Uhifadhi maana yake ni juhudi za kutunza na kudhibiti matumizi ya rasilimali za asili ili kuhakikisha zinadumu katika vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa maana nyingine tunaweza kusema kwamba ni jitihada za kudhibiti, kurejesha na kuendeleza rasilimali za asili. Hivyo neno uhifadhi limebebwa na mambo makubwa matatu “kudhibiti, kurejesha na kuendeleza.

Tunaposema mazingira kwa ujumla wake, ni mambo yote au vitu vyote vinavyomzunguka mwanadamu, ikiwa ni pamoja na hewa tunayovuta, ardhi, mimea, wanyama, madini na kila tunachokifahamu.

Sasa tunaposema Uhifadhi na Mazingira maana yake ni kuangalia uwiano uliopo kati ya kuhifadhi na mazingira yetu, iwe ni kuhifadhi hewa, misitu, wanyama, maji, madini kila kitu kwa ujumla wake kwa ajili yetu na kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Tunaweza kuwa na ari ya kuvitumia vitu hivi kwa pupa bila kuangalia kwamba watoto wetu na wajukuu wetu watahitaji kutumia vitu hivi hivi na pengine tunaweza kutumia tukiwa na mawazo ya kutengeneza maisha bora kwa watoto na wajukuu zetu badae lakini je tumetafakari ni namna gani sahihi ya kutumia vitu hivi kwa mjumuiko wetu na ongezeko letu pasipo kuharibu mazingira yetu?

Tumesikia habari mbalimbali za namna ambavyo viumbe hai vinapotea na vingine kuwekwa katika makundi ya “hatari (endangered) au hatari zaidi kutoweka (critically endangered). Hii ina maana kwamba tujitathmini juu ya njia zetu na matumizi yetu.

Kwa mfano tukimuangalia mnyama tembo, ni mnyama mkubwa na sio kwa mwili tu bali hata kazi zake kiikolojia zimeonekana kuwa na faida kubwa katika kuendeleza maliasili, lakini leo tembo hawa wapo katika kundi la wanyama ambao wapo hatarini kupotea kwa lugha nyingine “endangered species.”

Picha kutoka katika hifadhi ya taifa ya Serengeti, Tanzania

Tunaweza kuwa tunawaona tu katika hifadhi lakini pasipo kufuatilia takwimu zinazofanyika tunaweza kujikuta tunawapoteza kabisa.

Ukiacha maelezo ya juu ya maana ya uhifadhi wa mazingira, pia kuna faida nyingi ambazo tutazipata kama kila binadamu atakuwa balozi wa uhifadhi mazingira kama ambavyo zimeelezewa hapa chini;

  • Mazingira safi ni tija katika afya zetu, tunavyoepuka uchafuzi wa mazingira ndivyo tunavyopata hewa safi na hata kuepuka magonjwa ya milipuko kama kipindupindu.,
  • Tunaona serikali yetu inafanya jitihada kupitia miradi yake mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira na pia yapo mashirika binafsi ambayo yanapambania kwa hali na mali kuunga mkono jitihada za serikali katika kutunza mazingira. Hii yote inafanyika kwa sababu wanathamini afya zetu na wanatamani kuona tukitumia mazingira yetu bila kuumia.
  • Tunaona pia umuhimu wa uhifadhi kwa viumbepori kwa maana ya kwamba mbali na utalii ambao hutuingizia mapato yanayasaidia katika kuendeleza miradi ya jamii, mazingira yao pia hutumika kama kiburudisho cha macho na kutuliza akili. Leo hii kuna watu wanatafuta sehemu tulivu kwa ajili ya kukaa kutulia na kupoteza mawazo, na wengine pia wanatumia sehemu hizi kama mahali pa ibada zao binfasi.
  • Katika jiografia tunafundishwa namna mazingira yanavyoingiliana katika kusababisha vitu ambavyo tunavihitaji katika maisha yetu, mfano mzuri kabisa ni mvua. Watu wengi sasa wanashiriki katika kuharibu misitu hata mvua zimekuwa za shida na kupelekea mazao kuharibika kabla ya mavuno sababu ya ukosefu wa mvua.
  • Sera ya “kata mti panda mti” ilikuja ili angalau kupunguza makali ya ukataji misitu uliokuwa ukiendelea na hatuwezi kusema tumefanikiwa kwa sababu mambo haya yanatekelezwa katika mapori ya akiba lakini sehemu za jamii zetu imekuwa ngumu, kaa na kutafakari, leo hii nikipanda mti huu wa matunda ni faida ngapi nitakazopata kuliko kukata miti tu pasipokuwa na mbadala wa kudhibiti madhara yatokanayo na vitendo hivo.
  • Uhifadhi wa mazingira pia unatupatia maji ambapo vyanzo vingi vinazidi kukauka kwa sababu ya uharibifu wa mazingira. Mfano mzuri ni kukauka kwa Mto Ruaha mkuu ambapo takwimu zinaonesha kwamba upungufu wa maji katika mto huo unazidi kuongezeka kwa sababu ya vyanzo vyake kuharibiwa. Madhara ya kukauka kwa mto huu yanaenda mbali zaidi hadi kuathiri mabwawa ya umeme kama vile Mtera, Kidatu na Mwalimu Nyerere

Hizo ni baadhi ya faida chache ambazo tunaweza kuzipata kwa kuhifadhi mazingira na na ni jukumu letu kuunga mkono juhudi za serikali kwa kutunza mazingira yetu kwa kutumia mbinu/njia zifuatazo;

  1. Kupanda miti katika maeneo yetu yanayotuzunguka na pia kushiriki upandaji wa mti kama njia ya kurejeza uoto uliopotea.
  2. Kutumia njia ya recycling (kuchakata tena au kutumia tena) baadhi ya vitu ambavyo vimetumika. Kama vile chupa za plastic, vyuma chakavu, mabati n.k ili kupunguza uchafuzi wa mazingira.
  3. Kutumia nishati mbadala kama vile gesi, umeme na majiko banifu wakati wa kupika.
  4. Kufundisha Mitaala ya uhifadhi wa mazingira kuanzia shule za awali na pia kuwepo na klabu mbalimbali ambazo Watoto watajifunza uhifadhi huku wakifurahia. Hii itamjengea mtoto kupenda mazingira yake kuanzia akiwa mdogo na hivyo kuzingatia ule usemi wa wazee wetu “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”

Mwisho kabisa makala hii imetupa nafasi ya kujifunza kwa kina juu ya maana halisi ya kuhifadhi mazingira, faida zake na namna tunaweza kufanya ili kuepuka au kuhifadhi mazingira.

Yapo mengi kuhusiana na uhifadhi lakin kwa leo tutaishia hapo na usikose kuendelea kujifunza zaidi juu ya uhifadhi kwa kutendelea kusoma makala zetu na kuwashirikisha wengine.

Kwa maelezo zaidi, unaweza kuwasiliana na mwandishi wa Makala hii ndugu Lilian Ladislaus Mihambo kwa namba na barua pepe ifuatayo;

Imeandaliwa Lilian Ladislaus Mihambo na kuhaririwa na Alphonce Msigwa

Mawasiliano

Email: lilianladislaus@gmail.com

Mobile: +255 767686014/+255 713386396