Habari rafiki yangu, karibu tena siku ya leo tujifunze namna nzuri kabisa ya kufurahia tunapotembelea maeneo ya vivutio mbali mbali. Watu wanapopanga kutembelea hifadhi huwa na matazamio au mategemeo fulani kwamba anataka kumwona fisi, au simba tu, hana haja na wanyama wengine au vitu vingine vizuri vilivyoko huko. Sasa leo tunakwenda kuangalia kwa undani kwa nini watu wengi wakikosa walivyotegemea wanakosa raha, wanaona kama wamepoteza fedha zao, au wamejichosha kwa kazi ya bure. Hivyo fuatana na mimi kwenye makala hii tujifunze hatua kwa hatua jinsi unavyoweza kufurahia kila utakachokiona hifadhini au sehemu yoyote yenye vivutio.
Ipangilie safari yako na uamue kuifurahia
Watu wengi wanapanga safari za kutembelea hifadhi au maeneo mengine yenye vivutio kwa muda mrefu, wanaweka fedha kidogo kidogo, ili siku ikifika waende kutembelea maeneo ya vivutio mbali mbali. Hii pia inatakiwa iathiri saikolojia yako yote, yani ujiandae kisaikolojia kufurahia safari yako, safari yako uliyoipanga hakikisha inakuwa na furaha na ufurahie kila utakachokiona. Vile vile hakikisha umeondoka nyumbani ukiwa na moodi nzuri, sio kwa kukwaruzana na kukosa amani, hakikisha umeipangilia hata familia yako vizuri, na kila kitu umekiweka vizuri ili usisumbuliwe unapotembelea maeneo ya vivutio, jipange kuifurahia safari yako.
Jiandae kwa mategemeo/matarajio yako
Wengine wanakua na mategemeo tofauti tofauti kwenye safari yao, mwingine atapenda kuona wanyama wa aina fulani tu mwengine atapenda kuona mito na uoto wa asili, mwingine atapenda mandhari ya sehemu hiyo. Sio vibaya kuwa na matarajio au mategemeo hayo ni vizuri kabisa, ila ninachotaka tuone hapa ni jinsi ya kukufanya uifurahie safari yako hata kama utakosa vitu ulivyovitarajia kuviona.Hivyo sio mara zote mategemeo yako yatatimia kama ulivyopanga, ulipanga umwone simba au mbwa mwitu, lakini umefunga safari ya muda mrefu iliyokugharimu fedha na muda mwingi, halafu unakosa kile ulichokitazamia.
Hali ya namna hii ya kuwa na matazamio ya aina fulani tu, itakusababisha kutoona umuhimu na uzuri wa vivutio vingine muhimu vy hifadhi au sehemu nyingine yoyote. Hivyo angalia sana mategemeo yako. Ninacho kushauri fungua macho yako kwenye maeneo haya, unapotembelea hifadhi au maeneo ya vivutio mbali mbali, fungua macho yako, jifunze kwa kila unachokiona kitakufanya uitumie siku yako vizuri.
Vipo vitu vingi vya kuangalia na kujifunza
Unapokuwa hifadhini kuna kuwa na vitu vingi sana ambavyo hatuvijui, mfano miti, wanyama, ndege na hata miamba au mabonde na miinuko furahia yote hayo, angalia mazingira tu ya hifadhi , angalia hata udongo angalia hata nyasi angalia hata mito angalia hata hali ya hewa, jifunze kutochukulia kwa mazoea maeneo haya adimu na muhimu. Kuwa na kamera yako na upige picha mbali mbali kwa ajili ya ukukumbusho wako mwenyewe.
Kuna watu fulani walitembelea hifadhini wakaniambia hawajaona chochote, nilishangaa sana kwa kauli yao ya kwamba amezunguka hifadhini hajaona chochote, hili lilinifikirisha sana, kwenye hifadhi iliyojaa kila aina ya maliasili na viumbe hai wengine wazuri. Mtu kama huyo anaona kapoteza fedha na muda wake kutembelea hifadhi hii na pia wengine wanasema kwa wengine hifadhi fulani haina wanyamapori ambao yeye hajawaona. Kumbe yeye lengo lake ilikuwa kuwaona mbwa mwitu na chui amabo hajawahi kuwaona kwa macho yake.
Sasa ngoja nikupe siri, kila kitu kilichopo hifadhini ni kivutio, unaweza usione wanyama uliopanga kuwaona hata kwa siku tatu, unaweza usione ndege uliopanga kwamba utawaona kwasababu wanyamapori sio kama binadamu kwamba watutafute sisi, au kwamba wanaweza kukaa sehemu moja kwa ajili yetu tu hapana, wanyamapori wanaratiba zao pia, hata kama umetoa hela nyingi kiasi gani, unaweza usiwaone wanyamapori maeneo ambayo yamezoeleka, kwani huwa wanahama kwa ajili ya kutafuta chakula na au kwa mambo yao mengine. Hivyo usijiwekee asilimia zote kwamba lazima nitawaona wanyama fulani, unaweza usiwaone.
Wanyama kama simba, duma, fisi, chui, mbwa mwitu, kakakuona, ambao wanapendwa sana na watu ni wachache sana kwenye hifadhi zetu nyingi, kwa hiyo unaweza kubahatika kuwaona au usiwaone. Hivyo elewa hilo mapema kabisa kabla ya kupanga kwenda hifadhini. Lakini pamoj na hayo unaweza kufurahia wanyamapori wengine ambao wanapatikana huko, kama vile swala, twiga, tembo, nyani, ngiri na wengine wengi. Furahi kila utakachokiona huko ambacho huwezi kukiona kwenye maeneo mengine.
Ahasante sana kwa kusoma makala hii naamini itakuwa imekusaidia sehemu fulani;
Hillary Mrosso
Widlife Conservationist
0742092569/0683248681