Karibuni Wahifadhi Wote
Kuendelea na kukua kwa kasi ya teknologia katika dunia ya sasa imewezesha baadhi ya vitu vingi kugundulika na kufanyika kwa haraka. Hakuna wakati kwenye historia ya dunia mambo yanavyokwenda kwa kasi kama sasa. Kila kitu ambacho kilidhaniwa ndivyo kilivyo sasa kimebadilika, muundo wa Maisha na mifumo iliyowekwa kwa muda murefu hadi kufikia kuwa ni kama uamaduni kwa jamii husika sasa hauwezi tena kufua dafu mbele ya zama hizi za mabadiliko ya kasi na ukuaji wa teknologia nyingi kwenye kila eneo. Kila eneo, kila sekta inayogusa Maisha ya binadamu na ile isiyogusa Maisha ya binadamu, hakuna kitu ambacho hakijaguswa na mawimbi haya ya mabadiliko.
Lengo langu la kuandika Makala hii sio kuandika hadidhi nzuri yenye kuvutia kuhusu mabadiliko na historia ya dunia, hapana, nimeamua nianze hivyo ili tuweze kuwa na msingi mzuri wa uwelewa wetu kwenye mambo ninayotaka tujifunze leo, ambayo nayo yana uhitaji mkubwa wa kuchukulwa na kila upepo mzuri wenye kuleta ufanisi na mabadiliko chanya kwenye sekta hii ya uhifadhi wa Wanyamapori na maliasili kwa ujumla.
Ktokana na ukweli usiopingika kwamba ulimwengu tulionao na zama tunazoishi ni zama za taarifa, hii inamaana kwamba mwenye taarifa sahihi ndio mwenye nguvu na uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi muhihi kwenye nafasi husika. Hata hivyo kukosekana kwa taarifa za msingi na zenye kuleta mapinduzi kwenye sekta zote za maendeleo kumesababisha baadhi ya watu waliokaa kweneye nafasi hizo kwa muda mrefu kuondolewa kwa kuwa hawakutambua majira na zama husika.
Kuandika makala hii ni kiu na shauku yangu kwa watanzania wenzangu kuwa na ushirika na kuwa na uwanja mpana wa kufanya maamuzi kwenye muenendo wa hifadhi na maliasili zetu. Natambua kwa asilimia kubwa ya watu wanaojua kusoma na kuandika wanaweza kuwa kwa namna moja ama nyingine watumiaji wa mitandao ya kijamii. Hivyo basi utumiaji huu wa mitandao ya kijamii kwa ajili ya malengo au sababu tofauti tofauti, lakini kitu kikuu watu wanachotafuta ni taarifa mbali mbali.
Kuanzishwa kwa blog hii ya kitalaamu lengo ni kujifunza kwa pamoja, kupata maarifa, na uelewa wa mambo yote yanayohusu hifadhi zetu, maliasili zetu, mazingira yetu, na vivutio vyote vilivyopo Tanzania. Blog hii nimeamua kuiita Wildlife Tanzania kwa sababu kwa kiasi kikubwa ndio professional yangu na ndio niliyosomea kwa miaka 3, hivyo hapa patakuwa ni sehemu muhimu pa kupata maarifa kwa wanafunzi, walimu, na hata watalamu wengine wa mambo ya wanyamapori na maliasili. Pia kuandika kwa lugha ambayo kwa kiasi kikubwa itatoa mwanga na ukakasi kwa watanzania wengi, nimeamua kutumia Kiswahili kwenye makala hizi ili kuwe na uelewa wa moja kwa moja kwa wasomaji wengi wa Tanzania na nchi nyingine zinazozungumza Kiswahili.
Natamani kila mtanzania aelewe umuhimu wa maliasili zetu, kazi zake na namna nzuri ya kuendelea kuzihifadhi kwa ajili ya sasa na kizazi kijacho. Ndio maana nimeipa makala hii kichwa cha wahifadhi, natamani watanzania wote tuwe wahifadhi wa rasilimali hizi adimu zinazopatikana kwa wingi katika nchi yetu.
Hivyo kwa moyo mkunjufu, kwa moyo wa uzalendo niwakaribishe wote kufuatilia na kusoma Makala nitakazokuwa naandika kila siku kuhusu eneo hili muhimu kweneye nchi yetu. Karibuni, wasomi, wakulima, wafanyabiashara, walimu, watalamu wa misitu, watalamu wa mimea, watalamu wote wa wanyamapori, maaskari na watafiti wa maswala yote ya uhifadhi na mazingira. Karibuni kupata maarifa hapa.
Nawashukuru kwa kuungana nami katika kulinda kutunza na kuenzi maliasili zetu.
Makala hii imeandikwa na ;
Hillary Mrosso
0742092569

