Habari Mtanzaia mwenzangu? Karibu kwenye makala ya leo ambayo ni moja ya makala ya kusaidia kuamsha hamasa ndani ya kila mtu atakayesoma kupata uelewa na ufahamu kuhusu rasilimali na vivutio vyote vilivyopo katika nchi yetu, ili tutambue ni utajiri kiasi gani upo hapa nchini kwetu, na namna ya kunufaika na kuinufaisha nchi yetu, kwa ushiriki wako kwenye ukuaji wa utalii wetu na uchumi wa nchi yetu. Kama kichwa cha habari kinavyojieleza lazima kila Mtanzania afanye maazimio ndani ya nafsi yake kufanya jambo la kutembelea hifadhi za Taifa na vivutio vingine muhimu kabala ya kuondoka hapa duniani, au kufariki. Ni ukweli usiopingika kila mtu ataondoka hapa duniani, kila mtu atakufa, usikubali kujifia tu bila kuyatumia maisha yako ukiwa hapa duniani kutembelea na kuyafurahia maisha yako.
Maisha ya mwanadamu ya kuishi hapa duniani ni mafupi, yamejaa mambo mengi, changamoto nyingi, ambazo hutufanya kujisahau sana, pamoja na maisha kuwa na changamoto na mambo mengi lazima uamue kuyafurahia maisha yako, lazima ufanye mambo unayotaka kufanya kwenye maisha. Maisha tunayoyaishi hapa duniani hakuna sehemu nyingine utaenda kuyaishi tena, vitu unavyovifanya sasa hapa duniani hakuna sehemu utaenda kuvifanya tena ukishaondoka hapa duniani, hivyo unapopata nafasi ya kuishi hapa duniani tumia kila fursa uliyonayo kuyaishi maisha yako yote hapa duniani, tumia kila fursa uliyonayo kuyafurahia maisha yako hapa duniani, vitu unavyoviona hapa duniani vinavutia na kupendeza kama hujavitumia na kuvifurahia ukiwa hai, hakuna sehemu ambayo utavikuta ukishaondoka hapa duniani, hivyo pambana kuishi maisha yako na ndoto zako.
Kuna watu wanakufa wakiwa na ndoto zao za kusafiri dunia nzima, kuna mtu ana ndoto ya kutembelea dunia nzima kuiona dunia, kuna wenye ndoto za kwenda nchi mbali mbali hapa duniani kuna wenye ndoto za kutembelea kila mkoa katika nchi ya Tanazania kuna wenye ndoto ya kutembelea hifadhi zote zilizopo hapa Tanzania kuna wenye ndoto, kuna wenye ndoto za kutembelea sehemu zenye maajabu saba ya dunia. Ni vizuri sana kwa watu kuwa na ndoto za namna hii, lakini ukiangalia hali yako na majukumu uliyonayo unaona hata huwezi kutimiza hata moja kati ya ndoto zako. Ndio maana nimeandika makala hii kukuhamasisha na kukupa moyo, inawezekana kabisa kufikia ndoto zako, kwani unatamani kiasi gani kusafiri?
Unajua kwanini wengi wameshindwa kutimiza ndoto zao hizo? Kwasababu walitaka kuanzia na ndoto kubwa za kwenda labda Marekani au kuizunguka dunia, wakati hajawahi kutembelea hata hifadhi ya mikumi au hata kivutio kimoja hapa nchini Tanzania. Ngoja nikwambie siri kama unataka kufanya mambo makubwa anza na mambo madogo kwanza, ukiyaweza yale madogo yatakupa hamasa na utajiona mshindi kwa hatua unazopiga kwenye maisha yako. Kwa mfano unapenda kutembelea maeneo ya kihistoria kwenye nchi ya Misri au Israel au nchi yoyote ile, usisubiri mpaka upate fedha za kwenda huko Misri au Israel, anza na hapa nyumbani, tumia kwanza kile kilichopo karibu na wewe kabla ya kwenda mbali, anza kutembelea maeneo ya kihistoria yaliyopo hapa Tanzania, nenda Isimila, nenda Kondoa Irangi, nenda Oldupai George, nenda Kilwa, nenda Bagamoyo, nenda Zanzibar, nenda kwanza sehemu hizi za karibu, ukiziweza nakwambia utakuwa na uwezo mkubwa wa kwenda sehemu nyingine.
Sasa cha ajabu unakuta mtu hajawahi kwenada sehemu hizo hata moja wapo alafu anataka kwenda nchi nyingine, ndoto yako hiyo inaweza kuchukua miaka mingi kutimia, au isitimie kabisa. Sasa kama umefanikiwa kutembelea maeneo hayo ya karibu, hata ukishindwa kwenda sehemu nyingine lakini utakuwa na amani ndani ya moyo wako kwamba hata hivyo nimejaribu na kufanya yote niliyoyaweza, hutajihukumu tena kwenye nafsi yako, utasimulia mambo mazuri kwa watoto wako na wajukuu zako, utawaambia mwenzenu nilikuwa na ndoto za kusafiri dunia nzima kwenda kuangalia maeneo ya kihistoria lakini nilishindwa kwenda, lakini hata hivyo nimefanikiwa kutembelea vivutio vizuri vya hapa hapa Tanzania, waooo! Itakwa hadithi nzuri sana na ya kuvutia.
Fanya maazimio ndani ya moyo wako Mtanzania mwenzangu, fanya maamuzi hayo bila woga, kwamba kabla sijafa, kabla sijaondoka hapa duniani nitatembelea vivutio vyote vilivyopo hapa Tanzania, nitaizunguka nchi nzima na hata duniani. Ukiwa na malengo na ndoto za namna hii nakuwambia maisha yako yatabadilika, utaishi kwa kujituma sana, utakuwa na nidhamu ya pesa itakayokusaidia kutembelea sehemu unazopenda kwenda. Utaishi maisha ya furaha na maisha ya ndoto zako katikati ya dunia yenye mambo mengi. Kuwa mlevi wa aina hii, tenga fungu la fedha kwa ajili ya kufanya jambo hilo lenye manufaa kwako na kwa nchi nzima, utaimarisha afya yako ya akili na ya mwili na hata afya yako ya kiroho itaimarika kwa kutembelea sehemu mbali mbali.
Mwisho, mimi nimeazimia kutembelea hifadhi na sehemu zote za vivutio vilivyopo hapa Tanzania, na sehemu nyingine duniani. Ningependa kujua na wewe Mtanzania mwenzangu mwenye ndoto kama zangu, au unatamani kutembelea kivutio chochote hapa Tanzania, au hata kama ulishatembelea usisite kutoa maoni yako hapo chini mwisho wa makala hii, ningependa uniambie unapendelea kutembelea maeneo gani, nini kinakuvutia zaidi hapa duniani, ungependa kutembelea vivutio gani hapa Tanzania, tafadhali unaposoma unijulishe na mimi pia kwa kuandika sehemu hiyo hapo chini. Karibuni tufanye kazi kwa pamoja kuinua utalii wetu, inawezekana kabisa.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
0742092569/0683248681
www.mtalaamu.net/wildlifetanzania