Ni matumaini yangu umzima wa afya kabisa ndugu msomaji wa makala hizi za wanyamapori kwani tumepotezana kwa muda kidogo ila unapo patikana wasaa kama hivi hasi hatuna budi kujuzana machache kuhusu wanyama hawa. Huu ni mfululizo wa makala za wanyamapori ambazo nimekuwa nikikuletea mara kwa mara ili uweze kujua sifa, tabia, uhifadhi na uelekeo wa wanyama hawa hapaduniani hasa tukiangalizia hapa nchini kwetu Tanzania. Kwanikuna faida kubwa sana tuzizpatazo kutokana na uwepo wa wanyama hawa hawa nchini na hasa pato la taifa kutokana na shughuli za kitalii zinazo liingizia taifa fedha nyingi za kigeni.
Basi nikusihi uendelee kuwa nami mwanzo mpaka mwisho wa makala hii ili uweze kujua katika makala ya leo tunamzu ngumzia mnyama gani na ana sifa gani. Nina uhakuka mara tu utakapokuwa umeisoma makala hii mwanzo mpaka mwisho tena kwa ufasaha basi utakuwa umepata kitu kipya tena chenye faida kubwa kuhusu utambuzi wa mnyma ambae ataibeba makala hii ya leo.
Kama kawaida bado tunaendelea na mfululizo wa kuwaelezea wanyama jamii ya swala kwani kundi hili lina wanyama aina mbali mbali sana ambao kadri tunavopata wasaa tutazidi kujulishana mpaka hapo tutakapo fikia ukomo wa wanyama hawa hususani kwa ambao wanapatikana hapa nchini kwetu Tanzania. Katika makala ya leo tutamzungumzia swala ajulikanae kwa jina la “ISHA” ambae kwa lugha ya kiingereza anaitwa “STEENBOK”.
UTANGULIZI
Isha ni mnyama apatikanae kwenye kundi la wanyama jamii ya swala kama nilivokwisha dokeza hapo juu ambae anapatikana maeneo ya mashariki na kusini barani Afrika hususani hapa nchini. Mnyama huyu usipokuwa makini unaeza kumchanganya na mnyama Taya kwani wanafanana sana. Lakini kupitia makala hii naamini utaweza kuwatofautisha wanyama hawa ambao wanachanganya sana katika kuwatofautisha.
Na moja kwa moja sasa tuanze kuchambua kipengele kimoja hadi kingine katika kumjua mnyama isha ili ndugu msomaji wa makala hizi uweze kupata kile ambacho nimekuahidi kukipata mara tu utakapo kuwa umeisoma makala hii kwa utulivu na ufasaha zaidi.
SIFA NA TABIA ZA ISHA
Isha ni miongoni mwa swala wenye umbo dogo kama walivo kina taya.
Miili yao ina manyoa mafupi yenye rangi ya dhahabu inayoendana na kahawia au wakati mwingine manyoa yao huonekana kuwa na rangi ya wekundu.
Sehemu za mashavu, baadhi ya maeneo shingoni na kwa upande wa chini yaani kifuani mpaka tumboni wanyama hawa wana manyoa yenye rangi nyeupe.
Macho ya Isha ukiwaangalia vizuri utaona yamezungukwa na manyoa yenye rangi nyeupe na wana uwezo mkubwa sana wa kuona.
Wana masikio yaliyo chongoka ambayo sehemu za ndani za masikio yao yamezungukwa na alama nyeusi za mistari yenye umbo kama kidole. Hawa ni miongoni mwa wanyama wenye uwezo mkubwa sana wa kusikia.
Kwa pamoja madume na majike wana matezi yenye rangi nyeuusi ambayo yanaonekana sehemu ya mbele ya macho yao.
Wana kwato ngumu zilizo chongoka ambazo huwasaidia kuchimba vyakula vyenye asili ya mizizi.
Wanyama hawa wana miguu mirefu na iliyo nyooka zaidi.
Madume pekee ndo huwa na pembe ambazo zimenyooka, ziko sambamba, nyororo na zilizo chongoka. Pembe hizi hurefuka na kufikia urefu wa sentimita 7 hadi 19.
Isha ni wanyama ambao wanafanya shughuli zao majira ya asubuhi na mchana, na maranyingi kipindi cha joto kali hupendelea kupumzika kwenye kivuli chini ya miti.
Hupenda kujisaidia kwenye mashimo na kisha kuyafukia mashimo hayo. Hii huwasaidia wanyama hawa wasigundulike kirahisi maeneo waliyopo hasa kutokana na maadui zao.
Wanapohisi kuna adui wanyama hawa hutulia na kujificha lakini adui anapo wakaribia hukimbia na kutafuta maficho mengine hasa kwenye mashimo yaliyo achwa na wanyama kama mhanga.
Dume na jike huishi mbali mbali na hukutana kipindi wanapotaka kuzaliana tu hivyo dume mmoja huwa na jike mmoja tu na eneo lao huwa na ukubwa wa hekari 4 mpaka 100.
Tofauti na swala walio wengi, isha hawatumii matezi kuweka mipaka katika maeneo yao na maranyingi hutumia kinyesi tu au kuwafukuza isha wengine ambao wameingia kwenye eneo lao.
UREFU, KIMO NA UZITO WA ISHA
Urefu=Isha mkubwa hufikia urefu wa sentimita 70 hadi 95.
Kimo= kimo cha isha hufikia sentimita 45 hadi 60.
Uzito= wanyama hawa huwa na uzito wa kilogramu 7 hadi 16.
MAZINGIRA
Kama nilitangulia kusema hapo juu, wanyama hawa wanapatikana Afrika mashariki na kusini mwa Afrika tu na si kwingine kokote kule duniani. Wanapedelea mazingira yenye majani tu na tafiti zinaonesha kuwa wanyama hawa ni kwa nadra sana kuwaona katika maeneo ambayo kwa asilimia kubwa ardhi imetawaliwa na miti.
Nchi ambazo wanyama hawa wanapatikana ni Tanzania, Zambia, Angola, Botswana, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Kenya na Zimbabwe.
CHAKULA
Isha ni wanyama walao majani kama walivyo wanyama jamii ya swala wengine. Wana uwezo wakula mizizi pia pamoja na vyakula jamii ya vitunguu.
Wanyama hawa hawapendelei kunywa maji mara kwa mara kwani maji mengi huyapata kupitia chakula au aina ya majani wanayo kula mara kwa mara. Hivyo wana uwezo wa kuishi muda mrefu sana bila kunywa maji.
KUZALIANA
Kama nilivo tangulia kuandika hapo juu kuwa wanyama hawa dume mmoja huwa na jike mmoja tu na huishi mbali mbali ila hukutana kipindi wanapo hitaji kuzaliana tu. Isha hupandana majira yoyote ya mwaka japo maranyingi watoto huzaliwa kipindi cha mwezi wa Novemba au Disemba.
Mara tuu baaada ya kupandana jike na dume husambaratika na jike hukaa na mimba kwa muda wa miezi 5 hadi 6 kisha huzaa mtoto mmoja tu. Mtoto wa isha anapo zaliwa huchukua saa moja ndipo aweze kusimama na kuanza kutembea lakini kwa kipindi cha wiki chache za mwanzo mama humficha mtoto eneo salama lenye majani dhidi ya maadui. Mama huondoa kinyesi cha mtoto pamoja na kufukia viashiria vyiovyote vile ambavyo vinaweza kuwafanya maadui kugundua mahali alipo mtoto na kumuuwa.
Mtoto hutegemea maziwa ya mama kwa muda wa miezi 3 ya mwanzo. Watoto wa kike hufikia umri wa kujitegemea na kuweza kuzaa pale wafikishapo miezi 6 hadi 7 ila kwa watoto wa kiume nikuanzia miezi 9 japo mara nyingi huanza kujitegemea pale wafikishapo mwaka mmoja tu. Maisha ya isha huishi kwa takribani myaka 7 awapo porini japo umri unaweza kuongezeka kama isha anafugwa katika bustani maalumu za kufugia wanyamapori.
UHIFADHI
Ni jambo la kushukuru kuwa wanyama hawa bado hawajawa hatarini kutoweka duniani kutokana na taarifa za shirika linalosimamia uhifadhi wa maumbile asili duniani (International Union for Conservation of Nature-IUCN). Mwaka 1999 sensa ilifanyika na kubaini makadirio ya wanyama hawa kuwa 600,000 japo hii ilionekana kuwa ni makadirio ya chini na kwamba wanyama hawa huenda wakawa juu ya idadi hiyo. Idadi kubwa ya wanyama hawa inasemekana kuwa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.
Ingawa bado hakuna taarifa zinazo onesha wanyama hawa kuwa hatarini bado hatutakiwi kuridhika na hali hiyi kwani kuna baadhi ya nchi wameanza kutoweka kwenye baadhi ya maeneo nchini humo. Mfano nchini Lesotho isha wameanza kutoweka baadhi ya maeneo kutokana na sababu mbali mbali ambazo tutaziona katika kipengele kinacho fuata.
MAADUI NA CHANGAMOTO KWA ISHA
Katika mazingira asili ya wanyama hawa maadui wakubwa kwa isha ni chui, mbwa mwitu, mbweha, chatu na tai wakubwa.
Kutokana na taarifa zilizo tolewa na IUCN, changamoto kubwa kwa wanyama hawa ni kuwindwa na mbwa wafugwao. Watu wamekuwa na tabia ya kuwaachia mbwa wao na kuingia katika maeneo tengefu kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori kisha mbwa hawa kuwala isha. Hali hii inaweza kuoneka kama sio tatizo kubwa lakini isipo tiliwa mkazo italeta athari kubwa sana hapo baadae kwani tumeona hapo nchini Lesotho wanyama hawa wameanza kutoweka baadhi ya maeneo.
Changamoto nyingine ambayo imezungumziwa dhidi ya wanyama hawa ni vijana wadogo ambao wanachunga mifugo yao wamekua wakiwawinda wanyama hawa kwa siri kitu ambacho kinaweza pelekea kupungua kwa wanyama hawa katika maeneo mbali mbali.
NINI KIFANYIKE ILI IDADI YA WANYAMA HAWA IENDELEE KUWA YA KURIDHISHA KAMA ILIVYO SASA
Kama tulivoona hapo changamoto kubwa ni mbwa wafugwao, basi mamlaka za usimamizi wa wanyamapori hazina budi kuhakikisha mbwa hawa wanakuwa hawaingii katika hifadhi za wanyamapori lakini piawafugaji wa mbwa hawa wanatakiwa kuelezwa kuhusu athari zinazo sababishwa na mbwa wao kwa wanyama hawa.
Wizara ya mifugo pia inapaswa kusimamia sheria ya mifugo ipaswavyo ili kupunguza wimbi la mbwa wanao achiwa na kuzurura hovyo kitu ambacho kinaonekana kuleta athari hasi kwa upande wa wanyamapori. Wizara iwatoze faini wafugaji wote wa mbwa ambao wanawaachia mbwa wao kuzururz hovyo ili iwe fundisho kwa wengine na hapo tatizo la mbwa hawa kuvamia maeneo ya wanyamapori litakuwa limekwisha.
Vijana wadogo hawa wanachunga mifugo yao wapewe onyo kuhusu ujangili dhidi ya wanyama hawa kwani kadri wanavo zidi kuwawinda wanyama hawa itafika kipindi watapungua kwa kiasi kikubwa sana. Hivyo ni muhimu kuanza kulishughulikia tatizo hili kabla halijawa kubwa na la kutishia uhifadhi wa wanyama hawa.
Mbali na hayo inabdi kuhakikisha viashiria vyote ambavyo huwa ni changamoto kwa wanyamapori havijitokezi kwani kwa kufanya hivyo itasaidia wanyama hawa kubaki katika idadi inayo ridhisha kama walivyokwa sasa. Mambo ya kupambana nayo ambayo hayatakiwi kabisa kujitokeza ni kama uvamizi wa watui katika maeneo tengefu ya hifadhi za wanyamapori, uingizwaji wa mifugo katika maeneo hayo, uharibifu wa mazingira, biashara haramu ya wanyamapori na mgawanyo wa mazingira katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori.
HITIMISHO
Kwa sasa idadi ya wanyama hawa inaridhisha na tuna kila sababu ya kujivunia kwa hatua hii tulonayo kwa upande wa isha. Kama tulivyoona nchini kwetu Tanzania tunatajwa kuwa ni miongoni mwa nchi ambazo wanyama hawa wanapatikana kwa idadi kubwa sana hivyo hatuna budi kuhakikisha sifa hii inaendelea kuwepo hapa nchini kwetu.
Pongezi kubwa sana ziende kwa mamlaka mbali mbali ambazo zinasimamia uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini kama TANAPA, TAWA na NCAA kwa kazi kubwa sana wanayo ifanya ili kuhakikisha wanyama hwa wanaendelea kuwepo kwani ni dhahiri bila wao basi tusingekuwa na idadi ya kuridhisha ya wanyama hawa na huenda hata wasinge kuwepo kabisa. Nasi kama wanachi wenye uchungu, haki na jukumu la kuzisaidia mamlaka hizi, hatunabudi kutoa msaada wetu pale tutakapo hitajika ili kuwazuiya wachache ambao wanataka kutajirika kwa ubadhilifu wa rasilmali hizi za taifa.
Basi mpaa hapo sina la ziada ila nakusihi tu tukutane kwenye makala nyingine inayo fuata ili ujue mengi zaidi kuhusu wanyamapori hali kadhalika uelekeo wa wanyama hawa hususani hapa nchini kwetu Tanzania.
……MWISHO……
Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori, maoni kuhusu makalahizi na ushauri usisite kuwasiliana nami kupitia
Sadick Omary
Simu= 0714116963/0765057969/0785813286
Email= swideeq.so@gmail.com
Facebook= Sadicq Omary Kashushu
Instagram= @sadicqlegendary