Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania, karibu kwenye tafakari ndogo kuhusu hali ya utalii kwenye baadhi ya hifadhi za taifa na maeneo mengine muhimu kama vile Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Katika pita pita yangu nilijionea bango moja lenye taarifa na takwimu za wageni wanaoingia na kutalii kwenye Eneo la hifadhi ya ngorongoro. Nilifanikiwa kuuliza maswali kadhaa kwa wahusika na walinijubu vizuri sana. Katika bango nililoliona lilionyesha takwimu za wageni na wazawa kwa mwezi na mwaka mzima wanaotembelea hifadhi ya eneo la Ngorongoro. Takwimu hiyo ilionyesha taarifa za miaka kuanzia 2012 hadi 2016, nitaweka hapa kielelezo cha kuonyesha taarifa hizo.
Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni sehemu yenye mvuto kwa watu wengi sana duniani, hii ni kutokana na sababu mbali mbali ambazo hazipatikani katika hifadhi yoyote hapa Tanzania na duniani kwa ujumla. Ngorongoro yenye ukubwa wa kilomita za mraba 8292, ni moja kati ya Wilaya tatu za mkoa wa Arusha. Vivutio vilivyopo katika eneo hili vinafanya eneo hili kuwa maarufu zaidi duniani, maeneo na uoto wa asili kwenye eneo hili umekuwa na mvuto mkubwa sana kwa wageni, shimo la kreta na milima na mabonde yanayoizunguka eneo hili ndio yanachangia kutoa mvuto wa kipekee kwa hifadhi hii.
Licha ya kuwa na idadi kubwa ya wanyama na ndege adimu kama vile Faru, eneo hili ni moja ya maajabu nane ya dunia. Mfumo wa uendeshaji na maisha katika hifadhi hii unashangaza mamilioni ya watu, ni moja ya eneo pekee nchini Tanzania shughuli za uhifadhi na shughuli za kijamii huruhusiwa kufanyika sehemu moja. Yani hapa ni kwamba ni hifadhi ambayo shughuli nyingine za maendeleo kama vile kilimo na ufugaji hufanyika ndani ya hifadhi huku wanyamapori nao wakiendelea na maisha yao. Hii inashangaza watu wengi sana kwasababu kwa tunavyojua binadamu alivyo muharibifu anawezaje kuishi na wanyamapori kwenye eneo moja? Jamii inayoishi katika hifadhi hii ni jamii ya kifugaji yaani, wamasai. Hivyo lazima wawe na mifugo mingi na wengine waendeshe kilimo.
Hivyo wageni na wazawa wengi sana hupenda kutembelea eneo hili la Ngorongoro. Hali ya hewa, uwepo wa ndege wa aina nyingi, mimea, na mwonekano wa shimo la Kreta ndio umekuwa kivutio kwa watu wengi. Utamaduni uliodumu kwa karne nyingi upo kwenye eneo hili, mabaki ya kihistoria na bila kusahau ni eneo ambalo linasadikiwa kwa asilimia kubwa kuwa ndio binadamu wa kwanza aliishi na mabaki yake kuonekana hapo. Historia yake itakuacha mdomo wazi ukishangaa pale utakapoona na kuhadithiwa mambo ambayo unaweza usiyaamini kama yapo Tanzania na katika eneo hili la Ngorongoro.
Kwa takwimu za mwaka 2016, inaonyesha wageni waliotoka nje ya nchi kuja kutembelea Eneo la hifadhi ya Ngorongoro ni 284,794 huku takwimu za watanzania au wazawa zikiwa ni 265,845. Kwa mwenendo huu ni kwamba idadi ya wageni imeshuka mwaka katika miaka ya 2015 mwaka 2016, wakati idadi ya wageni kwa miaka ya nyuma ilikuwa ni kubwa kulinganisha na miaka miwili ya kuanzaia 2015 na 2016. Pamoja na hayo mabadiliko, bado tuna nafasi ya kuboresha utalii wetu wa ndani na kuvutia watu wengi zaidi. Kwa ufafanuzi mzuri nimekuwekea hapa takwimu za kuanzia mwaka 2012 hada 2016, kwa wageni na wazawa waliotembelea hifadhi ya eneo la Ngorongoro pekee.
Niseme kwamba Hifadhi ya Eneo la Ngorogoro haijabadilika wala kushuka hadhi yake, vivutio ni vile vile, tena vinazidi kuwa na mvuto kwa kadri siku zinavyokwenda. Hivyo kama unapanga kuja kutembelea eneo hili, karibu sana. Njoo uone mwenyewe usiishie kusimuliwa na mtu au kusoma tu kwenye vitabu na majarida, karibu uje ufurahi, ujifunze .
Ahasante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 248 681/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania