Nilikuwa nasafiri kwenda Iringa, kupitia barabara inayokatisha katika hifadhi ya Taifa ya Mikumi, tulipokuwa tunaingia hifadhi ya Taifa ya Mikumi ilibidi nigeuke upande wa dirishani kuangalia uzuri wa hifadhi ya Mikumi, niliona wanyama wengi kama vile swala, pundamilia, ngiri, twiga, nyani na ndege wengi.
Nilitamani dereva apunguze mwendo ili tuende taratibu niendelee kuangalia wanyama na ndege wengi wakiwa katika makazi yao ya asili wakila, wakicheza na kufurahia maisha ya mwitu. Nikiwa naendelea kuchungulia nje ya dirisha la gari, abiria wengine nao walikuwa wanashangaa sana na kufurahia uzuri na wanyama katika hifadhi hii.
Nakumbuka wakati nasoma Shahada ya kwanza ya Usimamizi wa wanyamapori, katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, nilibahatika kufanya mafunzo kwa vitendo katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, wakati tukiwa Mikumi tulielezwa habari mbali mbali za hifadhi hii ya kipekee.
Kuna baadhi ya mambo mengi kuhusu hifadhi ya Taifa ya Mikumi nayakumbuka vizuri sana tangu tulipofundishwa na Profesa pamoja na mkuu wa hifadhi hii mwaka 2014. Baadhi ya mambo hayo nimeyaandika hapa ili na wewe upate kuyajua ili uifahamu vizuri hifadhi hii ya kipekee.
Kwanza, tuliambiwa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ilianzishwa mwaka 1964, ni hifadhi iliyopo katika mkoa wa Morogoro, ni hifadhi inayoshika nafasi ya tano kwa ukubwa nchini Tanzania, ikiwa na ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 3230. Kwa wakati huo 2014, ilikuwa ikishika nafasi ya 4 kwa ukubwa, kabla ya kuanzishwa kwa hifadhi ya Taifa ya Nyerere mwaka 2019, ambayo ndio hifadhi kubwa kuliko zote kwa hapaTanzania.
Hifadhi ya Mikumi ipo umbali wa kilomita 283 kutoka Dar es salaam, ni hifadhi inayofikika kwa urahisi zaidi ukitokea mikoa yote Tanzania. Hifadhi hii imepakana na hifadhi ya taifa ya Nyerere kwa upande wa Kusini, ambayo ndio hifadhi kubwa kuliko zote nchini Tanzania, pia ipo miongoni mwa hifadhi kubwa sana duniani, ikiwa na ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 54,600, kabla ya hapo hifadhi ya taifa ya Nyerere ilikuwa sehemu ya Pori la Akiba la Selous. Aidha, hifadhi ya taifa ya Mikumi imepakana na hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa.
Kutokana na kuwa katika eneo bora la kijiografia, inayochangiwa na kuwepo katika ukanda wa safu za milima ya Tao la Mashariki, hifadhi ya Mikumi ina hali nzuri na hewa, na vipindi vya mvua za kutosha, kiasi cha kufanya kuwepo kwa ukanda wa mafuriko ndani ya hifadhi hii. Hali nzuri ya hewa imechangia kuwepo kwa uoto wa aina mbali mbali ambao umekuwa ni sehemu muhimu ya chakula na makazi ya wanyama, ndege na wadudu katika hifadhi hii.
Mandhari nzuri, uoto na hali ya hewa ya kuvutia imefanya hifadhi hii kuwa na idadi kubwa ya jamii nyingi za wanyamapori kama vile tembo, simba, nyati, swala, chui, pundamilia, aina nyingi za nyani, ngiri, twiga, mbwa mwitu nk. Kutokana na wingi wa jamii nyingi za wanyama katika hifadhi hii, imefanya mifumo mingi ya kiikolojia kufanya kazi vizuri na kuzidi kuvutia aina nyingi za wanyama na ndege.
Mkuu wa hifadhi alituambia hifadhi ya Mikumi inakadiriwa kuwa na zaidi ya spishi 400 za ndege. Profesa aliongeza na kusema, ukiona hifadhi ina idadi kubwa ya spishi za ndege ujue hifadhi au eneo hilo ni muhimu sana kwa uhifadhi wa wanyamapori. Ndege ni kiashiria kizuri cha kuonyesha afya ya mifumo ya kiikolojia ya eneo, hivyo hifadhi ya Mikumi inajitahidi sana kuhifadhi mazingira asilia ya wanyama na ndege ndio maana kuna idadi kubwa ya wanyama, ndege na wadudu.
Mkuu wa hifadhi aliendelea kutueleza kuwa hifadhi ya Mikumi inajulikana duniani kote, kutokana na upekee wake, na wageni kutoka kila kona ya dunia hufika katika hifadhi hii na kujionea vivutio vingi vinavyopatikana katika hifadhi hii. Profesa aliongezea kwa kusema, kutokana na jiografia ya hifadhi ya Mikumi, ni rahisi kuona wanyama wengi hata wale walio hatarini kutoweka kama vile mbwa mwitu.
Mkuu wa hifadhi aliendelea kuongea kuhusu shughuli za utalii katika hifadhi hii, aliongeza kwa kusema hata idadi ya watanzania wanatembelea hifadhi hii ni kubwa. Hii ni kwasababu ya gharama nafuu za kutembelea hifadhi hii, lakini pia miundombinu ya barabara ni mizuri, hivyo mtu anaweza kutoka Dar es salaam akaja kufanya utalii na kurudi siku hiyo hiyo bila shida, hivyo kama hifadhi tunajitahidi kuboresha huduma zetu ili tuweze kupata wageni wengi wanaokuja kutembelea hifadhi hii.
Baadaya maelezo mazuri kutoka kwa mkuu wa hifadhi, nilimuuliza ni changamoto gani wanazipata kama hifadhi, alishusha pumzi kidogo, akasema changamoto katika hifadhi hii ni nyingi, lakini kubwa ni migogoro ya watu na wanyama kama tembo na nyani, changamoto nyingine ni ujangili kwa ajili ya nyamapori, kuchoma mioto hovyo na nyingine kubwa ni uwepo wa barabara ya Iringa inayokatisha hapa hifadhini.
Mkuu wa hifadhi pamoja na Profesa walitumia muda mwingi kuelezea changamoto za wanyama wengi kugongwa na magari. Uwepo wa barabara kuu inayokatisha katika hifadhi hii una faida zake na hasara zake hasa kwa upande wa wanyamapori. Uwepo wa barabara kuu inayounganisha mikoa ya nyanda za juu kusini kama vile Iringa, Njombe, Mbeya, Katavi; pia nchi jirani kama vile Zambia na Malawi umekuwa na hatari kubwa kwa wanyamapori wengi katika hifadhi hii.
Mkuu wa hifadhi aliongeza kuwa, kila siku asubuhi lazima wapite kuokaota mizoga ya wanyamapori waliogongwa na magari, hali hii inasikitisha sana, maana idadi ya wanyamapori wanauwawa kwa magari inazidi kuongezeka kila siku, hali hii ni hatari sana kwa mustakabali wa wanyama na hifadhi kwa ujumla. Mkuu wa hifadhi alisema kwa wastani, kila siku mnyama moja anagongwa na gari. Lakini alibainisha kuwa, takwimu hizi ni makadirio ya chini sana, maana wanyama wengine wanaweza kugongwa na kukimbila porini na kufia huko au kuliwa na wanyama wengine wanaokula nyama kama vile fisi, bweha, simba, tumbusi.
Mkuu wa hifadhi alisema kama shirika (TANAPA) na serikali walishatoa maelekezo na maonyo mengi kwa watumiaji wa barabara hiyo inayokatiza kaitika hifadhi hiyo, aliongeza kusema kuna alama nyingi za kuashiria kupunguza mwendo, lakini bado tunaona tatizo linazidi kuwa kubwa na wanayama wengi wanapoteza maisha yao. Kwa kawaida inatakiwa mwendo kasi wa gari linapoingia hifadhini usizidi mwendo kasi wa kilometa 50 kwa saa wakati wa usiku, na wakati wa mchana mwendo kasi usizidi kilometa 70 kwa saa.
Aidha, mkuu wa hifadhi anakiri kuwa, baadhi ya madereva wa magari yanayopita katika barabara hiyo hawazingatii sheria na alama za barabarani zilizowekwa katika hifadhi hiyo, hivyo wanafanya makusudi na ndio mara nyingi hulete maafa kwa wanyama wetu. Vibao vya alama za mwendo zinaonyesha kuwa gari likiingia katika hifadhini linatakiwa kuwa na mwendo kasi uliowekwa na hifadhi husika.
Pamoja na hayo mkuu wa hifadhi alisema wanashirikiana kwa ukaribu na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani, ili kuwabaini wanaovunja sheria na kanuni za uendeshaji magari katika eneo la hifadhi, na endapo watabainika watatakiwa kulipa faini kulinaga na aina ya mnyama waliyemgonga.
Mfano, endapo twiga au tembo atagongwa faini yake ni dola za Marekani 15,000, sawa na shilingi za Tanzania 34,000,000. Chui akigongwa faini yake ni dola za Marekani 3,500 sawa na zaidi ya shiling za Tanzania 8,760,00, faini ya kugonga simba ni dola za Marekani 4,900 ambazo ni zaidi ya Shilingi za Tanzania 12,265,000, wakati faini ya kugonga nyati ni dola za Marekani 1,600 ambazo ni sawa na zaidi ya Shilingi za Tanzania 4,000,000. Bei hizi na faini hizi ni kwa mujibu wa sheria za uwindaji na sheria ya uhifadhi namba 5 ya mwaka 2009.
Je, kuna mpango wa kuihamisha barabara hiyo? Mkuu wa hifadhi alisema kuna mpango wa serikali wa kuhamisha barabara hiyo na kuipitisha sehemu nyingine ili wanyama wasiendelee kuuwawa kwa ajali. Je, mpango huo utaanza lini, mkuu wa hifadhi alisema, tayari mapendekezo yote yameshapelewa serikalini, na wanasubiria serikali kuamulia utekelezaji wa jambo hilo.
Sekta ya uhifadhi wa wanyamapori inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zote zinatishia uhifadhi endelevu wa maliasili zetu, hivyo kama nchi tunatakiwa kufanyia kazi yale ambayo yanaweza kupunguza athari hasi kwenye uhifadhi wa wanyamapori. Kama watu wameshindwa kusimamia sheria za barabarani, ni bora hiyo barabara ikahamishwa, na ikapita sehemu nyingine.
Wale madereva mnaokimbiza magari na kusababisha vifo kwa wanyamapori, mjue mnafanya makosa sana, mnaua wanyama wasio na hatia, madereva tunatakiwa kuheshimu sheria na alama za barabarani, mjue mnapita kwenye miji na makazi ya wanyama, hivyo tuheshimu wanyama.
Tukiona wanyama wanakatiza barabara, hatuna budi kusimama kuhakikisha wanapita kwanza wao, ni haki yao kupita na kutumia barabara hiyo kwa imepita kwenye makazi yao. Sheria za usimazizi wa wanyamapori zipo wazi ukigonga wanyamapori adhabu yake ni kubwa sana. Tujitahidi kuheshimu sheria za barabarani ili tulinde wanyama wetu waendelee kuwepo katika mazingira yao kwa vizazi vingi vijavyo.
Baada ya kupata maelezo na mafunzo kutoka kwa mkuu wa hifadhi na Profesa, wote tulielewa na kusikitika sana kuona idadi kubwa ya wanyama wanapoteza maisha yao kila siku kwa kugongwa na magari yanayopita katika hifadhi ya Mikumi. Wote tuliahidi kuwa mabalozi wazuri, kwa kutoa elimu na kuzingatia sheria za uendeshaji magari ndani ya hifadhi ili wanyamapori waendelee kuwepo. Naamini hata wewe baada ya kusoma makala hii utakuwa balozi mzuri wa uhifadhi, kwa kujazingatia sheria za barabarani, kutoa elimu ya uhifadhi, na pia utawashirikisha wengine makala hii ili na wao wajifunze kama wewe.
Imeandikwa na Hillary Mrosso, +255 683 862 481, hmconserve@gmail.com