SEHEMU A
Historia ya ujangili inaturudisha nyuma enzi za ukoloni wakati wakivamia maeneo yenye thamani kubwa mfano machimbo ya madini, mashamba makubwa yenye rutuba na maliasili zote. Wakoloni walitumia taratibu na sheria zao ili waweze kujinufaisha na rasilimali. Mabavu na nguvu zilitumika kuwaondoa waafrika waliokuwa wanakaa ndani na pembezoni mwa maeneo yenye rasilimali hizo. Pindi walipojaribu kukataa basi walijeruhiwa, waliua na wakati mwingine kufungwa gerezani. Walifanya hivyo kuimarisha ulinzi na kuweka mipaka kwenye maeneo yenye maliasili ili kurahisha utumiaji wao. Bila kutegemea ikazaliwa chuki na ujangili mioyoni mwa baadhi ya wanajamii waioishi maeneo hayo. Hii ni kutokana na utegemezi mkubwa katika maliasili hizo ambazo zilizuiliwa kutumika. Utegemezi huo ni pamoja na maeneo hayo kutumika kama sehemu za kufanyia ibada kwa miungu yao katika miti mikubwa na mapango, kudumisha mila na tamaduni zao mfano baadhi ya wanyama walitumika katika taratibu za uoaji kama simba dume ikiwa mwanaume kaweza kumuua alionekana ni shujaa kwa jamii ya wamaasai na nyani kwa jamii ya wadatoga, kujipatia kitoeo, ngozi zilitumika kutengenezea mavazi na vitanda, matunda na nishati ya kuni.
Wanajamii wengi kushindwa kupata mahitaji yao binafsi kuliwafanya waanze kuingia kwenye maeneo hayo kinyume cha sheria. Kwa sababu ya uchumi wao kuwa chini (wengi wao walikuwa wakulima na wafugaji) hivyo hawakuwa na pesa za kutosha kuweza kulipia vibali kwa ajili ya kupata dawa au kuni pamoja na sheria kali za upataji wa vibali hivyo. Hapo ndipo wanajamii mashujaa waliojaa chuki ya kunyang’anywa maeneo yao walijitoa na kuanza kufanya ujangili. Wanajamii hao hawakutishwa na serikali ya mkoloni ambayo haiweza kuvumilia uvunjwaji wa sheria na hivyo uliambatana na adhabu kali zilizopelekea kupoteza maisha au kwenda kutumika katika mashamba yao.
Katika kipindi hicho chote ujangili ulifanywa na idadi ndogo ya watu kulingana na takwimu zao. Silha zilizotumika zilikuwa duni na uwepo wa mila na desturi ambazo zilizuia uwindaji wa aina ya wanyama na kwa kipindi fulani cha mwaka. Pia baadhi ya maeneo kuzuiliwa kabisa kuingia kwa kuwa ni matakatifu hivyo kulisaidia idadi ndogo sana ya wanyama kuweza kuwindwa.
Maisha hayo yaliendelea hata kufika mnamo mwaka 1880 kipindi ambacho wajerumani waliingia nchini na hatimaye mnamo mwaka 1891 ilipitishwa nchi yetu (Tanganyika) kuwa chini ya koloni la mjerumani la Afrika Mashariki. Kaunzia hapo sheria na taratibu za uwindaji zilianzishwa nchini katika wilaya ya Moshi. Sheria na taratibu hizi zilianzishwa kama njia mojawapo ya kupinga ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo na pembe za faru zilizoendeshwa na waarabu ambao ndio wakoloni waliokuwa wametangulia kufika chini.
Ukuaji wa kasi wa teknolojia ulioambatana na faida nyingi kama kurahisisha kazi, kuokoa muda na kupunguza watu kuchoka umechangia kuteteleka kwa uhifadhi wa maliasili, kwani umekua na faida chache kuliko hasara ambapo utumiaji wa aina mbalimbali za usafiri na vifaa vya mawasiliano kama simu katika nchi nyingi umeweza kuunganisha mtandao mkubwa wa wafanyabiashara haramu wa meno ya tembo na pembe za faru pamoja na wanyama. Magenge Hayo ya uwindaji yalikuwa yanaratibiwa na watu kutoka China na Thailand. Hii imepelekea upoteaji mkubwa wa tembo nchini ambapo mnamo miaka ya 2009 mpaka 2015 kiasi asilimia 60% ya tembo nchini waliuliwa (Chanzo Makala ya Maraya Cornell, 2015 mwanajamii wa National geographic).
Hali ikawa mbaya zaidi kwa upande wa faru, ambapo biashara ya pembe zao ilishamili katika miaka ya 1970 mpaka 1990 hata kupelekea kuwa mnyama ambaye yupo hatarini zaidi kutoweka duniani. Hivyo serikali ikaingilia kati na kutangaza rasmi vita ya kupinga uwindaji wa faru (Chanzo Makala ya Robert Fyumangwa, 2010, black rhino conservation in Tanzania). Upazaji sauti wa serikali katika kupambana na ujangili ulisaidia wadau mbalimbali wa uhifadhi kusaidia uanzishwaji wa miradi ya kuwezesha jamii zinazoishi jirani na maeneo hayo pia kukaanzishwa uhifadhi unaohusisha maeneo ya vijiji kuwa chini ya umiliki wa serikali ya viijiji hivyo (Wildlife Management Area) na kuongeza hifadhi za taifa na mapori tengefu.
Aina ya uhifadhi wa maeneo ya vijiji na jitihada za wadau mbalimbali wa uhifadhi umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ujangili japokuwa jamii nyingine bado hazijakubaliana na jitihada hizo zote kwa kuwa bado zinajishughulisha na ujangili ambao unatumia sana mitego ya nyaya zenye vitanzi (snare) ambazo mnyama akiingia hapo sio rahisi kutoka Mitego hiyo mara nyingi husababisha kifocha maumivu makubwa ikifwatiwa. Vile vile sumu imekuwa ikitumiwa kwa kuwekwa kwenye maji, mizoga ya wanyama na hivyo wanyama na ndege wanaokula nyama hufa kwa wingi.
Usikose kufuatilia sehemu ya pili ya Makala hii ambayo inaeleza kwa kina juu ya mitgo ana sumu
Asante sana kwa kusoma Makala hii hadi mwisho, mhariri wa Makala hii ni Alphonce Msigwa, Mwikolojia Hifadhi za Taifa Tanzania.
Makala hii imeandaliwa na kuandikwa na
Leena Lulandala,
0755369684.