Mara zote naamini katika elimu na maarifa sahihi ili kuongeza ufanisi kwenye eneo lolote. Kukosekana kwa taarifa na maarifa sahihi huleta kutojiamini na kufanya kazi chini ya kiwango. Ili sekta ya wanyamapori na maliasili kwa ujumla wake iendeshwe na kufanya kazi zake vizuri suala la elimu na mafunzo halitakiwi kukosekana na wala halitakiwi kuisha. Sekta ya maliasili na wanyamapori inajumuisha vitu vingi sana na ambavyo bado havijulikani, kwenye uhifadhi kunahitajika elimu ya sayansi na elimu ya jumla ya kijamii na mazingira ambayo yote huitajika ili kila kitu kiendeahwe kwa utalaamu na kwa ufanisi. Kwa kutambua hilo serikali ikaweka utaratibu mzuri wa kuanzisha vituo na taasisi nyingine za mafunzo ya usimamizi wa wanyamapori ili kujenga uwezo na ufanisi katika utendaji wa majukumu yake.
Sehemu ya kumi na sita (Part VI) ya sheria hii inaeleza umuhimu wa elimu, mafunzo na utafiti kwenye sekta ya wanyamapori. Sheria hii ya wanyamapori ya mwaka 2009. Inaeleza kwa kina utaratibu wa kuanzisha vituo na taasisi za mafunzo kwa maofisa, maaskari na watu wanaofanya kazi kwenye sekta hii muhimu. Hivyo uchambuzi wetu utaanzia kwenye kifungu cha 96, karibu tuielewe sheria.
96. (1) Waziri anaweza, baada ya kutoa taarifa itakayo chapishwa kwenye Gazeti la Serikali, kuanzisha taasisi za mafunzo au vituo vya kuendeshea mafunzo mbali mbali na kutoa kozi mbali mbali za usimamizi wa wanyamapori tofauti na ambazo hutolewa na Vyuo vya Usimamizi wa Wanyamapori au taasisi nyingine za elimu ya juu. Ufafanuzi kidogo hapa ni kwamba, Waziri mwenye dhamana anaweza kuanzisha vituo na taasisi maalumu kwa ajili ya kuendeshea mfunzo ya usimamizi wa wanyamapori, vituo hivi atakavyoanzisha na vitakavyokuwa vinatoa elimu ya usimamizi wa wanyamapori vitakuwa tofauti na vile vya elimu ya juu.
(2) Waziri anaweza, kwa kufuata kanuni kwenye Gazeti la serikali, kuandaa uongozi na usimamizi wa taasisi na vituo vilivyoazishwa kwa ajili ya mafunzo chini ya sheria hii. Ufafanuzi hapa ni kwamba mambo ya uongozi/utawala na usimamizi wa vituo na taasisi hizi zinazotoa mafunzo ya usimamizi wa wanyamapori utafanywa na Waziri mwenye dhamana kwa kuendana na matakwa ya sheria hii.
(3) Kulingana na maelekezo yaliyotolewa na Waziri, uongozi na usimamizi wa taasisi hizi za mafunzo zilizoanzishwa chini kifungu kidogo cha (1) ya kifungu hiki utakuwa chini ya uangalizi wa Mkurugenzi. Kwenye kipengele hiki ni kwamba mambo yote ya uongozi na usimaizi wa taasisi hizi za mafunzo ya usimamizi wa wanyamapori utakuwa chini ya uangalizi wa Mkurugenzi wa wanyamapori, hivyo mkurugenzi ndiye mwangalizi wa vituo na taasisi hizi muhimu.
(4) Mkurugenzi anaweza, baada ya kushauriana na Waziri, kuwawezesha kiuwezo maofisa mbali mbali wa wanyamapori kwa kuwapa mafunzo. Kipengele hiki kinatoa nafasi kwa maofisa na makada wanaofanya kazi kwenye sekta hii kujengewa uwezo wa kufanya kazi zao kwa ufanisi baada ya kupewa mafunzo mbali mbali kama Mkurugenzi atakavyo pendekeza baada ya kushauriana na Waziri.
97.-(1) Uongozi na utaratibu wa utafiti wa wanyamapori utakuwa uansimamiwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania ambayo imeanzishwa chini ya Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania. Ufafanuzi wa hapa ni kwamba uongozi na uratibu wa utafiti wa wanyamapori utasimamiwa na TAWIRI (Tanzania Wildlife Research Institute) au kwa Kiswahili ndio inajulikana kama Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania, ambapo mambo yote ya utafiti wa wanyamapori husimamiwa na hutoa vibali vya utafiti.
(2) Mkurugenzi anaweza, baada ya kushauriana na kwa mujibu wa uratibu/utaratibu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania, kuanzisha utafiti kwenye mambo yanayohusiana na wanyamapori ndani na nje ya maeneo ya hifadhi ambayo yapo chini ya mipaka ya sheria hii.
- Mkurugenzi anaweza kuanzisha, kutekeleza na kusaidia kutoa maarifa na tarifa kwa umma pamoja na programu mbali mbali ambazo hutoa elimu kwenye masuala ya wanyamapori ili kuwezesha utoaji wa maarifa na kuwajengea uwezo kwenye masuala ya matumizi endelevu na usimamizi wa rasilimali za wanyamapori.
99.-(1) Hifadhi za Taifa Tanzania na Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na taasisi nyingine za wanyamapori kwa ujumla watawajibika na kulazimika kuchangia kifedha kwenye taasisi za mafunzo na utafiti Tanzania. Ufafanuzi hapa, kuendelea kwa mpango wa kuisaidia jamii au umma kupata elimu na maarifa pamoja na kuhakikisha taasisi na vituo vyote vya mafunzo ya usimamizi wa wanyamapori hapa Tanzania sheria hii inazitaka mamlaka husika kuchangia mamlaka hizo ni kama vile TANAPA, NCAA, na TAWA. Au taasisi nyingine zinazojihusisha na wanyamapori.
(2) Waziri anaweza kwa kufuata kanuni, kuelekeza nmna na njia ambazo zitatumika kujua kiasi kitakachochangiwa kama ilivyotajwa kwenye kifungu kidogo cha (1).Ufafanuzi hapa ni kwamba waziri ataangalia kiasi ambacho kila taasisi itatakiwa kuchangia kwenye kuendesha vituo vya mafunzo a wanyamapori Tanzania.
Hivi ndivyo tunavyomalizia uchambuzi kwenye sehemu ya kumi na sita ya sheria hii. Ambapo mengi umeyafahamu kuhusu mambo ya kutoa elimu, kuwapa watu taarifa na maarifa, pamoja na kufanya utafiti. Napenda nitoe pongezi kwa serikali kuweka sehemu hii ya sheria kwani inalazimisha maofisa na wadau wa sekta hii kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kujiimarisha na kufanya kazi zao vizuri na kwa weledi.
Nakushukuru sana Rafiki kwa kuendelea kuwa msomaji wa makala hizi naamini zinakusaidia na zinawasaidia wale unaowahirikisha pia. Naamini kupitia elimu hii tutaifanya nchi yetu kuwa nchi inayotegemea zaidi watalii wa ndani kuliko wa nje, sambamba na hilo tutashrikiana kwenye uhifadhi wa maliasili zetu. Karibu sana kwa maswali, maoni, ushauri au mapendekezo.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 248 681/+255 742 092 569