Ili kupambana na ujangili ni vizuri vitengo vyote vinavyopambana na ujangili kama vile vikosi vya kuthibiti ujangili au kwa kingereza wanasema “antipoaching units” vikapata mafunzo, mbinu, ujuzi na uwezo wa kiintelijensia ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi. Baada ya kutokea mauaji ya kutisha ya tembo katika miaka ya 1970 na 1980, askari wa wanyamapori waliuwawa mara kwa mara walipokutana na majangili. Ni katika kipindi hiki ndio juhudi za kuanza kuwekeza ujuzi, mbinu na mafunzo ya kisasa kwa askari wanyamapori zilianza ili kusimamia usalama wao na maliasili za wanyamapori walizozilinda.

Hata hivyo, pamoja na askari wanyamapori kupatiwa mafunzo, ujuzi na mbinu mbali mbali za kupambana na majangili bado walihitaji ushirikiano wa karibu na vitengo vingine vya ulinzi na usalama kama vile wanajeshi na pia jeshi la polisi katika kufanya kazi kwa ufanisi katika maeneo yao kuanzia Mashariki hadi Kusini mwa Afrika.

Rafiki yangu unayesoma makala hizi za wanyamapori, nakukaribisha tena katika sehemu hii muhimu ya uchambuzi wa ripoti, ELEPHANT IN THE DUST, THE AFRICAN ELEPHANT CRISIS. Ndani ya ripoti hii kuna mambo mengi sana, haya niliyoyaweka katika makala hii ni baadhi tu ya mambo muhimu yanayoweza kuisaidia jamii kuelewa kwa kina katika sekta hii ya maliasili na uhifadhi wa tembo ulivyo mashakani, karibu nikushirikishe yale ya muhimu.

Katika hali ya kuonyesha mafanikio, eneo la hifadhi ya Virunga ambalo lipo katika sehemu za nchi ya Uganda, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, askari wanyamapori (rangers) wamefanikiwa kulinda na kusimamia kuongezeka kwa idadi ya Sokwe wa Milimani waliopo katika eneo hilo muhimu la hifadhi licha ya eneo hilo kuwa katika vita na migogoro kwa miaka mingi.

Aidha, hayo yakiwa yanaendelea katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, hali si shwari kwa upande wa Afrika Magharibi, ambapo udhaifu katika uongozi, ukosefu wa vifaa na vitendea kazi umechangia sana askari kushindwa kufanya kazi yao kwa ufanisi na kusababisha tembo kupungua sana kwenye maeneo hayo. Maaskari wanyamapori wanafanya kazi katika mazingira magumu sana katika eneo hili la Afrika, vita, vikundi vya uasi na vya kigaidi na uingizaji wa silaha haramu umechangia sana tembo kupungua badala ya kuongezeka, hali ambayo inaelekea kutoweka kwao.

Vifaa muhimu kama vile magari, radio, ndege maalumu za doria ni muhimu sana kwa askari wa wanyamapori ili waweze kufanya kazi zao ipasavyo. Kukosekana kwa vifaa na vitendea kazi kumesababisha utendaji na usimamizi wa maeneo ya wanyamapori kuwa mgumu. Hii ni kwasababu sio maeneo yote ya doria utaenda kufanya doria kwa miguu, au kwa gari. Kulinagana na hali ya eneo lilivyo na mahitaji ya vifaa vyake inatakiwa iendane na hali halisi ya eneo hilo. Kwa kuzingatia hayo kazi za doria ambazo hufanywa na maaskari wanyamapori zitafanyika kwa ufanisi na hifadhi za wanyamapori zitabaki salama.

Vitengo vya ufuatiliaji vinatakiwa vianzishwe na viwe na upeo mkubwa wa kufuatilia majangili mchana na usku. Hali hii ya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kubaini njia na sehemu zote za majangili zitasaidia sana kupunguza vitendo vya kijangili kwenye maeneo ya wanyamapori, pia itawafanya majangili kukata tamaa wanapofuatiliwa kila mara, hivyo ujangili utapungua sana.

Ni wazi kabisa kama tunataka kukabiliana na janga hili la ujangili wa tembo barani Afrika, nchi zote ambazo zina wanyama hawa zikaunda vikosi vya ufuatiliaji na kudhibiti ujangili (antipoaching tracker units) ambavyo vitakuwa na mafunzo ya kisasa kabisa ili kukomesha ujangili wa tembo na wanyamapori wengine hapa Afrika.

Hata hivyo juhudi za kuunda vikosi vya kupambana na kudhibiti ujangili zimezaa matunda katika nchi ya Tanzania ambapo nchi hii imelichukulia jambo hili kwa uzito sana, hivyo kupelekea kuanzishwa kwa vyuo maalumu kwa ajili ya kutoa mafunzo na kozi muhimu kwa ajili ya kufuatilia na kupambana na ujangili, vyuo hivyo ni Chuo cha Mweka kama kinavyojulikana, Mweka College of African Wildlife Management na chuo cha Pasiansi kama kinavyojulikana, Pasiansi Wildlife Training Institute. Ambavyo vimetoa maaskari na watalaamu wa fani hii ya wanyamapori na uhifadhi wake.

Halikadhalika, pamoja na juhudi hizi, nchi zote za Kusini mwa Afrika zenye meneo ya wanyama hawa (range states) zinatakiwa kushirikishana mbinu mbali mbali za kiintelijensia, ujuzi na utalaamu wao kupitia kwenye makubaliano yao kama vile Makubaliano ya Lusaka (Lusaka Task Force Agreement). Kwa kufanya hivyo ujangili utapungua sana kama sio kuisha katika maeneo haya.

Kutokana na kusafirisha kiasi kikubwa cha meno ya tembo kutoka nchi za Afrika kwenda nchi za Asia. Mfumo wa ulinzi unatakiwa kuimarishwa kitaifa na kimataifa, kwa sababu ya kuvuka mipaka ya nchi mbali mbali, ushirikiano mkubwa unatakiwa kwenye maeneo yote ya vituo vya ukaguzi kuhakikisha sheria na usimamizi mkali unafanyika katika vituo na maeneo yote yanayohusika.

Katika kuongeza ufanisi katika usimamizi na ukaguzi katika  usafirishaji haramu wa meno ya tembo mamlaka zinazohusika na usimamizi wa wanyamapori zinatakiwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kimataifa zinazojihusisha na kudhibiti usafirishaji wa bidhaa haramu  kama vile Asasi ya Kimataifa inayohusika na Kupambana na Uhalifu dhidhi ya Wanyamapori (International Consortium on Combating Wildlife Crime, ICCWC) au kwa kushirikiana na Shirika la Forodha la Dunia (World Customs Organisation WCO), Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayojihusisha na Madawa na Uhalifu (United Nations Office on Drugs and Crime, UNODC) na Polisi wa Kimataifa yaani  INTERPOL.

Njia zote za majini na nchi kavu ambazo zinatumika katika uharamia wa usafirishaji wa meno ya tembo zinatakiwa kuchunguzwa na mashirika ya kamtaifa kama vile UNODC, CITES, INTERPOL na WCO ili waweze kudhibiti usafirishaji na upenyezaji haramu wa meno ya tembo. Katika kufanya juhudi hizi watafiti na waandishi wa ripoti hii wanasema itasaidia pia katika kukomesha uingiaji wa bidhaa nyingine unaofanyika kwa njia haramu kama vile madawa ya kulevya, uingizaji silaha za magendo nk.

Endapo nchi zanye wanyamapori hawa zitajihusisha na kushirikiana na masharika haya makubwa ya kimataifa ambayo yana ujuzi na uzoefu mkubwa katika masuala ya intelijensia, matatizo ya ujangili kwa ngazi za chini yanaweza kugundulika kwa urahisi na askari watakuwa na uwezo mkubwa wa kuwabaini wanaohusika na ujangili pamoja na mitandao yote inayojihusisha na biashara haramu.

Hata hivyo kuna mfumo ambao upo kwa ajili ya kushughulikia mambo haya ya ujangili na biashara haramu zinazovuka mipaka ya kimataifa. Licha ya kuwepo kwa watalaamu na wajuzi kutoka katika mashirika ya kimataifa kama yanayojihusisha na udhibiti wa madawa ya kulevya na biashara haramu, bado hakuna utekeleza kwenye mfumo huu wa kuzuia usafirishaji wa bidhaa haramu katika mipaka ya kimataifa.

Changamoto inayokabili utekelezaji kwenye mfumo huu ni kukosekana kwa fedha hivyo watalamu na watafiti wanashindwa kufanya kazi ya kupambana na mifumo hiyo haramu. Taarifa za ripoti hii katika kipengele hiki inasema endapo mifumo ya uendeshaji biashara haramu haitasumbuliwa na kupewa kashikashi, tutawapa wakati mgumu sana maaskari wetu ambao watazidi kuwa hatarini kila mara wanapojaribu kupambana na mifumo hii mikubwa inayojihusisha na ujangili wa tembo na pia wanapokuwa kwenye majukumu yao mengine.

Halikadhalika, maaskari na watumishi wa sekta hii watakapopata mafunzo muhimu na ujuzi katika masuala ya upelelezi na intelijensia watasaidia sana kupatikana kwa ushahidi muhimu sana ambao utasaidia kuonyesha kila kitu kilichohusika katika mfumo mzima wa biashara hii haramu. Ushahidi huo utasaidia pia kuwatia hatiani wahusika wakuu ambao mara nyingi hawakamatwi kwa sababu wapo nchi za mbali. Kwa kuwa na ujuzi na mbinu nzuri wahusika wote bila kujali mkubwa wala mdogo wote watafikishwa katika vyombo vya sheria na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao kwa kujihusisha na ujangili wa tembo.

Pamoja na kwamba kumekuwa na ukamataji mkubwa wa meno ya tembo katika sehemu nyingi za Afrika, bado watuhumiwa na watu wote wanaohusika na uingizaji, usafirishaji wa meneo ya tembo kwa njia haramu hawajafanywa chochote. Hii ni kusema hakuna kilichofanyika katika kuharibu au kusambaratisha mfumo huo haramu. Hivyo basi tunatakiwa kuongeza uwezo wa kufanya ukaguzi wa makontena, na vyombo vyote vinavyotumika katika usafirishaji, sambamba na hilo elimu hasa ya uelewa wa masuala haya ya wanyamapori na biashara haramu inatakiwa kutolewa kwa mamlaka zote zinazohusishwa na biashara hii hasa maeneo ya mipakani na kwenye bandari, viwanja vya ndege na sehemu nyingine nyeti za vituo vya usafirishaji.

Aidha, kuwa na askari wanyamapori wenye uwezo mkubwa wa kuzimudu kazi zao kutokana na weledi, maarifa na vitendea kazi vya kisasa itasaidia sana kuweka hali ya usalama sio tu kwa wanyamapori bali hata kwa maisha ya watu ambao wapo pembezoni mwa hifadhi, watumishi, wanafunzi na hata watafiti wanaokuja kujihusisha na masuala ya wanyamapori. Mazingira ya usalama kwa wanyamapori ni muhimu sana kwani itasaidia sana hata kukuza utalii na hivyo serikali kupata fedha nyingi za kigeni kwa ajili ya maendeleo ya kijamii.

Kufikia hapa sina la ziada katika uchambuzi wa sehemu hii muhimu ya ripoti yetu. Makala hii ni muhimu sana ikasomwa na kila mtu, hasa mamlaka za usimamizi wa wanyamapori, mashirika na wadau wa uhifadhi wa wanyamapori. Askari wa wanyamapori ni watu muhimu sana katika uhifadhi, wameyatoa maisha yao kulinda urithi na hazina hii muhimu ya nchi yetu. Hivyo naiomba serikali yetu, mashirika na wadau wa mazingira na uhifadhi wa maliasili kuwaboreshea maslahi yao, kuwapa vifaa na vitendea kazi vyote muhimu kwa ajili ya usalama wao na usalama wa maliasili zetu.

Ahsante sana kwa kusoma makala hii hadi mwisho!

Uchambuzi huu umeandaliwa na;

Hillary Mrosso

+255 683 862 481/255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania