Kakakuona wa ardhini (Temminck’s ground Pangolin) akitembea, utaona akiinua miguu ya mbele akiwa anatembea. Picha kutoka mtandaoni

Kakakuona ni wanyama jamii ya mamalia, wanyama hawa ni miongoni mwa wanyama wa kipekee sana kutokana na maumbile yao, maisha yao na mitazamo ya watu juu ya wanyama hawa.

Kakakuona ni aina ya mamalia wenye magamba, mwili wake umefunikwa na magamba magumu, magamba hayo ni mfano wa kucha za binadamu. Sehemu kubwa ya mwili wa kakakuona umefunikwa na magamba hayo magumu, kasoro sehemu ya tumboni na usoni, ambako hakuna magamba.

Magamba haya humsaidia kujilinda na maadui. Endapo anahisi hatari au kukutana na adui kama vile simba, fisi, mbwa, chui nk, hujikuja na kuwa kama mpira wa miguu. Hujikunja kwa namna ya kulinda sehemu ya tumbo ambayo haina magamba.

Duniani kuna aina au spishi 8 za kakakuona, spishi 4 zipo katika bara la Asia na spishi nyingine 4 zinapatikana katika bara la Afrika. Tanzania imebarikiwa kuwa na aina tatu za spishi za kakakuona. Spishi hizi za kakakuona ni kakakuona wa aridhini, ambaye kwa kingereza anaitwa ground pangolin, kakakuona tumbo jeupe, au kwa kingereza anaitwa white belied pangolin, na kakakuona mkubwa wa ardhini, au giant ground pangolin.

Kakakuona ni wanyama wasioonekana kwa urahisi, mara nyingi hutokea maeneo fulani kwa wakati fulani, sio rahisi kukutana na kakakuona porini. Ni wanyama adimu sana kuwaona.

Hata hivyo, ni wanyama ambao watu wengi huwahusisha na bahati, utabiri, dawa za baadhi ya magonjwa, kuondoa uchawi au laana katika kaya za watu au jamii fulani.

Licha ya kuwa ni adimu na ngumu kuonekana, taarifa kutoka mamlaka za usimamizi wa wanyamapori Tanzania zimekuwa zikikamata na kuwashikilia baadhi ya watu wakiwa wanajihusisha na ujangili na kufanya biashara haramu za wanyama hawa.

Maeneo ya vijijini wanapoonekana wanyama hawa, watu huwa kamamata na kuuza au kuwatumia kwa mambo ya jadi, imani za kishirikina na dawa za kienyeji. Taarifa zinaonyesha waganga wa kienyeji wamekuwa na mahitaji makubwa ya wanyama hawa kwa ajili ya kutengeneza dawa za kienyeji.

Utafiti wa hivi karibuni, uliofanywa na Shirika la Uhifadhi na Utafiti Tanzania, imebaini kuwa baadhi ya wafugaji, waganga wa kienyeji na watu wa kawaida wakihusishwa sana na matumizi ya kakakuona. Unaweza kusoma hapa kufamu kuhusu utafiti huo

Utafiti huo umeonyesha eneo la Ruaha ambako aina ya kakakuona wa ardhini huonekana mara kwa mara kuna matumizi ya kakakuona kama dawa, hasa kwa waganga wa kienyeji, kakaona pia amekuwa akihitajika na baadhi ya wafugaji kwa ajili ya ulinzi wa mifugo na pia kuongezeka mifugo.

Magamba ya kakakuona yameonekana kuwa na matumizi makubwa zaidi, sio tu hapa Tanzania, bali hata katika nchi za China, Nepal, Vietnam na India, hata hivyo, nchi hizi zimekuwa zikihusishwa na matumizi makubwa ya kakakuona kama chakula cha kifahari.

Watuhumiwa wakiwa wameshikiliwa na magamba ya kakakuona

Mahitaji na matumizi makubwa ya wanyama hawa, imepelekea kakakuona wa bara la Asia kuwa katika hatari kubwa ya kutoweka kabisa. Watafiti wa mambo haya wana wasiwasi mkubwa sana kwasbabu, kuisha na kupungua sana kwa kakakuona wa Asia, imepelekea watumiaji wa kakakuona katika nchi hizo kuhamia kwa kakakuona wa Afrika.

Hali hiyo imesababisha ongezeko la biashara haramu, ujangili na matumizi yaliyopitiliza ya wanyama hawa katika bara la Afrika, ikiwemo Tanzania.

Sehemu nyingi za nchi za Afrika, kama vile Afrika Magharibi, Afrika ya Kati na nchi zilizomo Kusini mwa Afrika zimeripotiwa kuwa na matumizi makubwa ya kakakuona kama kitoweo muhimu.

Licha ya changamoto hizo, hakuna taarifa za kutosha kuhusu wanyama hawa hasa hapa Tanzania. Taarifa muhimu zinazoonyesha maeneo walipo, idadi yao, biashara haramu, ujangili na ikolojia yao kwa ujumla.

Hata hivyo, kuna juhudi kubwa za serikali na mashirika binafsi kama TRCO, wanajitahidi kutafiti, na kutoa elimu kwa jamii kuhusu wanyama hawa, faida zake, na umuhimu wa uhifadhi wa wanyama hawa.

Tunaweza kuungana na serikali, mashirika binafsi, wadau wa uhifadhi katika kulinda na kutunza wanyama hawa wa kipekee wanaopatika Tanzania. Endapo utamuona kakakuona katika maeneo yenu, usisite kutoa taarifa kwa mamlaka husika, ambazo ni serikali ya kijiji,

  • Ofisi ya kijiji au mtaa unapoishi
  • Afisa wanyamapori wilaya (DGO)
  • Hifadhi za taifa Tanzania (TANAPA)
  • Mamlaka ya usimamizi wanyamapori Tanzania (TAWA)
  • Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro (NCA)
  • Wakala wa Huduma za misitu Tanzania (TFS)
  • Mashirika ya ubinafsi ya uhifadhi kama TRCO

Asante kwa kusoma makala hii, imeandikwa na Hillary Mrosso

Tunaandika makala hizi ili watu waongezewe uelewa kuhusu kulinda na kutumia Maliasili muhimu bila kuathiri uwepo wao wa sasa na baadaye; kazi hii tunafanya kwa kujitolea na hakuna malipo yoyote, endapo umefurahia kazi zetu kutuunga mkono kwa kiasi chochote ili tupate nguvu, na ari ya kuandika makala nyingine nzuri, usisite kuwasiliana nasi kwa maelezo zaidi

Hillary Mrosso

+255683862481

hmconserve@gmail.com