Biashara haramu ya meno ya tembo imeonyesha kukua na kushika kasi kubwa tangu mwaka 2007. Shughuli zote za ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo katika kipindi hiki unasemekana kuwa zaidi ya mara tatu ya ilivyokuwa katika miaka ya 1989. Tarifa za kitafiti kutoka katika Mfumo wa Taarifa wa Biashara ya Tembo (ETIS), CITES na MIKE pamoja na vyanzo vingine vya taarifa zinasema tembo wanakabiliwa na kipindi kibaya sana katika historia ya uhifadhi wake tangu mwaka 1989.

Makontena yakiwa katika bandari ya Mombasa ili yasafirishwe kwenda katika nci za Asia

Rafiki yangu unayesoma makala za mtando huu wa wildlifetanzania, karibu tena kwenye makala ya uchambuzi wa ripoti hii inayoitwa ELEPHANT IN THE DUST, THE AFRICAN ELEPHANT CRISIS, hii ni ripoti iliyotoka mwaka 2013 ikielezea kwa kina mambo yaliyotokea kwa wanyama hawa ambayo yemehatarisha kwa kiasi kikubwa uwepo wao katika uso wa dunia. Ni ripoti ambayo nimeichambua kwa kina ili kukupa maarifa na taarifa muhimu kwa ajili ya uhifadhi wa maliasili zetu muhimu, karibu kwenye uchambuzi huu.

Taarifa na takwimu za mfumo wa biashara za tembo zinasema nchi ya Kenya na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa ndio njia kuu za kusafirishia bidhaa za meno ya tembo na nyara nyingine kwa njia haramu. Wakai hayo yakiendelea taarifa za ukamataji wa bidhaa haramu unasema kiasi cha asilimia 47 ya meno ya tembo ilikamatwa katika bandari za mataifa haya mawili katika bahari ya Hindi katika kipindi cha miaka ya 2009 na 2011.

Hata hivyo wakati hayo yakiendelea katika Pwani ya Afrika Mashariki, kuna taarifa za hivi karibuni zikiitaja nchi ya Afrika ya Kusini kuwa kinara wa kusafirisha bidhaa haramu kupitia bandari yake kwenda kwenye nchi za nje. Nchi ambazo zimekuwa ndio sehemu ya kupeleka meno ya tembo zimekuwa ni nchi za China na Thailandi, hizi ndio kipaumbele katika uagizaji wa meno ya tembo hasa kutoka Afrika. Wakati nchi za Hong Kong SAR, Malasia, Ufilipino na Vieti namu zikiwa ni sehemu bidhaa hizi haramu hupitia ili kufika kwenye maeneo makuu yaliyokusudiwa.

Nchi hizo ndio hutajwa sana na kuhusishwa katika biashara haramu za meno ya tembo, pia ni nchi ambazo zina masoko na vinu kwa ajili ya utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na meno ya tembo kama vile mihuri, midoli, na mapambo mengine ya ndani, hivyo ni sehemu ambayo biashara hii ya meno ya tembo inafanyinka sana, hali ambayo inachochea sana ujangili wa tembo kwenye nchi ambazo zina hazina ya wanyamapori hawa duniani.

Hata hivyo, katika taarifa zilizokusanywa na vitengo vya uchunguzi na ukusanyaji wa taarifa za tembo na biashara haramu, imehusisha nchi nyingine ambazo nazo kwa kiasi kikubwa zinatiliwa shaka katika kusaidia sana usafirishaji au utoaji wa meno ya tembo kutoka eneo moja kwenda eneo jngine, nchi hizo ni Cameroon, Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Misri, Ethiopia, Gaboni, Mozambiki, Nigeria, Uganda na Taiwani.

Katika maeneo yote ambayo yanahusishwa na biashara haramu ya meno ya tembo, imegundulika kuwa mfumo wa biashara hii haramu una mtandao mkubwa sana ambao unasaidiwa na watu wengi na kwa kiasi kikubwa rushwa na udhaifu wa kusimamia sheria ndio inayosababisha kushamiri kwa biashara hii na kutishia kutoweka kwa wanyamapori hawa muhimu katika mfumo wa ikolojia ya wanyamapori na mimea.

Aidha, wakuu wa mashrikika ya uhifadhi na wanachama wa CITES walifanya mkutano wao wa 16 ili kujadili hatua za kuchukua baada ya kuona hali ya kutisha kwa wanyamapori hawa wanaoteketea kila kukicha, walitoa mapendekezo ambayo yangesaidia sana katika usimamizi, ulinzi na uhifadhi wa tembo. Pamoja na hayo kuweka sawa mfumo wa taarifa zianazopatikana kuhusu tembo ili ziweze kuleta uwiano mzuri ambao utapelekea wajumbe na wanachama wa CITES kuchukua hatua za makusudi katika uhifadhi wa tembo.

Tangu mfumo huo wa ukusanyaji wa taarifa uanze kufanya kazi zaidi ya  matukio 19000 ya ukamataji yametokea tangu mwaka 1989 hadi januari mwaka 2013. Ikionyesha zaidi ya nchi 90 kuhusishwa na kufuatiliwa kuhusu biashara haramu za wanyamapori. Hii ni jambo zuri kutokea baada ya kuanza utekelezaji wa makubaliano ya mkutano huo na mapendekezo yaliyotolewa katika kupambana na ujangili.

SOMA; UCHAMBUZI WA RIPOTI; (Flash Mission Report Port of Mombasa, Kenya), Bandari Ya Mombasa Na Usafirishaji Wa Nyara Na Bidhaa Haramu

Kuwepo na kuanza kufanya kazi kwa mfumo wa taarifa wa biashara za tembo umesaidia sana kujua mambo mengi yanayoendelea kuhusu biashara hii haramu, ujangili na wahusika, baadhi ya maembo mengi ambayo yemefikiwa na kuibuliwa kwa uwepo wa kitengo hiki kama kinavyojulikana kwa kingereza Elephant Trade Information System (ETIS) ni njia za usafirishaji, nchi ambazo zinatoa malighafi za wanyama hawa, nchi zinazonunua au kuhitaji meno ya tembo, matumizi ya meno ya tembo na mambo mengine mengi yanayosaidia kushamiri kwa biashara hii haramu kama vile udhaifu wa sharia, vita, rushwa, umasikini na kukosekana kwa uzalendo, mambo hayo yote na megine ambayo sijayataja yanachangia sana kupungua kwa tembo katika bara la Afrika na sehemu nyingine duniani.

Halikadhalika, taarifa za ukamataji wa meno ya tembo maeneo mbali mbali ndio unaonyesha kiwango cha kushamiri kwa biashara hii haramu, pia inaonyesha ni kwa namna gani ujangili unaendelea kwenye maeneo husika. Kenya na Tanzania ndio zinazoongoza kwa mujibu wa taarifa za ripoti hii katika usafirishaji wa nyara na bidhaa haramu za wanyamapori kama vile tembo. Bandari za nchi hizi ambazo zipo katika pwani ya bahari ya Hindi zimetajwa sana kwenye ripoti nyingi za uchunguzi na usafirishaji haramu wa meno ya tembo na nyara nyingine.

Hata hivyo, uchambuzi wa ripoti hii ya mwaka 2013 unasaidia kutoa ujumbe kwa jamii kuwa, nini kinaendelea au nini kilifanyika katika maliasili zetu na maeneo nyeti yanayohusika na kusafirisha meno ya tembo. Hivyo ingawa mambo haya yalitokea katika kipindi cha nyuma na ni watu wachache sana wana taarifa hizi za kina kuhusu hali ya mambo katika maliasili zetu, makala hii imejikita katika kuweka wazi mambo hayo ili jamii na wadau wa masuala haya, maafisa usalama, polisi, na wakaguzi wa mizigo kwenye maeneo ya usafirishaji wajue na wawe makini katika shughuli zao za kila siku ili kudibiti ujangili kwenye nchi zetu.

Naamini kabisa kwa kipindi hiki, mambo yamebadilika, hata ujangili umepungua hii ni kutokana na uimara wa serikali ya nchi yetu ya Tanzania na uzalendo wa watumishi wake kwenye maeneo yao ya kazi. Hivyo napenda kuwaasa watanzania wenzangu pamoja na majirani zetu Kenya ambao tumetajwa katika ripoti hii kuwa vinara wa usafirishaji wa bidhaa haramu za meno yatembo kwenye bandari zetu, tuungane na tusimame katika kukomesha kabisa mambo haya ya aibu yaliyofanyika katika nchi zetu ili yasije yakatokea tena.

Watanzania, tushirikiane na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa maliasili zetu ili kwa pamoja tuwe walinzi na wahifadhi wa maliasili zetu kwa ajili ya manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Ahsante sana kwa kusoma makala hii hadi mwisho!

Uchambuzi huu umeandaliwa na;

Hillary Mrosso

+255 683 862 481/255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania