Moja ya vitu vinavyofanya watu wachukulie maanani baadhi ya mambo yanayoendelea na kutokea  kwenye maisha ni vile vitu vikubwa vinavyogusa hisia za watu wengi, vitu hivi huwa na sauti vinapotokea hivyo watu wengi huweza kuwa na  taarifa za vitu hivyo. Lakini kuna vitu ambavyo ni vidogo vidogo ambavyo ukivigusa au vikiharibiwa sauti yake haisikiki sana. Hivyo ndivyo maisha yalivyo kwa watu wengi. Watu wanaochukulia mambo kawaida na kwa juu juu au bila kuwa na umakini wa kutosha hawataweza kuwa na uelewa zaidi ya hapo. Bali watu wenye macho matatu watafikiria na kujua matokeo makubwa ya baadaye husababishwa na hatua na vitu vidogo vidogo vinavyotokea na kufanywa kwenye maisha kwa muda mrefu.

Ujangili unapotamkwa na kusikiwa kwa watu wengi ndivyo ulivyo na ndivyo unavyochukuliwa na watu wa kawaida wanaochukulia kikawaida. Tukiweka hisia pembeni na kwenda kwenye  sera ya wanyamapori ya mwaka 2007 na sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 na sharia zinginee zinazohusu uhifadhi wa wanyamapori utaelewa ujangili unaelezwa kwa njia tofauti na unajumuisha vitu vingi. Ujangili kwa watu wengi ni kuua tembo na faru, biashara ya maeno ya tembo na pembe za faru. Sikatai kwamba huo sio ujangili, nakubaliana na wewe kwa asilimia mia moja kufanya mambo hayo ni ujangili na ni kazi haramu sana. Kwa sababu ya vishindo vyao watu wamekuwa na uelewa na kujua unapozungumzia ujangili basi ni kuua tembo na faru.

Kwa mapana yake na jinsi inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria, ujangili unajumuisha kufanya mambo yafuatayo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kwa mujibu wa sharia.

kurina asali,

kuvua samaki,

uwindaji kwa ajili ya nyama, au wa uwindaji wa kitamaduni

kukata miti kwa ajili ya ujenzi au mambo mengine,

kuokota kuni au kukata kuni,

kuchuma au kukata miti ya dawa za kienyeji,

kuchukua mawe au mchanga,

kuchukua mayai au watoto wa ndege,

kuokota au kuchuma matunda,

kukata nyasi

kuchuma au kukata Kamba za miti

kuokota nyara au mabaki ya mnyama, kama vile mifupa, Ngozi, pembe, kucha, manyoya, nk

kuua wanyama, au kuwajeruhi.

Mambo hayo kwa mujibu wa sharia na sera za wanyamapori yakifanyika kwenye maeneo ya hifadhi za wanyama au maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ni ujangili na ni kosa kubwa. Hivyo watanzania na watu wote ambao walifikiri ujangili ni jambo dogo inabidi waangalie mambo niliyoorodhesha hapo juu. Nimeandika na kuyataja mengine yanaonekana madogo lakini kwa mujibu wa sharia sio dogo hata kidogo.

Hivyo kwa kupeana ufahamu na maarifa haya itafanya kuwa na uajasiri wa kutembelea hifadhi na maeneo yaliyohifadhiwa bila uoga au wasi wasi. Ukielewa sharia na kanuni za mahali fulani utaishi vizuri na kufanikiwa haraka. Pia itasaidia kutunza na kuwa wahifadhi wazuri wa mazingira, naamini tukiacha kufanya shughuli za kijangili nilizotaja hapo juu tutainusuru misitu yetu, hifadhi na makazi ya viumbe hai wengi yatabaki salama. Endapo tutaendelea kufanya ujangili wa mambo haya tunayoyaona kuwa madogo baadaye yatakuwa makubwa na yatatushinda kudhibiti tena. Na uharibifu utakuwa mkubwa sana kwenye maliasili zetu.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania