Makala mbili zilizopita nilandika kuhusu Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara na hifadhi ya Tarangire zote zikiwa zina patikana Kaskazini mwa Tanzania. Tuliangalia vitu muhimu kwenye kila hifadhi na kwa kweli vilikuwa vitu vizuri sana ambavyo vitakufanya uelewa wako kuhusu hifadhi hizi uwe mkubwa. Naamini kama tunaenda pamoja kwenye kila makala ninayoiandika utapata mwanga mkubwa ili uweze kujichagulia ni hifadhi gani ni nzuri kutembelea kipindi unapopanga kutembea hifadhi. Leo tuangazie macho yetu kwenye hifadhi moja ya kipekee kuliko zote Tanzania. Ni hifadhi ambayo kwa kingereza wanasema where the beach meets the bush, akimaanisha kwamba ni hifadhi ambayo ufukwe wa bahari unakutana na hifadhi. Ni hifadhi ambayo ipo upande wa Mashariki mwa nchi yetu.
Hifadhi hii ambayo ilianza kama Pori Tengefu (Game Reserve) tangu miaka ya 1960, baada ya hapo hifadhi hii ilipandishwa kutoka kuwa Pori Tengefu hadi kuwa Tifadhi ya Taifa ya Saadani mnamo mwaka 2005, baada ya kupanuliwa kuongeza msitu wa Zaraninge na Ranch ya Mkwaja. Hifadhi hii yenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,100, ni hifadhi ambayo ilikuwa na matukio mengi ya ujangili kwenye miaka ya 1990, lakini baadya ya juhudi za makusudi hali hii imebadilika kabisa, kwa sasa ndani ya hifadhi hii unaweza kuona makundi ya wanyamapori kama tembo, nyani, ngiri, simba, twiga, swala, fisi na hata chui. Ni hifadhi ya kipekee inayopakana na bahari ya Hindi kwa upande wa Mashariki, ambapo watu wa Pwani ndio wanaoishi karibu zaidi na hifadhi hii, mfano Tanga, Bagamoyo, na hata Dar es salaam. Ni hifadhi yenye vivutio vingi vya tofauti kabisa na hifadhi nyingine za Tanzania kutokana na mambo mengi hasa utamaduni wa watu waishio karibu na hifadhi hii.
Hii ni hifadhi ambayo inafikika kwa urahisi na watu wengi, na pia ni hifadhi inayofikika kila wakati au kila msimu wa mwaka, yani kuwe na mvua au kusiwe na mvua unaweza kufika katika hifadhi hii kipindi chochote cha mwaka. Kwa hiyo ni hifadhi ambayo kama upo Dar es salaam, Tanga, au mikoa ya karibu kama Bagamoyo, Pwani, unaweza kutembelea hifadhi hii kwa gharama nafuu sana. Na pia unaweza kutembelea na vivutio vingine vilivyopo hata nje ya hifadhi hii, vingi vikiwa ni vya kihistoria, kwa mfano Bagamoyo, na Makumbusho ya Dar es salaam.
Vivutio ambavyo unaweza kuviona katika Hifadhi hii ni vingi sana vikiwemo vya kihistoria na vya kitamaduni, kama vile maboma ya mawe yaliyojengwa na Wajerumani, hali nzuri ya hewa katika ufukwe wa bahari ya hifadhi hii ya Saadani, na mandhari nzuri sana ya ufukwe wa pwani ya bahari ya Hindi inayopakana na hifadhi hi kwa kiasi kikubwa, bila kusahau tamaduni za watu wa Pwani hasa kwenye mavazi, vyakula na hata kuongea. Pia kwenye hifadhi hii yenye misitu ya jamii ya mikoko (Mangrove forest) ndio kivutio kizuri sana kwa hifadhi hii, misitu hii yenye mandhari nzuri kwa wanyama jamii ya nyani na kima, pia na ndege wengi sana huishi na kuzaliana katika misitu hii mizuri ya pwani ya hifadhi hii ya kipekee.
Uoto wa asili wa hifadhi hii ambao ni mchanganyiko wa savanna, misitu yenye nyasi fupi, vichaka vidogo vidogo pamoja na misitu iliyopo kando kando ya bahari ya hifadhi ya Saadani ndio mandhari nzuri sana kwa hifadhi hii, pia wanyama wengi hupenda sana mazingira ya namna hii ili kuzaliana na kupata chakula chao kwa wingi.
Kuna sifa nyingine ya kipekee sana kwenye hifadhi hii ya Saadani ambayo ni pale maji safi, maji yasiyo na chumvi kutoka katika mto Wami hukutana na maji ya chumvi kutoka bahari ya Hindi. Sifa hii sio tu imevutia watalii na watafiti wengi bali hata wanyama wengeni imekuwa ndio sehemu nzuri na salama ya kuishikwa wanyama na samaki, wanyama wa majini kama kiboko na mamba,huonekana sana kwenye mto huu unaotiririsha maji yake kwenda bahari ya Hindi.
Pia kutokana na uwepo wa mto Wami kupita katika hifadhi hii, imechangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa ndege wengi kama vile Flamino, ambao hupenda kwenda kwenye mwambao wa ufukwe kula baadhi ya vyakula vilivyotokana na mazingira ya chumvichumvi kwenye ufukwe wa hifadhi hii. Pia samaki aina ya Dolfini pamoja na Nyangumi huwa wanaonekana nje ya ufukwe wa Saadani kwa miezi ya Agasti na Septemba. Hivyo kwa wageni na watu wanaopenda mazingira ya namna hii basi hapa ndio sehemu ya kuona vivutio hivi adimu kabisa.
Kutokana na sehemu ambayo hifadhi hii ipo, imezungukwa na miji na majiji yaliyoendelea na pia ni sehumu zinazotembelewa na wageni wengi, hifadhi hii imepakana na Zanzibar, Bagamoyo, Pangani, na Dar es salaam. Jambo jingine muhimu utakapotembelea hifadhi hii ya Saadani utapata fursa nzuri ya kuona Meli na Boti au Mashua za wavuvi wa samaki na pia utalii wa aina hiyo baharini na kwenye mto Wami. Hivyo kwa wageni wanaotembelea sehemu hizo ni vizuri pia wakatembelea na hifadhi hii, ambayo ipo karibu kabisa ili kujionea vivutio vizuri zaidi.
Kuna Watanzania ambao hawajawahi kuona wanyamapori, wala hawajawahi kuona bahari, nawashauri sehemu nzuri ya kuanzia ili uone vyote ni kuanzia hifadhi hii ya Saadani, hapo ndipo utapata uelewa na ufahamu wa kutosha kuhusu wanyama na mambo menngine mazuri ya kihistoria.
Asante sana kwa kusoma makala hii, nakutakia kila la kheri kwenye maandalizi yako ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
0742092569