Habari msomaji wa wildlife Tanzania, karibu tuendelee na mfululizo wa makala zetu za kila siku ambapo tunaichambua sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009. Na kama tulikuwa tunafuatana vizuri utajua bado tunaichambua Sehemu ya saba ya sheria hii muhimu. Nimepanga kuchambua kila kipengele ili kila tunachojifunza kuhusu wanyamapori kieleweke vizuri na kitumiwe vizuri ndani ya muktadha wa sheria mama ya uhifadhi wa wanyamapori. Na kwa kuwa wewe umechagua kusoma na kijifunza mambo mbali mbali kuhusu wanyamapori, maisha yao, tabia na faida za uwepo wa wanyamapori kwa nchi yetu na jamii nzima kwa ujumla.

Katika makala ya leo ambayo tunajifunza kuhusu non-consumptive utilization wildlife tourism, ikiwa na maana ya utalii wa wanyamapori usiohusisha matumizi ya wanyamapori. Kabla ya kwenda mbali nataka tuelewe kidogo kuhusu utalii, utalii upo wa aina 2 kubwa, kuna utalii ambao unahusisha matumizi ya wanyamapori au wanaita utalii wa uwindaji, na utalii mwingine ambao hauhusishi matumizi ya maliasili au wanyamapori kama vile kupiga picha au utalii wa picha.

Utalii ambao unahusisha matumizi ya wanyamapori, au kwa namna nyingine utalii ambao unahusisha uwindaji mara nyingi hufanyika kwenye maeneo ya hifadhi ya mapori ya Akiba, Mapori Tengefu, maeneo ya Hifadhi ya Jamii, na maeneo ya wazi au Mapori ya Vijiji, huku ndiko wanakoruhusu utalii wa uwindaji, kwa mfano unaweza kusikia uwindaji unafanyika katika pori la Akiba la Seluu, au Selous, pia unaweza kusikia shughuli za uwindaji zikifanyika kwenye maeneo ya hifadhi ya jamii kama vile, Mbomipa, Burunge, Ikorongo nk. Hizi ni sehemu ambazo uwindaji unatajwa na kufanyika. Pia utalii wa picha unfanyika kwenye maeneo haya. Hivyo basi aia zote za utalii zinaweza kufanyika katika maeneo haya ambayo sio hifadhi za Taifa na wala hayasimamiwi na TANAPA.

Lakini kwa upande mwingine kuna utalii ambao hauruhusu matumizi ya wanyamapori, utalii huu unajulikana kama utalii wa picha, ambao ndio umekua utalii maarufu sana kwa sababu uanashauriwa sana na ndio unaosaidia sana kwenye masuala ya hifadhi ya wanyamapori. Utalii wa picha mara kwa mara na mara zote hufanyika katika Hifadhi za Taifa TANAPA, hawa ndio kwa kiwango kikubwa hutangaza na kuendeleza utalii huu wa picha. Kamwe huwezi kusikia shughuli za uwindaji wa kitalii ukifanyika kwenye ndani ya Hifadhi za Taifa. Hapa ninapozungumzia hifadhi za taifa namaanisha maeneo kama, Hifadhi ya taifa ya Ruaha, hifadhi ya taifa ya Katavi, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Hifadhi ya taifa ya Serengeti, Hifadhi ya Taifa ya Gombe nk.

Naamini sasa unaelewa tukisema maeneo ambayo shughuli za uwindaji wa kitalii unafanyika na maeneo ambayo shughuli za utalii wa picha zinafanyika, au maeneo ambayo shughuli za uwindaji wa kitalii hazifanyiki. Mambo haya ndio yaliyoelezwa kwenye sheria hii ya uhifadhi wa wanyamapori sehemu ya saba kipengele kinachohusu utalii ambao hauruhusu matumizi ya wanyamapori. Kuanzia kifungu cha 54 (1) kinaelezea sehemu hii ya sheria ya wanyamapori.

Hata hivyo sheria inasema kuanzia kifungu kidogo cha (1) kwamba hakuna mtu yeyote ambaye atajihusisha au atafanya shughuli za utalii usio na matumizi au utalii wa picha bila leseni ya kufanya hivyo kutoka kwa mamlaka husika. Lesseni hii ambayo hutolewa kwa mujibu wa Sharia ya utalii yam waka 2008.

Kifungu kidogo cha pili kinaeleza namna Waziri anavyoweza kuweka vigezo na masharti ya kufanya shughuli za utalii wa picha au utalii ambao hauhusishi matumizi ya wanyamapori kulingana na matakwa ya kanuni na sheria za utalii.

Naamni kufikia hapa unaelewa kuhusu utalii wa aina mbili ambao kwa kiasi kikubwa unafanyika katika nchi yetu. Nchi yetu ina maeneo mengi sana ya utalii wa aina zote kwa hiyo ni sisi wenyewe watanzania kuamka na kuwekeza kwenye sekta hii. Tanzania ingawa inamaeneo mazuri nay a asili kwa utalii mbali mbali bado Hakuna miundombinu ya kutosha nay a kisasa.

Kwa mfano maeneo manegi ya kusini mwa Tanzania bado hayajachangamka kwenye utalii, hivyo kuna changamoto kubwa sana katika ukuaji wa utalii kwenye maeneo haya ya kusini mwa Tanzania, licha ya kuwa na vivutio vingi na vya kutosha bado hifadhi za Taifa za Kusini na maeneo mengine yenye vivutio hayajulikani ipasavyo na pia hayatoi mchango mkubwa na unaotakiwa kwa wanajamii wa maeneo hayo. Hivyo hata mwamko wa watu kwenye mikoa na maeneo haya wapo nyuma sana linapokuja suala la utalii na kutalii.  Endelea kufuatilia mtandao huu na kujifunza kushauri na kuuliza maswali, pamoja tushirikiane kwenye ulinzi, utunzaji na usimamizi wa rasilimali zetu, hasa wanyamapori

Ahasante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania