Leo tutaingia darasani kumjua mnyama TWIGA ambae hujulikana kutokana na maringo yake na hata watu kumwita mnyama mwenye maringo. Kabla hatujaenda kwenye maudhui ya makala hii napenda ndugu msomaji ufahamu kwamba twiga ni wanyama wenye asili ya Afrika na endapo utawaona twiga nje ya bara la Afrika basi ujue twiga hao walichukuliwa barani Afrika na kupelekwa huko ulipo waona nje ya bara la Afrika. Pia napenda ujue kuwa twiga wamegawanyika katika jamii kuu nne ambazo ni

  1. Twiga wa kaskazini, ambao hawa wamegawanyika katika makundi madogo manne
  2. Twiga wa kusini ambao nao wamegawanyika kwenye makundi madogo mawili
  3. Twiga retikulamu/Twiga Somali na
  4. Twiga Masai au Kilimanjaro.

Picha ya twiga masai kutoka katika hifadhi ya Taifa ya Saadani; Picha na Elisante Kimambo

Tofauti kubwa ya twiga hawa huwa ni mpangilio wa rangi katika miili yao na baaadhi tu ya sifa ndogo ndogo kama uzitio na urefu.

Ila sifa karibu nyingi zilizobaki twiga hufanana kwa kiasi kikubwa sana. Labda tunaweza kusema mazingira pia wanayo patikana jaamii husika ya twiga huenda ikawa pia ni namna ya kuwa tofautisha wanyama hawa. Bonyeza hapa kufahamu zaidi kuhusu twiga.

Sasa leo hapa kwa undani tutamchambua twiga aina moja halafu hao wengine tutawapangia siku. Na moja kwa moja leo tutamzungumzia TWIGA MASAI AU TWIGA KILIMANJARO.

Sifa na tabia za Twiga Masai / Twiga Kilimanjaro

  • Hawa ndio twiga wakubwa kuliko jamii nyingine zote za twiga nilizo taja hapo juu. Lakini ukumbuke pia twiga ndio wanyama wenye kimo kirefu kuliko wanyama wote waishio ardhini duniani.
  • Ni wanyama wenye miguu mirefu yenye nguvu sana ambao wana uwezo wa kupiga kwa kutumia miguu ya nyuma naya mbele pia.
  • Ndio wanyama pekee duniani ambao miguu ya mbele na ya nyuma ya upande mmoja hujongea kwa wakati mmoja. Yani anapoinua mguu wa mbele wa kulia basi hufuatana na mguu wa nyuma wa kulia tofauti na wanyama wengine lakini hata binaadamu pia kwasababu mguu wa kushoto huenda na mkono wa kulia.
  • Ni mnyama mwenye moyo mkubwa sana na wenye nguvu, wenye uzito wa takribani kilogramu 11kg ambao unaweza kusukuma lita 60 – 75 za damu kwa muda wa dakika moja.
  • Hawa ndio wanyama wenye mkia mrefu kuliko wanyama wote waishio ardhini ambapo mkia huwa na urefu wa hadi futi 3.3.
  • Twiga masai jike huwa na nywele nyingi kichwani wakati dume huwa ana nywele chache sana.
  • Ulimi wa twiga hawa huwa na urefu kati ya inchi 18 – 20.
  • Wana uwezo wa kukimbia umbali wa kilometa 55km – 60km kwa saa. (55-60km/saa).
  • Wana shingo ndefu ambayo hufika hadi inchi 78.
  • Twiga hawa wana mabaka ambayo yaonekana bila mpangilio, dume akiwa na mabaka mengi meusi kuliko jike. Muonekano wa mabaka haya ndio huweza kuwatofautisha twiga hawa na jamii nyingine za twiga.
  • Katika mashingo yao wana mifupa sawa kama ilivyo mifupa ya binaadamu shingoni.
  • Twiga hawa wanapo chezesha au kupigiza shingo ni sawa na mtu aliye beba mzigo wa uzito wa kiligramu 240kg – 250kg.
  • Ni wanyama ambao huishi kwa makundi, na kundi linaweza kuwa na idadi ya twiga hadi 14.
  • Twiga hutumia muda mfupi sana kulala ukilinganisha na muda anaotumia kwenye kula masaa 4-5 kulala.
  • Ni wanyama ambao huishi kwa kuvumiliana sana wawapo kwenye kundi hususani majike. Huishi kwa upendo bila kunyanyasana tofauti na ilivyo kwa madume hasa unapofika msimu wa kuzaliana.
  • Uzito, huwa kuna utofauti kati ya uzito wa dume na jike ambapo dume huwa na uzito mkubwa kuliko jike. Dume hufikia uzito wa kilogramu 1100kg – 1900kg(sawa na tani 1.1-1.9) wakati jike huwa na uzito wa kilogramu 700kg – 1200kg(sawa na tani 0.7-1.2).
  • Kimo, kama ilivyo kwenye uzito hata urefu pia huwa kuna tofauti kati ya jike na dume japo huwa sio kubwa sana kama kwenye uzito. Dume hufika urefu wa futi 19(sawa na mita 5.5) huku jike akiwa na urefu wa futi 16 -18(sawa na mita 4m – 5m.

Je, Wajua?

Twiga ni wanyama wanao zaliwa wakiwa na pembe? Hii ni sifa ya wanyama wachache sana na inasemekana ni twiga pekee tu, japo kuna baadhi ya tafiti zinaonyesha kuna baadhi ya jamii za kina pofu huwa wanazaliwa na pembe. Lakini hii kwa hakika twiga huzaliwa akiwa na pembe.

Ndio wanyama pekee duniani ambao miguu ya mbele na ya nyuma ya upande mmoja hujongea kwa wakati mmoja. Yani anapo inua mguu wa mbele wa kulia basi hufuatana na mguu wa nyuma wa kulia tofauti na wanyama wengine lakini hata binaadamu pia kwasababu mguu wa kushoto huenda na mkono wa kulia. Zaidi soma hapa; Haya Ndio Mambo Usiyoyajua Tunayofanana Binadamu Na Mnyama Twiga

Mazingira na sehemu wanazo patikana Twiga Masai

Twiga ni wanyama ambao wana uwezo wa kuishi katika mazingira mbali mbali yakiwemo maeneo ya savanna, maeneo yenye nusu jangwa lakini pia maeneo yenye miti miti mingi na vichaka.

Mazingira haya ni mazuri kwani huwa na chakula cha kutosha kwa wanyama hawa kwani ni wanyama wanaokula chakula kingi sana.

Nchi ambazo utaweza kuwapata jaami hii ya twiga ni Tanzania na Kusini mwa Kenya. Japo inasemekana walikuwa wakipatikana pia nchini Ethiopia na Somalia, katika kipindi cha miaka mingi iliyopita, pia kuna namna watafiti wa wanyama hawa wanaamini aina hii ya twiga ilishatoweka maeneo hayo.

Picha ya Twiga Masai katika hifadhi ya Taifa ya Nyerere; Picha na Hillary Mrosso                                                                                                                                                                                        

Chakula

Twiga ni jamii ya wanyama walao majani na hutumia muda mwingi sana kwenye kula kuliko kupumzika. Wanaweza kutumia masaa 16 – 20 wakiwa wanakula tu au kama hawajapata chakula basi wanaweza kutumia masaa hayo kutafuta chakula na kupumzika masaa manne tu.

Twiga ni wanyama ambao matumbo yao yamegawanyika katika sehemu nne kama walivyo ng’ombe, nyati, pofu na baadhi ya wengine pia.Huweza kula kilogramu 30kg – 35kg kwa siku. Baada ya kula majani huyahifadhi tumboni na baadae kuya cheuwa kasha huyatafuna upya na kuyameza moja kwa moja.

Asilimia 75% ya chakula cha twiga hutokana na jamii ya miti ya michongoma na akasia. Mdomo na ulimi wa twiga humsaidia kuweza kula hata maeneo yenye miba na hasa majani machanga yaliyo juu kabisa ya mti. Wanapo kula dume huwa anakula sehemu ya juu kabisa huku jike akila sehemu ya chini na hii ni kutokana na tofauti ya kimo iliyopo baina yao.

Twiga huweza kukaa siku 2-3 bila kunywa maji kwasababu maji mengi huyapata kupitia majani wanayo kula. Anapo fika sehemu yenye maji hupata shida sana wakati wa kunywa maji kutokana na miguu ya mbele ilivyo mirefu. Huwa anakunywa hadi lita 37 za maji kwa siku endapo atakuwa anayapata kila siku.

Kuzaliana

Inapofika wakati wa kuzaliana madume huwa wanapigana sana kwa kutumia mashingo na dume anaeshinda ndio huwapanda majike. Kupigana huku kunaweza chukua nusu saa hadi saa zima mpaka mmoja atakapo shindwa. Huwa hakuna msimu maalumu wa kuzaliana kwa twiga hawa na hii huweza tokea wakati wowote wa majira ya mwaka.

Twiga hawa huwa na uwezo wa kuzaa au kupanda wafikishapo umri wa miaka 3 – 4 japo kwa upande wa madume huwa hawawezi kupanda majike mpaka wafishapo kuanzia miaka saba. Hii ni kwasababu wanakuwa hawajapata uwezo wa kupigana hivyo kwa kipindi hiki hujifunza kwanza kupigana kupitia madume wakubwa.

Mara baada ya kupandana jike hukaa na mimba kwa muda wa miezi 14- 15, kisha huzaa mtoto mmoja tu. Twiga ni baadhi ya wanyama wachache wanaozaa wakiwa wamesimama kitu ambacho unaweza sema mtoto anapo dondoka aridhini ataumia.

Kumbe haipo hivyo kabisa huwa hapati hata jeraha moja wakati wa kuzaliwa kutokana na anavyo dondoka chini. Mtoto wa twiga huzaliwa akiwa na uzito wa takribani kilogramu 90 na mara baada ya dakika 20 au saa moja baada ya kuzaliwa mtoto huanza kutembea.

Mtoto hutegemea maziwa ya mama kwa muda wa mwaka mzima kwani katika kipindi hiki anakuwa hana uwezo wakula majani vizuri hasa majani ya juu kama waliyo twiga wakubwa.

Mama hujitahidi kumlinda mwanae kwa hali na mali na huwa anageuka mara kwa mara kuangalia maadui wakati wa kula ili mwanae awe katika hali salama.

Asilimia 50% mpaka 75% ya watoto wa twiga huwa wana uwawa na maadui katika kipindi cha miezi ya mwanzoni baada ya kuzaliwa. Ila watoto wanao fanikiwa kukua zaidi ya mwaka mmoja au miwili huwa wanajiunga na kundi la twiga wakubwa na hapo maisha huendelea kama kawaida.

Twiga anaweza kuishi mpaka miaka 25 awapo katika maeneo yake asili. Japo umri huo unaweza kuogezeka kidogo kama atakuwa chini ya uangalizi au kama anafugwa.

Uhifadhi

Twiga hawa kwa sasa ni wanyama ambao wapo katika uangalizi mkubwa sana hususani hapa nchini kwetu Tanzania kwani kuna baadhi ya nchi wameshatoweka kabisa. Idadi ya wanyama hawa inapungua sana na ni kutokana na matatizo mbali mbali wanayo kumbana nayo katika maeneo asilia ambapo matatizo mengine sio ya asili husababishwa na vichocheo nje ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori.

Baadhi ya taasisi na mashirika mbali mbali kwa sasa yanaanza kutekeleza miradi ya uhifadhi wa wanyama hawa wasije toweka kabisa hata kwenye nchi walizo salia.

Maadui wakubwa sana kwa twiga hawa ni simba na fisi, japo maadui hawa huwa wana wanyemelea sana twiga wadogo. Hii ni kwasababu kumuuwa twiga mkubwa ni kazi kubwa sana kwani hata simba au fisi huwa wana muogopa sana kutokana na uwezo wa twiga kupiga mateke kwa kutumia miguu yote ya mbele na nyuma.

Kwa upande wa matishio sasa, kuna matishio manne ambayo ndio kwa kiasi kikubwa sana yamechangia kupungua kwa idadi ya wanyama hawa. Matishio hayo ni,

  • Ujangili uliyo kithiri kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori umepelekea sana kupungua kwa idadi ya twiga hawa kwani wamekuwa wakiwindwa kutokana na kuongezeka kwa biashara haramu ya wanyamapori na nyama pia.
  • Uharibifu wa mazingira hasa utokanao na shughuli za upanuzi wa maeneo ya kilimo, ukataji miti hovyo hasa maeneo ya hifadhi, matumizi mabaya ya ardhi na uongezekaji wa idadi ya watu hasa karibu na hifadhi za wanyamapori.
  • Matatizo ya kijamii hasa yatokanayo na matatizo ya kisiasa au migogoro ya ndani ya nchi pamoja na shiguli za kijeshi ambazo huwafanya raia kuhama makazi yao na kukimbilia maeneo ya hifadhi za wanyama kasha kuharibu mazingira au kuongezekakwa tatizo la ujangili.
  • Mabadiliko ya ikolojia ambayo kwa kiasi kikubwa husababishwa na shughuli za uchimbaji madini na shughuli za kilimo kwani mazingira huaribika sana nakufanya wanyama hawa kukosa mahitaji muhimu ikiwemo chakula.

Nini Kifanyike Ili Kuepuka Kupungua Kwa Twiga Hawa Hasa Hapa Kwetu Tanzania

  • Menejimenti ya mazingira na ulinzi kupitia sheria za wanyamapori vitiliwe mkazo na mamlaka husika kwani vitasaidia kwa kiasi kikubwa sana kupunguza uvamizi wa maeneo tengefu ya uhifandi wa wanyamapori.
  • Kuishirikisha jamii katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori lakini pia kuwapa sehemu ya faida itokanayo na uhifadhi wa wanyamapori ama kwa kuwajengea shule, zahanati au kuanzisha miradi mbalimbali kama kilimo cha kisasa ili waweze kujikwamua kiuchumi.
  • Kuongeza idadi ya askari wa doria katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori ambao pia watakuwa na uzalendo katika kufanya kazi zao kwa ufanisi na kwa moyo ili kupambana na majangili katika maeneo yote yanayo zunguka maneno ya hifadhi za wanyamapori.
  • Kutokana na baadhi ya maeneo kuharibiwa sana na kupelekea uhaba wa mahitaji ya twiga hawa, mamlaka husika hazina budi kupunguza idadi ya wanyama hawa na kuwa hamishia sehemu nyingine zenye mahitaji ya kutosha ili waweze kupata chakula cha kutosha lakini pia eneo kubwa na kuweza kuzaliana pia.

Hitimisho

Twiga ni wanyama muhimu sana hasa kwenye ikolojia ya eneo husika lakini pia mnyama huyu hutumika kama nembo ya taifa letu. Miongo michache iliyo pita takwimu zinaonesha twiga wamepungua kwa asilimia 52%. Hali kama itaendelea kuwa hivi basi wanyama hawa wataingizwa katika kundi la wanyama ambao wapo hatarini kutoweka duniani.

Kama tulivyoona hapo jamii hii ya twiga wamebaki hasa katika nchi mbili ambazo ni Tanzania na Kenya basi hatuna budi kupambana na kila hali ili kuwanusuru twiga hawa.

Maeneo ya Kusini mwa Afrika hutoa mpaka vibali vya watu binafsi kuwafuga twiga hasa wapatikanao katika maeneo yao ili kuongeza angalau idadi ya twiga wao. Hii imeleta matokeo chanya pia kwani idadi ya twiga wameongezeka katika maeneo yao.

Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori na ushauri juu ya makala hizi endelea kufuatilia makala zijazo lakini pia unaweza kuwasiliana na mwandishi kupitia,

Sadick Omary

Simu= 0714 116963 / 0765 057969 / 0785 813286

Email= swideeq.so@gmail.com

Au tembelea= www.wildlifetanzania.co.tz  

Tunaandika makala hizi ili tuongeze uelewa wetu kuhusu wanyamapori, tunaamini tukipata uelewa tutachukua hatua kushiriki katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake asilia.Kazi hii tunafanya kwa kujitolea na hakuna malipo yoyote, endapo umefurahia kazi zetu unaweza kutuunga mkono kwa kiasi chochote ili tupate mtandao, vifaa vyua kufanyia kazi kama kamera na komputa. Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana kwa mawasiliano haya; hmconserve@gmail.com  |+255-683-862-481