Kijito (stream) ni mto mdogo, kijito kwa kawaida huwa na kiasi cha maji yanayotiririka ndani yake kuliko mto.

Ikolojia ya Kijito ni namna mfumo wa kifizikia, kikemikali na kibaiolojia unavyoingiliana katika mazingira ya Kijito. Mfumo wa Kijito hubadilika kutokana ushawishi wa haidrolojia (mzunguko wa maji), jiomofolojia, mabadiliko ya matumizi ya ardhi na athari za viumbe hai.

Afya ya Kijito ni hali ya Kijito kutokuwa na ishara za hatari katika mfumo wake wa maji, au ukosefu wa hatari au vitisho vinavyosukuma muundo, au utendaji kazi wa ikolojia ya Kijito.

Ikolojia ya Kijito ni miongoni mwa ikolojia iliyo katika hatari zaidi ulimwenguni, hivyo kuelewa hali ya ikolojia (afya) ya Kijito ni mhimu sana kwa ajili ya maisha ya viumbe hai.

Kwa kuelewa hali ya kifizikia, kikemikali na kibaiolojia ya Kijito  ni muhimu sana kwa kutekeleza kwa ufanisi mikakati  ya uhifadhi na usimamizi kabla ya afya ya Kijito  kibaiolojia kuathiriwa.

Viumbe wasio na uti wa mgongo wanao onekana, kama viumbe viashiria vya ikolojia (afya) ya kijito

Viumbe ashiria ni viumbe au spishi ambazoo huashiria kwa urahisi hali ya afya ya mazingira kibaiolojia, kikemikali na kifizikia, sifa kubwa  ni  viumbe wanaoathirika na mabadiliko ya mazingira kwenye makazi, jamii au mfumo ikolojia.

Watalaam wa ikolojia ya kijito walikubaliana kutumia viumbe hai ambao ni muhimu kutahthimini ikolojia ya kijito, ambao ni Viumbe wasio na uti wa mgongo wanao onekana kwa macho (microinvertbarate)

Viumbe wasio na uti wa mgongo wanao onekana kwa macho (microinvertbarate), ni viumbe wa dogo ambao kupitia wao ni rahisi kutathimini hali ya afya ya Kijito kwa urahisi kuliko viumbe wengine.

Wataalamu wa viumbe wasio na uti wa mgongo wemekuwa wakifanya sampuli ya viumbe wasio na uti wa mgongo kutoka kwenye Kijito, hasa vifaa malaamu vya kufanya sampuli ni kama Surber, D-frame dip, na kick neti.

Jamii ikishiriki katika Tafiti ili kujua afya ya kijito, mafunzo yaliyotolewa na taasisi ya Nature Tanzania, katika msitu wa asili wa Amani Tanga

Viumbe wasio na uti wa mgongo wametumika sana kama viashiria vya kibaiolojia katika nchi nyingi zilizoendelea kama vile Ulaya, Kanada na Marekani na wamejumuishwa katika viwango vyao vya kitaifa na kiufundi vya ufuatiliaji wa ubora wa maji.

Hata hivyo, kwa sasa, tafiti chache sana zimeanza kutumia Tanzania River Scoring System (TARISS). TARISS ni fahirisi ya viumbe hai wasio na uti wa mgongo wanao onekana kwa macho kwa ajili ya tathmini ya haraka ya kibiolojia ya mito ambayo imetengenezwa hivi karibuni.

Tathmini ya ubora wa maji nchini Tanzania hufanywa kwa kuchanganua vigezo vya kemikali-fizikia.

Pia hutumia kipimo cha kinyesi kama ilivyobainishwa katika muunganisho wa viwango vya kitaifa vya mazingira na Shirika la Viwango Tanzania, Tanzania Bureau of Standards (TBS).

Mwandishi wa makala hii Boniface Mwendapole (kushoto) akiwa katika Mafunzo ya  kuangalia afya ya kijito (streams) katika hifadhi ya msitu wa Amani, Tanga

Kwanini viumbe wasio na uti wa mgongo wanao onekana kwa macho hutumika kama kiashiria cha hali ya afya ya kijito?

  • Hutumia hadi mwaka mmoja kwenye vyanzo vya maji.
  • Kuwa na uhamaji mdogo
  • Wanapatikana kwa wingi
  • Chanzo kikuu cha chakula cha samaki wengi
  • Ni rahisi kufanyiwa sampuli
  • Kuathiriwa kwa urahisi na mabadiliko tabia nchi, upotevu wa makazi, uchafuzi wa kikemikali.

Makundi ya viumbe wasio na uti wa mgongo wanao onekana kwa macho kulingana na afya ya kijito

Kundi la 1 – Kundi lisilostahimili uchafuzi wa mazingira yake

Mifano, mayflies, stoneflies, caddisflies

Kundi hili ni viumbe hai wasio na uti wa mgongo wanaoekana kwa macho ambao wanaathiriwa sana na uchafuzi wa aina yoyote kwenye Kijito au hawawezi kukaa kwenye Kijito chenye maji machafu. Hivyo uwepo wa viumbe hawa katika Kijito ni ishara ya kuwa hali ya afya Kijito ni salama.

Picha za baadhi ya wadudu wasioweza kustahimili uchafuzi wa mazingira yake: picha na Joan Schumaker Chadde, M.S. Water Resource Specialist.                           

Kundi la 2 – Wanaoweza kuhimili uchafuzi kiasi

Kereng’ende, mende maji, ni jumla ni viumbe vinavyoweza kuhimili uchafuzi wa kijito kwa kiasi Fulani, wanaweza kuhimili kuishi katika Kijito kwa sababu mahitaji yao makubwa ni makazi. Hivyo hata oksijeni au kiwango cha kemikali kikiwa kimepungua kwa kiasi wadudu hawa wanaweza kuishi vizuri, wadudu hawa sio rahisi kuwatumia kwenye kutathimini afya ya Kijito.

Picha za kundi la wadudu wanaoweza kuhimili uchafuzi kiasi wa mazingira yao ya maji: picha na Joan Schumaker Chadde, M.S. Water Resource Specialist.

Kundi la 3 – Kundi stahimilivu kwa  uchafuzi

Wadudu wasio na uti wa mgogongo kama vile minyoo ya majini, mabuu ni aina ya wadudu ambao wanaweza kustahimili uchafu kwenye Kijito pia wanaweza kuishi kwenye oksijeni kidogo, pH ya chini/juu, maji ya joto. Kutokana na watalaamu wa wadudu (entomolojia) uwepo wa wadudu hawa kwenye Kijito ni ishara ya kuwa na uchafuzi katika eneo hilo.

Picha za wadudu wanaostahimili uchafu kwenye mazingira yao: picha na Joan Schumaker Chadde, M.S. Water Resource Specialist.

Vitisho vya ikolojia ya kijito

Ulimwenguni kote, tishio kuu la ikolojia ya Kijito ni mabadiliko ya haraka yanayotokea katika matumizi ya ardhi, hali ambayo imeongezeka zaidi ya miaka kumi iliyopita.

Ubadilishaji wa  matumizi ya ardhi umekuwa wa uzalishaji wa mazao, ambayo unaathiri mifumo ikolojia wa Kijito.

Matumizi ya mbolea na dawa za kuulia wadudu zinazotumiwa katika kilimo huathiri vibaya mifumo ikolojia ya maji baridi kwa kutiririka kwenye mito yenye viumbe hawa.

Zaidi ya hayo, matumizi makubwa ya ardhi ya kilimo mara nyingi husababisha uharibifu wa misitu, ambayo mara nyingi hufika kwenye ukingo wa mito ambayo ni makazi ya viumbe hawa.

Ukataji miti hasa kwenye vyanzo vya maji unachangia kuharibika kwa makazi ya viumbe hawa muhimu, ukataji miti unachangia kuongezeka kwa joto na mwanga kwenye makazi ya wadudu hawa.

Umuhimu wa jamii kushiriki katika uhifadhi wa kijito

Jami zina maarifa muhimu ya kimapokeo ya ikolojia  kuhusu hali ya kihistoria ya Kijito, mifumo ya mtiririko wa maji, na upatikanaji wa spishi.

Ujuzi huu ni muhimu kwa kutengeneza mikakati ya uhifadhi ambayo inafaa kitamaduni, inayofaa ikolojia, na iliyoundwa mahsusi kulingana na hali ya mahali hapo.

Jamii zinaposhiriki kikamilifu katika kupanga, kutekeleza, na ufuatiliaji wa mipango ya uhifadhi, wanakuza hisia ya umiliki na uwajibikaji.

Hii inakuza kujitolea kwa muda mrefu kudumisha afya ya Kijito au mto, na kufanya uhifadhi kuwa endelevu zaidi na kustahimili mabadiliko ya nje.

Sera na kanuni zinazotengenezwa kwa mchango wa jamii zina uwezekano mkubwa wa kueleweka, kukubalika na kufuatwa.

Jamii husika pia zinaweza kuchukua jukumu muhimu katika kufuatilia shughuli haramu (kwa mfano, uvuvi haramu, utupaji taka, ukataji miti) na kuziripoti.

Jamii zinaweza kuchangia kazi, nyenzo za ndani, na hata rasilimali za kifedha (kwa mfano, kupitia mifuko ya jamii au ushuru) kwa miradi ya uhifadhi, kupunguza utegemezi wa ufadhili wa nje na kufanya mipango kuwa na faida zaidi kiuchumi.

Kushirikisha wadau mbalimbali ndani ya jamii kunaweza kusaidia kutambua na kupunguza migogoro inayoweza kutokea kuhusu matumizi ya rasilimali.

Michakato ya kufanya maamuzi shirikishi inaweza kujenga uaminifu, kuimarisha mitandao ya kijamii, na kukuza mshikamano kuhusu lengo la pamoja la uhifadhi.

Vitisho vingi vya kuhatarisha afya vinatokana na shughuli za kibinadamu (kwa mfano, ongezeko kwa kilimo, utupaji taka usiofaa, ukataji miti).

Kuwezesha jamii kuelewa athari hizi na kuendeleza ufumbuzi wa ndani ni muhimu ili kukabiliana na sababu za msingi za uharibifu.

Asili inayobadilika ya mifumo ikolojia ya mtiririko inahitaji usimamizi unaobadilika. Jamii, wakiwa waangalizi wa moja kwa moja wa mabadiliko, wanaweza kutoa maoni ya wakati halisi juu ya ufanisi wa hatua za uhifadhi, kuruhusu marekebisho na maboresho kwa wakati.

 Ushiriki wa jamii kwa vitendo uhifadhi wa ikolojia ya kijito

Kutoa mafunzo kwa watu wanaojitolea kukusanya taarifa za ubora wa maji (kwa mfano, sampuli za wanyama wenye uti wa mgongo mkubwa, pH, oksijeni iliyoyeyushwa) na kuripoti matokeo kwa mamlaka. Hii sio tu inakusanya data muhimu lakini pia huongeza ufahamu ndani ya jamii.

Jamii  kuaandaa mipango ya upandaji miti kando ya kingo za mito ili kuleta utulivu wa udongo, kupunguza mmomong’oko wa udongo, kutoa kivuli, na kuchuja maji..

Jamii kundaa programu za ukusanyaji na urejelezaji taka za ndani ili kuzuia uchafuzi wa mazingira usiingie kwenye vijito na mito.

Kuundwa kwa kamati za washikadau mbalimbali zinazojumuisha wakazi wa eneo hilo, wakulima, vikundi vya kiasili, na wawakilishi wa serikali ili kupanga kwa pamoja na kutekeleza mikakati ya uhifadhi wa maeneo mazima.

Kuhuisha na kurekebisha desturi za kiasili kwa ajili ya uhifadhi wa maji, udhibiti wa mafuriko, na marekebisho ya desturi ambayo yamejikita katika utamaduni na maarifa ya jamii.

Hitimisho

Afya ya kijito ni mahimu sana kwa maisha ya kila ya binadamu, hasa kujipatia maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Kupunguza mabadiliko tabia nchi, mbali na faida ya vijito, binadamu hao hao ndio kichochezi kikubwau uharibufu na uchafuzi wa vijito na mito.

Hivyo kipitia makala hii fupi, tujenge tija katika uhifadhi wa vijito na mito kwa manufaa yetu sote.

Hakikisha unakuwa mstari wa mbele kutunza na kuhifadhi ikolojia ya vijito na mito inayotuzunguka.

Twende tukawaeleze jamii umuhimu na faida ya vijito na mito, ili jamii iwe na elimu ya uhifadhi ya vijito na mito.

Makala hii imeandikwa na Boniface Mwendapole na imeririwa na Hillary Mrosso. Unaweza kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa mawasiliano hapo chini.

Makala hii imeandikwa na

Boniface J. Mwendapole

boniphacejames69@gmail.com

+255743038781