazo zimetengenezwa kabla ya mwaka 1947.

Vifaa vya muziki ambavyo vilitengenezwa kabla ya mwaka 1975 na viwe vina kiasi cha chini ya asilimia 20 ya meno ya tembo.

Bidhaa au vile vitu muhimu sana ambavyo vina angalau miaka 100, vitu hivyo vitakaguliwa na kuchunguzwa na wataalamu kabla ya msamaha huo kutolewa.

Msamaha maalumu utatolewa kuwa vitu vidogo sana ambavyo vinajumuisha michoro ya aina mbali mbali ambayo imechorwa na kiasi kidogo sana cha meno ya tembo na pia kama inahusisha biashara kati ya makumbusho ambazo zimeruhusiwa kisheria.

Kila linalowezekana linatakiwa kufanyika ili kusitisha na kuzuia kabisa biashara ya meno ya tembo sehemu yoyote ile duniani, kwa sababu endapo kutakuwa na kibali cha kuuza, kununua au kusafirisha meno ya tembo sehemu yoyote ile duniani, basi tujue tutakua tumeamsha tena mambo magumu amabayo yatatusumbua na kutugharimu kuyadhibiti tena.

Vita dhidi ya ujangili vinatugharimu vitu vingi sana, ukiachilia mbali fedha na rasilimali nyingine, kupambana na ujangili inatugharimu maisha yetu, siku zote maisha ya watu ambao wanasimamia rasilimali hizi yapo hatarini. Hii ni kutokana na tamaa ya utajiri, rushwa, umasikini, sheria dhaifu za uhifadhi na usimamizi; na yote inachochewa na kitu kimoja kikubwa, mahiaji makubwa ya meno ya tembo kwenye nchi nyingi za Asia, Ulaya na Marekani.

Naamini kabisa hatua amabzo nchi mbali mbali zinachukua ili kunusuru tembo wetu ni muhimu sana, na tunataka dunia yote ifahamu jambo hili moja hakuna kizazi chochote cha sasa au baadaye kitakachofurahia unyama huu dhidi ya wanyamapori hasa tembo. Tuwaache wanyamapori waendelee kuwepo kwa faida ya wengi.

Ripoti hii niliyoichambua ina mambo mengi ambayo yapo kwa mifano na picha, napongeza juhudi zote hizi katika kutumia teknolojia kupambana na ujangili, hii ni hatua moja kubwa sana ambayo itasaidia kuchukua hatua nyingine kubwa zaidi katika uhifadhi wa wanyamapori na maliasili kwa ujmla. Tutumie kila tulicho nacho kwa manufaa zaidi na kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi si kwa binadamu pekee bali hata wanyamapori na viumbe hai wengine.

Nakushukuru sana kwa kusoma makala hii, tukutane tena hapa hapa kwa makala nyingine kubwa zaidi.

Asante sana!

Mchambuzi wa ripoti hii ni;

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania