Ujangili ni kitendo cha uwindaji haramu usio na kibali chochote chini ya mamlaka husika za wanyama pori.

Mfano nchi yetu imebarikiwa sana wanyamapori pamoja na mazingira mazuri ya kuwatunzia lakini kwa bahati mbaya baadhi yetu wanaingiwa na tamaa na kuwinda kwa manufaa yao binafsi, labda kwa lengo la kujipatia pesa au matumizi mengine ambayo yamapelekea ongezeko kubwa la kupungua kwa wanyamapori na kuwa  mbioni kutoweka duniani kama faru, simba na tembo. Kutokana na utafiti uliofanywa chini ya Umoja wa Mataifa wamegundua tembo 100 kila siku barani Afrika wanauawa.

Mnamo Mwaka 2016 utafiti mwingine ulifanywa  na shirika la Umoja wa mataifa la kupambana na Dawa za kulevya na Uhalifu( UNODC), Benki ya Dunia(WB), na Shirika la Kimataifa la Polisi (Interpol) kwa kutumia vina saba( DNA) lilipima meno ya tembo yaliyokamatwa, mfano Julai 2006 kilo 2500 meno ya tembo yaliyokamatwa nchini Taiwan yalipimwa na kugundulika kuna nchi mbili Afrika zinazoongoza kwa uuaji wa tembo ambazo ni Tanzania na Kongo.

Miundo na ngazi za Ujangili

Miongoni mwa masomo ambayo alifundisha Dk.Robert Mande(mwenyewe kiti wa kudhibiti Ujangili) na mjumbe wa wizara ya mali asili na utalii, siku ya forum Chuo kikuu cha Dar es salaam tar.14 April 2018, alisema zipo ngazi tano za Ujangili ambazo ni;

Ngazi ya kwanza

Mara nyingi ni majangili ambao wanakaa pembezoni mwa mbuga za wanyama na mapori ya akiba Mfano; waganga wa kienyeji

Ngazi ya pili 

Illegal hunters au wawindaji haramu basipo kibali chochote  na hawa huwinda kwa ajili ya mboga na ufahari, pia wakati mwingine wanatumiwa na ngazi ya tatu.

Ngazi ya tatu

Transportes au wasafirishaji hawa mara nyingi hawaingii porini, kazi yao kusafirisha vitu ambavyo wamefanya ngazi ya pili. Mara nyingine huingia porini.

Ngazi ya nne

Employed by dealers au watu maalumu walioajiriwa kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya ngazi ya tatu, wapo juu ya ngazi ya tatu na pia hawaingii porini.

Ngazi ya tano

Money lounders/ dealers au watakatishaji fedha haramu, Mara nyingi hukaa mbali kabisa ya bara la Afrika, hawa ndio wamiliki wa masoko ya ndovu na pembe kinyume cha sheria.

Pia ngazi hii hawaijui hata njia ya kuingilia porini.

Zijue sababu ambazo watu wengi wamekuwa wakijiingiza kwenye Ujangili pasipo kuogopa nguvu kubwa ya Serikali ya Tanzania na Umoja wa mataifa iliyowekezwa katika uhifadhi.

  1. Rushwa na matumizi mabovu ya mamlaka. Imepelekea wanyama wengi kupotea kutokana na baadhi ya viongozi kutokuwa wazalendo juu ya mali za nchi yao pia kuonea aibu majangili katika kuitenda sheria wakiogopa kutengwa na hata kukosa marafiki.
  2. Utambuzi mdogo juu ya Uhifadhi. Majangili wa ngazi ya chini, ngazi ya kwanza na ya pili wamekuwa na utambuzi mdogo juu ya uhifadhi, wanawinda wakiamini wanyama hao wataendelea kuwepo kitu ambacho hakipo.
  3. Kutokushikilia sheria kiufasaha na kuwepo kwa askari wachache. Majangili wengi wakubwa sio kwamba hawakamatiki, bali ni vile sheria isivyoshikiliwa kifasaha juu yao na kuwafanya wakomae katika Ujangili , pia askari kuwa wachache kwenye maeneo yaliyohifadhiwa inapelekea maeneo mengi kutofikiwa kwa muda mrefu na kupelekea majangili kupata nafasi.
  4. Elimu ndogo juu ya jamii inayonufaika na viumbe hao. Wapo wananchi wasiojua jinsi viumbe hao kupitia Utalii  wanavyonufaisha jamii kwa miradi mbali mbali kama vile kujengewa madarasa ya shule, kuimarishwa kwa barabara na hata zahanati , hivyo hujikuta wanawinda kama kukomoa Serikali.
  5. Imani potofu juu ya matumizi yatokanayo na pembe za faru na meno ya tembo. Pia wapo wanaofanya  Ujangili wa pembe za faru wakiamini ni dawa, kitu ambacho sio kweli kwa sababu “material” au malighafi yaliyounda  pembe za faru ni sawa na kucha na nywele zetu
  6. Tamaa ya umaarufu na mali za mkupuo. Ngazi ya tano sio ni watu wenye njaa Bali ni tamaa ya kujulikana  kibiashara zaidi na kuongeza mali kwasababu kama ni pesa, tayari wanazo.

Ngazi ya pili ambayo mara nyingi wakifanya uwindaji haramu na kutoa pembe za faru na meno ya tembo hulipwa labda 20,000Tsh kitu ambacho ni uonevu hii ni kwa sababu jino moja haliwezi uzwa kwa pesa ndogo hivo lakini tamaa ya pesa inawaponza.

Madhara ya Ujangili

I.Kiikologia

– wanyama aina mbalimbali kuingizwa kwenye kundi la wanyama walio mbioni kutoweka.

Mfano, faru ambao kwa sasa wanapatikana mbuga chache sio zaidi ya tano nchini hii ni kutokana na Ujangili.

Simba ambao nao wamepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na Ujangili wa ngozi yao na kucha.

Tembo hajaingizwa kwenye kindi hilo ila tusipokaa sawa wataingizwa nao kwa sababu idadi yao imeshuka kwa 62% kutoka muongo uliopita na ujangili ukiendelea Umoja wa Mataifa(UN) wanasema hawata kuwepo tena.

Wanyama kuharibika kisaikolojia . Pia ujangili umepelekea wanyama wengi kuharibika kisaikolojia na kushindwa kuzaliana kutokana na yale matukio walioshuhudia ndugu zao wakifanyiwa na kujikuta wakiishi pasipo amani tena.

Ikolojia ya mazingira ya wanyama kushindwa kujiweka katika mstari wake (ecosystem fail to balance).

Kutokana na Ujangili inapelekea ikolojia na miingilianao ya wanyama kushindwa kufanyika.

Mfano, Ujangili wa simba unapelekea ongezeko kubwa la uzalianaji wa wanyama walao nyasi na majani na kufanya mazingira na uoto uliopo kushindwa kuhimili na kuwatunza wanyama hao na mwisho wanyama kutoweka.

  1. Kiuchumi

Watalii kupungua  kuingia nchini. Kama Ujangili utaendelea watalii watakuja kuona nini ikiwa Utalii wetu mkubwa ni wanyama  pori, hivyo pesa kazi zitapungua na kuurudisha uchumi nyuma.

Kusafirisha wanyama kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine kitu ambacho kinagharimu fedha nyingi.

Mfano, faru weusi kutoka Afrika Mashariki waliopelekwa Afrika Kusini mwaka1961. Na May 2018 faru weusi kutoka Afrika Kusini kurudishwa Serengeti. Pia kitendo hichi hupelekea ugumu wa kuishi kwa wanyama hawa na baadhi yao kupoteza maisha kabisa.

Hata za kuchuku

  1. Uwazi wa mapato ya Uhifadhi pamoja na matumizi yake. Ili kupunguza ujangili njia moja wapo ni uwazi wa mapato kwa wananchi na jinsi pato hilo linavotumika kujenga taifa na kunufaisha jamii kwa ujumla, hii itasaidia hasa kwa wale wanaofanya ujangili kwa nia ya kuikomoa serikali kuacha Mara moja.
  2. Ulinzi shirikishi kwa wananchi. Serikali chini ya wizara ya Maliasili na Utalii, napenda kuishauri izidi kutoa mafunzo kwa vijiji karibu na mbuga na mapori ya akiba maana hii itasaidia upatikanaji wa haraka wa majangili kwa sababu wananchi wanajuana na mara nyingine ina kuwa ngumu kutajana ila ulinzi shirikishi utasidia  majangili kuacha ikiwa tayari wao wamepata kazi hiyo watajua vizuri hata ujanja wa kuwakamata majangili wengi.
  3. Kupitia sheria zilizotungwa juu ya ujangili kazi kuzifanyia kazi. Naamini sheria zilizopo ni nzuri kabisa katika kutokomeza ujangili ila sasa tunahitajika kuzipitia vizuri zaidi na kuziweka wazi kwa wananchi ili zitakapofanyiwa kazi asiwepo wa kujitetea.
  4. Elimu kwa watu kuhusu Uhifadhi. Inawezekana watu wengine bado hawajui kama ujangili una maafa makubwa kama niliyotaja hapo juu hasa wanyama kutoweka kabisa duniani hivyo elimu na semina za wanyama pori zikifanyika sana itasaidia kuokoa wanyama na kupunguza ujangili kwa kiasi kikubwa.
  5. Kuongeza askari kwenye mbuga zote na mapori ya wanyama pori. Ningependa kuwasilisha wazo hili kwa wizara ya Maliasili na Utalii ili waokoe viumbe hawa, maana askari ndio wapo lakini bado ni wachache mno kitu ambacho kinapelekea ujangili uzidi kushamiri, kwasababu maeneo yanayofikiwa kwa wakati ni machache sana.

Nashukuru kwa muda wako uliotumia kusoma makala hii, Tuongee kwa niaba yao!!!, ukishindwa  kuongea jaribu kufikiria ungekuwa wewe ndio mnyama jinsi gani inauma kushuhudia ndugu zao wanauliwa tena mkiwa nyumbani kwenu kabisa??

Ntakushukuru zaidi kama sote tukiungana na kupinga vita Ujangili.

Makala hii nzuri sana na nzito imeandikwa na Leena na kuhaririwa na Hillary Mrosso. Leena ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu Dar es salaam, akisoma shahada yake ya kwanza katika Sayansi ya Uhifadhi wa Wanyamapori.

Kwa maoni ushauri, maswali kuhusu makala hii unaweza kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa mawasiliano hapo chini.

Asanteee sana

 Leena Lulandala

UDSM-student

+255 755 369 684

lulandalaleena@gmail.com