Habari msomaji wa mtandao wetu wa Wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo ambayo tutatafakari kwa pamoja kuhusu thamani ya kitu ambacho kipo kwenye jamii yetu, kwenye kichwa cha habari hapo juu nimeeleza kuwa watu wataendelea kuthamini, kuheshimu na kulinda kile kitu ambacho kina manufaa kwao au kinafaida kwao. Hii ni asili ya binadamu sehemu yoyote ile duniani, binadamu hupenda kuona matokeo ya kile kitu anachokilinda au alichonacho, kwa upande mwingine binadamu huwa hapendi kushindwa au kuendelea na kitu ambacho kinamshinda na kumletea matokeo ambayo hakuyategemea, na hali hii ipo kwenye ufanyaji wa kila jambo.

Jana niliandika makala kuhusu  uanzishwaji wa maeneo ya hifadhi ya jamii kuwa yamesaidia sana kuinua uelewa wa jamii kwenye masuala ya wanyamapori, uhifadhi na rasilimali nyingine. Kwenye makala hiyo nilielezea sababu za kuanzishwa kwa maeneo haya ya hifadhi ya jamii yajulikanayo kama WMAs (Wildlife Management Areas), kwamba lengo kuu ni kuihusisha jamii moja kwa moja kwenye usimamizi wa wanyamapori na rasilimali nyingine zinazopatikana kwenye maeneo hayo. Kwa mantiki hiyo maeneo haya yapo kwenye mikono ya jamii, na jamii ndio inayoamua ustawi na matokeo ya uwepo wa maeneo hayo karibu nao. Pia uwepo wa maeneo haya na kumilikiwa au kusimamiwa na jamii ulilenga kuwa dhana ya jamii kumiliki na kushiriki kwenye maliasili zao utajenga uzalendo na mtazamo mzuri kwenye maliasili za nchi yetu.

SOMA MAKALA HII;Uanzishwaji Wa Maeneo Ya Asasi za Kijamii umesaidia sana Kuinua Uelewa Wa Jamii Kuhusu Wanyamapori Na Maliasili Kwa Ujumla

Aidha pamoja na mambo hayo ukweli ni kwamba maeneo mengi ya WMAs yanakabiliwa na changamoto nyingi, hali hii inatishia kupotea kwa maana ya maeneo haya kwenye jamii, maeneo haya yalipo anzishwa sera na sheria za uendeshaji, mifumo na njia za kupata faida kutokana na uwepo wa rasilimali zilizopo kwenye maeneo haya umebakia kwenye makaratasi na vitabu. WMAs nyingi zinasua sua katika utekelezaji wa sera zake, na jambo hili ndio linapelekea kukosekanakwa matokeo mazuri kama ilivyotazamiwa au ilivyoelekezwa kwenye sheria. Kutokana na hali hiyo jamii imekosa nguvu na shauku ya dhati ya kuyasimaia maeneo haya, kwa mfano kama jumuiya ilitakiwa kuwa na vyanzo vya mapato kupitia utalii wa aina mbali mbali kama wa picha na uwindaji na hakuna uwekezaji wowote kwenye jumuiya hiyo kwa miaka mingi jambo hili linapelekea nguvu na hamasa za kuendeleza maeneo haya kupotea.

Kama nilivyotaja kwenye kichwa cha makala hii kama maeneo haya ya hifadhi ya wanyamapori na maliasili nyingine yaliyopo kwenye jamii hayataleta faida inayotakiwa, ni jambo gumu kwa jamii kuendelea kuthamini na kuheshimu uwepo wa maeneo haya. Maeneo haya tangu kuanzishwa kwake yalitakiwa kutoa matokeo mazuri na pia kutoa mchango mzuri ambao jamii inauona kuwa umetokana na uwepo wa jumuiya yao, jambo ambalo halijafanikiwa kwenye WMA nyingi. Na hii ndio sababu imepelekea maeneo mengi ya hifadhi ya jamii kushindwa kufanya vizuri kutokana na watu au jamii kupoteza ari na shauku ya kuyatunza; kuna wakati nilikuwa na wanajamii wanaosimamia WMA ya MBOMIPA wakawa wanasema “kwa sasa hii asasi imeshakufa na hatuoni faida yake ni bora wawarudishie vijiji ardhi yao walime na wachungie mifugo yao humo maana hatuoni faida yake”. Kwa kauli kama hizi ni dhahiri kuwa kuna shida na changamoto nyingi kwenye maeneo haya, na changamoto hizi zinahitaji kutatuliwa mapema.

Nimeandika makala hii sio kwamba naungana na baadhi ya wanajamii ambao wana mawazo ya kuzifunga na kurudisha ardhi ya vijiji ambavyo vilitoa kwa ajili ya kuunda maeneo ya jumuiya ya hifadhi wanyamapori la hasha! Na sio kwamba naandika makala hii kuonyesha kwamba uwepo wa maeneo haya hauna faida kwa jamii na wala haujaisaidia jamii kwa jambo lolote. Kuna maeneo machache ya hifadhi ya jamii yanafanya vizuri, kwa mfano WMA za Kaskazini mwa Tanzania zinafanya vizuri na zinatengeneza mapato makubwa sana ambayo huwekwa wazi kwa jamii ,Ikona, Enduimet, Burunge nk. ni baadhi ya WMA ambazo zinapiga hatua nzuri sana.

Naamini ukuaji wa utalii au sekta ya utalii umechangia sana ukuaji wa maeneo haya ya hifadhi ya jamii, kama wengi tunavyofahamu Kaskazini mwa Tanzania utalii umekua sana kulinganisha na Kusini mwa Tanzania, hivyo moja kwa moja sababu hiyo ndio inayopelekea ukuaji wa WMA zilizopo kwenye maeneo hayo. Ni jambo la muda na mipango mathubuti kwa hifadhi za jamii zilizopo maeneo mengine kuanza kutengeneza faida kubwa na mapato kwa jumuiya zao. Jinsi ambavyo utalii unaendelea kushika kasi kwenye maeneo ya Kusini pia hata hifadhi hizi zitanufaika na mbadiliko hayo. Jambo kubwa la kufanya kwenye asasi hizi ambazo zinachangamoto ni kuandaa na kupitia mara kwa mara malengo yao na njia za kuwaingizia kipato kwenye WMA zao. Na jambo hili linatakiwa kufanyika kwa njia ya wazi na jamii ifahamu kwa kina ni nini kinaendelea na ni hatua gani zinachukuliwa ili kutengeneza faida kwenye maeneo yao waliyo yatoa kuunda WMAs.

Hivyo basi ili kunusuru hali hii ya jamii kususia uwepo wa maeneo haya ya hifadhi ya jamii, uongozi wa asasi, bodi ya washauri wa rasilimali, na wadau wengine na jamii kwa ujumla wake wakae na kufanya mikutano na vikao vyenye lengo la kutatua changamoto zao, pia ni vizuri jamii nzima kushirikishwa kwa uwazi juhudi zote wanazochukua viongozi wao ili waone matumaini na wawaunge mkono. Endpo mambo yatafanyika bila uwazi jamii itakaa gizani na hawataelewa nini kinaendelea hivyo wataona wao sio sehemu ya jumuiya hiyo, jambo ambalo litapelekea kukosa ushirikiano kwenye uhifadhi wa maliasili za maeneo yao.

Ahsante sana kwa kusoama makala hii, naamini itasaidia kitu kwenye kuchukua hatua na maamuzi ya kufanya WMAS zetu kuwa na manufaa makubwa na yaliyokusudiwa kwa jamii husika. Endelea kufuatilia na kujifunza kila siku kwenye blog yetu hii na pia hata kwa njia ya facebook unaewza kutupata pia kwa jina la Hillary Mrosso.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania