Katika makala zilizopita nilijikita sana katika kuelezea kundi la wanyama jamii ya swala na kwa uchache ndege. Makala ya leo napenda kutambulisha mfululizo wa kundi lingine la wanyama ambao wanajulikana kama REPTILIA (watambaaji).

Makala hii itazungumzia reptilia kwa ujumla kisha tutakuwa tunagusia viumbe mbali mbali ambao wanapatikana katika kundi hili na kwa kuanza tutaanza na kuwazungumzia nyoka hasa nyoka wanaopatikana hapa nchini Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.

Nitakuwa nikimchambua nyoka mmoja baada ya mwingine mpaka pale tutakapo fikia kikomo cha kuwajua nyoka wapatikanao hapa nchini kwa wale wenye sum una wasio na sumu pia.

Hivyo nakusihi ndugu msomaji kuwa Pamoja nami mwanzo mpaka mwisho wa makala hii kwani utajifunza mambo mengi sana kuhusu kundi hili lijulikanalo kama reptilia.

Aina mbali mbali za Reptilia. Picha kutoka: lookingfordiagnosis.com

UTANGULIZI

REPTILIA; Reptilia ni kundi la viumbe hai ambalo asili ya jina lake limetokana na namna viumbe hawa wanajongea kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Maana halisi ya jina hili ni kutambaa (tambaaji), hii ni manma ya mjongeo kwa wanyama hawa. Kutokana na tafiti za kisayansi, kundi hili la wanyama jamii ya reptilia limetokana na kundi la wanyama jamii ya amfibia ambalo humo kuna wanyama kama vyura na wengine. Ukaribu kati ya reptilia na amfibia umefanya viumbe hawa kwa pamoja kusomwa kwenye somo moja lijulikanalo kama Herpetology (Hepetolojia).

Reptilia ndio kundi la kwanza kabisa la viumbe hai wenye ugwe mgongo (Kodata) kuweza kukabiliana na hali ya kuishi nchi kavu kuliko wanyama wote wapatikanao kwenye faila ya kodata. Kwa bahati mbaya wanyama hawa hawana sifa ya kipekee ambayo unaweza kusema inawatofautisha na viumbe hai wengine. Hii ni kwasababu tafiti zinaonesha kuwa sifa za viumbe hawa ni muunganiko au wamechukua kutoka kwa wanyama mbali mbali hasa samaki na amfibia sifa nyingine chache wakichukua kutoka kwa ndege na mamalia.

Mtu anaweza kushangaa kwanini tunawaita viumbe hawa wanyama?, hii ni kutokana na uainishaji (classification) wa viumbe hai kibaiolojia kuanzia ngazi ya himaya mpaka spishi. Uainishaji huu upo katika mtiririko uufuatao, (Himaya → Faila → Ngeli → Oda → Familia → Jinasi → spishi).

Katika mfululizo huu reptilia wote huingia katika himaya ijulikanayo kama himaya ya wanyama(Kingdom Animali) na hii ndio sababu ya kuwaita reptilia wanyama.

Hivyo reptilia kwa ufupi wanapatikana katika Himaya ya wanyama, Faila ya kodata na Ngeli ya watambaaji. Baada ya Ngeli kinacho fuata ni Oda ambapo kuna zaidi ya Oda 8 lakini mpaka sasa zimebaki Oda nne tu dunia nzima huku nyingine zikiwa zimesha toweka duniani. Oda ambazo zipo kwa sana ni Testudinata, Crocodilia, Squamata na Rhynchocephalia.

Katika Oda Testudinata tunawapata kobe na kasa, Oda Crocodilia tunawapata mamba na jamii zake, Oda Squamata tunawapata nyoka na mijusi huku Oda Rhynchocephalia tunawapata tuatara ambao wanafanana na mijusi ila wanapatikana nchini New Zealand pekee. Miongoni mwa Oda zilizo kuwepo duniani za reptilia ambazo kwa sasa zimesha toweka duniani ni Procolophonia, Araeoscelidia, Avicephala, Younginiformes, Sauropterygia na Prolacertiformes.

Kutokana na tafiti, mpaka sasa kuna Spishi za reptilia zinazo kadiriwa kuwa 9,500 duniani kote. Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinajivunia kuwa na idadi kubwa ya wanyama hawa kwnye maeneo mbali mbali ambayo bado hayaja haribiwa na shughuli za binaadamu na hapa namaanisha hasa maeneo ambayo yamehifadhiwa kwaajili ya uhifadhi wa wanayamapori au misitu.

SIFA NA TABIA ZA REPTILIA

  1. Miili yao ina uwezo wa kugawanyika katika sehemu mbili zinazo fanana (bilateral symmetry) huku ikiwa na sehemu nne ambazo ni kichwa, shingo, kiwiliwili na mkia. Hawa ni miongoni mwa wanyama ambao wana mifupa mingi sana ya uti wa mgongo.
  2. Wana jozi mbili za miguu ambayo ina vidole vitano ambavyo vina kucha zilizo jikunja mfano wa pembe. Kuna baadahi ya mijusi hawana miguu huku nyoka wote wakiwa hawana miguu kabisa.
  3. Wana mifupa ya nje ambayo hujulikana kama magamba ambayo yamezunguka miili yao na huwasaidia kama kinga dhidi ya hatari lakini pia kulinda sehemu ya ngozi zao. Ngozi zao huwa kavu na hazina matezi.
  4. Midomo yao ipo sehemu ya kichwani/juu huku ikiwa na taya zenye meno yaliyo kaa au kunana na pia. Kwa kobe na kasa meno haya yapo kama mifupa migumu mfano wa mdomo wa ndege.
  5. Wana mifupa ndani ya mwili (skeletoni) huku fuvu likiwa na mfupa mmoja tu sehemu ya nyuma (occipital condyle). Mifupa ya mabegani imetengeneza alama ya herufi T.
  6. Miyoyo yao huwa na vyumba vitatu japo kwa upande wa reptilia jamii ya mamba miyoyo yao huwa na vyumba vine.
  7. Hawa ni miongoni mwa wanyama wenye damu baridi ambao jotoridi la miili yao hubadilika kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa ya mazingira waliyopo.
  8. Japo kuna ambao wanaishi kwenye maji, ila mfumo wa upumuaji kwa reptilia wote hutumia mapafu kama ilivyo kwa mamalia na ndege.
  9. Mfumo wao wa taka mwili ambazo zinatokana na naitrojeni huwa ni acidi ya yurea kama ilivyo kwa ndege.
  10. Urutubishaji wa mayai hutokea ndani ya mwili wa jike na mara zote jike hutaga mayai sehemu ya nchi kavu na mara zote watoto hufanana na wakubwa.
  11. Japo kwa baadhi huonekana wakiwatunza watoto kipindi kifupi baada ya kutoka kwenye mayai, uhalisia ni kwamba viumbe hawa hawana tabia ya kuwatunza watoto katika kipindi chao cha ukuaji hivyo zaidi ya 99% watoto hupambania maisha yao wenyewe mpaka kufikia umri wa kuzaliana.
  12. Reptilia ni miongoni mwa viumbe waoga sana na mara nyingi huwa wanakimbia pale wanapo hisi kuna hatari. Ni wachache sana ambao huweza kumshambulia binaadamu bila uoga hasa mamba.

UHIFADHI

Kama nilivyo tangulia kusema hapo juu, kuna takribani spishi 9,500 za reptilia duniani kote. Hii ni kutokana na tafiti zilizofanywa na shirika la umoja wa mataifa linalo shughulika na uhifadhi wa maumbile asili (International Union for Conservation of Nature- IUCN). Kwa Afrika Mashariki kuna zaidi ya spishi 420 za reptilia. Tanzania tunajivunia kuwa na zaidi ya spishi 275 za reptilia ambao wengi wao wanapatikana hapa nchini tu na katika maeneo machache ambao wameorodheshwa kwenye orodha ya IUCN. Wanyama hawa wanapitia changamoto nyingi sana ambazo zinapelekea wanapungua sana duniani kote na kutoweka kwa baadhi ya maeneo.

UMUHIMU WA REPTILIA KWENYE IKOLOJIA

Reptilia wana umuhimu mkubwa sana kwenye ikolojia kama walivyo viumbe wengine. Kwa mtazamo wa haraka haraka mtu anaweza asione umuhimu wa wanyama hawa kwasababu haulengi moja kwa moja mafanikio ya binaadamu ambayo tunaweza kuyaona kwa macho lakini mchango wao ni mkubwa sana kwenye usawa wa kiikolojia. Viumbe hawa wanasaidia sana kupunguza viumbe hai waharibifu kwenye jamii hasa kwa upande wa afya na uchumi. Mfano nyoka wamekuwa na msaada mkubwa sana katika kupunguza idadi ya panya kwenye baadhi ya maeneo. Panya ni miongoni mwa viumbe waharibifu sana kwenye mazao lakini pia ndio wanyama au viumbe ambao wanabeba vimelea wa magonjwa mengi kuliko kiumbe yoyote yule.

Mbali na kwenye ikolojia, reptilia pia hutumika kma chakula, dawa lakini pia watu hujipatia pesa kupitia biashara ya wanyama hawa. Baadhi ya mataifa yanaingiza pesa nyingi za kigeni kupitia utalii ambao unatokana na uwepo wa reptilia katika maeneo yao.

CHANGAMOTO KWA REPTILIA

Reptilia wengi wanapitia changamoto kutokana na muonekano wao na dhana iliyo jengeka katika jamii nyingi. Watu wengi wana wachukia reptilian na kulazimika kuwauwa bila hata sababu. Mfano nyoka atakapo onekana popote basi watu humshambulia na kumuuwa.

Baadhi wamekuwa wakiwindwa kutokana na Imani za kishirikina hali inayo pelekea wanyama hawa kupungua kwa kasi sana kani wanyama hawa kama tulivyoona hawana tamaduni ya kulea watoto. Hivyo anaweza kuwana watoto zaidi ya 20 kwenye uzao mmoja lakini asikue hata mmoja au wakakua 2 tu.

Uharibifu wa mazingira pia ni changamoto kubwa kwa reptilia hasa uchomaji moto wa misitu na maeneo tengefu ya wanyamapori. Kuna baadhi ya wakulima wanatabia ya kuchoma au kuongoza ukubwa wa mashamba yao ufikapo msimu wa kilimo, hii hupelekea kuharibu makazi ya wanyama hawa.

MUHIMU

Kuna kila sababu ya kutoa elimu kwa watu kuhusu viumbe hawa na umuhimu wao kwani wana mchango mkubwa sana kwenye maisha ya binaadamu tofauti na watu wanavyo wachukulia. Elimu kuanzia ngazi za mashuleni mpaka vyuo lakini hata kwa jamii ni muhimu sana kwani itasaidia kuendelea kuwatunza wanyama hawa. Hata uanzishwaji wa vituo vya uhifadhi na maonesho ya reptilia ili watu wawe wanahudhuria na kupata taarifa au elimu kuhusu reptilia.

HITIMISHO

Miongoni mwa viumbe ambao wamesahaulika sana ni hawa reptilia. Kwasasa kumekuwa na umuhimu mkubwa sana wa kuwafahamu viumbe hawa kwani tunapo elekea tutaanza kuwapoteza na hatimae baadhi watatoweka duniani kabisa. Makala hii nimejaribu tu kukuelezea kwa ufupi kuhusu reptilia kwa ujumla. Katika makala ijayo tutaanza kuelezea reptilia mmoja baada ya mwingine na tutaanza na kundi la nyoka.

Tutakuwa tukimchambua nyoka mmoja mmjoa hasa kwa wale nyoka ambao wanapatikana hapa nchini Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla. Hivyo nikusihi ndugu msomaji wa makala hii kuwa mfuatiliaji wa makala zijazo kwani utajifunza mambo mengi sana kuhusu nyoka na namna ya kuepukananao lakin pia utajifunza kutofautisha nyoka wenye sumu na ambao hawana sumu.

Kwa maelezo na maoni kuhusu makala hizi za wanyamapori basi wasiliana nami kupitia;

 

Sadick Omary Hamisi

Simu=0714116963

Email= swideeq.so@gmail.com

Facebook=Sadicq Omary Kashushu

Instagram= wildlife_articles_tanzania

Au tembelea tovuti= www.wildlifetanzania.co.tz

 

Marejeo (References)

1.Explering the world of reptiles and amphibia:Authors (Jen Green; Richard Spilsbury & Barbara Taylor.

2.Field guide to the amphibians and reptiles of Arusha ational Park (TANZANIA). Authors (Ediardo Razzetti & Charles Andekia Msuya).

3.A field guide to the reptiles of East Africa. Authors (Stephen Spawls, Kim Howel, Robert Drewes & James Ashe)

4.Herpetology:An Introductory Biology of Amphibians and Reptiles. Authors (Laurie J. Vitt & Janalee P. Caldwell).

5.Pocket guide to the reptiles and amphibians af East Africa. Authors (Stephen Spawls, Kim M. Howell & Ribert C. Drewes)