Hifadhi ya Taifa Kitulo inapatikana Nyanda za juu Kusini mwa Tanzania katika mikoa ya Mbeya na Njombe. Hifadhi hii ipo kati ya kilele cha Milima ya Kipengere, Poroto na  Safu za Milima ya Livingstone. Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ina ukubwa wa kilomita za mraba  412.9. Hii ni hifadhi ya kwanza kabisa barani Africa kuanzisha kwa lengo la kutunza mimea yake hususani jamii ya maua.

Uzuri wa Bustani ya Mungu, hifadhi ya Taifa ya Kitulo, Picha na Alphonce Msigwa

Awali hifadhi hii ilijulikana kama “Elton Plateau” baada ya kugunduliwa na Fredrick Elton aliyepita eneo hilo mwaka 1870. Baadaye mwaka 1960 Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) lilichukua eneo hili na kulitumia kwa matumizi ya kilimo cha ngano na ufugaji wa kondoo. Hata hivyo eneo hilo  lilikuja kugeuzwa kuwa shamba la ng’ombe ambalo bado lipo mpaka sasa. Ila kutokana na umuhimu wa eneo hilo watu mbalimbali na wadau wa mazingira walipendekeza eneo hili litangazwe kuwa hifadhi ya Taifa ili kulinda aina mbalimbali na za kipekee za maua na mimea adimu inayopatikanakatika eneo hili.

Jitihada za kulifanya eneo hilo kuwa hifadhi ya Taifa zilianza mwaka 2002 kutangazwa rasmi kuwa hifadhi ya Taifa na serikali mwaka 2005.

Watu wengi hupendelea kuiita hifadhi hii “Bustani ya Mungu”. Hii ni kutokana na uzuri wa hifadhi hii uliopambwa na aina mbalimbali za maua mazuri yakuvutia yenye rangi nzuri na harufu za kipekee ambayo hupatikana eneo hili tu  duniani kote. Wengine wameenda mbali zaidi kwa kifananisha hifadhi ya Kitulo na ile ya Serengeti. Kutokana na hilo wataalamu wa mimea wakaamua kuiita “Serengeti ya Maua” kutokana na utajiri wa aina nyingi za maua yanayopatikana hifadhini na kuifanya moja ya sehemu ya maonesho ya maua mazuri Duniani.

Muonekano wa hifadhi ya Kitulo

Hifadhi ya Kitulo ina spishi tofauti za maua zipatazo 350 ambapo aina 40 za maua haya hazipatikani popote duniani na aina 45 za okidi za ardhini ambazo huibuka na maua ya viwango tofauti wakati wa mvua kuu mwishoni mwa mwezi Novemba mpaka April kila mwaka.  

Upekee wa hifadhi ya Kitulo ni pamoja na kuwepo kwa ndege aina ya tandawili machaka “Denhams bustard” wenye uwezo wa kuruka kutoka Bara moja hadi jingine. Hifadhi ya Kitulo ndiyo eneo pekee ambalo ndege  hawa hutaga mayai na kuzaliana kwa wingi kabla ya kwenda katika mabara mengine. Katika misimu fulani ndege hawa huruka na kufika katika hifadhi ya Kitulo kwa ajili ya kutaga mayai na kuangua vifaranga kutokana na mazingira ya hifadhi hii kuwa ni mahali pekee duniani penye hali ya hewa rafiki kwa ndege hawa kuzaliana.

Tafiti zinaonesha kuna ndege aina ya tandawili machaka ambao waliwekwa alama wakiwa katika hifadhi ya Kitulo na baadae kuonekana katika bara la Australia wakiwa na alama zile zile walizowekewa katika hifadhi ya Kitulo.

Hifadhi ya Kitulo hupatikana pia ndege aina mbalimbali kama vile Abdims stock, blue swallow, mpasua mbegu mweusi “kipengere seed eater” na wengineo ambao wametoka sehemu mbalimbali kama Afrika kusini, Afrika kaskazini, Australia na Ulaya na hutumia hifadhi ya Kitulo kama eneo lao la makazi katika misimu tofauti tofauti ya mwaka.

Pia hifadhi ya Taifa ya Kitulo kuna aina mbalimbali za wanyama wakiwemo jamii mpya ya nyani aina ya kipunji ambao waligundiliwa mwaka 2003, hata hivyo hifadhi hii ina pundamilia na swala ambao waliletwa kutoka hifadhi ya taifa ya Mikumi. Vile vile kuna aina mbalimbali za vipepeo ambao husaidia kuchavusha maua,  vinyonga, mijusi na vyura ambao huongeza utajiri wa kibailojia katika hifadhi ya Kitulo.

Pamoja na vivutio lukuki ambavyo  vinapatikana katika hifadhi hii, vile vile  kuna  uwanda wa tambarare, mabonde,vilima na maporomoko ya maji na mabwawa ambayo ni muhimu kwa ustawi wa mto Ruaha Mkuu ambao ni tegememezi kwa hifadhi ya Taifa Ruaha. Maporomoko haya ni kivutio kikubwa cha watalii wengi wanaofika hifadhi ya Kitulo hasa kwa utalii wa picha na mazingira “adventure tourism”.

Picha na Christina, Office Secretary Hifadhi ya Taifa ya Kitulo

Eneo la Kitulo linafikika kwa urahisi kabisa ambalo ni kilomita 110 kutoka  wilaya ya Mbeya Mjini. Muda mzuri wa kutembelea hifadhi ya Kitulo na kuona utajri wa mandhari nzuri ya maua ni mwezi wa kumi na mbili mpaka mwezi wa nne ambapo okidi nyingi za maua huchanua na kuwa na maua mazuri yanayovutia. Kuanzia mwezi wa tisa hadi wa kumi na moja ni muda mzuri wa kupanda mlima huku mwezi wa sita hadi wa nane ni miezi ya baridi kali

Karibu sana hifadhi ya taifa ya Kitulo kwa utalii wa maua ujionee bustani hii nzuri iliyopambwa na maua mbalimbali. Unasubiri nini kujionea bustani ya Mungu,unasubiri nini kuona maajabu ya Dunia?

Shukrani kwa Alphonce Msigwa (alphonce84@yahoo.com ), Mwikologia hifadhi za taifa Tanzania kwa kuhariri Makala hii.

Mwandishi wa makala haya ni

Cecilia Mwashihava

mwashihavacecilia@gmail.com

+255 747 268 217

Mhifadhi wa wanyamapori