Wanyama tajwa hapo juu ni wanyama jamii ya paka, wanyama hawa wanaochanganya sana hasa ukiwatizama kwa haraka ni kama wanafanana sana lakini pia wanatofautiana. Na kabla hatujaangalia kuhusu tofauti zao zifuatazo ni taarifa fupi za kukufahamisha mchanganuo wao wa kisayansi (Classification) ili tunapokwenda mbele zaidi zikupe ufahamu wa kina kuwahusu wanyama hawa hapa ndipo utakapogundua jambo zuri na la kuvutia kuwahusu wanyama hawa.
Chui (Leopard Duma (Cheetah) Chui milia (Tiger)
Jedwali 1; Mchanganuo wa kisayansi wa wanyama Chui, Duma na Chui milia(simba marara)
CHUI(Leopard) | DUMA(Cheetah) | CHUI MILIA(Tiger) | |
KINGDOM | Animalia | Animalia | Animalia |
PHYLUM | Chordata | Chordata | Chordata |
CLASS | Mammalia | Mammalia | Mammalia |
ORDER | Carnivora | Carnivora | Carnivora |
SUBORDER | Feliformia | Feliformia | Feliformia |
FAMILY | Felidae | Felidae | Felidae |
SUBFAMILY | Pantherinae | Felinae | Pantherinae |
GENUS | Panthera | Acinonyx | Panthera |
SPECIES | P.pardus | A.jubatus | P. tigris |
Ukitazama mchanganuo hapo juu utagundua kuwa wamechangia kuanzia kwenye hatua ya Kingdom hadi Family(jamii) wamekuja kutofautiana kwenye hatua ya Subfamily, Genus pamoja na hatua ya species japokuwa Chui na Chui milia wao wametofautiana kwenye hatua ya spishi tu. Hii inaashiria kwamba wamefanana vitu vingi sana, ndio maana kwenye makundi mengi zaidi wamewekwa pamoja.
Mbali na kuwa wamechangia maeneo mengi kwenye mchanganuo wa kisayansi (Classification),
Vifuatazo ni baadhi ya vitu vinavyowafanya wafanane kwenye maeneo mengi
- Wote ni wanyama pori jamii ya paka (Felines).
- Wote wanazaa na kunyonyesha kitaalamu wanaitwa mammals
- Wote hawa ni wanyama wanaokula nyama au kwa kitaalamu wanaitwa carnivores
- Rangi ya ngozi zao zina fanana kwa muonekano wake zina rangi ya manjano inayofanania na rangi ya dhahabu yenye michirizi na madoa meusi.
Wanyama hawa pia wana namna wanatofautiana ki muonekano, kitabia, Uwezo wao pamoja na Ki Ikolojia (mazingira wanayopatikana),
- Tukianzia ki muonekano
Hii ni sehemu yenye changamoto sana kwa watu wengi sana lakini ni sehemu pekee na ya muhimu sana katika kuwatofautisha wanyama hawa.
Jedwali 2; Tofauti ya muonekano wa wanyama tajwa hapo chini
Chui(Leopard) | Duma(Cheetah) | Chui milia(Tiger) | |
Ngozi zao | Ngozi yake ina madoa yaliyoungana kuchora viduara (Rosettes) |
Ngozi yake ina madoa ambayo yame sambaa hayana muunganiko wowote
|
Ngozi yake ina mistari(milia) na hapa ndipo lilipotokea jina la Chui milia
|
Nyuso zao | Hana alama za machozi (Tear marks)
|
Uso wake una alama za machozi (Tear marks
|
Hana alama za machozi ila ana michirizi mingi usoni
|
Maumbile yao kwa ujumla | Wana miili mikubwa na miguu mifupi yenye ujazo na wana vichwa vikubwa
|
Wana miili myembamba (Slender bodies) miguu mirefu myembamba na vichwa vidogo
|
Katika jamii ya paka huyu ndiye paka mkubwa kuliko wote amefanana na simba ila yeye ni mkubwa kuliko simba
|
Hizi ni baadhi ya tofauti za ki muonekano walizonazo wanyama pori hawa
- Tofauti za Kitabia na uwezo walio nao
- Chui pamoja na chui milia ni wanyama wanaochangamka sana wakati wa usiku kwa sababu ni wanyama wenye aibu sana (Shy animals) haswa chui milia hivyo hupenda sana kujificha wakati wa mchana na hata kuwinda wao huwinda vizuri zaidi wakati wa usiku na kama ni mchana basi liwe ni eneo lililo jificha sana (mbali na binadamu).
Sababu nyingine inayowafanya wapende sana kujitokeza usiku ni aina ya macho waliyo nayo, uoni wa macho yao ni hafifu sana wakati wa mchana na huwa na nguvu zaidi wakati wa usiku kwa kitaalamu wanaitwa nocturnal animals
Duma katika hili yuko tofauti na wenzake yeye ni mchangamfu zaidi wakati wa mchana kwa sababu yeye ana uoni mzuri wakati wa mchana na mara nyingi huonekana akiwinda mawindo yake mchana kitaalamu wanafahamika kama diurnals
- Chui ana uwezo wa kukimbia hadi kilometa 58 kwa saa(58km/h), wakati
Chui milia ana uwezo wa kukimbia hadi kilometa 49 had 65 kwa saa.
Duma ana uwezo wa kukimbia kwa mwendokasi hadi wa kilometa 112 kwa saa.
Hivyo basi miongoni mwa wanyama hawa Duma ndio mnyama mwenye kasi zaidi kuliko wenzake wote lakini pia ndie mnyama mwenye kasi zaidi ya wanyama wote duniani.
- Chui ana tabia ya kuvamia hapendi kukimbiza mawindo yake tangu akiwa mbali anajitahidi awasogelee kwa ukaribu zaidi kisha kufanya uvamizi wa kushtukiza, na mara baada ya kumuua mnyama amuwindae hupanda naye juu ya mti ili kuepuka bughudha kutoka kwa wanyama wengine kama fisi simba n.k. Hii ni tabia ya kipekee ambayo inamfanya chui kuwa tofauti na wanyama wengine wote.
Chui milia yeye pia hana tabia ya kukimbiza akiwa umbali mrefu lakini hujitahidi sana kusogea karibu ikiwezekana hadi mita 10 karibu na mnyama amuwindae kisha kufanya uvamizi wa kustukiza akiisha kuua anamvuta mnyama hadi kwenye machaka yenye utulivu tayari kwa chakula.Ni mnyama mwenye taya zenye nguvu sana anaweza kumvuta mnyama mkubwa jamii ya nyati hadi umbali wa mita 12 bila kupumzika. Kitu cha ajabu alichonacho chui milia ni kuwa pindi atakapogundua yule amuwindae amekwishagundua uwepo wa chui milia, chui milia huacha na kukata tamaa kumpata mnyama huyo pindi atakapohisi amegundulika.
Duma Yuko tofauti pia maana yeye kwake sio lazima sana kusogea karibu sana na mnyama amuwindae, ana uwezo wa kuanza kumkimbiza mnyama hata aliye umbali wa hadi mita 100 (sawa na urefu wa kiwanja kimoja cha mpira wa miguu) na hii ni sababu anauamini sana uwezo na kasi aliyonayo.
- Tofauti za ki Ikolojia (maeneo wanayopatikana)
- Chui milia wanapatikana kwa wingi sana bara la Asia. Lakini wamegawanyika katika maeneo tofautitofauti kulingana na jamii zao,
- Chui milia jamii ya siberia (siberian tiger) Hawa ndio chui milia wakubwa zaidi wanapatikana sana Kaskazini mwa bara la Asia tena maeneo yenye baridi sana kama Mashariki mwa Urusi, Kaskazini mashariki mwa China
- Spishi au jamii zilizo baki huwa ni za Chui milia wadogo kwa mfano jamii ya sumatran,Balinese, Malayank Hawa hupatikana upande wa kusini wa bara la Asia hizi ni sehemu zenye joto kama vile, India, Bangladesh, Nepal, Vietnum, Malaysia n.k
Huu ni mchanganuo mdogo tu kuonyesha mgawanyiko wa jamii zao lakini kwa ujumla wanapatikana sana Bara la Asia.
Wanapendelea sana kukaa misitu ya ki jangwa (Arid forests), Misitu ya mikoko(flooded mangrove forest), Misitu ya kitropiki(Tropic forest) pamoja na misitu ya taiga, japo mgawanyo wa maeneo tajwa hapo inategemea na spishi sio kila spishi anaweza kukaa kila eneo.
- Chui hawa wao hupatikana bara la Afrika kwa wingi na katika maeneo mengi pia japo sio yote. Mbali na bara la Afrika pia wanapatikana pia Bara la Asia kuanzia mashariki ya kati (Middle East) mpaka umoja wa Soviet (Soviet Union), Korea, China, India na malaysia.
Wana uwezo wa kuishi kwenye maeneo ya aina nyingi ikiwemo misitu, milimani, savanna( maeneo yaliyotawaliwa na nyasi) na hata jangwani pia wapo.
- Duma Hupatikana kukatisha bara la Afrika haswa Kaskazini mwa Afrika; Sahel (eneo la mpito kati ya sahara, kaskazini, pamoja na Savanna ya Ki Sudani (Sudanian savanna), kuelekea kusini); na wamesambaa kwa uchache kukatisha mashariki pamoja na kusini mwa Afrika, pia kwa uchache sana wanapatikana Iran.
Duma wanaishi maeneo tofauti tofauti kwenye misitu ya ki jangwa, maeneo tambarare yaliyo wazi (open plains) pamoja na maeneo ya majangwa. Pia hawa hitaji sana maji mengi wao hupata maji mengi hasa kupitia chakula wanachokula.
Hizi ni baadhi ya taarifa kidogo zinazoweza kukupa mwanga kuwa husu wanyama hawa pia napenda kutoa shukrani zangu kwa wasomaji wote maana najua kupitia ninyi elimu hii itawafikia wengi zaidi hata wasio na uwezo wa kusoma kwa pamoja tunafurahia elimu hii na nnaamini itakuwa msaada kwa jamii kwa namna moja au nyingine.
Cha zaidi kuhusu wanyama hawa ni kuwa kulingana na tafiti na takwimu mbalimbali kutoka mashirika tofauti yanayojihusisha na uhifadhi kama vile TAWIRI, TANAPA, IUCN, WWF, AWF n.k zinasema kuwa wanyama hawa wako hatarini kutoweka ulimwenguni. Hivyo basi ni wito wangu kwa jamii mbalimbali za Tanzania, Afrika, na popote pale duniani kwa yeyote yule asomaye makala hii tuwe sehemu ya kuwapenda na kuwahifadhi wanyama hawa ambao Mungu ametupa wawe sehemu ya maisha yetu uwepo wao ni fahari yetu pia.
Imeandaliwa na
Amos. B. George
0765304204
amosmazula333@gmail.com