Utangulizi

Biashara ya hewa ukaa ni miongoni mwa biashara kubwa duniani hususani katika nchi zinazoendelea ambapo uchafuzi wa mazingira haujakithiri kwa kiasi kikubwa. Ni fursa mpya ya biashara ambayo bado haijajulikana na watu wengi.

Bila shaka hata wewe msomaji wa makala hii licha ya kuwa na shauku ya kuifanya biashara hii mpya lakini utakuwa bado unajiuliza maswali mengi kuhusu namna ya kuiendesha pamoja na kujua wateja wake wako wapi, malipo yakoje, shamba la miti linatakiwa kuwa na ukubwa gani au miti ya aina gani inapewa kipaumbele zaidi n.k

Lakini ukweli ni kwamba biashara hii ya hewa ukaa ambayo pia inajulikana kama hewa ya kaboni, imekuja kuwa mwarobaini wa kudhibiti uchafuzi wa mazingira.

Katika misitu yetu pamoja na maeneo yaliyohifadhiwa, na tunaweza kutengeneza matajiri wakubwa hususani Watanzania watakao sajili kampuni ambazo zitajihusisha katika biashara hii katika kipindi ambacho dunia imetilia mkazo suala la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Hewa ya ukaa au hewa ya kaboni ni gesijoto ambayo hupatikana angani na huchangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabianchi.

Gesi hii ya kaboni imeingia katika rekodi ya dunia kwa kusababisha ongezeko la joto duniani ambapo nchi  nchi zaidi ya 120 duniani zimeamua kuelekeza nguvu kubwa katika kudhibiti changamoto hii.

Lakini yote hayo yamekuwa yakisababishwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu ambazo zinaathiri mazingira kwa kiasi kikubwa. Binadamu hawezi kustawi kama mazingira yanayo mzunguka yameharibiwa.

Hewa ukaa hutumiwa na misitu yetu au mimea kwa ujumla wakati wa kujitengezea chakula kupitia kitendo kiitwacho “usanisi nuru” na katika mchakato huo mmea hutoa hewa safi iitwayo oksijeni ambayo hutumiwa na binadamu pamoja na viumbe wengine.

Kwahiyo misitu yetu hutumia gesi chafu ya kaboni kama maIighafi muhimu, kwa muktadha huo inamaanisha unapokata mti bila kupanda mti unasababisha hii hewa ya kaboni ambayo ni gesijoto ikose sehemu ya kwenda hivyo hujikusanya kwa wingi angani na kusababisha madhara ambayo tunayaona katika dunia ya sasa.

Hivyo, matumizi ya misitu ambayo hayazingatii sera ya ” kata mti, panda mti” ni kinyume na maagizo ya serikali.  Baadhi ya shughuli za binadamu ambazo zinachangia kuongezeka kwa hewa ukaa ni pamoja na kilimo, ukataji miti hovyo, usafirishaji husasani suala zima la uchomaji mafuta, uzalishaji wa moshi kutoka viwandani, uchimbaji madini n,k

Historia ya uanzishwaji wa biashara ya hewa ukaa

Biashara ya hewa ukaa ilianzishwa baada ya dunia kugundua kuwa ongezeko la joto pamoja na mabadiliko mengine ya tabianchi yanaongezeka kwa kasi Sana.

Kwahiyo viongozi wa nchi mbalimbali zaidi ya 120 ziliamua kuwekeza nguvu kubwa katika utunzaji wa mazingira ili kuinusuru dunia katika haya majanga yanayoikumba.

Ukame, vipindi vya mvua visivyotabirika, mafuriko na milipuko ya moto isiyotarajiwa ni matukio ambayo yamekuwa yakiripotiwa katika maeneo mbalimbali duniani. Yote haya yamechagizwa na uchafuzi wa mazingira uliokithiri.

Mnamo miaka ya 1997 na 2005 ilifanyika itifaki ya Kyoto (Kyoto protocol) huko nchini Japani na makubaliano ya Paris (Paris agreement), ufaransa 2015, Glasgow, Scotland na badae huko Dubai katika COP 28 ambapo nchi wanachamana na Tanzania ikiwemo walikaa na kuweka mipango ya utungaji sera na mikataba ya utunzaji wa mazingira.

Katika mkutano huo walikubaliana kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na walisaini mikataba iliyoshinikiza nchi zilizoendelea kiuchumi na viwanda kupunguza uzalishaji wa gesi chafu pamoja na kutoa fedha za ufadhili katika nchi zinazoendelea ili kuunga mkono juhudi za utunzaji wa mazingira.

Lakini mikataba hiyo pia ilishinikiza utungaji wa sera ambazo zitalenga kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.

Makubaliano hayo na mikataba ililenga maeneo makubwa manne ambayo ni; kutoa fedha za ufadhili ili kutunza mazingira katika nchi zinazoendelea ambapo uchafuzi wa mazingira haujawa mkubwa ukilinganisha na mataifa ya Asia, Amerika na Ulaya.

Kuzuia uzalishaji wa gesi ya kaboni katika maeneo mbalimbali duniani, kuandaa mkakati wa kudhibiti uzalishaji hewa ukaa hasa katika yale maeneo yaliyoharibiwa na shughuli za kibinadamu.

Kuwajengea uwezo mataifa yanayoendelea juu ya namna bora na teknolojia bora ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Baada ya hayo yote kuwa yamefanyika ndipo biashara ya kuuza na kununua kaboni ilipoanza ramsi na sasa inafanyika katika nchi mbalimbali duniani

Namna biashara ya hewa ukaa inavyofanyika

Mataifa yaliyoendelea kiuchumi na viwanda ambayo ndio wachafuzi wakubwa wa mazingira hutoa pesa pamoja na ruzuku nyingine kwaajili ya kusaidia nchi zinazoendelea.

Lakini pia pesa hizi hulenga miradi ya kimkakati na miradi ya maendeleo ambayo inazingatia kanuni za kimataifa za kufikia malengo ya maendeleo endelevu(Standard Development Goals) katika jamii.

Miradi hyo ni kama vile, ujenzi wa shule, vituo vya afya, miundombinu ya maji safi, ugawaji wa nishati safi ya kupikia ambayo ni rafiki kwa mazingira na utoaji wa mikopo kwa wananchi ili kujikwamua kiuchumi ili kuondoa utegemezi wa wananchi kwenye misitu kujipatia kipato, kutokomeza janga la njaa na kuondoa umasikini katika nchi zinazoendelea kiuchumi.

Pesa hizi zinapotolewa huwa na ufuatiliaji kutoka kwa wakaguzi wa ndani na wakaguzi wa kimataifa kuhakikisha kwamba pesa hizo zinawafikia wananchi na zinafanya kazi iliyokusudiwa.

Ili uweze kufanya biashara hii lazima ukubali kutunza misitu inayotunzunguka. Hapa kwetu Tanzania kuna baadhi ya maeneo machache ambayo yalikubali kutunza misitu yao na mpaka sasa wameanza kunufaika na miradi ya hewa ukaa.

Mfano, mkoa wa Katavi katika Halmashauri ya wiliya ya Tanganyika walivuna Bilioni 22.25 huku mkoa wa Manyara ukivuna zaidi ya Bilioni 4 kutokana na mauzo ya hewa ukaa.

Uwekezaji katika Hewa ya ukaa huwa na michakato kama ilivyokatika uwekezaji mwingine, mwekezaji katika biashara hii huhitaji kuwekeza kiasi cha pesa katika kuandaa mradi.

Mwekezaji atapata faida baada ya kuuza viwango vya kaboni vilivyopatikana katika eneo lake la mradi. Mchakato huu huchukua muda mpaka zoezi likamilike na kupata viwango sahihi vya kaboni chini ya usimamizi wa wataalamu, huchukua mpaka miaka minne .

Kwahiyo, unaweza kuona jinsi ambavyo biashara hii inalipa na tunaweza kupata matajiri wapya duniani watakaojihusisha na biashara hii ya hewa ukaa au kaboni kwa kuthubutu bila woga.

Lakini kitu kikubwa na cha muhimu zaidi kwa watanzania ni kujua kwamba biashara ya hewa ukaa hii ni biashara mtambuka. Biashara hii hailengi upande wa misitu pekee bali hugusa sekta mbalimbali.

Sekta zinazoguswa na biashara hii ni pamoja na kilimo hasa kilimo kinacholenga kuboresha afya ya udongo. Mfano, matumizi ya mbolea ya asili pamoja na uozo wa asili (dead organic matters) ambayo huongeza mboji na rutuba kwenye udongo.

Wataalamu wa mambo haya wanabainisha kuwa, kuna kiasi kikubwa cha kaboni ambacho hutunzwa kwenye udongo.

Lakini pia kuna sekta ya usafirishaji ambapo kama sera zikihimiza matumizi ya vyombo vya moto ambavyo havitoi hewa ukaa inaweza kuwa sehemu ya mradi.

Mfano nchini Tanzania serikali imekuwa ikiunga mkono michakato hii na mifumo tayari imeshaanza kwenye vyombo vya moto kuanza kutumia mifumo ya gesi badala ya mafuta kama dizeli na petroli ambazo huwa na kiasi kikubwa cha kaboni.

Ukanda wa bahari ni sehemu muhimu pia kwenye miradi hii ya kaboni. Maeneo ya bahari yamechangia kwa kiasi kikubwa katika kufyonza hewa ukaa.  Misitu ya baharini, matumbawe pamoja misitu ya mikoko husaidia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Teknolojia ya kubuni njia mbadala za nishati Safi. Miradi pia ya kaboni huangazia namna ya kutengeneza nishati safi ambayo haiathiri ustawi wa mazingira na kupunguza hewa ukaa.

Sambamba na hilo, upande wa misitu kuna mgawanyo, kuna miradi ya kaboni inayolenga misitu ya asili, misitu ya kupandwa, kurudisha uoto ulioharibiwa n.k na kila nyanja inamiongozo yake.

Kwa mantiki hiyo, biashara ya hewa ukaa ni suala pana itategemeana na unazungumzia au unataka kujifunza biashara hii kwa nyanja ipi , inaweza kuwa nyanja ya kiuhifadhi, kimahusiano, kimakubaliano ya kimataifa, kijamii na hata kisiasa.

Miradi hii ya kaboni huchukua eneo kubwa la ardhi ndio maana uendeshaji wa biashara hii kwa mtu binafsi inakuwa ngumu kutokana na gharama za uendeshaji.

Mapori makubwa yaliyohifadhiwa na Halmashauri za vijiji na Wilaya ndio wanufaika wakubwa wa miradi hii kwasababu huwa na maeneo makubwa ya uwekezaji ambapo huhitajika angalau hekta 100,000 kwaajili ya kuanza miradi hii.

Katika utekelezaji wa miradi hii ya kaboni haihusishi kuhamisha watu kutoka kwenye makazi yao bali hulenga kuwanufaisha wananchi kutokana na namna ambavyo wametunza mazingira bila uharibifu wowote.

Faida kubwa wanayoipata watu kutokana na miradi ya hewa ukaa inaendelea kuwahamasisha na kuwapa motisha katika kutunza mazingira kutokana na ukweli kwamba binadamu anaasili ya kupenda kutunza kitu kinachompa faida inayoonekana na inayomsaidia.

Pichani: Mhe, Dr. Seleman Jafo-Waziri wa mazingira akikabidhi hundi ya fedha yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 4 katika Mkoa wa Manyara kutokana na mauzo ya hewa ukaa. Chanzo: mtandaoni

Uvunaji wa hewa ukaa katika misitu

Watu wengi hujiuliza maswali mengi juu ya namna gani hewa ukaa inavunwa wakati haionekani kwa macho. Lakini hewa ukaa inavunwa kwa namna yake tofauti na mazao mengine kwani hutumia njia za kitaalamu zaidi.

Hewa ya kaboni inayofyonzwa na misitu yetu hutunzwa katika mti wenyewe na kiasi kingine cha kaboni hutunzwa ardhini katika udongo (soil carbon sequestration).

Misitu midogo au michanga huwa na uwezo wa kufyonza kiasi kikubwa cha hewa ukaa lakini pia kiasi cha hewa ukaa kinachopatikana katika udongo hutofautiana kutokana na aina ya udongo wa eneo husika.

Maeneo mengi ya Tanzania yanafaa kwa biashara hii japo viwango vya kaboni vinaweza kutofautiana kutegemea aina ya uoto.

Mfano viwango vya kaboni vinavyopatikana kwenye misitu minene yenye bayoanuai nyingi huwa ni viwango vikubwa vya kaboni.

Hivyo maneo ya aina hii huwa ni muhimu na yana kiasi kikubwa cha hewa ukaa au kabon, hivyo utunzaji wa maeneo haya hulenga pia kutunza bayoanuai hizi ambazo bila kutunzwa na kulindwa huweza kutoweka katika mazingira yetu. Pia yenye uoto wa migunga na miombo yana  viwango tofauti na miti imingine.

Kwahiyo wakati wa kuvuna hewa hii ya kaboni/ukaa huwa zinachukuliwa sampuli (sampling plots) katika eneo la mradi kwa ajili ya kwenda kufanya vipimo.

Mtafiti akipima mti ili ajue kiasi cha hewa/carbon kilichopo katika mti huo; picha kutoka katika mtandao wa Nature Conservancy

Uvunaji wa hewa ukaa katika maeneo yaliyohifadhiwa katika miradi hii ya kaboni hufanywa na wataalamu wa kitaifa na kimataifa kutoka katika muungano wa nchi wanachama wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, UNFCC.

Tanzania imekuwa mstari wa mbele kwa kuzalisha wataalamu mahususi wenye ujuzi wa kuvuna hewa hii ya ukaa kupitia vituo maalumu vya kitaifa.

Kituo cha kitaifa kinachojihusisha na masuala ya kaboni cha Tanzania National Carbon Monitoring Center, (NCMC) kimekuwa kikifanya kazi kubwa ya kusimamia miradi yote ya kaboni na kurasimisha makampuni mbalimbali yanayotaka kuwekeza katika biashara hii.

Mpaka sasa kuna zaidi ya miradi 73 ya kaboni na  makampuni mengi ambayo tayari yamejisajili kwaajili ya kuingia katika biashara ya hewa ukaa lakini kampuni ya Carbon Tanzania ndo kampuni pekee ambayo tayari imenufaika na mpango huo katika uvunaji wa hewa ukaa.

Wataalamu hawa mara nyingi wakiwa katika eneo la mradi huhitaji kurekodi taarifa zinazoelezea aina ya miti iliyopo kwenye eneo la mradi, urefu , upana, ukubwa wa eneo la mradi wako pamoja na kubaini aina ya udongo wa eneo hilo.

Taarifa hizo zinawasaidia wataalamu kuweza kufanya hesabu zao za makadirio ili kujua viwango vya kaboni vinavyopatikana katika eneo lako.

Baada ya kujua viwango vya kaboni vinavyopatikana katika eneo la mradi kinachofuata baada ya hapo ni kufuata taratibu za uuzaji wa viwango hivyo vya kaboni vilivyopatikana kwa kufuata miongozo ya serikali.

 

Pichani: Muonekano wa misitu iliyohifadhiwa vizuri 

Miongozo ya uendeshaji wa biashashara ya Hewa Ukaa

Baada ya kupata viwango vya kaboni katika eneo la mradi kinachobaki ni kujua namna ya kupata pesa kupitia uuzaji wa hewa ukaa pamoja na kujua taratibu za kufuata ili kuuza hewa hii.

Kiufupi ni kwamba Tanzania inazaidi ya hekta milioni 48 ambazo zimehifadhiwa vizuri ambayo ni sawa na asilimia 55 za ardhi yote ya Tanzania.

Kwahiyo, serikali kupitia kwa Waziri mwenye dhamana ya mazingira imetoa nafasi kwa kila mtanzania mwenye shauku ya kufanya biashara hii.

Biashara ya hewa ukaa inaweza kufanywa na mtu binafsi, asasi za kiraia au serikali ambapo unaweza ukawa mmiliki wa mradi au mpendekezaji wa mradi.

Kwahiyo, serikali imeweka miongozo mbalimbali ambayo itamsaidia mtu yeyote ambaye atahitaji kufanya biashara hii na miongozo hii imebainisha hata asilimia ya faida utakayoipata baada ya mauzo ya hewa ukaa.

Yafuatayo ni mambo ya kuzingatia ili uweze kufanya biashara hii;

  1. Andaa eneo la mradi ambalo limehifadhiwa vizuri, lisiwe na uharibifu wowote wa mazingira na lisiwe na migogoro ya ardhi.
  2. Fanya upembuzi yakinifu ili uweze kubaini changamoto ambazo zinaweza kuathiri mradi pamoja na kupata taarifa za awali zitakazokusaidia wakati wa kufanya mradi wako. Kama wewe sio mtaalamu unatakiwa kuambatana na wataalamu katika zoezi hilo.
  3. Andaa andiko la mradi ilikubainisha taarifa zote muhimu kwa utoshelevu wake ukielezea jinsi gani utaendesha mradi wa hewa ya kaboni, njia utakazotumia katika zoezi zima na umuhimu wa mradi huo katika jamii. Ainisha pia viwango vya kaboni vilivyopatikana katika eneo lako la mradi ili kumsaidia mnunuzi kujua ni kiasi gani cha kaboni atanunua kwako.
  4. Omba fomu ya biashara ya hewa ukaa. Katika marekebisho ya kanuni za uthibiti na usimamizi wa biashara ya kaboni, Waziri mwenye dhamana kwa kushirikiana na kamati ya kiufundi ya kitaifa ya kutathmini miradi ya kaboni wamepewa mamlaka ya kushughulikia maombi ya fomu ya biashara ya kaboni kwa waombaji wote na wale wafanyabiashara wanaotaka kuhamisha viwango vya kaboni.
  5. Omba barua ya idhini ya kuanzisha na kuendesha mradi wa biashara ya hewa ukaa. Barua hizo zinamsaidia mwekezaji anayetaka kufanya biashara hii kuifanya kwa weledi bila kuvunja sheria za nchi na kuchangia katika kukuza pato la nchi. Lakini hii pia huwavutia wateja kununua viwango vingi vya kaboni kwa kuona ushiriki wa serikali katika mradi unaouendesha.
  6. Andaa ada za uendeshaji wa mradi ambapo kwa mtanzania huanzia dola 250 ambazo. Ada nyingine kwa mzawa hulipwa kulingana na asilimia za mauzo ya kaboni.
  7. Andaa ripoti ya mwaka. Mara nyingi katika miradi hii ya kimkakati huwa mwekezaji anatakiwa kuandaa ripoti ya mwaka inayoainisha utekelezaji wa mradi, kiasi cha pesa kilichopatikana kutokana na mauzo ya kaboni pamoja na miradi mbalimbali iliyotekelezwa kutokana na mradi huo.

Soko la hewa ukaa

Hewa ukaa/kaboni ina soko la uhakika na kwa hapa Tanzania tuna masoko mawaili, soko la hiari (voluntary market) na soko ambalo liko chini ya mikataba ya kimataifa (compliance market).

Kwahiyo, makampuni yaliyosajiliwa hapa Tanzania hutakiwa kuuza viwango vya kaboni vilivyovunwa katika maeneo yao ya miradi.

Kuna makampuni ya kimataifa yanayonunua viwango hivyo vya kaboni, japo kwa Tanzania soko ambalo linafanya vizuri ni soko la hiari kulingana na wepesi katika namna ya kufanya kazi.

Mfano, Carbon Tanzania ni kampuni ambayo inatengeneza miradi ya biashara ya kaboni (Project developers) na baada ya uvunaji wa viwango vya kaboni katika maeneo yao ya miradi huuza viwango hivyo kwa kuzingatia miongozo iliyowekwa na serikali.

Lakini pia kuna masoko ya nje kama The EU Emissions Trading system pamoja na masoko mengine mengi. Kiwango kimoja cha kaboni (1 Carbon credit) huweza kuuzwa mpaka dola 15, ingawa bei inabadilika kulingana na aina ya wanunuzi waliopatikana.

Lakin pia faida atakayopata mwekezaji itategemeana na viwango vya kaboni vilivyopatikana katika eneo la mradi. Kwahiyo mwekezaji atachagua auze wapi kwenye maslahi mazuri kulingana na wateja atakaowapata.

Kwa kuhitimisha makala hii, nitoe rai yangu kwa watanzania kuchangamkia fursa hii ili kuondokana na umasikini hususani wananchi ambao wanakaa katika maeneo yenye sifa za kuingizwa kwenye mradi kuendelea kuyatunza mazingira hayo ili miradi itakapofika kwenye maeneo yao waweze kufaidika.

Lakini pia napenda kuishauri serikali hususani Waziri mwenye dhamana kuunda sera bora za kuwahimiza wakulima washiriki kuhifadhi mazingira kwa kuhimiza kilimo cha mazao ya kimkakati.

Mazao hayo ni kama korosho, parachichi, karafuu, kakao, kahawa mazao ambayo ni rafiki kwa mazingira ambapo mkulima anashiriki katika kutunza mazingira na akipata kipato kutoka shambani.

Hali kadhalika, wafugaji wapewe elimu juu ya ufugaji unaozingatia ukubwa wa eneo ili kuepusha mifugo kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa.

Matumizi ya nishati jadidifu au nishati safi ya kupikia, matumizi ya vyombo vya moto visivyozalisha hewa ukaa, utoaji wa elimu ya uhifadhi wa mazingira, kilimo hai kinachotunza mazingira na utungaji wa sera imara ya upandaji miti itakuwa mwarobaini wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Asante Sana kwa kusoma makala hii na karibu kwa maoni na ushauri ili tuzidi kuboresha makala zetu ziwe nzuri na zenye kutoa elimu nzuri kwa jamii.

Pia nipende kuwakaribisha makampuni ya kaboni kutupa nafasi vijana tuweze kuonyesha uwezo wetu pamoja na kupata uzoefu kwa vitendo ili tuzidi kuwa na wataalamu wa kutosha katika nchi yetu.

Imeandaliwa na Victor Obadia Wilson; Barua pepe ; wilsonvictor712@gmail.com simu; : +255620861002

Na kuhaririwa na Alphonce Msigwa-Mwikolojia wa Hifadhi za Taifa Tanzania, pamoja na Hillary Mrosso

 

Tunaandika makala hizi ili tuongeze uelewa wetu kuhusu wanyamapori, tunaamini tukipata uelewa tutachukua hatua kushiriki katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake asilia.Kazi hii tunafanya kwa kujitolea na hakuna malipo yoyote, endapo umefurahia kazi zetu unaweza kutuunga mkono kwa kiasi chochote ili tupate mtandao, vifaa vyua kufanyia kazi kama kamera na komputa. Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana kwa mawasiliano haya; hmconserve@gmail.com  |+255-683-862-481

 

 

 

 

you might also like