Ni mwanzo wa juma, ukiwa umeshajipangia majukumu yako ya kufanya wiki nzima nimekuandalia Makala bora kabisa ambayo utajifunza mambo mapya kuhusu wanyamapori, uhifadhi na mengine mengi kama itakavyoelezwa kwenye Makala hii kwa kina. Kwa hakika kupitia makala hizi utajifunza mengi ambayo ulikuwa huyajui kuhusu wanyamapori kwa kuangalia mambo kama sifa za mnyama husika, mazingira wanayoishi wanyama hawa, kuzaliana, changamoto zinazo wakumba wanyama hawa na nia za kutatua changamoto hizo bila kusahau uhifadhi wa wanyama hawa ambao ndio msingi mkubwa wa makala hizi ndugu msomaji.
Katika miongo michache iliyopita kumekuwepo na tatizo kubwa sana la kupungua kwa idadi ya wanyamapori kutokana na sababu mbalimbali ambazo asilimia zaidi ya tisini ya sababu hizo zinaweza kutatuliwa na kuisha kabisa kama kila mmoja wetu atakuwa na utayari na uthubutu katika kutatua matatizo hayo. Ni suala linalo hitaji umakini mkubwa sana katika kutatua changamoto hizo kwani harakati nyingi za utatuzi wa matatizo hayo umekuwa ukikumbwa na vikwazo vingi sana nakufanya kuwa ni vigumu kuzitatua.
Basi nakusihi kuwa nami kuanzia mwanzo hadi mwisho wa makala hii ili uweze kujua mambo mengi kuhusu mnyama ambae nimekusudia kumuweka mezani siku ya leo kisha ujue na matatizo mbalimbali yanayo wakumba wanyama hawa ili na wewe uwe mmoja wapo katika kusaidia suala la uhifadhi hapa nchini. Bila kusahau sio kwamba utajua changamoto tu bali utajifunza mambo mengi pia huku ukibaki na elimu na burudani kubwa sana pale utakapo maliza kusoma makala hii.
Leo tena narudi upande wa wanyama jamii ya swala huku nikiiandaa kukuletea darasani mnyama mzuri mwenye umbo la kuvutia hata kwa kumuangalia tu jinsi alivyo. Na bila kupoteza muda leo utamjua mnyama ajulikanae kwa jina la “NYAMERA” ambae kwa lugha ya kigeni (Kingereza) huitwa “TOPI”.
UTANGULIZI
Wanyama hawa ukiwaangalia haraka haraka unaweza kuwafananisha na wanyama ambao nimewaelezea kwenye makala iliyopita kwani wana fanana sana. Nyamera na Kongoni wanafanana sana hasa kimaumbile hivyo inahitajika umakini katika kuwatofautisha kwani kuna sifa mbalimbali ambazo zinawatofautisha wanyama hawa. Kuna takribani spishi sita za wanyama hawa bara zima la Afrika ambao hufanana karibu kwa asilimia 85%.
Nyamera ni wanyama ambao wanapatikana barani Afrika tu. Hadi kufikia miaka ya 1900 wanyama hawa walikuwa wanapatikana maeneo mengi sana hapa barani Afrika. Ni wanyama ambao wanaishi kijamaa sana na hasa tabia yao ya kuchanganyika na wanyama wengine. Wanyama hawa wamekuwa wakipungua sana kutokana na sababu mbali mbali na hata kufikia kutoweka baadhi ya maeneo ambayo hapo zamani walikuwa wakipatikana kwa wingi sana.
Katika nchi ambazo bado zinaendelea kujivunia uwepo wa wanyama hawa kwa idadi kubwa kuliko nchi nyingine ni hapa nchini Tanzania na maeneo ya kusini mwa nchi ya Ethiopia. Hali hii inafanya baadhi ya mataifa yaone kama bado nchi yetu inapambana kuhakikisha wanyamapori wanaendelea kuwepo. Pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wanyama hawa bado wanakumbwa na matatizo mbali mbali ambayo tusipokuwa makini na sisi tuta wapoteza kabisa.
SIFA NA TABIA ZA NYAMERA
Nyamera ni wanyama jamii ya swala wenye maumbile ya wastani ambao wanapatikana kwenye familia moja na wanyama kama nyati, pofu, nyumbu, kongoni na wengineo.
Wana miili yenye rangi ya wekundu/kahawia huku sehemu ya juu ya miguu ya mbele wakiwa na alama nyeusi na sehemu ya mapajani. Alama hizi usipokuwa makini unaweza kusema ni matope au alama za kuungua kama umeangalia kwa mbali zaidi. Kumbe hizi ni alama ambazo wanyama hawa huzaliwa nazo. Rangi ya dume huwa imefifia au yenye weusi zaidi kuliko jike.
Miguu ya nyamera huwa na rangi ya njano ambapo unaweza kusema wanyama hawa wameva soksi kama hujawachunguza vizuri kwenye miguu yao.
Wana alama neusi ambayo inaanzia sehemu ya mbele kichwani hadi maeneo ya puani.
Madume na majike wote wana pembe ndefu ambazo zimepinda kuelekea upande wa nyuma. Pembe hizi zimekaribiana sana eneo la kikonyo na zina maduara kuanzia chini hadi juu. Urefu wa pembe hizi unakadiriwa kufikia sentimita 30 – 40.
Wana vichwa virefu na wameinuka maeneo ya mabegani kitu ambacho kina wafanya wanyama hawa kufanana sifa na Kongoni kutokana na miguu ya mbele kuwa mirefu kidogo kuliko ya nyuma. Ukiwachunguza vizuri utaona kabisa kuanzia mabegani kuelekea upande wa nyuma mgongoni kuna kama muinamo kidogo.
Nyamera ni wanyama ambao wanaishi kiujamaa sana. Hupenda kuishi kwenye kundi hasa kina mama na watoto. Makundi haya huwa na wanyama takribani 15 – 20. Japo kuna wakati wanyama hawa huwa wanakuwa hadi wanyama miamoja na zaidi katika kundi moja hasa kipindi wanapokuwa wana hama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya kutafuta chakula.
Madume hupigana sana ili kuweza kumiliki kundi la kina mama na watoto. Dume anapo tawala kundi huakikisha anatafuta sehemu yenye majani ya kutosha kisha sehemu hiyo inakuwa na sehemu ya muinuko katikati mfano wa kichuguu ambayo mara nyingi dume huitumia ili kuwaonesha madume wengine kuwa yeye ndio mtawala wa kundi hilo la majike. Sehemu hiyo pia hutumiwa na majike katika kupeana taarifa endapo kuna hatari au wakati adui anawanyemelea. Kazi ya kulinda himaya hufanywa kwa ushirikiano baina ya dume na majike chini ya uongozi wa dume huyo.
Kwakuwa dume ndo huwa mtawala mkuu wa kundi, basi majike wote hulazimika kufuata amri ya dume huyo awapo kwenye kundi. Ikitokea dume ameondoka mara moja na kwenda matembezini, basi jike mkubwa mwenye mamlaka huongoza kundi hilo mpaka pale dume atakaporudi kutoka kwenye safari zake.
Dume hutumia kinyesi na maji maji ambayo hutoka kwenye matezi yaliyopo kwenye macho kuweka mipaka katika himaya yake. Anapokuja dume mwingine ndani ya himaya hiyo basi mtawala hulazimika kupigana, na hupigana wakiwa wamepiga magoti miguu ya mbele kisha kutumia pembe kwa kusukumana.
Nyamera ni wanyama ambao wanakuwa vizuri katika kuona na michezo wakati wa asubuhi na kipindi cha jioni. Katika mida hii wanyama hawa hutumia kutafuta chakula na maji kisha kupumzika mida ya mchana na usiku pale giza linapoanza kushamiri.
Ni wanyama wenye uwezo mkubwa sana wa kuona na kusikia. Jike huwa ana uwezo wa kuona au kutambua hatari mara mbili zaidi hasa kipindi cha kuzaa. Na kwa wakati huu anapo hisi hatari jike ana uwezo wa kujizuiya kuzaa kwa muda mpaka pale atakapo hisi hali ya wasiwasi imepungua katika maeneo hayo.
Wanyama hawa hupendelea kuoga kwenye matope na kusambaza matope mwili mzima ili kupunguza joto katika miili yao hasa kindi cha jua na joto kali.
Nyamera ni miongoni mwa wanyama wenye uwezo wa kukimbia kwa kasi kubwa sana katika wanyama jamii ya swala. Wanyama hawa wana uwezo wa kukimbia umbali wa kilometa sabini kwa saa (70km/saa).
KIMO, UREFU NA UZITO WA NYAMERA
Kimo= kimo cha wanyama hawa hususani miguu ya mbele kuanzia chini hadi mabegani huwa na urefu wa sentimita 100 – 130.
UREFU= Kuanzia kichwani, kuwiliwili hadi mwisho wa mkia wanyama hawa hukadiriwa kufika urefu wa sentimita 213.
UZITO= Uzito wa wanyama hawa unakadiriwa kuwa kilogramu 68 – 155, japo kwa majike huwa na uzito wa chini kidogo kuliko madume.
MAZINGIRA
Nyamera hupendelea sana maeneo ya majani ambayo huwa na mafuriko mara kwa mara na sehemu zenye savanna ya wazi. Wakati mwingine huonekana kwenye maeneo yenye mito miti mingi. Na mara nyingi wanyama hawa huonekana katika maeneo ambayo ni tambarare yenye kunyooka pasipo na miinuko mingi sana.
CHAKULA
Nyamera ni miongoni mwa wanyama walao majani na huepuka kula majani ambayo yameanza kurefuka kidogo. Kwakuwa huwa wanatumia muda wa asubuhi na jioni kutafuta chakula, wanyama hawa hutumia muda wa mchana hasa kipindi cha jua kali wanatafuta sehemu zenye kivuli na kupumzika katika eneo hilo.
Endapo watapata sehemu yenye majani mengi na yenye umbijani nzuri, wanyama hawa wana uwezo wa kuishi muda mrefu bila kunywa maji kwani maji mengi huyapata kutoka kwenye majani wanayokula. Hii ni kwasababu mimea hutunza maji mengi sana kupitia majani.
KUZALIANA
Nyamera ni wanyama ambao wanazaa mara moja kwa mwaka na watoto wengi huzaliwa kipindi cha mwishoni mwa majira ya kiangazi kwasababu ni kipindi ambacho mvua zinatarajiwa kuanza hivyo muda mfupi tu kunakuwepo na chakula cha kutosha kutokana na kunyesha kwa mvua.
Kwa upande wa wanyama hawa msimu wa kuzaliana huwa kuna tofauti kidogo na jamii nyingine za swala. Unapofika msimu wa kupandana madume hujikusanya sehemu moja na kutengeneza kundi kubwa la madume katika eneo moja. Ndani ya kundi hilo, makundi mbalimbali ya majike huchagua madume wayapendayo kwa ajili ya kupandwa na baada ya hapo madume hayo ndio hutawala kundi hilo la majike baada ya kuyapanda. Katika kundi hilo la madume, majike hutumia takribani siku moja hadi mbili katika kuchagua madume sahihi wa kuzaa nao nakuwa watawala wao.
Kipindi hiki majike huwa na hasira na kulazimisha madume kuwapanda haraka zaidi mara tu baada ya kuwachagua. Hii inatokana na kwamba kwa wanyama hawa majike, siku ya kupata mimba huwa inadumu kwa takribani masaa 24 sawa na siku moja tu. Hivyo endapo hawatopandwa basi inabidi kusubiri hadi mzunguko mwingine tena.
Mara baada ya kupandana jike hubeba mimba kwa muda wa miezi saba na nusu hadi miezi minane (makadirio ya siku 248) na kisha huzaa mtoto mmoja tu. Mtoto wa Nyawera huzaliwa akiwa na uzito wa takribani kilogramu 11. Mara tu baada ya kuzaliwa mtoto huchagua mwenyewe kufuatana na kundi la nyamera wakubwa kisha kulindwa na kina mama au wanaamua kujikusanya kundi la watoto na kuishi kwa kufichama kwa muda wa siku 3 hadi 12. Watoto wa nyamera huanza kuota pembe na kuwa na rangi ya nyamera wakubwa wafikishapo umri wa miezi 3.
Watoto huwa chini ya uangalizi wa kina mama kwa muda wa mwaka mzima na baada ya hapo kwa watoto wa kike hujiunga na kundi la kina mama huku watoto wa kiume hufukuzwa na dume mtawala kisha huenda kutengeneza kundi lao la watoto wa kiume. Watoto wa kike huwa tayari kwa kuzaliana wafikishapo miezi 16 hadi 18 huku watoto wa kiume ni hadi miaka 3. Japo madume huweza kupanda majike wafikishapo miaka 3, bado huwa hawawezi kuanza kuyapanda majike kipindi cha umri huu kwasababu wanakuwa hawajawa na uwezo wa kupigana na madume wakubwa ili kuweza kutawala kundi la majike.
Maisha ya nyamera awapo katika mazingira asili hukadiria kuwa ni miaka 12 – 15. Japo umri huu unaweza ukazidi endapo nyamera atakuwa anafugwa katika bustani za ufugaji wa wanyamapori.
UHIFADHI
Nyamera ni wanyama ambao wanachukuliwa hali ya kundi la wanyama ambao bado hawapo kwenye hatari ya kutoweka dunia kutokana na tafiti zilizo fanywa na shirika la umoja wa mataifa linalo shughulika na masuala ya uhifahi wa maumbiliasili (International Union for Conservation of nature – IUCN). Hii ni kutokana na idadi ya wanyama hawa kuridhisha katika maeneo mbalimbali hapa barani Afrika hasa katika maeneo tengefu ya uhifadhi wa wanyamapori.
Mpaka sasa bado haijawekwa mikakati na taratibu maalumu ya kusimamia uhifadhi wa wanyama hawa kutokana na hilo kwamba bado hawajawa hatarini kutoweka duniani. Nadhani itakuwa ni jambo la furaha na umakini kuanza mikakati ya kunusuru wanyama hawa kabla hawajafikia kwenye hatua ya kutoweka duniani kwani sio jambo la kushangaa taarifa zikabadilika ghafla na kuwa kinyume na sasa hasa kutokana na hali ya ujangili ilivyo kwa sasa.
Kama tulivoona hapo juu kwenye utangulizi, mbali na kuwa wanyama hawa bado wapo wengi na idadi yao ina ridhisha hapa barani Afrika na hapa nchini kwetu Tanzania na nchini Ethiopia, kuna baadhi ya maeneo wanyama hawa walikuwa wanapatikana kwa wingi barani Afrika lakini kwa sasa wanyama hawa wamesha toweka kabisa. Hali kadhalika idadi ya wanyama hawa imekuwa ikipungua siku baada ya siku kutokana na sababu, balimbali ambazo kipengele kinacho fuata tutaziona sababu hizo. Kwa nchi kama Nigeria wanyama hawa wana sadikika kuwa wamesha toweka kabisa huku nchini Swaziland wamefanya kurudishwa tena baada ya kutoweka kwa miaka michache iliyo pita.
MAADUI WA NYAMERA
Kipengele hiki kinagusa maadui wa asili wa wanyama hawa hasa katika mazingira yao asilia. Maadui wakuu wa wanyama hawa ni simba, chui, duma, fisi na mbwa mwitu. Uwepo wa maadui hawa wa asili kwa nyamera ni lazima uwepo ili kusaidiakatika kuweka sawa ikolojia katika mazingira waishio wanyama hawa. Endapo watakosa maadui asilia basi watazaliana na kuwa wengi sana kitu ambacho kitafanya mazingira au nafasi kuwa ndogo na kusababisha chakula kuwa kichache hivyo wengine wataanza kufa kwa njaa au magonjwa mbali mbali.
Mbali na maadui hawa kuna adui mwingine ambae hausiki kabisa na uasilia wa wanyama hawa ambae ni binaadamu. Binadamu amekuwa ni adui kwa wanyama wengi sana nakusababisha maelfu ya wanyama kupoteza uhai wao kutokana na tamaa tu za kimaisha za mwanadamu.
CHANGAMOTO NA TISHIO KWA NYAMERA HUSUSANI HAPA NCHINI TANZANIA
Ujangili uliyo kithiri katika maeneoya hifadhi za wanyamapori umekuwa tatizo kubwa sana kwa wanyama hawa. Japo bado wanyama hawa wapo wengi hapa nchini ila takwimu zinaonyesha wanyama hawa wamekuwa wakiwindwa sana hasa kutokana na biashara haramu ya wanyamapori na malighafi zao. Watu wengine wamekuwa wakiwawinda kwa matumizi ya nyama majumbani. Wanapo wawinda bila kufuata utaratibu husababisha athari kubwa sana katika kuzaliana kwa wanyama hawa kwasababu majangili huwa hawachagui mnyama wakumuwinda bila kujali kama mnyama ana mimba, ni mtoto au ana afya nzuri au mbovu. Hii husababisha idadi ya wanyama hawa kupungua kwa kiasi kikubwa sana na inaweza fika kipindi wanyama hawa wakaanza kutoweka kwenye baadhi ya maeneo hapa nchini kama yalivyo baadhi ya maeneo huko nchini Burundi, Gambia, Mali, Msumbiji, Mauritania na Senegali.
Uingizaji wa mifugo katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori nalo pia limeonekana ni tatizo ambalo linasababisha wanyama hawa kuhama baadhi ya makazi yao. Hii ni kutokana na kuwepo kwa changamoto ya kugombania chakula kati ya wanyama hawa na mifugo kwani mifugo imekuwa ikitumia sehemu kubwa sana ya chakula cha wanyama hawa. Hali hii imefanya wanyama hawa kuanza kuhama baadhi ya maeneo kwani hali ya upatikanaji wa chakula imekuwa ni tete sana huku baadhi ya eneo lao kubwa sana kwa ajili ya makazi likiharibiwa na ongezeko la mifugo.
Uharibifu wa mazingira na uvamizi wa maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Kumekuwepo na tabia ya watu kuvamia maeneo ya Hifadhi za Taifa na kuanzisha makazi katika maeneo hayo. Hali hii inapelekea uharibifu wa mazingira kwa kiasi kikubwa sana na kusababisha tatizo la ujangili kuwa kubwa sana katika maeneo haya. Ni wazi kwamba katika jamii mbali mbali za watu ndimo wahalifu huamua kujificha lakini hata baadhi ya wananchi wakishiriki katika kuwaficha wahalifu hao. Hali hii ni tatizo kubwa sana katika maendeleo ya uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini.
NINI KIFANYIKE ILI KUTATUA CHANGAMOTO HIZI KWA NYAMERA
Serikali kupitia wizara husika ijitahidi kuandaa mikakati madhubuti na njia za kisasa ili kupambana na tatizo la ujangili kwai linaonekana kuwa ni tatizo sugu kwa upande wa wanyamapori. Kwa kuishirikisha jamii inaweza kuwa pia njia rahisi sana yakuweza kuwafichua majangili kwani kama nilivosema hapo juu majangili wengi tunaishi nao ndani ya jamii zetu. Suala la kuongeza idadi ya askari wa wanyamapori na kusimamia uadilifu wa askari hao kujiepusha na masuala ya rushwa pia ni la kutilia mkazo kwani kama hatutakuwa na askari waadilifu ni dhahiri kwamba askari hawa wanaweza kuwa ni chanzo cha kuendeleza rushwa na kusababisha wanyama hawa kuwindwa sana na watu wachache wenye tamaa za mali bila kujali maslahi ya wananchi wengine hapa nchini.
Zitengenezwe sera nzuri na ufuatiliaji mzuri wa sheria zinazo simamia matatizo ya uingizaji wa mifugo katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Migogoro ya wafugaji na mamlaka za uhifadhi wa wanyamapori inaonekana kuongezeka siku hadi siku kutokana na ukiukwaji wa sheria na usimamizi mbovu wa sheria hizi. Kila aliye na mamlaka ya kusimamia sheria hii ahakikishe anatekeleza wajibu wake bila kujali au kuangalia kabila kwani endapo tukianza kuleta suala la ukabila na kuangalia aliye kamatwa na mifugo ndani ya hifadhi ninani basi hatutofika mbali daima. Wafugaji waelekezwe maeneo ya kulishia mifugo kwa nchi hii ni kubwa sana na ina maeneo mengi sana ambayo hayajaguswa hivyo wanaweza kuanzisha ufugaji katika maeneo hayo bila kubughuziwa na mtu yoyote.
Wizara ya makazi na mipango miji kwa kushirikiana na wizara ya maliasilina utalii kwa pamoja zihakikishe zina tatua suala la uvamizi wa maeneo tengefu ya hifadhi za wanyamapori kwani kwasasa watu wamekuwa wakivamia sana maeneo haya na kusababisha uharibifu mkubwa sana wa mazingira lakini pia kuongeza tatizo la ujangili katika maeneo haya. Mfano mzuri ni maeneo ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kuna uvamizi mkubwa sana kiasi kwamba hata mapitio ya wanyama kwa sasa yamezibwa kabisa. Wanyama walikuwa wakitumia maeneo haya kama minjingu kuhama kutoka hifadhi ya Tarangire kwenda Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara. Kwasasa eneo hili limezibwa kabisa na hakuna tena mapitio ya wanyama.
HITIMISHO
Nyamera ni wanyama ambao wana faida kubwa sana katika kuliingizia pato Taifa letu kupitia sekta ya utalii hivyo kwa pamoja tuna jukumu la kuhakikisha wanyama hawa wanaendelea kuwepo kwa faida yetu na vizazi vijavyo. Kwani endapo wanyama hawa wata toweka basi dhambi hii haita tuweka salama huko mbele na tuwe tayari kujibu kwa neema tulopewa tukachezea.
Kama baadhi ya nchi wanyama hawa walikuwepo na wametoweka kabisa kutokana na usimamizi mbovu wa uhifadhi wa wanyamapori basi na sisi tusipokuwa makini tutawapoteza pia. Hakuna mtu atakayetoka huko nakuja kuthamini maliasili zetu kama sisi wenyewe hatujaanza kuonesha mfano mzuri wa kupambana kunusuru wanyama hawa na hatimae itabaki kuwa majuto tu.
Natoa pongezi nyingi sana na za dhati kwa mamlaka mbalimbali zinazosimamia uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini kama TANAPA, TAWA na NCAA kwa kazi kubwa sana wanayoifanya. Pia shirika la WWF kwa hatua na miradi mbalimbali ya kusaidia suala la uhifadhi wa wanyamapori natambua mchango wenu katika sekta hii. Nasi kupitia elimu ndogo tuliopata ya wanyamapori hatujabaki nyuma katika kuelimisha jamii iweze kutambua thamani ya uwepo wa wanyama hawa na faida zao kwenye pato laTaifa na kukua kwa uchumi wetu.
Basi sina la ziada ila tu nakualika tena kufuatilia makala hizi na kujiandaa kwa makala ijayo uweze kujifunza mengi na kufurahia mambo kuhusu wanyamapori hapa nchini kwetu na kwingineko barani Afrika.
..Ahsante..
Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori na ushauri kuhusu makala hizi usisite kuwasiliana nami kupitia
Sadick Omary
Simu= 0714 116963/ 0765057969/ 0785813286
Email= swideeq.so@gmail.com
Au tembelea= www.mtaalamu.net/wildlifetanzania
……”I’M THE METALLIC LEGEND”……